KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 27, 2011

SKENDO LA PAPIC


WAKATI hali ikiwa si shwari ndani ya klabu ya Yanga, imebainika kuwa, wachezaji wengi wa timu hiyo hawana mikataba inayoeleweka kutokana na kuchakachuliwa na baadhi ya viongozi.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, wachezaji pekee wenye mikataba ya uhakika hawazidi watano na kuongeza kuwa, wengine mikataba yao ni hewa.
Kwa mujibu wa habari hizo, kufuatia kubainika kwa uchakachuaji huo, mfadhili mkuu wa Yanga, Yusuf Manji ameuagiza uongozi wa klabu hiyo kukusanya mikataba yote ya wachezaji kwa ajili ya kuhakikiwa.
Uamuzi wa Manji kukusanya mikataba hiyo umekuja siku chache baada ya kukutana na wachezaji wote wa timu hiyo katika kikao kilichofanyika Jumatatu iliyopita, makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam. Manji alikutana na wachezaji hao kwa lengo la kusikiliza madai yao ya pesa za usajili na malipo mengine kulingana na mikataba yao. Aliutaka uongozi uwe umemaliza kazi ya kukusanya mikataba hiyo jana.
Katika kikao hicho, baadhi ya wachezaji walimweleza Manji kuwa, hawajalipwa pesa zao za usajili, kauli iliyomshtua mfadhili huyo kwa vile alishawapatia viongozi fedha zote.
Wachezaji wengine walimweleza mfadhili huyo kuwa, wamekuwa wakilazimika kuwalipa baadhi ya viongozi sehemu ya malipo yao kama fadhila kutokana na kufanikisha usajili wao.
Mbali na hilo, wachezaji wengine walimweleza Manji kuwa, wamekuwa wakiishi kwa hofu kutokana na baadhi ya viongozi kujenga chuki dhidi yao kwa kukataa kuwapa chochote.
Miongoni mwa wachezaji wanaodaiwa kuonja machungu ya viongozi hao ni pamoja na viungo Athumani Idd 'Chuji' na Ernest Boakye, ambaye aliwahi kutimuliwa katika kambi huko Tanga baada ya kudai anaumwa tumbo.
Wachezaji wengine, ambao pia inadaiwa wamekumbana na adha hiyo ni Mohamed Mbegu, ambaye naye aliwahi kusimamishwa kwa muda kwa tuhuma za utovu wa nidhamu. Wengine ni Fred Mbuna na Chacha Marwa, ambao wamekuwa hawapati namba kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Uchunguzi wa Burudani umebaini kuwa, baadhi ya viongozi wa Yanga walikuwa wakiingia mikataba kinyemela na wachezaji wa timu hiyo na kuwaandikia kiasi kikubwa cha malipo, lakini fedha walizokuwa wakiwapatia zilikuwa kiduchu.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya Yanga kimeeleza kuwa, kufuatia Manji kubaini kuwepo kwa mikataba hewa ya wachezaji, baadhi ya watendaji wakuu wa klabu hiyo wameamua kujiuzulu.
Miongoni mwa viongozi waliojiuzulu ni Katibu Mkuu, Lawrence Mwalusako, Meneja wa timu, Emmanuel Mpangala na Kocha Mkuu, Kostadin Papic.
Alipoulizwa jana kuhusu tuhuma za matumizi mabaya ya pesa na uchakachuaji wa mikataba ya wachezaji, Mwenyekiti wa Yanga, Llyod Nchunga alisema wameshaanza kufanya uchunguzi, ambao ndio utakaobaini iwapo ni kweli au la.
Nchunga alisema ukaguzi wa hesabu ndio utakotoa majibu iwapo viongozi waliojiuzulu wanahusika na tuhuma hizo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
Hata hivyo, Nchunga alimtetea Mwalusako kwa kusema hahusiki na tuhuma hizo na kusisitiza kuwa, kujiuzulu kwake kumetokana na matatizo ya kiafya kama taarifa yake kwa vyombo vya habari ilivyoeleza.
Kuhusu Papic, Nchunga alisema kocha huyo ameamua kujiuzulu baada ya kukataa kufanya kazi na Fred Minziro, ambaye ameteuliwa kuwa kocha msaidizi wa timu hiyo.
“Kwa vile hakutaka kufanyakazi na msaidizi wake, hakukuwa na sababu ya yeye (Papic), kubaki kwa sababu Yanga si ya mtu mmoja na ni lazima benchi la ufundi kama linamahitaji, lifanyiwe kazi,”alisema.
Kwa upande wake, Mwalusako alisisitiza kuwa, sababu alizozitoa kuhusu uamuzi wake wa kujiuzulu ni sahihi na hazina shaka na kuongeza kuwa, yupo tayari kuchunguzwa. Mpangala hakuweza kupatikana.

Z'bar kupata uanachama FIFA 2012

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema Zanzibar itakuwa mwanachama kamili wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ifikapo mwaka 2012.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdillahi Jihadi Hassan wakati akijibu swali na nyongeza la Mwakilishi wa Kiwani, Hijja Hassan Hijja aliyetaka kujua mchakato wa Zanzibar kuwa mwanachama wa FIFA utakamilika lini. Jihadi alisema mchakato huo unakwenda vizuri na tayari FIFA imeshaanza kuonyesha dalili za kuikubalia Zanzibar kuwa mwanachama.
Alisema mchakato huo unatarajiwa kukamilika rasmi ifikapo mwaka 2012 wakati wa mkutano mkuu wa FIFA, unaotarajiwa kufanyika mjini Zurich, Uswisi. “Nataka kuwaambia wajumbe kwamba, yapo matumaini makubwa ya Zanzibar kukubaliwa kuwa mwanachama wa (FIFA). Mchakato huu unakwenda vizuri na mkutano wa mwaka 2012 ndio utakaotoa idhini ya maombi yetu,”alisema. Zanzibar imekuwa katika mikakati na juhudi za kuomba uanachama wa FIFA tangu mwaka 2002, ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano imetoa baraka zote. Katika kutoa baraka hizo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekuwa likikisaidia Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) kwa hali na mali ili kiweze kupata uanachama huo.
Zanzibar inataka kuwa mwanachama wa FIFA ili iweze kufaidika na misaada mbalimbali inayotolewa na shirikisho hilo, ikiwemo ya fedha na kiufundi na pia kupatiwa wataalamu wa kukuza mchezo wa soka.

