KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, October 31, 2011

22 waitwa Taifa Stars



KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen leo ametangaza kikosi cha wachezaji 22 kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Chad itakayochezwa Novemba 11 mwaka huu jijini N’Djamena.

Mchezaji aliyeitwa kwa mara ya kwanza ni kipa Mwandini Ally wa Azam huku pia akimjumuisha kwenye kikosi chake mshambuliaji wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes), Thomas Ulimwengu.

Kikosi kamili ni makipa Juma Kaseja (Simba) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris
(Azam), Juma Nyoso (Simba), Idrissa Rajab (Sofapaka, Kenya), Erasto Nyoni (Azam), Nadir Haroub (Yanga), Godfrey Taita (Yanga) na Juma Jabu (Simba).

Viungo ni Henry Joseph (Kongsvinger IL, Norway), Nurdin Bakari (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Abdi Kassim (DT Long An, Vietnam), Ramadhan Chombo (Azam) na Shomari Kapombe (Simba).

Washambuliaji katika kikosi hicho ni Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada), Mrisho Ngassa (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Dan Mrwanda (DT Long An, Vietnam), Athuman Machupa (Vasalund IF, Sweden), Hussein Javu (Mtibwa Sugar) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC).

Timu itaingia kambini Novemba 3 mwaka huu jijini Dar es Salaam, na inatarajiwa kuondoka nchini Novemba 9 mwaka huu kwenda N’Djamena kwa ajili ya mechi hiyo. Stars na Chad zitarudiana Novemba 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Salha aitangaza vema TZ katika Miss World

Mrembo wa Tanzania, Salha Israel (kushoto) akiwa na baadhi ya washiriki wenzake wa shindano

la kumsaka mrembo wa dunia, wakipita jukwaani na vazi la ufukweni. Shindano hilo limepangwa kufanyika wiki ijayo mjini London, Uingereza.

Miyeyusho azima ngebe za Matumla

Bondia Francis Miyeyusho akionyesha furaha ya hali ya juu baada ya kuvishwa mkanda wa ubongwa wa WBO na Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova baada ya kumdunda Mbwana Matumla kwa pointi katika pambano lao lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.


Salha wamooo

Mwakilishi wa Tanzania katika shindano la kumsaka mrembo wa dunia, Salha Israel akiwa katika vazi la ufukweni. Picha hii ni miongoni mwa picha tatu za mrembo huyo zilizomo kwenye mtandao wa Miss World.


Simba, Yanga zaingiza mil 337/-



Mechi namba 78 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Simba iliyochezwa Oktoba 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 337,537,000.

Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 53,366 ambapo kiingilio kilikuwa sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 kwa VIP A.

Baada ya kuondoa gharama za mchezo na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 51,488,694 na gharama za awali za mchezo sh. 27,405,250 kila timu ilipata sh. 77,592,916.

Mgawo mwingine ulikwenda kwa uwanja (sh. 25,864,305), TFF (sh. 25,864,305), Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu- FDF (sh. 12,932,152), gharama za mchezo (sh. 25,864,305), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam- DRFA (sh. 10,345,722) na Baraza la Michezo la Taifa- BMT (sh. 2,586,430).


TAIFA STARS YAPANGIWA MSUMBIJI CAN 2013

Tanzania (Taifa Stars) imepangwa kucheza na Msumbiji katika kinyang’anyiro cha kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwaka 2013 nchini Afrika Kusini.

Upangaji ratiba wa mechi hizo za mchujo ulifanywa juzi (Oktoba 28 mwaka huu) na kamati ndogo ya michuano hiyo mjini Malabo, Equatorial Guinea. Jumla ya nchi 47 ikiwemo mwenyeji Afrika Kusini ndizo zilizothibitisha kucheza michuano hiyo.

Nchi 16 zilizofuzu kucheza fainali za mwakani nchini Gabon na Equatorial Guinea zenyewe zimepitishwa moja kwa moja hadi raundi ya mwisho ya mchujo itakayoanza baada ya fainali za 2012.

Raundi ya kwanza ya awali itahusisha nchi nne ambazo kwenye ubora wa viwango ndizo ziko chini ili kupata mbili zitakazoingia raundi ya pili ya awali itakayokuwa na nchi 28. Nchi hizo ni Swaziland, Sao Tome, Lesotho na Shelisheli.

Stars imepangiwa kucheza na Msumbiji katika raundi hiyo ya pili ya awali. Tarehe za mechi hizo ambazo zitachezwa katika nusu ya kwanza ya mwaka 2012 zitatangazwa baadaye.

Mechi nyingine za raundi hiyo zitakuwa kati ya Ethiopia na Benin, Rwanda na Nigeria, Congo na Uganda, Burundi na Zimbabwe, Algeria na Gambia, Kenya na Togo, Sierra Leone na mshindi kati ya Sao Tome na Lesotho.

Nyingine ni Guinea Bissau na Cameroon, Chad na Malawi, mshindi kati ya Shelisheli na Swaziland dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Misri, Madagascar na Cape Verde na Liberia na Namibia.

Timu 14 zitakazopita hatua hiyo zitaungana na 16 zilizofuzu kwa ajili ya fainali za Gabon/Equatorial Guinea kucheza raundi ya mwisho kupata 15 zitakazoungana na wenyeji Afrika Kusini kwa ajili ya fainali za 2013. Raundi hiyo itachezwa kati ya Septemba na Oktoba mwakani.

Thursday, October 27, 2011

Airtel Tanzania na TLTC kupanda miti Tanga



Wa kwanza kushoto ni Afisa Mazingira wa Airtel Tanzania, Mkama Manyama akimkabidhi mfano wa hundi ya shilling million tatu Katibu Mkuu wa SHIMIWI, Ramadhani Sululu (wapili toka kulia) ikiwa ni udhamini wa Airtel kwenye michezo ya SHIMIWI, ambayo itafanyika mwaka huu mkoani Tanga. Wakishuhudia makabidhiano hayo (katikatu) ni Afisa Uhusiano wa Airtel , Jane Matinde na (kulia) ni Naibu Katibu wa SHIMIWI, Moshi Makuka.


Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kwa kushirikiana na Kampuni ya Tanzania Leaf Tobacco
Company (TLTC) leo zimetangaza dhamira yao katika kutunza mazingira kwa kuchangia na kushiriki zoezi la kupanda miti mkoani Tanga.

Tukio hili la kupanda miti litakafanyika mwanzoni mwa mwezi Novemba kama sehemu ya ufunguzi wa michezo ya SHIMIWI itakayofanyika kitaifa mwaka huu mkoani Tanga.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari Afisa Mazingira wa Airtel Tanzania Bwana Manyama Mkama alisema “Airtel Tanzania kwa kushirikiana na TLTC tutapanda miti zaidi ya elfu tatu katika shule ya sekondari ya ufundi Tanga na shule ya sekondari ya kilimo Galanosi ikiwa ni katika kuendeleza mchakato uliowezesha miti mengine zaidi ya elfu tatu kupandwa katika maeneo ya barabara ya Sahare, Shule ya Sekondari Kihere, Kombozi, Yusuf Makamba, pamoja na Shule ya Msingi Msamaweni na TLTC mwaka jana.

Pamoja na kupanda miti Airtel Tanzania tunadhamini mashindano haya na kutoa kiasi cha shilling milion tatu kama ikiwa ni udhamini wetu pia kufanikisha mashindano ya SHIMIWI.

Hii ni moja kati ya jitihada tulizonazo katika kutambua umuhimu wa mazingira na kuyatunza.

Airtel na TLTC tumejiunga na waandaaji wa mashindano ya SHIMIWI kukamilisha jitihada hizi baada ya kutathmini mchanganuo wao ulioainisha kupambana na changamoto mbalimbali zinazokumba jamii na nchi kwa ujumla zikiwemo kumomonyoka kwa udongo, kuongezeka kwa gesi ya ukaa inayopelekea kuongezeka kwa joto kwenye uso wa dunia na nyingine nyingi ambapo hupelekea nchi kuwa na uhaba wa chakula na maji.

Airtel Tanzania imekua ikichangia sekta mbalimbali ikiwemo elimu kwa kugawa vitabu mashuleni, kuinua michezo nchini, kuboresha mawasiliano hasa vijijini na katika mradi huu, imejikita kutunza mazingira kwa kupanda miti mkoani Tanga.

Ni imani yetu kuwa Airtel na TLTC tumechukua hatua sahihi kwa kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa kushirikiana na SHIMIWI mwaka huu kupanda miti mkoani
Tanga.

TLTC ni wadau washiriki katika mipango mbalimbali ya kutunza misitu Tanzania ikishirikiana na wazalishaji wa tumbaku katika mikoa yote. TLTC tumelenga katika kuwaelemisha na kutoa mafunzo kwa wakulima katika kupanda vitalu na kutengeneza mashamba ya miti, kwa vile miti ni sehemu ya uzalishaji wa tobacco TLT inashirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikiksha inaimarisha uzalishaji bora wa bei nafuu na uunguzaji yakinifu.

Hadi ifikapo mwaka 2020 TLTC inadhamiria kuwa imefikia kiwango kikubwa cha upandaji wa vitalu vitakavyo wasaidia wakulima wa tobacco kuacha kutegemea rasilimali ya misiti iliyopo sasa.

Platini ampiga dongo Beckham



PARIS, Ufaransa
RAIS wa Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA), Michel Platini ameitaka klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) kumsahau nahodha wa zamani wa England, David Beckham.
Nguli huyo wa zamani wa Ufaransa, alisema juzi kuwa, Beckham (36) hana kiwango bora kama zamani na amebaki jina, kauli ambayo huenda ikaibua mzozo kati yake na kiungo huyo wa Los Angeles Galaxy ya Marekani.
Kauli hiyo ya Platini imekuja baada ya kuwepo na taarifa kuwa, PSG inataka kumsajili winga huyo wakati wa usajili wa dirisha dogo Januari mwakani.
Platin alisema kitendo cha PSG kumsajili Beckham ni sawa na kupoteza muda au fedha.
"Beckham amekuja Paris kununua vitu, nampenda sana, lakini kwa sasa si mchezaji bora kama zamani," alisema Platini.
Alisema nguli huyo amekwenda Ufaransa kununua bidhaa na si kusajiliwa. Beckham, amepewa ofa ya kujiunga na klabu ya PSG kutoka kwa mkurugenzi wa ufundi, Leonardo aliyewahi kumfundisha AC Milan alipocheza kwa mkopo.
Mkataba wa mchezaji huyo unamalizika mwezi ujao na klabu kadhaa za Ulaya zimetuma maombi ya kumsajili. Klabu hizo ni Queens Park Rangers na Tottenham Hotspurs.

Simba haina imani na Mbaga


KLABU ya Simba imesema haina imani na mwamuzi Oden Mbaga wa Dar es Salaam, aliyepangwa kuchezesha mechi ya ligi kuu kati yao na Yanga.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, uongozi umetatizwa na uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kumteua Mbaga kuchezesha mechi hiyo.
Kamwaga alisema Mbaga ndiye aliyechezesha mechi ya mwisho ya ligi kuu kati ya timu hizo na kusababisha linusurike kuvunjika kutokana na uamuzi wake wa utata.
Alisema katika pambano hilo, Mbaga alikataa bao la wazi la kusawazisha la Simba lililofungwa na Mussa Hassan Mgosi na baadaye kulikubali, hali iliyosababisha vurugu kubwa.
“Udhaifu huu wa kimaamuzi ungeweza kusababisha maafa makubwa uwanjani. Ndio maana Simba imetatizwa na uamuzi wa TFF kumteua tena Mbaga kuchezesha mechi hiyo,”alisema Kamwaga.
Hata hivyo, Kamwaga alisema hawatasusia pambano hilo kwa namna yoyote, lakini wanapenda kuweka wazi msimamo wao kwamba, hawana imani na mwamuzi huyo.
Katika mechi hiyo, Mbaga atasaidiwa na Hamisi Chang'walu wa Dar es Salaam na John Kanyenye wa Mbeya. Kamisaa wa mchezo huo atakuwa Mohamed Nyange wa Dodoma.
Nayo Yanga imesema, hawana uwezo wa kupinga maamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumteua Mbaga kuchezesha mechi hiyo.
“Ni kweli tulikutana na kumjadili, lakini tumeona hatuna sababu ya kumpinga na tunapaswa kuheshimu maamuzi ya TFF maana hata tukimtaka mwamuzi mwingine, tukifungwa, hadithi itakuwa ni ileile,”alisema.

