KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, September 2, 2011

LEPA: Nimefunga ukurasa na mume wangu








LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu nyota wa kike wa Nigeria, Folashade Omoniyi amesema kwa sasa ameamua kufunga ukurasa wa mumewe wa zamani, Kassim.
Folashade, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Lepa Shandy, alisema kwa njia ya simu wiki hii akiwa mapumzikoni Dublin, Ireland kwamba, ameshampata mwanaume mwingine wa nguvu, hivyo hapendi kuirejesha akili yake kule alikotoka.
Mwanadada huyo, aliyecheza filamu kedekede kama vile ‘Breaking Point’, ‘Feyi Pitan’, ‘Enitan’, ‘Oyato’, ‘Owo Ajanu’, ‘Iyawo Elenu Razor’, ‘Back To Africa’, ‘Omi Ewuro’, ‘Yeye Oge’ na ‘Il anu Oluwa’, alitengana na mumewe huyo miaka saba iliyopita.
Alipoulizwa alikuwa wapi tangu alipotangaza kutengana na mumewe, Lepa alisema: “Nilikuwa Ulaya. Na kwa sasa nipo Dublin (Ireland). Nimekuwa nikijaribu kujiweka sawa kimaisha. Kiukweli nimekuja hapa kupumzika.”
Lepa alisema alifululiza kufanyakazi kwa miezi kadhaa hivyo ameona huu ni wakati mwafaka kwake kupumzika. Alisema safari yake hiyo barani Ulaya haihusiani kitu na kuvunjika kwa ndoa yake.
Mwanadada huyo alisema si kweli kwamba alikimbia kwao kwa sababu ya shinikizo kutoka kwa wazazi wake la kumtaka arejee kwa mumewe wa zamani.
Alisema kamwe wazazi wake hawakuwahi kuiunga mkono ndoa yake na pia hawajawahi kumshinikiza arejee kwa mumewe.
Lepa alisema mama yake alijaribu kidogo kufanya hivyo kabla hajafariki, lakini baada ya kuomba mambo hayaendi vizuri, alikata tama na kumuacha afanye anavyotaka..
“Nilikuwa pekee niliyevaa viatu vyangu, hivyo naelewa wapi mwiba ulinichoma. Hivyo ndoa yangu imevunjika. Nilijaribu kuifanya idumu, lakini mume wangu alikatisha tamaa jitihada zangu,”alisema.
“Hata pale alipoacha kuwasiliana na mimi, niliendelea kufanya hivyo na mara mbili nilikwenda London ili kuona jinsi tunavyoweza kurekebisha mambo, lakini jitihada hizo hazikufua dafu,”aliongeza.
“Hivyo kwa sasa mimi nipo tena peke yangu, lakini sitafuti mwanaume, nahitaji muda kuweka mambo yangu sawa na pia kuwa na amani,”alisema mwanadada huyo.
Lepa asema hatarajii kurejea tena kwa mumewe hata kama atamtaka afanye hivyo. Alisema kamwe hawezi kusema usiku mwema na asubuhi njema kwa wakati mmoja.
Mrembo huyo alisema si kweli kwamba kazi yake ya uigizaji ndiyo iliyochangia kwa kiasi kikubwa kusambaratika kwa ndoa yake. Alisema alikutana na mumewe kabla ya kujitosa kwenye fani hiyo hivyo alikuwa akitambua vyema majukumu yake.
Alisema ndoa yao ilivunjika kwa sababu ya tofauti zilizojitokeza kati yao. Hata hivyo, hakuwa tayari kuzizungumza kwenye vyombo vya habari kwa madai kuwa, hayo ni masuala ya ndani kati yao.
Lepa alikiri kuwa, ni kweli kwamba kwa sasa ameshampata mpenzi mpya, lakini hataki ajulikane kwenye vyombo vya habari. Alisema yeye ni mwanamke na kamwe hawezi kuishi pweke muda wote.