TINO: Filamu ya Shoga itatikisa


MTUNZI na mwigizaji mkuu wa filamu inayozungumzia tabia na vitendo vya ushoga, Hisani Muya amesema tayari kazi ya kuitayarisha imeshakamilika na inatarajiwa kuingizwa sokoni wakati wowote.
Muya, maarufu zaidi kwa jina la Tino alisema wiki hii mjini Dar es Salaam kuwa, filamu hiyo ilichelewa kuingizwa sokoni kutokana na kazi ya kuihariri kufanywa kwa umakini zaidi.
Tino alisema, awali filamu hiyo ilipewa jina la Painfull, lakini wameamua kulibadili, ambapo sasa itajulikana kwa jina la Shoga.
Mwigizaji huyo mwenye mvuto alisema kwa sasa yupo kwenye maandalizi ya mwisho kwa ajili ya uzinduzi wa filamu hiyo, ambao alitamba kuwa utakuwa wa aina yake.
Alisema ameamua kuandaa uzinduzi wa filamu hiyo kwa lengo la kuitangaza zaidi ili ujumbe wake uweze kuifikia jamii kiurahisi.
“Ni kweli tangu nilipoingia kwenye gemu, sijawahi kufanya uzinduzi wa filamu, lakini kumbuka mambo yanakwenda yakibadilika kila siku na tunataka kuwa kama wenzetu waliotangulia,” alisema.
Akifafanua kuhusu uamuzi wake wa kucheza filamu hiyo kama shoga, Tino alisema haoni kama kuna tatizo kwa vile hiyo si tabia yake bali amejaribi kuvaa uhusika huo kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa jamii.
Alisema filamu hiyo ni tofauti sana na zingine alizowahi kuzitayarisha kutokana na maudhui na ujumbe wake ndio sababu imezua utata kwa jamii inayomzunguka na watu wake wa karibu.
“Utata ninaouzungumzia hapa ni kama lilivyo jina lenyewe. Kwa mara ya kwanza Tino aliyezoeleka katika filamu za mapenzi anaigiza kama shoga badala ya filamu za malavidavi,”alisema mcheza filamu huyo huku akitabasamu.
Tino alisema hastushwi na hisia zilizoanza kujengeka kwa baadhi ya watu wanaodhani yeye ni shoga kwa sababu msanii anaweza kucheza nafasi yoyote anayopangwa.
“Wengi tayari wameshaanza kuhisi hii ni tabia yangu, lakini ukweli hii ni sanaa tu, haina maana kwamba ukiigiza kama shoga basi hiyo ndiyo tabia yako. Kwangu mimi hii si changamoto tu bali ni matatizo,”alisema.
Kijana huyo mtanashati alisema haoni iwapo filamu hiyo itamletea matatizo kwa waumini wenzake wa dini ya kiislamu kwa sababu alichokifanya ni kukemea tabi hiyo.
Alisema dini zote mbili, ya kiislamu na kikristo haziruhusu vitendo hivyo na kwamba katika filamu hiyo amejaribu kukemea tabia hiyo na kuonyesha madhara yake. Tino alisema haamini iwapo filamu yake hiyo inaweza kuchochea na kuhalalisha vitendo vya kishoga hadharani ama kuwakera viongozi wa dini hizo mbili kubwa nchini.
“Katika filamu hii, mimi nimeonyesha athari za ushoga, kwa ujumla ni kwamba shoga huyo katika filamu yangu anapata maambukizi ya ukimwi, lakini vilevile mkewe baada ya kugundua, anaamua kumuua kwa hiyo kupitia filamu hii, tumeona madhara ya ushoga,”alisema.
Kwa mujibu wa Tino, uzinduzi wa filamu hiyo umepangwa kufanyika Februari 4, 2011 katika ukumbi wa Travertine uliopo Magomeni, Dar es Salaam. Alisema uzinduzi huo utapambwa kwa burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali, likiwemo kundi la Mapacha Watatu.
Tino ameitaka jamii kuwa makini na vitendo vya ushoga kwa sababu vipo, lakini baadhi ya watu wanavifumbia macho na hawatakiKuvizungumza kwa kuvionea aibu.

MWALUSAKO: Kuongoza Yanga matatizo



SWALI: Pole na matatizo ya kuumwa. Hivi ni kweli kwamba hiyo ndiyo sababu hasa iliyokufanya uamue kujiuzulu uongozi wa Yanga?
JIBU: Ukweli ni kwamba mimi ninaumwa. Nimekuwa nikisumbuliwa kwa muda mrefu la tatizo la moyo, ugonjwa ambao nimegundua unaweza kufupisha maisha yangu.
Tatizo hilo limetokana na kutumia kwangu muda mwingi kufanyakazi bila ya kupumzika, hali ambayo wakati mwingine imekuwa ikiniweka kwenye wakati mgumu.
Unajua ukiwa kiongozi wa klabu kubwa kama Yanga, hasa katika nafasi ya utendaji niliyokuwa nikiitumikia mimi, unakuwa ukipigiwa simu mara kwa mara za kutakiwa kutatua tatizo hili na lile. Hali hii ilikuwa ikisababisha wakati mwingine napitisha hata muda wa kunywa dawa zangu nah ii ni hatari.
Licha ya tatizo hilo, nilijitahidi kufanyakazi zangu kwa ufanisi, lakini wapo baadhi ya wanachama au watu binafsi waliokuwa wakiniona sifanyi lolote.
SWALI: Kwanini unasema hivyo? Au kuna shinikizo umelipata kutoka kwa mfadhili mkuu wa Yanga, Yusuf Manji?
JIBU: Hapana, Manji hajanipa shiniko lolote kuhusu kujizulu, isipokuwa nimeamua kukaa pembeni ili niweze kujiuguza.
Pamoja na hilo, bado nina kila sababu ya kukaa pembeni kwani nimegundua wapo watu walikuwa wananiandama kwa sababu mbalimbali.
Pale Yanga wapo baadhi ya wanachama wakitaka jambo lao, ambalo pengine linahitaji maamuzi ya pamoja, na ukimweleza mtu asubiri na kisha likakataliwa, tayari mtu huyo atakuchukia.
Lakini ukweli ni kwamba yapo mambo mengi, ambayo kwa asilimia kubwa yamechangia mimi kufikia uamuzi huu ili kukwepa kujiumiza.
SWALI: Tangu ulipoteuliwa kuwa katibu mkuu wa Yanga, nini hasa kilitokea kukukera na pengine kuchangia kwa kiasi kikubwa wewe kujiuzulu katika wadhifa huo mbali ya ugonjwa?
JIBU: Kwa kweli nimekuwa nikichukizwa na baadhi ya watu, ambao wanaeneza chokochoko ndani ya Yanga. Watu hawa wamekuwa wakichonganisha watu, hasa viongozi na kufikia hatua ya kuigawa klabu kitu, ambacho ni kibaya.
Pia nimekuwa nikikerwa sana na tabia ya uzushi wa mambo na wakati mwingine watu kufikia hatua ya kuchafuana.
Wapo baadhi ya watu au wanachama walioeneza uvumi kwamba mimi na viongozi wenzangu tumekula pesa nyingi za Yanga kitu, ambacho si kweli kwani mambo yote yapo wazi.
SWALI: Je, upo tayari kushirikiana na wakaguzi wa hesabu ili kuchunguza mapato na matumizi ya klabu ya Yanga kwa kipindi chote cha uongozi wako?
JIBU: Nipo tayari kushirikiana na watu hao ili niweze kuweka wazi mambo kwani tabia ya kuchafuana si nzuri na jambo hilo ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha nijiondoe ndani ya uongozi wa Yanga. SWALI: Mwishoni mwa wiki hii Yanga itacheza na timu ya Dedebit ya Ethiopia katika mechi ya awali ya michuano ya Kombe la Shirikisho. Je, huoni kama kujiuzulu kwako kunaweza kuwachanganya wachezaji kwa kukosa huduma yako?
JIBU: Sidhani kama hilo linaweza kutokea. Wapo watendaji wengine, ambao naamini watafanyakazi zangu kwa ufanisi. Lakini binafsi nitaendelea kushirikiana na uongozi kwa vile mimi ni mwanachama wa Yanga.
Lakini nitafanya hivyo kama afya yangu itaniruhusu kwenda kufanya kazi za klabu iwapo nitahitajika. Kikubwa nawaomba wachezaji wa Yanga wajitume zaidi ili kuhakikisha wanashinda mchezo huo.
Pia nawaomba viongozi, wanachama na wapenzi wa Yanga tuwaunge mkono wachezaji wetu kwa kuwashangilia kwa nguvu ili waweze kushinda mchezo huo.
SWALI: Hivi sasa umeshajiondoa katika uongozi wa klabu ya Yanga, nini matarajio yako kwa siku zijazo?
JIBU: Natarajia kuendelea na kazi yangu niliyokuwa nikiifanya kabla ya kujiunga na Yanga huku nikiangalia afya yangu kwa ukaribu zaidi ili niweze kupona kabisa.
Naamini naweza kurejea kazini siku zijazo kwa ajili ya kujitafutia riziki, lakini nitaendelea kuwepo Yanga na milango ipo wazi wakati wowote kwa viongozi iwapo watanihitaji kuwapa ushirikiano kama hali yangu itakuwa nzuri kiafya.