YANGA: Tutamlipa Timbe haki zake zote



KLABU ya Yanga imesema inatarajia kumalizana na kocha wake wa zamani, Sam Timbe kabla ya mechi yao dhidi ya Simba keshokutwa.
Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga, Mohamed Bhinda alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, ameshaandaa malipo yote kwa ajili ya kocha huyo.
“Mimi ndiye niliyekabidhiwa jukumu la kusimamia malipo ya Timbe na nimeshamkabidhi mhasibu, hivyo tunatarajia kumlipa madai yake ndani ya siku mbili,”alisema.
Bhinda alisema fedha atakazolipwa kocha huyo ni mishahara yake yote kwa miezi iliyobaki na malipo mengine kwa mujibu wa mkataba.
Hata hivyo, Bhinda hakuwa tayari kuweka wazi kuhusu malipo hayo kwa madai kuwa ni siri ya klabu na Timbe.
Yanga imeamua kukatisha mkataba na Timbe kwa madai ya timu kushuka kiwango na pia kutokuwa tayari kupokea maelekezo ya mabosi wake. Mkataba wa kocha huyo ilikuwa umalizike Mei mwakani.
Badala yake, klabu hiyo sasa imemrejesha kocha wake wa zamani, Kostadi Papic kutoka Serbia, ambaye alitimuliwa Februari mwaka huu.

Seagull kudhamini ligi kuu Z'bar kwa mil. 41/-


KAMPUNI ya boti ya Seagull imejitokeza kudhamini michuano ya soka ya ligi kuu ya Zanzibar.
Meneja Masoko wa kampuni hiyo, Rehema Yusuf aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa, Seagull itadhamini ligi hiyo kwa sh. milioni 41.5.
Rehema alisema, udhamini huo utakuwa ni wa msimu mmoja wa ligi, ambayo inatarajiwa kuanza Novemba Mosi mwaka huu.
Hata hivyo, Rehema alisema wanatarajia kuendelea kuidhamini ligi hiyo kwa kutegemea ushirikiano mzuri utakaojitokeza na Wazanzibari katika kuiunga mkono boti hiyo.
Kwa mujibu wa Rehema, katika udhamini huo, watagharamia usafiri wa ndani, vifaa vya michezo kwa timu shiriki na zawadi za bingwa na mshindi wa pili.
Alisema wameamua kudhamini ligi hiyo kutokana na kujali mchango mkubwa wanaoutoa Wazanzibari katika kuitumia boti hiyo.
Rehema alisema katika udhamini huo, sh. milioni 15 zitatumika kama zawadi kwa bingwa na mshindi wa pili. Alisema bingwa atapata sh. milioni 10 na mshindi wa pili sh. milioni tano.
Alisema sh. milioni saba zitatumika kwa ajili ya vifaa vya michezo wakati sh. milioni 18 zitatumika kwa ajili ya usafiri wa timu kwenda vituoni.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Msaidizi wa Chama Cha Soka Zanzibar (ZFA), Masoud Attai alisema kuwa ligi hiyo itaanza kwa mechi ya ufunguzi kati ya Jamhuri na Super Falcon. Alisema mchezo huo utachezwa Uwanja wa Gombani uliopo Pemba.
Attai alisema ligi hiyo itazishirikisha timu 12, tatu kutoka Pemba na tisa kutoka Unguja. Alisema ligi hiyo itazinduliwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdilahi Jihadi Hassan.

TEVEZ ALIMWA FAINI BIL. 1/-


LONDON, England
KLABU ya Manchester City ya England imemtoza faini ya pauni 800,000 (sh. bilioni 1.8) mchezaji wake Carlos Tevez na ipo tayari kukatisha mkataba wake wa miaka mitatu.
Man City imempa adhabu hiyo Tevez kwa madai ya kugoma kucheza mchezo wa ligi ya mabingwa wa Ulaya dhidi ya Bayern Munich ya Ujerumani, uliopigwa mwezi uliopita kwenye Uwanja wa Allianz Arena.
Kufuatia adhabu hiyo, Tevez amesema atamshitaki Kocha wa Man City, Roberto Mancini kwa kumchafulia jina kwa kumtuhumu kugoma kucheza mchezo huo.
Kabla ya adhabu hiyo, Tevez anayelipwa mshahara wa pauni 198,000 (sh. milioni 455) kwa wiki, alifungiwa kwa wiki mbili.
Wakati huo huo, Mancini amesema Mwenyekiti wa klabu hiyo, Khaldoon al Mubarak amechukizwa na kitendo cha utovu wa nidhamu kilichoonyeshwa na Tevez kwa madai kimewavunjia heshima mashabiki na Manchester City.
Licha ya mshambuliaji huyo wa Argentina kutakiwa na klabu za Ulaya na Brazil, Man City imesema haitamuuza kwa bei rahisi.
Tayari klabu za Corinthians, Boca Juniors na Juventus zimesema zipo tayari kumsajili katika usajili wa dirisha dogo Januari mwakani.
Rais wa Corinthians, Andres Sanchez amesema wana uhakika wa kumsajili na mashabiki wanamsubiri kwa hamu. Man City imesema mchezaji huyo anauzwa kwa pauni milioni 40 (sh. bilioni 92).

