KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 22, 2011

SIMBA CHUPUCHUPU



SIMBA jana ilipunguzwa kasi ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kulazimishwa kutoka sare ya mabao 3-3 na Toto African katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini hapa.
Sare hiyo ilikuwa ya pili mfululizo kwa Simba baada ya wiki iliyopita kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar katika mechi iliyochezwa mjini Bukoba.
Pamoja na kulazimishwa kutoka sare, Simba bado inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi saba wakati Toto African inaendelea kushika nafasi ya tano ikiwa na pointi tisa sawa na Yanga, lakini zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
Simba ililianza pambano hilo kwa kasi na kubisha hodi kwenye lango la Toto African dakika ya saba wakati Emmanuel Okwi alipotanguliziwa mpira mrefu, lakini shuti lake lilipanguliwa na kipa Maganga Seif.
Mshambuliaji Felix Sunzu aliifungia Simba bao la kuongoza dakika ya nane alipounganisha kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na Juma Jabu kutoka pembeni ya uwanja.
Darlington Enyima aliisawazishia Toto African dakika ya 19 kwa njia ya penalti baada ya beki Obadia Mungusa wa Simba kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari wakati wa harakati za kuokoa.
Pambano hilo lililazimika kusimama kwa muda dakika ya 29 baada ya mbwa wa polisi kuingia katikati ya uwanja na kusababisha wachezaji Haruna Moshi na Sunzu kukimbilia kwenye benchi la Toto kwa lengo la kujiokoa.
Toto iliongeza bao la pili dakika ya 37 lililofungwa na Mohamed Sudi kwa shuti kali la mbali lililotinga moja kwa moja wavuni.
Dakika nane baadaye, Enyima nusura aiongezee Toto bao la pili baada ya kufumua shuti kali lililomshinda kipa Juma Kaseja na mpira kurudi uwanjani. Timu hizo zilikwenda mapumziko Toto ikiwa mbele kwa mabao 2-1.
Timu zote mbili zilikianza kipindi cha pili kwa kushambuliana kwa zamu, Simba wakicheza pasi ndefu huku Toto wakigongeana pasi fupi fupi.
Simba ilisawazisha dakika ya 59 kwa bao lililofungwa na Sunzu baada ya kuunganisha wavuni kwa shuti krosi kutoka kwa Okwi.
Dakika moja baadaye, Iddi Mobb aliiongezea Toto bao la tatu baada ya kudokolewa mpira na Sudi huku mabeki wa Simba wakizembea kumfuata kwa kudhani ameotea.
Patrick Mafisango aliisawazishia Simba dakika ya 65 kwa kiki kali iliyomshinda kipa Maganga wa Toto.
Toto ilipata pigo dakika ya 70 baada ya beki wake, Philemon Mwendasile kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya Mafisango.
Katika pambano hilo, mashabiki wapatao 100, baadhi wakiwa na tiketi, walivunja geti kuu la kuingilia uwanjani kutokana na kukosa uvumilivu wa kupanga foleni.
SIMBA: Juma Kaseja, Nassoro Cholo, Juma Jabu, Obadia Mungusa, Victor Costa, Patrick Mafisango, Ulimboka Mwakingwe/Gervas Kago, Jerry Santo, Felix Sunzu, Haruna Moshi, Amri Kiemba na Emmanuel Okwi.
TOTO AFRICAN: Maganga Seif, John Bosco, Philemon Mwendasile, Laban Kambole, Ladslaus Mbogo, Lulanga Mapunda, Emmanuel Swita, Mohamed Sudi, Darlington Enyima/ Mwita Kemronge, Iddi Mobb na Fabian James.

No comments:

Post a Comment