KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 15, 2011

Oge: Sina matatizo na mume wangu


LAGOS, Nigeria
MWIGIZAJI machachari wa Nigeria, Oge Okoye amekanusha madai kuwa, ndoa yake na mumewe imevunjika ama ipo hatarini kuvunjika.
Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari wiki hii, Oge amesema madai hayo si ya kweli na yamelenga kuchafua jina lake.
Oge amesema amechoka kupokea simu na meseji nyingi kutoka kwa ndugu, jamaa na rafiki zake wakimuuliza iwapo taarifa hizo zilizotolewa na vyombo vya habari ni za kweli.
“Mimi na mume wangu wiki chache zilizopita tulisherehekea siku ya kuzaliwa ya mtoto wetu wa mwisho, hivyo sielewi kwa nini watu wanaeneza tuhuma ambazo hazipo,”alisema.
“Najisikia vibaya ninaposoma taarifa hizi na inaonekana kama vile yupo Oge Okeye mwingine. Mimi nipo salama na hakuna chochote kilichotokea baina yangu na mume wangu,”aliongeza.
Oge alisema ndoa yake haijawahi kukumbwa na matatizo yoyote na kusisitiza kuwa, mumewe na wifi zake wanafurahia maisha yao na kumuonyesha upendo mkubwa.
Amewataka waandishi wa habari na wanaoeneza uvumi huo kwenda kutafuta kazi zingine za kufanya ili wawe bize kwa sababu yeye na mumewe hawana muda wa kupoteza kusoma taarifa zao.
Katika hatua nyingine, Oge amesema anatarajia kuigiza filamu mpya hivi karibuni, ambayo picha zake zitapigwa nchini Canada. Pia alisema amepata nafasi ya kucheza filamu na waigizaji kadhaa nyota kutoka Hollywood.

No comments:

Post a Comment