DK. SHENI: Serikali kujenga studio ya kisasa Zenj


RAIS wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Sheni amesema, serikali yake imetenga bajeti maalumu kwa ajili ya kujenga studio ya kisasa ya muziki visiwani humo.
Dk. Sheni amesema lengo la kujengwa kwa studio hiyo ni kuwawezesha wasanii wa muziki wa taarab kurekodi nyimbo za kiasili za muziki huo.
Kwa mujibu wa Dk. Sheni, studio hiyo pia itakuwa wazi kwa wasanii wa aina nyingine ya muziki katika visiwa hivyo.
Dk. Sheni alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa uzinduzi wa kikundi cha taarab cha Tausi Women Musical Club uliofanyika kwenye hoteli ya Bwawani mjini hapa.
"Tumepanga katika bajeti ijayo, kuweka fungu maalumu kwa ajili ya kujenga studio, ambayo itawasaidia wasanii wa muziki wa taarab na mingineyo kurekodi nyimbo zao kwa gharama nafuu,”alisema.
Dk. Sheni alisema lengo la serikali ni kuendelea kuuenzi utamaduni wa Zanzibar, hasa muziki wa asili wa taarab ili usipotee.
Alisema serikali yake inathamini mchango mkubwa wa muziki wa taarab asilia kwa vile ni utamaduni pekee unaosaidia kuvitangaza visiwa hivyo kimataifa.
Aliupongeza uongozi wa kikundi hicho cha Tausi kwa uamuzi waliochukua katika kuendeleza muziki wa taarab asilia na kuongeza kuwa, serikali ina kila sababu ya kukiunga mkono.
"Napenda kutoa shukurani za dhati na pongezi kwa uongozi wa Tausi kutokana na kusimama kwao kidete katika kuuendeleza utamaduni wa Zanzibar kupitia muziki wa taarab asilia,”alisema.
Dk. Sheni aliwapongeza wasanii wa Tausi, kikundi kinachoundwa na akina mama watupu kwamba na kuongeza kuwa, anaamini kitadumu kwa muda mrefu.
Mkurugenzi wa kikundi hicho, Maryam Hamdani alisema, kilianzishwa mwaka 2009, kikiwa na wasanii 22, wote wakiwa wanawake watupu.