Umri wangu bado mdogo kuolewa-Halima

LAGOS, Nigeria
MWIGIZAJI machachari wa Nollywood, Halima Abubakar amesema hatarajii kufunga ndoa hivi sasa kwa sababu umri wake bado ni mdogo.
Halima (20) alisema wiki hii mjini hapa kuwa, hatafuti mwanaume na kamwe hakuwahi kusema hivyo.
“Watu hawapaswi kuwa na haraka juu yangu. Haya ni maisha yangu na ninaishi ninavyotaka mimi, hivyo hawapaswi kufuatilia mambo yangu,’alisema.
Halima alisema atafunga ndoa pale tu wakati utakapomruhusu kufanya hivyo na kamwe hawezi kushinikizwa na yeyote. Alisema hakuna anayeweza kumshinikiza mtu yeyote kufunga ndoa.
“Ukweli ni kwamba ndoa huweza kudumu kadri unavyotaka iwe hivyo nami nataka ndoa yangu idumu milele,”aliongeza.
Hata hivyo, Halima alikiri kuwa, kwa mila na desturi za kwao, watoto wa kike wamekuwa wakipewa waume tangu wakiwa wadogo naye iliwahi kumtokea hivyo.
“Kuna mwanaume alikuja na kutaka kufunga ndoa na mimi, lakini nilikataa kwa sababu bado nilikuwa mdogo,”alisema.
Halima alisema aliamua kujitosa kwenye fani ya uigizaji kutokana na kuvutiwa na filamu za Kihindi. Alisema alivutiwa na filamu nyingi tofauti na kutamani awe kama waigizaji wa kike wan chi hiyo.
Binti huyo alisema uhusiano wake na waigizaji wenzake wa kike wa Nigeria ni mzuri, lakini alikiri kuwa si rahisi kupendwa na wote.
“Kuna watu wengi ambao ni rafiki zangu kutokana na kazi yangu. Hata hivyo, siku zote utakuwa na marafiki, ambao Mungu amekupangia,”alisema.


Naya hajutii kurejea Nigeria


LAGOS, Nigeria
BINTI machachari katika fani ya uigizaji filamu nchini Nigeria, Beverly Naya amesema kamwe hajutii uamuzi wake wa kurudi nchini humo na kuendeleza libeneke la mzigo huo.
Naya alikuwa akiishi Uingereza na wazazi wake kwa zaidi ya miaka 14 kabla ya kurejea Nigeria mwaka jana, ambako amekuwa aking’ara kutokana na umahiri wake katika fani hiyo.
“Nauheshimu uamuzi wangu wa kurejea Nigeria kutoka London, ambako niliishi kwa miaka 14. Ni kweli naikosa familia yangu na rafiki zangu waliopo Londoa, lakini kazi yangu ni muhimu na ninaifurahia,”alisema.
Naya alisema tangu aliporejea Nigeria mwaka jana, ameshiriki kucheza filamu saba. Alizitaja baadhi ya filamu hizo kuwa ni pamoja na ‘Home in Exile’, ‘Mystery of Destiny’, ‘Make me a heart’, ambazo alizicheza kwa kushirikiana na Desmond Elliot, Rita Dominic, Jackie Appiah na Francis Duru.
Binti huyo alisema anaridhishwa na maendeleo ya fani hiyo nchini Nigeria hivi sasa kutokana na mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika utengenezaji wa filamu.
Naya alisema alipata baraka zote kutoka kwa wazazi wake kabla ya kujitosa kwenye fani hiyo ikiwa ni pamoja na kumpa moyo kwamba anaweza.
Mwigizaji huyo aliwataka mashabiki wa fani ya filamu nchini Nigeria watarajie kuona vitu vingi zaidi kutoka kwake. Alisema uwezo wake katika fani hiyo umekuwa ukiongezeka kadri siku zinavyosonga mbele.
Naya alisema kwa sasa hana haraka ya kufunga ndoa mpaka hapo atakapofanikiwa kutimiza malengo yake katika uigizaji.

1 comment:

  1. hello,
    Hii ni kuwajulisha wananchi kwa ujumla kuwa Bibi, kiutamaduni matumaini binafsi mkopo wakopeshaji ina kufungua nafasi mpya za fedha kwa kila mtu katika haja ya msaada wowote wa kifedha. Sisi kutoa mkopo saa 2% riba kwa watu binafsi, makampuni na makampuni chini ya sheria wazi na ya kueleweka na hali hiyo. wasiliana nasi leo na e-mail (merithope6@gmail.com)

    ReplyDelete