KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, September 2, 2011

DIAMOND: Sina bifu la kudumu na Bob Junior


MSANII Nasseb Abdul, maarufu kwa jina la Diamond, amesema si kweli kwamba amekuwa na bifu la kudumu na mtayarishaji maarufu wa muziki nchini, Bob Junior.
Diamond (22) alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, ni kweli kwamba zilijitokeza tofauti ndogo kati yake na Bob Junior, lakini kwa sasa mambo hayo yamekwisha.
Alisema hawezi kuwa na bifu la kudumu na Bob Junior kwa sababu wote wapo kwenye fani zinazofanana na kila mmoja anamtegemea mwenzake katika kufanikisha malengo yake.
Diamond alisema amekuwa akirekodi nyimbo zake mara kwa mara kwenye studio ya Bob Junior, inayojulikana kwa jina la Sharobaro Records, kwa sababu ya ukali wake katika kutengeneza mipigo ya ala za muziki.
“Mimi na Bob Junior hatukuwa na ugomvi wowote wa kutisha, zilijitokeza tofauti ndogo tu kati yetu, lakini watu wakakuza mambo,”alisema Diamond.
“Unajua yeye (Bob Junior) ni prodyuza mzuri wa nyimbo na mimi ni mtunzi, hivyo ninapokuwa na nyimbo yangu, ambayo naamini anaweza kuitengenezea beats (mipigo) kali, nakwenda kwake, hivyo tuna uhusiano mzuri wa kimuziki,”alisema.
Diamond na Bob Junior walikuwa maswahiba wakubwa, lakini uhusiano wao ulionekana kusuasua baada ya kuzuka tofauti kati yao, ambazo zilihusishwa na uhusiano wao kimapenzi na mwanadada Wema Sepetu.
Kuna wakati Bob Junior aliwahi kumfungulia kesi Wema kwenye Mahakama ya Kinondoni, Dar es Salaam, kwa tuhuma za kumtukana hadharani, lakini kesi hiyo ilifutwa baada ya wasanii hao wawili kuamua kumaliza tofauti zao nje ya mahakama.
Kwa sasa, Wema ana uhusiano wa kimapenzi na Diamond na wamekuwa wakionekana sehemu mbalimbali pamoja, huku ikidaiwa kuwa, mwanadada huyo ndiye aliyekufa zaidi kimapenzi kwa mwenzake.
Kabla ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Diamond, mwanadada huyo, aliyewahi kunyakua taji la Miss Tanzania mwaka 2006, alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki Chalz Baba na baadaye Steven Kanumba. Wema ni muigizaji wa filamu za kibongo.
Alipoulizwa kwa nini ameamua kubadili mipigo ya nyimbo zake kutoka ile ya taratibu na kubembeleza na kwenda ile ya kasi, Diamond alisema ni kutokana na mabadiliko ya nyakati.
Alisema si jambo zuri kwa sababu kuzoeleka kwa mashabiki kutokana na aina yake moja ya muziki, ndio sababu ameamua kubadili mapigo ili kupima upepo.
Hivi karibuni, msanii huyo aliibuka na kibao kipya cha miondoko ya Kwaito, ambacho kimemfanya aonekane kuwa na mabadiliko makubwa kimuziki.
“Unajua muziki ni biashara inayokwenda na wakati. Ni kweli mashabiki wamezoea kusikia nyimbo zangu zikiwa za mapenzi zaidi na miondoko ya taratibu, lakini kwa sasa nimeamua kubadili upepo,”alisema.
Alisema anashukuru kwamba, mashabiki wamekipokea vizuri kibao chake kipya cha miondoko hiyo, ambacho kimekuwa kikipigwa mara kwa mara kwenye vituo vya radio nchini.
Diamond alianza kung’ara kimuziki baada ya kushusha mpini unaojulikana kwa jina la Nenda kamwambie. Kibao hicho kilimwezesha Diamond kutwaa tuzo tatu za muziki za Kilimanjaro
Baadaye aliibuka na kibao cha Mbagala, ambacho kilizidi kumfanya ang’are kimuziki na kupata nafasi ya kualikwa katika nchi kadhaa za Ulaya kama vile Uingereza, Italia, Uholanzi na katika baadhi ya nchi za Scandinavia.
Msanii huyo amekiri kuwa, muziki wa kizazi kipya umemwezesha kupata mafanikio makubwa kimaisha, ikiwa ni pamoja na kuishi sehemu nzuri na kumiliki gari aina ya Toyota Celica.

No comments:

Post a Comment