JOTI: Mimi ni jembe kweli kweli






UNAPOWATAJA ama kuwazungumzia wasanii wa fani ya maigizo ama vichekesho hapa nchini, huwezi kukosa kutaja jina la Lucas Mhavile, maarufu zaidi kwa jina la Joti.
Ni msanii mwenye vipaji lukuki kwani ana uwezo wa kuigiza kiufasaha nafasi ya mzee, binti mdogo, mwanafunzi, mwanamke, mpemba na hata mlemavu.
Uwezo wake wa kuigiza nafasi hizo ni miongoni mwa mambo yaliyomfanya apate umaarufu na kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki kupitia kundi lake la Ze Komedi Orijino.
Awali, kundi hili lilikuwa likionyesha vitu vyake kupitia kituo cha televisheni cha East Africa, lakini baadaye kilihamishia maonyesho yake kupitia kituo cha TBC 1.
Joti amekuwa kivutio kwa watazamaji kutokana na ubunifu wake katika kuigiza nafasi, ambazo huwa akishiriki kuigiza.
Kwa mfano, siku za nyuma alikuwa akivutia watazamaji kutokana na kusoma taarifa ya habari ya Orijino Komedi akiigiza sauti ya Kipemba. Alisoma taarifa hiyo kwa kushirikiana na Masanja Mkandamizaji.
Msanii huyu mfupi lakini machachari, pia alijipatia sifa kemkem alipoigiza kipande cha ‘Aliyefulia’ na baadaye, Asha Ngedele. Joti pia ndiye msanii anayevutia zaidi anapoigiza kama babu au mtoto mtukutu.
Sifa yake nyingine ni kujibadilisha kuwa kama binti ama mwanamke pashkuna. Hana tofauti na yule msanii maarufu wa vichekesho barani Ulaya, marehemu Charle Chaplin.
Pengine kikubwa zaidi kilichompa umaarufu ni ule ubunifu wake wa staili ya utembeaji, ambayo imekuwa ikipendwa na vijana wengi. Hata waimbaji taarabu wameisifu na kuiimba staili hiyo kwenye nyimbo zao.
Akihojiwa na mtandao wa Filamucenter hivi karibuni, Joti alisema kwa kawaida, anapokuwa kazini, lazima ahakikishe kuwa, anafanyakazi kwa nguvu zote ili kazi yake iwe bora.
Joti alisema yeye ni tofauti na wasanii wengine, ambao hujisahau baada ya kuwa na mashabiki wengi na kubweteka kwa mafanikio waliyoyapata.
Kwa mujibu wa Joti, sera za kundi lake la Ze Komedi Orijino ni kazi na si kuchekesha pekee. Alisema kila wanapokuwa kazini, huheshimu kazi yao.
“Kuna watu hawapendi kuambiwa ukweli kuhusu wanachokifanya. Wao wanapenda sana sifa, ambazo si mali yao,”alisema.
“Unapokuwa Ze Komedi Orijino, ni kazi tu mtindo mmoja, ndiyo maana Joti unayekutana naye kitaani (mtaani) si Joti wa TBC 1,” aliongeza.
“Nikiwa kazini, nalima tu. Si unajua kuwa mimi ni Jembe, ukiniweka popote nalima. Babu, mtoto, nakamua. Si unajua maisha na hasa ukichukulia kwamba, sanaa hivi sasa inachemka,” alisema msanii huyo.
Joti alisema yeye na wasanii wenzake wa Ze Komedi Orijino wamekuwa wakitumia muda mwingi kujituma kwenye kazi sa sanaa ili kunufaika na si vinginevyo ndio sababu thamani yao ipo juu.
Kwa upande wake, Meneja Uzalishaji wa kundi hilo, Sekioni Davidi, maarufu kwa jina la Seki, alisema kundi lake limepata mafanikio makubwa kutokana na kutambua thamani ya sanaa.
Seki alisema ni kutokana na kutambua hilo, wamepanga viwango vya juu katika malipo yao kwenye maonyesho mbalimbali, ambayo huwa wakialikwa kuyafanya.
Mbali na kupata fedha kutokana na matangazo yanayorushwa kwenye kipindi chao cha Orijino Komedi, Seki alisema wamekuwa wakipata fedha nyingi kupitia maonyesho.
“Yeyote anayelihitaji kundi letu kwenye onyesho, lazima achukulie sanaa yetu kama kazi. Hatutaki mtu anayeichukulia sanaa kama zamani, tunataka mialiko michache, lakini yenye thamani kubwa kwetu,” aliongeza Seki.

'Sijivunii makalio yangu'



LAGOS, Nigeria
MWIGIZAJI filamu machachari wa Nigeria, Anita Joseph amesema si kweli kwamba, amekuwa akiyatumia makalio yake makubwa kama kishawishi cha kupata nafasi ya kucheza filamu nyingi.
“Mimi ni mwanamke mzuri na kila sehemu ya mwili wangu ina thamani kubwa. Kama nitapoteza mkono leo, hayo makalio yangu hayawezi kuwa na mvuto,”amesema Anita katika mahojiano na mtandao mmoja mjini hapa juzi.
Anita alisema pia kuwa, uamuzi wake wa kujitosa katika fani ya muziki haukulenga kupata mafanikio ya haraka.
Alisema biashara ya muziki sio sawa na sherehe ya kunywa chai na kuongeza kuwa, inachukua muda mrefu kwa mwanamuziki kupata mafanikio.
“Ninachokifanya ni kujitahidi kutoa kitu bora ili kuhakikisha, kila atakayetoa pesa na kutumia muda wake kununua albamu yangu, anafurahia kazi yangu,”alisema.
Anita, ambaye moja ya sifa zake ni kujazia kike, alisema kwa sasa anajiandaa kuibuka na singo zake mbili, zinazojulikana kwa majina ya ‘Yem something’ na ‘Money’.
Mwanadada huyo amekiri kuwa, katika siku za hivi karibuni amekuwa bize kutokana na kushiriki kucheza filamu zaidi ya saba kwa wakati mmoja.
Alizitaja baadhi ya filamu hizo kuwa ni Place scandal, Open and close, Under my bed, Million love, Festival of madness, Prince and Princess , The Kingdom is mine, I am the king naBest dancer.
Anita ameitaja filamu ya Titanic battle kuwa ndiyo iliyompa changamoto kubwa kwa vile alikaribia kupoteza maisha kutokana na nafasi aliyoicheza.
Alisema mara baada ya tukio hilo, alifikiria kujitoa kwenye fani hiyo, lakini alilazimika kufikiria upya uamuzi huo kabla ya kubadili mawazo.
Mcheza filamu huyo amesema, amekuwa akishiriki kucheza filamu zilizoandikwa vizuri kwa vile anakuwa na uhakika wa kutoa mchango wake kuzipendezesha.

