KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, September 2, 2011

AMIN: Tunakuja na taarab mpya ya kisasa


MMILIKI wa kikundi kipya cha T Moto Modern Taarab, Amin Salmin ‘Mourinho’ amejigamba kuwa, kundi lake litatingisha anga la muziki huo nchini kwa vile linaundwa na wasanii wengi nyota.
Akizungumzia kundi hilo kwa mara ya kwanza mjini Dar es Salaam wiki hii, Amin alisema ameamua kuleta mabadiliko na ushindani katika muziki wa taarab baada ya kubaini kuwa umepoteza mwelekeo.
Amin alisema kundi hilo litaibuka na aina tofauti ya muziki wa taarab na tayari vijana wake wameshaingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya kuipua albamu yao ya kwanza.
Kiongozi huyo wa T Moto Modern Taarab alisema, amekuwa makini katika kuliunda kundi hilo kwa sababu amepania kuliona likidumu kwa muda mrefu na kutoa ushindani wa hali ya juu kwa vikundi vilivyopo sasa.
Amin alisema alikuwa na ndoto ya kuanzisha kundi hilo muda mrefu uliopita, kutokana na kuwa na mapenzi makubwa na muziki wa taarab, lakini alikuwa akikatishwa tamaa na baadhi ya wasanii.
“Kuna wasanii wengi waliopoteza vipaji vyao ama kushindwa kuwa na maisha mazuri, licha ya kufanyakazi nzuri na kubwa, ambayo imekuwa ikipendwa na mashabiki wengi na kuuzika,”alisema.
Amin, ambaye amelifananisha kundi hilo na klabu ya Real Madrid ya Hispania alisema, mara kundi hilo litakapoanza mazoezi, ana hakika mashabiki watasuuzika nafsi zao kwa vibao moto watakavyoviipua.
Alisema aina ya muziki watakaoupiga itakuwa ya pekee kwa vile watatumia magita yote matatu na pia ala tofauti za muziki kwa lengo la kuleta ladha mpya.
Aliwataja waimbaji wanaounda kundi hilo, vikundi wanavyotoka vikiwa kwenye mabano ni mkongwe Mwanahawa Ally, Mosi Suleiman (Dar Modern Taarab), Jokha Kassim (Five Stars), Hasina Kassin (New Zanzibar Modern Taarab), Hassan Ali (Five Star) na mshindi wa shindano la BSS mwaka 2011, Mrisho Rajabu.
Wapiga ala ni Jumanne Ulaya (solo) kutoka Jahazi, Amour Salehe ‘Zungu’, Moshi Mtambo, Omary Kisila, Fadhili Mnara, Rajabu Kondo na Mussa Mipango.
Kwa mujibu wa Amin, albamu ya kwanza ya kundi hilo itajulikana kwa jina la ‘Aliyeniumba hajanikosea’, ikiwa na vibao sita. Kibao hicho kilichobeba jina la albamu kitaimbwa na Mwanahawa.
Vibao vingine ni ‘Mtoto wa Bongo’, kinachoimbwa na Hassan Ali, ‘Unavyojizani mbona hufanani’, kinachoimbwa na Joha, ‘Mchimba kaburi sasa zamu yake imefika’ cha Mrisho, ‘Mwenye kustili Mungu’ na ‘Kumbe wewe ni shoti’ za Mosi.
Amin alisema kundi hilo lilianza kurekodi rasmi nyimbo zake juzi na zinatarajiwa kuanza kurushwa hewani hivi karibuni kwenye vituo mbalimbali vya radio nchini.

No comments:

Post a Comment