ASHA APATA TIMU UTURUKI


MCHEZAJI Asha Mohamed wa Mburahati Queens na timu ya soka ya taifa ya wanawake, Twiga Stars hivi karibuni alisajiliwa na klabu ya Atasehir Belediyespor ya Uturuki kwa ajili ya kucheza soka ya kulipwa nchini humo. Asha amesajiliwa na timu hiyo baada ya kufuzu majaribiona vipimo vya afya. Pichani, Asha akiwa katika matukio tofauti ndani ya majengo ya klabu hiyo iliyopo mjini Istanbul.

Monday, January 24, 2011

OMOTOLA ATIMIZA AHADI YAKE












MCHEZA Filamu na mwanamuziki nyota wa Nigeria, Omotola Jalade hivi karibuni alitimiza ahadi ya kuwasaidia watoto yatima na wenye matatizo baada ya kutembelea nyumba ya Heart of Gold Hospices iliyopo Isolo, Lagos. Katika ziara yake hiyo ya siku mbili, Omotola alipata nafasi ya kucheza na watoto hao, kuelezwa matatizo yao na kupiga nao picha ya pamoja.


Wednesday, January 19, 2011

OMOTOLA JALADE NA WANAWE!

HUWEZI kuamini! Mwigizaji nyota wa Nigeria, Omotola Jalade (katikati) akiwa na watoto wake wanne pamoja na mwigizaji mwenzake nyota wa nchi hiyo, Genevieve Nnaji (wa pili kushoto) wakati wa sherehe za kutoa tuzo za MAMA'S zilizofanyika hivi karibuni nchini humo.

Msimbazi wamnasa Mcameroon


KLABU ya Simba imefanikiwa kukinasa kifaa kipya kutoka Cameroon, ambacho itakitumia katika mashindano ya soka ya klabu bingwa Afrika yanayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.
Habari kutoka ndani ya Simba zimemtaja mchezaji huyo kuwa ni Cosmas Ekeh, anayecheza nafasi ya kiungo na ushambuliaji kutoka klabu ya Metro Security, inayocheza ligi daraja la kwanza nchini humo.
Kwa mujibu wa habari hizo, Ekeh alitua nchini mwishoni mwa wiki iliyopita na kupewa mkataba mnono, lakini uongozi wa Simba umekataa kuuweka hadharani.
Akizungumzia ujio wa mchezaji huyo, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri alisema amefurahi kupata mchezaji mwenye sifa zinazokubalika ndani na nje ya uwanja.
Phiri alisema kwa kipindi alichokaa na mchezaji huyo, amebaini kuwa, kiwango chake kipo juu na anaweza kuisaidia timu yake katika michuano hiyo.
Kocha huyo kutoka Zambia alisema, iwapo Ekeh atafanya vizuri katika michuano hiyo, huenda akasajiliwa na Simba katika msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Ekeh anatarajiwa kuanza kuonyesha cheche zake leo wakati Simba itakapomenyana na Atletico Paranaense ya Brazil katika mechi ya kirafiki ya kimataifa, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Naye Ekeh alisema amekuja nchini kucheza soka na kuisaidia Simba ili iweze kufanya vizuri katika mashindano hayo makubwa ya ngazi ya klabu barani Afrika.
Ekeh alisema tayari ameshatia saini mkataba wa kuichezea timu hiyo, lakini hakuwa tayari kuuweka wazi kwa madai kuwa, hiyo ni siri yake na uongozi wa klabu.
Simba inatarajiwa kukata utepe wa michuano ya Afrika kwa kumenyana na Elam ya Comoro. Iwapo itashinda, itakutana na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika raundi ya kwanza.

Yanga ubabe mtupu



HAKUNA kinachoeleweka! Ndivyo unavyoweza kuuelezea mgogoro uliozuka sasa kati ya uongozi wa klabu ya Yanga na viongozi wa matawi ya klabu hiyo ya mjini Dar es Salaam.
Wakati viongozi wa matawi wameitisha mkutano leo kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayoihusu Yanga, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Llyod Nchunga ametangaza kutoutambua na kuupiga marufuku.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari juzi, Nchunga alisema ameupiga marufuku mkutano huo kwa sababu unaweza kuchafua hali ya hewa ndani ya Yanga.
Lakini Mwenyekiti wa matawi ya klabu hiyo, Mohamed Msumi aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, lazima mkutano huo ufanyike kama ulivyopangwa.
Nchunga alisema mkutano huo hauna madhara kwa uongozi kwa vile lengo lao ni kujadili matatizo yaliyopo ndani ya Yanga na kuyatafutia ufumbuzi.
Alizitaja ajenda zinazotarajiwa kujadiliwa kwenye mkutano huo kuwa ni hali ya kutokuelewana kati ya Nchunga na makamu wake, Davis Mosha pamoja na uteuzi wa Mbunge wa Temekem, Abbas Mtemvu (CCM), kuwa mdhamini wa klabu.
Ajenda nyingine ni matumizi ya sh. milioni 200 zilizotolewa na mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Yusuf Manji kwa ajili ya usajili wa wachezaji Davis Mwape na Juma Sefu wakati wa usajili wa dirisha dogo.
Msumi alisema mkutano huo ni haki ya wanachama na hauna lengo la kuupinga uongozi uliopo madarakani, hivyo Nchunga hapaswi kuuhofia kwa sababu lengo lao ni kuweka mambo sawa.
Mgogoro kati ya uongozi na wanachama ulizuka siku chache baada ya Yanga kuchapwa mabao 2-0 na Simba katika mechi ya fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, iliyochezwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Mapema jana asubuhi, mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Yusuf Manji aliwaita wazee wa klabu hiyo ofisini kwake barabara ya Nyerere, Dar es Salaam kwa ajili ya kuteta nao ili kuweka mambo sawa.
Haikuweza kufahamika mara moja kilichojadiliwa katika kikao hicho, lakini kuna habari kuwa, Manji amewasihi wazee hao watulize mzuka ili kuepuka kuiingiza klabu kwenye mgogoro mpya.

SIMBA HAOOO BRAZIL

MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Simba wamepewa ahadi ya kukwea pipa kwenda Brazil iwapo wataishinda Atletico Paranaense ya nchini humo.
Simba na Atletico, inayoundwa na wachezaji wengi wadogo kiumri, zinatarajiwa kumenyana leo katika mechi ya kirafiki ya kimataifa, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwenyeji wa Wabrazil hao, Fatma Al-Kharoos aliwaambia waandishi wa habari juzi kuwa, ataipeleka Simba nchini Brazil kwa ajili ya mechi ya marudiano kati ya timu hizo mbili iwapo tu itashinda leo.
Katika mechi yake ya kwanza iliyochezwa juzi kwenye uwanja huo, Atletico iliichapa Yanga mabao 3-2.
“Napenda kuiona Simba ikiifunga na Atletico na iwapo itafanya hivyo, nitaipeleka Brazil kwa ajili ya mchezo wa marudiano,”alisema Rahma.
Mwanamama huyo pia amewapa ofa mashabiki wa soka wa Dar es Salaam kushuhudia mechi hiyo bure ili waweze kupata uhondo kutoka kwa timu hizo mbili.
Katika mechi hiyo, Simba itamkosa mshambuliaji wake nyota, Emmanuel Okwi, ambaye amerejea kwao Uganda kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya mguu.
Okwi aliumia wakati Simba ilipomenyana na Ocean View katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi, iliyochezwa wiki iliyopita mjini Zanzibar.
Hata hivyo, Simba huenda ikawachezesha wachezaji Juma Kaseja, Juma Nyoso, Kelvin Yondani, Jabir Azizi na Abdalla Shiboli waliokuwa na kikosi cha Taifa Stars nchini Misri. Timu hiyo ilirejea nchini juzi usiku.
Mchezo huo ni wa pili wa kimataifa kwa Simba ndani ya wiki moja. Mwishoni mwa wiki iliyopita, Simba ilichapwa mabao 2-1 na ZESCO ya Zambia katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru.

HUENDI POPOTE!


Mchezaji Omega Seme (kushoto) wa Yanga akimtoka Bruno Costa (chini) wa Atletico ya Brazil wakati timu hizo zilipomenyana juzi katika mechi ya kirafiki ya kimaraifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Atletico ilishinda mabao 3-2. (Picha na Bashir Nkoromo).
KIPA Juma Kaseja (kulia) na mchezaji mwenzake wa timu ya taifa, Taifa Stars wakiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam juzi usiku wakitokea Misri, ambako timu hiyo ilikwenda kushiriki katika michuano ya Kombe la Mto Nile. (Picha na Khamis Hamad).

MZEE YUSUF ALAZWA HOSPITALI


Mwimbaji nyota wa nyimbo za muziki wa taarab na Mkurugenzi wa kikundi cha Jahazi, Mzee Yusuf amelazwa kwenye hospitali ya Dokta Bakhe iliyopo Kibaha mkoani Pwani baada ya kufanyiwa operesheni ya mguu. Habari kutoka kwa watu wa karibu na mwimbaji huyo zimeeleza kuwa, Mzee alilazwa kwenye hospitali hiyo tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini hali yake inaendelea vizuri. Pichani, Mzee akijuliwa hali na mkewe, Leila Rashid, ambaye pia ni mwimbaji wa kikundi hicho. (Picha kwa hisani ya tovuti ya Dida).

Papic: Nipo tayari kwa lolote


KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Yanga, Kostadin Papic amesema yupo tayari kwa lolote, kufuatia timu hiyo kufanya vibaya katika michuano mbalimbali.
Akizungumza mjini Dar es Salaam juzi, Papic alisema kufanya vibaya kwa Yanga katika mechi mbalimbali kumechangiwa na sababu zilizo nje ya uwezo wake.
Kauli hiyo ya Papic ilikuja saa chache baada ya Yanga kuchapwa mabao 3-2 na Atletico Paranaense ya Brazil katika mechi ya kirafiki ya kimataifa, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Alizitaja baadhi ya sababu hizo kuwa ni pamoja na mwingiliano wa mashindano mbalimbali, unaotokana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokuwa na kalenda ya uhakika.
"Hebu fikiri, Yanga inashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho,tumepanga programu zetu, mara yanazuka mashindano ya Kombe la Mto Nile, wachezaji wangu muhimu wanakwenda Misri,"alisema kocha huyo kutoka Serbia.
Alisema mwingiliano huo wa mashindano umesababisha programu yake ya mazoezi kuvurugika na mambo mengi kwenda kinyume na alivyoyapanga.
Papic pia aliushutumu uongozi wa Yanga kwa kushindwa kukamilisha uhamisho wa mchezaji Kenneth Asamoah, kitendo ambacho alidai kuwa kimemkera na kumvurugia mipango yake.
Mserbia huyo alikwenda mbali zaidi kwa kusema, baadhi ya wakati amekuwa akishindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na wachezaji wengi pamoja na yeye binafsi kushindwa kulipwa haki zao kwa wakati mwafaka.
Kocha huyo, aliyelipwa mshahara wake wa mwezi uliopita mwanzoni mwa wiki hii alisema, kasoro hizo zimechangia kuwafanya wachezaji wacheze chini ya kiwango na timu kuvurunda.
“kutokana na sababu hizo na zinginezo, nipo tayari kwa lolote kutokana na timu kufanya vibaya,”alisema.
Papic pia alisema hana taarifa kuhusu kuteuliwa kwa Fred Felix Minziro kuwa msaidizi wake, lakini alisisitiza, yupo tayari kufanyanaye kazi pamoja.

G-Nako aamua kutoka kivyake


MSANII George Nako wa kundi la Twenty Eleven lenye maskani yake mkoani Arusha, ameamua kurekodi singo yake inayojulikana kwa jina la ‘Oooh’.
George, ambaye pia anajulikana kwa majina ya G-Nako, The Finest of AR na Mr. Swagnificent amerekodi singo hiyo kwa kushirikiana na msanii Jade.
Msanii huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto amesema, singo yake hiyo ni utambulisho wa albamu yake ya kwanza inayotarajiwa kutoka hivi karibuni ikiwa na nyimbo nane.
"Nakuja na albamu yangu itakayokuwa na nyimbo nane, tano nimekwishazitengeneza na nyingine tatu ziko jikoni zinapikwa, zikiwa tayari naingiza albamu sokoni," alisema.
Hata hivyo, G-Nako alisema maandalizi ya albamu yake hiyo hayawezi kuathiri kazi za kundi lake, ambalo linatesa vikali kimuziki ndani ya jiji la A-Town.
"Nipo kazini kotekote. Nikiwa na kundi langu nakamua mpaka mwisho na nikiwa solo, mwendo ni huo huo. Mashabiki wangu na wa kundi wanalijua hilo," alisema G-Nako.
Msanii huyo alisema, iwapo atatokea mtu na kumuuliza anunue albamu ipi, kati ya ile ya kwake na ya kundi iwapo zitaingizwa sokoni pamoja, alisema: " Ukimpenda G-Nako, utawapenda Nako2Nako Soldiers, hivyo hapo itabidi tu ununue albamu zote ili ufaidi," alisema.
Kwa mujibu wa G-Nako, amerekodi kibao cha Oooh katika studio za Sababisha Records chini ya watayarishaji muziki, B. Hits na Panchi Latino.

