KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, September 9, 2011

Nchunga kiongozi halali Jangwani


KAMATI ya Sheria, Katiba, Maadili na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imesema uongozi wa klabu ya Yanga uliopo madarakani ni halali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, mwenyekiti wa kamati hiyo, Alex Mgongolwa, alisema uongozi huo chini ya Lloyd Nchunga, uko madarakani kihalali, kwa mujibu wa katiba ya Yanga ya mwaka 2010.
Kamati hiyo ilikutana Septemba 3, mwaka huu, katika Ofisi za TFF kujadili mgogoro wa kikatiba uliopo ndani ya klabu ya Yanga na kuridhia kuwa ni viongozi halali.
Mgongolwa alisema baada ya kupokea nyaraka zilizowasilishwa mbele ya kamati, wamebaini kwamba katiba ya Yanga ya mwaka 2010 iliyosajiliwa katika ofisi ya msajili wa vyama vya michezo, inatambulika kisheria.
“Mchakato wa kupata katiba hiyo, ulifuata maagizo sahihi ya FIFA (Shirikisho la Soka Duniani) na TFF,” alisema.
Mgogoro wa uongozi wa Yanga, uliibuka ghivi karibuni baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Dar es Salaam kukubaliana na ombi la wanachama waliofungua kesi kuwapinga Nchunga na wenzake.
Wanachama hao, wakiongozwa na Juma Mwambelo, walifungua kesi Na. 98 ya mwaka 2010 katika mahakama hiyo wakidai kuwa uongozi wa Yanga chini ya Nchunga, uliwekwa madarakani na katiba ambayo ni batili, hivyo hawaopaswi kuongoza klabu hiyo.
Walidai kuwa katiba hiyo ni batili kwa kuwa haitambuliwi na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA- zamani Kabidhi Wasii Mkuu), badala yake katiba inayotambulika ni ile ya mwaka 1968, ambayo ilisajiliwa rasmi mwaka 1972.
Uamuzi wa wanachama hao, ulikuwa kinyume na sheria na kanuni za FIFA ambazo zinakataza mashauri ya michezo kufikishwa mahakamani, bali yanapaswa kufuata ngazi husika katika vyama na mashirikisho ya michezo kuanzia ngazi ya nchi hadi FIFA.
Kutokana na hatua hiyo, kamati ya Mgongolwa imeuagiza uongozi wa Yanga kuwachukulia hatua za kikatiba wanachama hao waliopeleka shauri hilo mahakamani.
“Iwapo klabu ya Yanga itashindwa kutekeleza agizo hilo, TFF haitasita kuichukulia hatua za kikatiba kwa mujibu wa katiba ya TFF na ya FIFA,” alisema Mgongolwa katika taarifa yake. Hatua hiyo ya wanachama ilishaanza kuathiri maendeleo na shughuli za klabu. Uamuzi huo wa mahakama ulizuia mkutano wa wanachama, uliokuwa umepangwa kufanyika Jumapili iliyopita kwenye bwalo la maofisa wa polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment