KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 15, 2011

Kuziruhusu Simba na Yanga kucheza Chamazi ni kuhatarisha usalama

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) iliyopita lilitangaza kuziruhusu timu za Simba na Yanga kuutumia uwanja wa Chamazi, unaomilikiwa na klabu ya Azam kwa ajili ya baadhi ya mechi zao za ligi.
Uamuzi huo wa TFF umetokana na agizo la serikali kutaka uwanja mpya wa Taifa uliopo Dar es Salaam kutumika kwa mechi mbili tu za ligi kwa wiki.
Serikali ililazimika kutoa agizo hilo ili kuepuka uwanja huo kuharibika iwapo utachezewa mechi nyingi za ligi kama ilivyokuwa wakati wa michuano ya Kombe la Kagame, iliyofanyika nchini mapema mwaka huu.
Awali, Simba na Yanga zililazimika kuhamishia mechi zake kwenye viwanja vya Jamhuri mjini Morogoro na Mkwakwani mjini Tanga baada ya serikali kuufunga uwanja wa Taifa usitumike kwa mechi za ligi.
Lakini baada ya maombi ya TFF, serikali imekubali uwanja huo uendelee kutumika, lakini kwa masharti ya mechi mbili kwa wiki. Hiyo ndiyo sababu kubwa iliyozifanya Simba na Yanga ziombe kucheza Chamazi kwa ajili ya mechi zingine.
Kwa mujibu wa ratiba, Simba ilianza kuutumia uwanja huo jana kwa mechi kati yake na Polisi Dodoma wakati Yanga itaanza kuutumia leo kwa mechi kati yake na African Lyon.
Uamuzi wa TFF kuziruhusu Simba na Yanga zicheze Chamazi ni wa kushangaza kidogo. Hii ni kutokana na mazingira halisi ya uwanja huo pamoja na wingi wa mashabiki wa klabu hizo.
Kwa mujibu wa taarifa za TFF, uwanja wa Chamazi una uwezo wa kuchukua mashabiki 5000 na kwamba tiketi zitakazouzwa kwa mashabiki, hazitazidi idadi hiyo.
Lakini shirikisho hilo limesahau kuwa, halina uwezo wa kuwadhibiti mashabiki kuingia kwenye uwanja huo kuziona Simba na Yanga. Kazi hiyo itakuwa ngumu na inahitaji nguvu ya ziada ya Jeshi la Polisi.
Licha ya uwanja huo kuwa na maeneo machache ya kukaa mashabiki, hakuna uzio wa kuwazuia kuingia uwanjani. Hali hiyo inaweza kusababisha maisha ya waamuzi, viongozi na wachezaji kuwa hatarini.
Kwa mfano, katika kipindi hiki ambacho viongozi wa Yanga wamekuwa wakiwatuhumu wachezaji wao kucheza chini ya kiwango, inaweza kuwa hatari kwao kwa sababu mashabiki watakuwa na uwezo wa kuingia uwanjani na kuwashughulikia kwa sababu ya hisia hizo.
Vivyo hivyo kwa waamuzi watakaochezesha mechi za timu hizo mbili kongwe, ambapo tayari Yanga imeanza kuwatuhumu vibaya baadhi yao kwa madai kuwa, hawaitendei haki timu yao na kwamba wanachezesha kwa lengo la ‘kuinyonga’.
Kwa kuzingatia ukweli huo, nadhani TFF imefanya kosa kubwa kukubali Simba na Yanga zicheze uwanja huo. Na huenda imefanya hivyo kwa lengo la kuzifurahisha klabu hizo mbili, lakini madhara yake yanaweza kuwa makubwa.
Kama viwanja vingi vilivyopo sasa hapa nchini si salama kwa wachezaji, viongozi na mashabiki, sidhani kama uwanja wa Chamazi unaweza kuzifaa Simba na Yanga katika ligi. Ipo hatari ya mashabiki kushuhudia matukio ya ajabu ajabu, ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wao.
Lakini kikubwa zaidi ni kwamba, hii ni aibu na fedheha kwa Simba na Yanga, zilizoanzishwa miaka zaidi ya 70 iliyopita kutangatanga bila kuwa na viwanja vyao vya soka. Je, viongozi waliowahi kuziongoza klabu hizo, wataacha kumbukumbu gani kwa vizazi vijavyo? Na je, watakumbukwa kwa mambo gani waliyotenda kwa klabu hizo?
Klabu ya Yanga iliwahi kutangaza kuwa, itaufanyia ukarabati mkubwa uwanja wake wa Jangwani, ikiwa ni pamoja na kuuwekea nyasi za bandia na kujenga majukwaa ili utumike kwa mechi za ligi, lakini hadi sasa hakuna lolote la maana lililofanyika.
Alichoweza kukifanya mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Yusuf Manji ni kufanya ukarabati mkubwa kwenye jengo la makao makuu, ambapo kwa sasa linatumika kama ofisi za viongozi na hosteli kwa wachezaji. Kwa hilo, Manji anastahili pongezi.
Kwa upande wa Simba, uongozi wake uliopo sasa madarakani umeahidi kujenga uwanja mpya wa kisasa maeneo ya Bunju, Dar es Salaam, ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000. Ni vigumu kuamini iwapo ahadi hii itatekelezwa ama itakuwa ni blabla za viongozi wanapoingia madarakani. Tusubiri tuone.

No comments:

Post a Comment