Genevieve akana kuwa mja mzito

LAGOS, Nigeria
MWIGIZAJI nyota wa kike wa Nigeria, Genevieve Nnaji amekanusha madai kuwa, ana uja uzito wa mwanamuziki nguli wan chi hiyo, D’Banji.
Genevieve, ambaye amecheza filamu zaidi ya 200 za Kinigeria, alisema wiki hii kuwa, japokuwa uvumi huo ni taarifa za heri, lakini hauna ukweli wowote.
“Sitaki kumvunjia mtu heshima kwa kusema uongo, lakini ukweli ni kwamba hakuna cha kujibu kuhusu hilo,”alisema mwigizaji huyo mwenye mvuto.
Alikuwa akijibu swali aliloulizwa na mwandishi mmoja wa gazeti la The Sun la Nigeria iwapo ni kweli ana uja uzito wa mwanamuziki huyo.
“Nimesikia uzushi mwingi kuhusu mimi, lakini angalau safari hii ni habari nzuri, japokuwa hazina ukweli,”alisema.
Hata hivyo, Genevieve alikiri kuwa ni kweli ana uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki huyo machachari wa Afrika Magharibi.
Alisisitiza kuwa, iwapo habari hizo ni za kweli, hilo litabainika kadri miezi inavyosonga mbele kwa sababu mimba huwa haijifichi.

Aki, Ukwa sasa kutengeneza filamu zao


LAGOS, Nigeria
BAADA ya kutamba kwa miaka mingi katika fani ya uigizaji filamu, Osita Iheme (Aki) na Chinedu Ikedieze (Ukwa) wameamua kutayarisha filamu zao wenyewe.
Aki na Ukwa walielezea mikakati yao hiyo wiki hii katika mahojiano maalum na mtandao wa Nigeria Films.
Mbali na kutengeneza filamu zao wenyewe, waigizaji hao wafupi na wenye vichekesho vya kuvunja mbavu, pia walikanusha madai kuwa hawaelewani na wana mpango wa kutengana.
Aki alisema si kweli kwamba wameamua kila mmoja kufanyakazi kivyake ndio sababu wameamua kushirikiana na kuandaa filamu zao wenyewe.
Kwa mujibu wa Aki, hawana haraka katika kuandaa filamu zao, lakini wanatarajia kuanza mpango huo mwaka huu. Alisema wataandaa filamu hizo kupitia kampuni yao ya APEN- (Aki and Pawpaw Entertainment Nigeria).
Naye Ukwa alisisitiza kuwa, bado wapo pamoja na anaamini vitu vyao vitaanza kuonekana hivi karibuni. Alisema kilichopangwa na Mungu hakuna anayeweza kukipangua.
“Sisi tumeunganishwa na Mungu,”alisema Ukwa na kudokeza kuwa, wanavyo pia vipaji vya uimbaji, lakini hakutaka kuzungumzia zaidi suala hilo.
Waliwataja waigizaji wenzao wanaowavutia na kufurahia kufanyanao kazi pamoja kuwa ni Rita Dominic, Nkem Owoh, John Okafor, Ini Edo, Sam Loco-Efe na Genevieve Nnaji.

Jordan atengana rasmi na mumewe


LONDON, England
BAADA ya kuwepo kwa wiki kadhaa za tetesi na uvumi, hatimaye mwigizaji na mwanamitindo nyota wa Uingereza, Katie Price ‘Jordan’ ametangaza kutengana na mumewe Alex Reid.
Jordan (32) ametangaza kutengana na mumewe miezi 11 tangu walipofunga ndoa na kuishi kama mume na mke.
Mama huyo wa watoto watatu alitoa taarifa hiyo juzi jioni baada ya Reid (35) kupigwa picha akionekana anahama kutoka nyumbani kwao eneo la Surrey na kurejea kwa wazazi wake eneo la Hampshire.
Jordan alikiri kuwa, ndoa yao ilikumbwa na matatizo mengi katika miezi michache iliyopita, ikiwa ni pamoja na msuguano kati yake na Reid kuhusu kuzaa naye mtoto. Kutengana kwa wanandoa hao kumekuja wiki chache baada ya kuvinjari kwa siri kwenye kisiwa kimoja kilichopo bahari ya Hindi kwa ajili ya mapumziko.
Mara baada ya kurejea England, Jordan aliwaeleza wasomaji wa mtandao wake kuwa, taarifa kuhusu ndoa yake kukumbwa na matatizo zilikuwa za kweli.
Katika taarifa yake, Jordan alimshutumu mumewe kwa kuwa na mabadiliko makubwa tofauti na alivyokuwa wakati alipojitosa kimapenzi kwake.
Jordan na Reid walianza kuwa na uhusiano wa kimapenzi Julai, 2009, ikiwa ni wiki nane baada ya mwanamama huyo kutengana na mumewe wa kwanza, Peter Andre. Wakati huo, Reid alikuwa mmoja wa waigizaji nyota wa filamu.
Kwa mujibu wa Jordan, walipanga kutoa taarifa ya pamoja kuhusu kutengana kwao mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini alilazimika kusubiri baada ya kushawishiwa na mumewe, aliyetaka apewe muda wa kufikiria.
Lakini baada ya Reid kupigwa picha akiwa anamfundisha mtoto wa Jordan kupigana kwenye gym, mwanamama huyo aliamua kubadili mawazo.
Jordan amemshutumu Reid kwa kuvitumia vyombo vya habari kupata umaarufu kwa kumpiga picha kadhaa akiwa na mtoto wake Junior na pia kuchapisha habari kuhusu ndoa yao.
Alisema Reid anafahamu wazi kwamba hakuwa akitaka habari zinazohusu watoto wake zichapishwe hadharani kwa vile wanaweza kuathirika kisaikolojia.
Kwa upande wake, Reid alisema amekuwa akimuunga mkono Jordan katika uamuzi wake wa kuwaepusha wanawe na mapaparazi, lakini alishangaa kuona picha yake akiwa na Jordan imeuzwa kwenye chombo kimoja cha habari.
Alisisitiza kuwa, bado ataendelea kuvaa pete ya harusi kati yake na Jordan na pia kuipigania ndoa yake. Wanandoa hao walikutana kwa mara ya kwanza kwenye sherehe ya mwanamuziki Michelle Heaton kutimiza miaka 30 iliyofanyika Julai 19, 2009 kabla ya kufunga ndoa mwaka uliofuata.

Friday, January 14, 2011

Ndlovu kuishtaki Yanga CAF

BEKI wa zamani wa Yanga, Wisdom Ndlovu amesema atawasilisha malalamiko yake kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ili kuishinikiza klabu hiyo imlipe haki zake.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Malawi jana, Ndlovu alisema hakubaliani na uamuzi wa Kamati ya Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF ya kuishinikiza Yanga imlipe haki zake mchezaji Ally Msigwa pekee.
Ndlovu, Msigwa, John Njoroge pamoja na kipa Steven Marashi ni miongoni mwa wachezaji wanne waliowasilisha malalamiko yao kwa kamati hiyo wakiitaka Yanga iwalipe haki zao baada ya kukatisha mikataba yao.
Hata hivyo, TFF imeitaka Yanga imlipe Msigwa sh. milioni saba, ikiwa ni malipo ya miezi 36 yaliyokuwa yamebaki kwenye mkataba wake, lakini imetupilia mbali malalamiko ya wachezaji wengine watatu kwa madai kuwa walishindwa kuhudhuria vikao mara mbili.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema juzi kuwa, Ndlovu, Njoroge na Marashi suala lao limeondolewa kwenye kamati hiyo kwa sababu hiyo.
Kufuatia uamuzi wa kamati hiyo, TFF imeizuia Yanga kusajili mchezaji yoyote mpya au kuuza mchezaji msimu wa 2011/2012 hadi itakapomlipa Msigwa haki zake.
“Mimi kwa sasa nipo Malawi, lakini nasikitika kusema kwamba sikuwahi kuitwa kujieleza na kamati hiyo, hivyo nitakuja Tanzania kufuatilia haki zangu,”alisema Ndlovu.
Alisema iwapo Yanga itaendelea kumpiga chenga, atawasilisha malalamiko yake CAF ili imsaidie kupata haki zake.
Naye kipa Marashi amesema hakuwahi kuitwa na kamati hiyo kwa ajili ya kujieleza na kuwasilisha vielelezo kuhusu malalamiko yake dhidi ya Yanga.
Marashi alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, hakuna kiongozi yeyote wa TFF aliyewahi kuwasiliana naye kuhusu suala hilo, hivyo hakubaliani na uamuzi wa kuyatupa malalamiko yake.
“Hadi naondoka Tanzania kwenda Botswana, sikuwahi kupigiwa simu na kiongozi yeyote wa TFF kwa ajili ya kuitwa kwenye kikao,”alisema kipa huyo. Kikao hicho kilifanyika Desemba 30 mwaka jana na Januari 7 mwaka huu.

