KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 15, 2011

Vodacom kudhamini semina ya TASWA



MENEJA Uhusiano na Habari za Mtandao wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusiana na udhamini wa Vodacom kwa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo na Burudani Tanzania(TASWA) kwa ajili ya semina kwa wanachama wake. Katikati ni Katibu Mkuu wa Taswa, Amiri Mhando na kulia ni Katibu Mkuu Msaidizi, George John. (Na Mpiga Picha Wetu)


MAFUNZO kwa ajili ya waandishi wa habari za michezo nchini yaliyopangwa kufanyika mkoani Morogoro, Oktoba Mosi na pili mwaka huu, yatadhaminiwa na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Amir Mhando, alisema, maandalizi ya mafunzo hayo yanakwenda vizuri na wana matumaini yatakuwa na manufaa makubwa.
Mhando aliishukuru Vodacom Tanzania kwa kudhamini mafunzo hayo na kuongeza kuwa, ni hatua nzuri katika kutekeleza mikakati ya TASWA kuendesha mafunzo kwa wanachama wake na waandishi wa habari za michezo kwa ujumla chini ya kauli mbiu ya chama hicho isemayo: TASWA Mafunzo Zaidi.
Alisema mafunzo hayo yatahusisha washiriki 40 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Pwani na kuongeza kuwa, mwanzoni mwa Novemba mwaka huu, wataendesha mafunzo kama hayo mkoani Arusha, yakihusisha washiriki kutoka Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Manyra na baadhi ya washiriki kutoka Dar es Salaan.
Mhando alisema mwishoni mwa Novemba mwaka huu, TASWA pia itaendesha mafunzo kwa wahariri wa habari za michezo, ambayo yatakuwa nje ya Dar es Salaam na kwamba mkoa husika utatangazwa baadaye.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa TASWA, mafunzo ya Morogoro na Arusha yatahusisha masuala ya maadili ya uandishi wa habari,, masuala ya sheria za mambo ya habari na sheria za michezo mbalimbali.
Alisema washiriki wataelimishwa namna ya kuripoti habari za michezo ya mpira wa wavu, kikapu na riadha na kwamba kama mambo yataenda vizuri, pia utaingizwa na mchezo wa ngumi.
Aliongeza kuwa, wakufunzi katika mafunzo hayo ni baadhi ya walimu wa mambo ya habari, wahariri wazoefu, wanasheria na pia wakufunzi wa michezo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano na Habari za Mtandao wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu, alisema kampuni yake inajisikia fahari kubwa kudhamini mafunzo hayo na kwamba itaendelea kufanya hivyo kadri itakavyoweza na kwamba, mafunzo ya Morogoro yatagharimu kiasi cha sh. milioni saba.
“Vodacom Tanzania inajisikia fahari kwa kudhamini mafunzo haya kwani hii siyo mara ya kwanza kwa Vodacom kudhamini mafunzo ya aina hii, mwaka jana tuliendesha mafunzo ya wahariri wa habari za michezo. Mwaka huu tunadhamini mafunzo ya TASWA, yote haya tukiwa na lengo la kuboresha tasnia ya habari. Mafunzo ya Arusha pia tutadhamini, lakini bajeti yake itaangaliwa baadaye,” alisema Nkurlu.
Naye Katibu Msaidizi wa TASWA, George John alisema katika mkutano huo kuwa, chama chake kimeamua kuendesha mafunzo hayo kwa ajili ya kuwoangezea uelewa zaidi waandishi wa habari za michezo.
“Mafunzo yatasaidia sana kwani kwenye ripotingi yetu, mfano mchezo wa mpira wavu, huwa wengine wanauliza wameshinda kwa mabao mangapi? Wakati kule huwa ni mambo ya seti si mabao,” alisema John, ambaye pia ni Katibu Msaidizi wa Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA).

No comments:

Post a Comment