KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 5, 2016

SERIKALI YAUFUNGIA WIMBO WA CHURA WA SNURA


Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini toka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi. Zawadi Msalla (katikati) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapopichani) wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu kusitishwa kwa wimbo wa Msanii Snura Mushi ujulikanao kwa jina la Chura kwa kukiuka maadili kushoto ni Mwanasheria wa wizara hiyo Bw. Patrick Kipangula na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Utamaduni Bibi. Lily Beleko.
Serikali imesitisha wimbo na Video ya Muziki wa Chura wa Msanii Snura Mushi  kuchezwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuanzia leo mpaka pale msanii  huyo atakapoifanyia marekebisho video ya wimbo huo.

Usitishwaji huo umetokana na maudhui ya utengenezwaji wa Video hiyo ambayo haiendani na maadili ya Mtanzania.

Pia Serikali imesitisha maonyesho yote ya hadhara ya mwanamziki huyo mpaka pale atakapo kamilisha taratibu za usajili wa kazi zake za Sanaa katika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Serikali inawataka wasanii kujiuliza mara mbili kabla ya kubuni kazi zao za Sanaa. Wafikirie wazazi, ndugu, jamaa na marafiki zao watazipokeaje? Wavae nafasi ya wale wanaowadhalilisha, Waelewe kwamba Sanaa si uwanja wa  kudhalilisha watu hata kidogo..

Aidha Serikali imechukizwa na kazi hiyo ambayo si tu inadhalilisha tasnia ya Muziki bali inadhalilisha utu wa mwanamke na inaifanya jamii kuanza kuhoji hadhi ya msanii, weledi na taaluma ya Sanaa kwa ujumla.

Serikali inawakumbusha wananchi wote kutokujiingiza katika makosa ya sheria ya mtandao kwa kusambaza wimbo huu kwa njia yoyote ile ya kimtandao

Pia inavitaka Vyombo vya habari viwe vya kwanza kuchuja maudhui ya kazi yoyote ya Sanaa kabla ya kuwa mawakala wa uharibifu wa jamii kupitia kucheza kazi chafu za Sanaa.

Serikali inatoa wito kwa wasanii wote kuzingatia maadili ya Kitanzania kabla ya kutoa kazi zao kwani haitawavumilia ‘wasanii’ wachache ambao wanataka kuigeuza tasnia ya Sanaa kuwa sehemu ya uvunjifu wa maadili.

Imetolewa na Zawadi Msalla

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

No comments:

Post a Comment