Babi atema cheche Vietnam


KIUNGO wa zamani wa klabu ya Yanga, anayecheza soka ya kulipwa klabu ya Dong An ya Vietnam, Abdi Kassim 'Babi' amesema ameanza mazoezi rasmi na kikosi hicho kwa ajili ya kujiandaa na mechi za ligi.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Vietnam jana, Kassim alisema amepokewa vizuri na uongozi pamoja na wachezaji wa klabu hiyo na matarajio yake ni kucheza soka ya kiwango cha juu kwa lengo la kupeperusha vyema bendera ya Tanzania kimataifa.
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes alisema anaamini katika wa soka, hakuna linaloshindikana iwapo mchezaji ataamua kufuata misingi ya uchezaji na kuongeza kuwa, amekwenda Vietnam kucheza mpira akiwa na matarajio ya kwenda Ulaya.
Kassim amewataka wachezaji wanaocheza soka ya ridhaa nchini, kuongeza kasi na kuweka malengo ya kucheza soka nje ya nchi. Lakini ameonya kuwa, jitihada hizo zitafanikiwa iwapo wadau wa soka, vyama vya soka na viongozi wa klabu watakuwa mstari wa mbele kutaka kuinua kiwango cha mchezo huo.
"Kwa ufupi nimeshaanza kuzoea maisha mapya. Kama unavyofahamu, nipo ugenini. Napenda kutoa changamoto kwa wachezaji wenzangu niliowaacha nyumbani, kucheza kwa bidii na malengo yao yawe kucheza soka ya kulipwa nje," alisema mchezaji huyo.
Kiungo huyo anayetumia zaidi mguu wa kushoto, alisema anashukuru ameondoka akiwa na baraka za viongozi wa klabu ya Yanga, ambayo aliitumikia kwa moyo wote tangu alipojiunga nayo akitokea Mtibwa Sugar. Kassim alikuwa nahodha msaidizi wa Yanga akimsaidia Fredi Mbuna.
Klabu ya Don An, ilimsajili Kassim kwa kitita cha dola 40,000 (sh. milioni 60). Mbali ya kuitumikia Zanzibar, kiungo huyo alikuwa mchezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars. Alijiunga na Mtibwa mwaka 2003 kabla ya kutua Yanga msimu wa 2006.

Poulsen yaleyale ya Maximo


Na Mwandishi Maalum, Cairo
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Jan Poulsen amewapoza Watanzania kwa kuwataka wasikate tamaa licha ya timu yao kushindwa kufuzu kucheza nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mto Nile.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Poulsen alisema Taifa Stars ni timu nzuri, isipokuwa wachezaji wake wanakosa umakini katika baadhi ya mechi.
Kauli hiyo ya Poulsen imekuja baada ya Taifa Stars kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Uganda katika mechi yake ya mwisho iliyochezwa juzi kwenye uwanja wa Polisi mjini hapa.
Kufuatia kipigo hicho, Taifa Stars sasa inawania nafasi ya tano kwa kutegemea matokeo ya mechi ya mwisho kati ya Burundi na Misri itakayochezwa kesho.
Poulsen alisema kimchezo, Taifa Stars inacheza vizuri, lakini makosa madogo ya kiufundi ndiyo, ambayo yamekuwa yakiigharimu katika baadhi ya mechi na kusisitiza kuwa, ipo haja ya kulifanyiakazi tatizo hilo.
"Nimesikitishwa sana kushindwa kufuzu kucheza nusu fainali, lakini ndiyo soka ilivyo na jirani zetu Uganda na Kenya wao wameingia hatua hiyo, huo ndiyo mchezo ulivyo," alisea kocha huyo raia wa Denmark.
Kocha huyo alisema tatizo kubwa la Taifa Stars lipo kwenye safu yake ya ulinzi kujichanganya na ile ya ushambuliaji kushindwa kuzitumia vyema nafasi inazopata kufunga mabao.
Amewataka watanzania wasikatishwe tamaa na matokeo hayo kwa vile bado yupo kwenye mikakati ya kujenga kikosi imara kwa ajili ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 2012.
Nahodha wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa alisema wamefedheheshwa na matokeo hayo, lakini katika soka kuna kushinda, kufungwa ama kutoka sare.
Katika mechi yake ya kwanza, Taifa Stars ilinyukwa mabao 5-1 na wenyeji Misri kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 na Burundi. Stars inatarajiwa kumenyana na Sudan kesho katika mechi ya kutafuta mshindi wa tano.
Mechi za nusu fainali pia zinatarajiwa kuchezwa kesho, ambapo Misri itamenyana na Kenya wakati Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo itavaana na Uganda.

