KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 22, 2011

Uzinduzi Chupa Nyeusi wafunika Burundi


UZINDUZI wa filamu mpya ya Chupa Nyeusi, uliofanyika mjini mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Bujumbura, nchini Burundi, ulifunika kutokana na kuhudhuriwa na watu kedekede.
Mbali na uzinduzi huo kuhudhuriwa na mashabiki lukuki, baadhi ya washiriki waliocheza filamu hiyo walikuwa kivutio cha aina yake kila walipokatika katika mitaa ya jiji hilo.
Baadhi ya mashabiki hao walikuwa wakigombea kupiga picha na wacheza filamu hao wa kitanzania kwa ajili ya ukumbusho wao na wengine kuzungumza nao.
Mtayarishaji wa filamu hiyo, Husna Poshi ‘Dotnata’ alisema wiki hii kuwa, hawakutarajia kupata mapokezi makubwa kiasi hicho, ambayo aliyalinganisha na yale wanayopewa viongozi wa kiserikali.
Alisema tangu walipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Bujumbura, msafara wao ulikuwa na msururu mkubwa wa magari na uliongozwa na mkuu wa Jeshi la Polisi, aliyemtaja kwa jina moja la Mohamed.
Dotnata alisema heshima waliyoipata kutoka kwa wananchi wa Burundi ni kubwa na imeonyesha wazi jinsi wasanii wa Tanzania wanavyothaminiwa na kupendwa wanapokuwa nje ya nchi yao.
“Kwa kweli tunajisikia faraja kubwa kutokana na mapokezi tuliyoyapata katika Jiji la Bujumbura. Wananchi walitupokea kwa shangwe, kila mtu alikuwa akitaka kupiga picha na sisi,”alisema.
Dotnata alitoa shukurani za pekee kwa Meya wa Jiji hilo, ambaye hamkumbuki kwa jina, ambaye alisema aliwakaribisha ofisini kwake na kuzungumza nao kwa dakika kadhaa kwa lengo la kubadilishana mawazo.
Baadhi ya wasanii waliocheza filamu hiyo, walioshiriki kwenye uzinduzi huo ni Irene Uwoya, Mohamed Posh, Hisani Muya ‘Tino’, Patcho Mwamba na muongozaji wao, Moses Mwanyilu.

No comments:

Post a Comment