Thursday, January 13, 2011

JENNIFER, Nyota inayochipukia katika filamu


KWA kumtazama tu, mtoto Hanifa Daudi anaonekana kuwa mpole, mwenye aibu na asiye na makeke. Ni mtoto anayependa kuwa karibu na watoto wenzake, wakicheza na kufanya hili na lile. Hivyo ndivyo ilivyo kawaida kwa watoto.
Lakini hali hubadilika anapokuwa akitekeleza majukumu yake ya uigizaji wa filamu, akiigiza matukio mbalimbali yanayohusu filamu husika. Huwa akiwasilisha vyema uhusika wake kiasi cha kuifanya filamu yoyote anayoigiza iwe na mvuto wa aina yake.
Hivyo ndivyo ilivyo katika filamu za ‘This is it’ na ‘Uncle JJ’ zilizotungwa, kutayarishwa na kuongozwa na mwigizaji nyota nchini, Steven Kanumba ambaye ndiye aliyevumbua kipaji cha Hanifa. Ni mwigizaji chipukizi mwenye kipaji cha aina yake.
Kipaji alichonacho katika tasnia hiyo ndicho kilichomwezesha Hanifa, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Jennifer, kuibuka na tuzo ya mwigizaji bora kupitia filamu ya ‘This is it’ iliyotolewa na Min Zanzibar International Film Festival (MIN-ZIFF) mwishoni mwa mwaka jana.
Katika filamu ya ‘This is it’, Jennifer ameigiza kama mtoto mlozi au mshirikina. Filamu hiyo pia ilishinda tuzo ya filamu bora na kupata nafasi ya kuingia katika shindano la Panafrican Film and Television Festival (FESPACO) litakalofanyika baadaye mwaka huu mjini Ouagadougou- Burkina Faso.
Kufuatia kushinda tuzo hiyo, Kampuni ya Steps Entertainment Co Ltd, ambayo inajihusisha na kutengeneza na kusambaza filamu nchini, nayo iliamua kumzawadia Jennifer tuzo maalumu ya kumpongeza katika hafla iliyofanyika hivi karibuni mjini Dar es Salaam.
Akizungumzia ushindi wa Jennifer katika tuzo hiyo, Kanumba alisema binafsi anampongeza kwa hatua aliyofikia akiwa bado na umri mdogo na kwamba anajivunia mafanikio yake hayo.
Kanumba alisema alivumbua kipaji cha Jennifer mwanzoni mwa mwaka 2010 kupitia kampuni yake baada ya kuendesha zoezi la kusaka watoto wenye vipaji vya uigizaji filamu, ambao hawakuwahi kuonekana kwenye luninga.
“Nilifanikiwa kuwapata watoto zaidi ya 40, ambao niliwafundisha na kuwachuja mpaka akapatikana Jennifer na Patrick, ambao chini ya uangalizi wa wazazi wao, niliingia nao makubaliano ya kutocheza filamu yoyote nje ya kampuni yangu,”alisema Kanumba.
“Pia nilihakikisha maendeleo yao shuleni yanapanda na tulikubaliana kwamba, mtoto atakayeshika namba tano kushuka chini, namuondoa kwenye kampuni yangu. Niliwapa changamoto ya kushika nafasi ya kwanza hadi ya nne na nashukuru kwamba wametimiza matakwa yangu,”aliongeza.
“Kwa mihula miwili sasa, Jennifer anaongoza kwa kushika namba moja na hivi karibuni kabla ya kwenda naye Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, alishika nafasi ya pili darasani wakati Patrick amekuwa akishika nafasi ya tatu, ambayo si mbaya,” alisema Kanumba. Jennifer ni mtoto wa Daudi Kibavu na mama yake ni Rose Mogella. Ni mwanafunzi wa shule ya msingi ya Upanga mjini Dar es Salaam, umri wake ni miaka 11 na mwaka huu ameingia darasa la sita.
Binti huyo mwenye sura yenye mvuto hakushinikizwa na mtu yeyote kujitosa kwenye fani hiyo. Amekuwa akiipenda na mara nyingi alikuwa akimsumbua mama yake, akimtaka ampatie nafasi hiyo kwenye kituo chochote cha televisheni.
Ndoto za Jennifer zilianza kutimia baada ya anti yake, Maya Mrisho kumpeleka kwa Kanumba kwa ajili ya majaribio na hatimaye akafanikiwa kupata nafasi ya kucheza filamu zake mbili. Wakati huo Kanumba alikuwa ametoa tangazo la kutafuta watoto 40 wenye vipaji kwa ajili ya kuwafanyia usaili.
Jennifer anaamini kuwa, alipata nafasi hiyo kwa sababu ana uwezo mkubwa wa uigizaji ndio sababu aliweza kushika vyema mafunzo waliyopewa na Kanumba.
Binti huyo anasema alipopewa nafasi ya kuigiza kama mtoto mshirikina, hakuogopa kwa sababu anafahamu huo ni uigizaji tu, na yeye si mshirikina.
Anamshukuru Kanumba kuwa ndiye aliyemsaidia na kumwezesha kuubeba uhalisia wa nafasi aliyotakiwa kuigiza kutokana na mafunzo aliyompatia.
Jennifer anaamini kuwa, yeye ni mtoto wa kawaida popote anapokuwa, japokuwa wapo baadhi ya watoto wenzake, ambao huwa wakimshangaa.
“Kila ninapopita mitaani, watoto wengi hupenda kuniita kwa jina la Jennifer! Jennifer!” Anasema binti huyo, ambaye nyota yake imeanza kung’ara vyema katika fani ya filamu.
Kwa sasa, Jennifer amekuwa mwigizaji maarufu nchini kutokana na kucheza filamu hizo mbili, lakini anaamini hilo haliwezi kumwathiri katika masomo yake. Amesisitiza kuwa, maendeleo yake kimasomo hadi sasa ni mazuri.
Ndoto za Jennifer si kuishia kwenye fani ya uigizaji pekee kwani angependa kujihusisha na taaluma nyingine, ambayo bado hawezi kuiweka wazi kwa sasa.
Jennifer anapenda watoto wenzake wote nao wapate nafasi ya kusoma kwa ajili ya maendeleo na maisha yao ya baadaye na kusisitiza kuwa, asiyependa kwenda shule, hawezi kuwa rafiki yake.
Pia amewataka wazazi kutowakataza watoto wao kuonyesha vipaji vyao kwa vile vinaweza kuwanufaisha katika maisha yao ya baadaye badala ya kutegemea elimu ya darasani pekee.
Kwa upande wake, mama wa Jennifer amekiri kuwa, kipaji cha uigizaji amezaliwa nacho na kuongeza kuwa, kimechangiwa na baba yake mzazi, ambaye naye ni mpenzi wa fani hiyo.
Rose haamini kuona binti yake huyo kwa sasa ni muigizaji bora chipukizi na ameweza kuibuka na tuzo ya ZIFF. Anasema kutoamini kwake huko ndiko kulikomfanya atokwe na machozi siku Jennifer alipopabidhiwa tuzo hiyo.
Mama huyo wa Jennifer anasema kama si mzazi mwenzake Daudi, huenda binti huyo asingekuwepo duniani hivi sasa kwa sababu alipata uja uzito wake akiwa shuleni na kutokana na woga na kufukuzwa nyumbani na wazazi wake, alitaka kuuharibu.
“Lakini tazama, leo hii mtoto wangu amekuwa mwigizaji maarufu na kushinda tuzo,”alisema Rose.
Kwa sasa, Rose na Daudi hawaishi pamoja, lakini wote wawili wanapenda kuwa karibu na binti yao huyo na wamepania kuhakikisha anapata mafanikio kimaisha.

Mgogoro wa ZFA utaikosesha Zanzibar uanachama wa FIFA

MGOGORO wa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) wiki hii uliingia kwenye sura mpya baada ya kamati ya utendaji ya chama hicho kusema haiitambui kamati ya uchaguzi.
Kamati ya Utendaji ya ZFA ilitangaza kutoitambua kamati hiyo kwa madai kuwa, kuwepo kwake madarakani ni batili kwa sababu haikupewa baraka na chama hicho.
Uamuzi wa ZFA kutoitambua kamati hiyo ulikuja siku chache baada ya kutangaza kurudiwa kwa uchaguzi mkuu wa chama hicho, kufuatia baadhi ya wagombea kuwa na kasoro.
Baadhi ya kasoro hizo ni pamoja na madai kuwa, mgombea wa urais, Ali Ferej Tamin hakuwa na sifa kutokana na kushindwa kuwasilisha cheti cha elimu yake ya kidato cha nne. Ferej ndiye aliyeshinda wadhifa huo baada ya kuwabwaga wagombea wenzake watatu.
Hata hivyo, siku chache baadaye, Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Ali Suleiman Ali, maarufu kwa jina la Shihata alisema, kamati ya utendaji ya ZFA haina uwezo wa kutoitambua ama kuifuta kamati yake.
Shihata alisema, ili kamati hiyo ya utendaji ya ZFA isiitambue kamati yake, inapaswa kuwa na uongozi uliokamilika, akiwemo rais na makamu wawili wa rais kutoka Unguja na Pemba.
Kufuatia kuzuka kwa mgogoro huo, kamati ya uchaguzi imewateua Kombo Juma Hassan kuwa rais wa muda wa ZFA wakati Fadhil Ramadhani na Khamis Ameir Juma wameteuliwa kuwa makamu wawili wa rais kutoka Pemba na Unguja.
Pamoja na kuteuliwa kwa viongozi hao wa muda, Katibu Mtendaji wa ZFA, Mzee Zam Ali amesisitiza kuwa, uamuzi waliouchukua dhidi ya kamati ya uchaguzi ni sahihi na utabaki palepale.
Kwa mtazamo wangu, kilichojidhihirisha katika mzozo huu ni kutokuelewana kwa baadhi ya viongozi wa ZFA waliomaliza muda wao na wale wa kamati ya uchaguzi kutokana na baadhi yao kuweka mbele zaidi maslahi yao.
Hii ni kwa sababu haieleweki kwa nini ZFA iliwaruhusu wajumbe kutoka vyama shirikishi vilivyo chini yake kushiriki kwenye uchaguzi huo wakati uwepo wao madarakani ulikuwa batili.
Kadhalika haieleweki ni kwa nini kamati ya uchaguzi ilimruhusu Ferej ashiriki kwenye uchaguzi huo iwapo ni kweli kwamba hakuwasilisha cheti chake cha elimu ya sekondari kama taratibu zinavyotaka.
Uamuzi wa ZFA kutoitambua kamati ya uchaguzi pia ni wa kichekesho kwa sababu inakuwaje wanafikia uamuzi huo baada ya kamati hiyo kufuta matokeo ya uchaguzi na kutaka urudiwe upya?
Kutokana na hali ilivyo, nadhani ni vyema kwa vyombo vinavyosimamia michezo visiwani Zanzibar kuingilia kati mgogoro huo ili suluhu iweze kupatikana na kuinusuru ZFA isisambaratike.
Uamuzi pekee unaoweza kukinusuru chama hicho ni kurudiwa kwa uchaguzi huo na kuhakikisha taratibu zote katika kuuendesha hadi kupatikana kwa viongozi wapya zinaheshimiwa.
Haipendezi kuona kuwa, katika kipindi hiki ambacho Zanzibar inapigana kufa na kupona ili kupata uanachama wa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), ZFA imekumbwa na mgogoro mkubwa na haieleweki nini hatma yake.
Ni vyema Baraza la Michezo la Zanzibar (BMTZ) na wizara husika, kuitisha kikao kati ya pande husika ili kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo na kuondosha uwezekano wa FIFA kupuuza maombi ya visiwa hivyo kupatiwa uanachama.

Mnyama aitafuna Yanga

RAIS wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein akikabidhi kombe la ubingwa wa Michuano ya Mapinduzi kwa nahodha wa Simba, Nico Nyagawa baada ya timu hiyo kuwachapa watani wao wa jadi Yanga mabao 2-0 katika mechi ya fainali, iliyochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar. (Picha na Bashir Nkoromo-picha zingine uk.4)

Na Abood Mahmoud, Zanzibar

SIMBA jana ilitwaa kwa mara ya pili ubingwa wa michuano ya soka ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuwachapa watani wao wa jadi Yanga mabao 2-0 katika mechi ya fainali, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.
Mabao yaliyoiwezesha Simba kutoka uwanjani kifua mbele yalifungwa na Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Shija Mkina, moja katika kila kipindi, ikiwa ni mara ya pili kulinyakua kombe hilo baada ya mwaka 2008.
Mechi hiyo iliyoshuhudiwa na maelfu ya mashabiki, akiwemo Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ilikuwa ya kusherehekea miaka 46 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Simba na Yanga kumenyana kwenye uwanja huo katika kipindi cha miaka 19 iliyopita. Kwa mara ya mwisho zilikutana mwaka 1992 katika mechi ya fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati, ambapo Simba ilishinda kwa penalti 5-4.
Ushindi huo ulikuwa wa kulipiza kisasi kwa Simba, kufuatia kuchapwa bao 1-0 na Yanga katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa Oktoba 16 mwaka jana mjini Mwanza.
Kwa ushindi huo, Simba ilizawadiwa kitita cha sh. milioni tano wakati Yanga ilizawadiwa sh. milioni tatu. Timu zingine zilizoshiriki michuano hiyo ni Mtibwa Sugar, Azam, Zanzibar Ocean View, KMKM na Jamhuri.
Katika mechi hiyo, timu zote mbili zilicheza bila ya wachezaji wake kadhaa nyota waliopo kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars kinachoshiriki michuano ya Kombe la Nile, inayoendelea nchini Misri.
Simba iliwakosa kipa Juma Kaseja, mabeki Juma Nyoso na Kelvin Yondani pamoja na mshambuliaji Jabir Azizi wakati Yanga iliwakosa mabeki Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Nadir Haroub na kiungo Nurdin Bakari.
Pamoja na kuibuka na ushindi, timu zote mbili hazikucheza soka ya kuvutia na kufanya mashambulizi ya kupanga. Kila timu ilicheza mpira wa kubutua na pasi za kubahatisha.
Simba ingeweza kupata bao dakika ya 13 wakati Patrick Ochan alipopewa pasi na Mussa Hassan ‘Mgosi’ akiwa ndani ya mita 18, lakini shuti lake liliokolewa na kipa Yaw Berko wa Yanga.
Mgosi alipoteza nafasi nyingine nzuri ya kufunga bao dakika ya 35 baada ya kushindwa kuunganisha krosi ya beki Haruna Shamte, aliyepanda mbele kusaidia mashambulizi.
Mshambuliaji huyo aliyetemwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars alisahihisha makosa yake dakika ya 33 baada ya kuifungia Simba bao, kufuatia pasi maridhawa ya Ochan.
Kiungo Omega Seme aliyeingia dakika za mwisho za kipindi cha kwanza badala ya Razak Halfan nusura aifungie bao Yanga dakika ya 44 alipopiga mpira wa adhabu ndogo umbali wa mita 20, lakini shuti lake lilipanguliwa na kipa Ally Mustafa ‘Batrhez’. Simba ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Bao la pili la Simba lilifungwa na Shija Mkina, aliyeingia kipindi cha pili badala ya Hillary Echessa. Alifunga bao hilo baada ya kutanguliziwa pasi ndefu na Ochan.
Katika mechi hiyo, mwamuzi Ramadhani Mbega Kibo aliwaonyesha kadi za njano Ernesta Boakye, Juma Sefu na Salum Telela wa Yanga pamoja na Meshack Abel, Mohamed Banka na Haruna Shamte wa Simba.
Simba: Ally Mustapha, Haruna Shamte, Amir Maftah, Meshack Abel, Jerry Santo, Abdulrahim Humud, Mohamed Banka/Mbwana Samatta, Hillary Echessa/Shija Mkina, Mussa Hassan/Azizi Gila, Patrick Ochan na Nico Nyagawa.
Yanga: Yaw Berko, Salum Telela, Abuu Ubwa, Issack Boakye, Job Ibrahim, Ernest Boakye, Geofrey Bonny/Nsa Job, Juma Sefu/ Kigi Makasi, Razak Khalfan/Omega Seme, Idi Mbaga, Davis Mwape.