OMONI: Sina matatizo na Genevieve


LAGOS, Nigeria
MSHINDI wa tuzo ya mwigizaji bora wa kike wa Nigeria wa mwaka jana, Omoni Oboli amekanusha madai kuwa, haelewani na mwigizaji mwenzake nyota, Genevieve Nnaji.
Omoni alisema mjini hapa wiki hii kuwa, hana matatizo na Genevieve na wamekuwa wakifanyakazi kwa ushirikiano mkubwa.
Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti hivi karibuni kuwa, waigizaji hao wawili wamejikuta wakiingia kwenye bifu kali baada ya Omoni kutangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo.
Wakati Omoni akitangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo, Genevieve alitajwa na shirika la habari la CCN la Marekani na mtangazaji Oprah Winfey kuwa mwanamke mwenye mvuto wa Nollywood.
“Nina urafiki mzuri na waigizaji wenzangu karibu wote. Sidhani kama nina tatizo na mwigizaji yeyote, awe wa kike au wa kiume,”alisema Omoni.
“Mimi ni rafiki wa kila mtu. Hata Biblia inasema, tunapaswa kupendana,”aliongeza mwanamama huyo, aliyetesa vilivyo katika filamu za The Figurine na Anchor Baby.
Omoni, ambaye hivi karibuni aliingia mkataba wa mamilioni ya naira kwa ajili ya kucheza filamu nchini Ukraine, alisema siri kubwa ya mafanikio yake ni kufanya kile anachokiamini.
Mwanamama huyo amesema, anafurahia mafanikio aliyoyapata katika filamu ya Anchor Baby, ambayo imepata tuzo nyingi ndani na nje ya nchi hiyo.
Omoni alisema, siku zote huwa hakatishwi tamaa kutokana na yale watu wanayoyasema juu yake wakati anatambua wazi kuwa, anachokifanya ni sahihi.
“Kama nina imani kwamba hivi ndivyo nitakavyopata mafanikio, nashikilia papo hapo. Hivi karibuni, mtayarishaji mmoja wa filamu Canada aliniita kwa ajili ya kucheza filamu yake, lakini nikamwambia nipo bize,”alisema.
“Ni kwa sababu hadithi ya filamu hiyo haikuwa nzuri na si aina ya filamu, ambayo napaswa kuifanya ili iweze kufanya vizuri sokoni,”aliongeza.
Omoni alisema, kwa kuwa filamu zake mbili zilizopita zimefanya vizuri sokoni, huku filamu ya Feathered Dream aliyocheza Ukraine ikisubiriwa kwa hamu kubwa, hawezi kushiriki kucheza filamu nyingine isiyokuwa na mvuto.

Watu wanapenda kuniita 'mtu wa totoz'-Van Vicker


LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu Van Vicker kwa sasa si mgeni tena katika fani hiyo nchini Nigeria. Ni mzaliwa wa Ghana, lakini amejipatia sifa kubwa kwa kucheza filamu za Kinigeria.
Mbali ya kuwa mwigizaji nyota, Van Vicker amejaliwa kuwa na sura nzuri na umbo lenye mvuto, kiasi kwamba mioyo ya wanawake wengi hufa kwake.
Akihojiwa na mtandao mmoja nchini Nigeria hivi karibuni, Van Vicker alisema licha ya mafanikio aliyofikia katika fani hiyo, changamoto kubwa kwake ni kukosekana kwa ushindani nchini Ghana.
Van Vicker alisema wapo wacheza filamu wengi nchini Ghana, lakini idadi yao haiwezi kulinganishwa na ile iliyopo Nigeria.
“Tunahitaji kuwa na waigizaji wengi zaidi, ndio sababu najisikia vibaya,”alisema mwigizaji huyo, anayepapatiwa na akinadada wengi kutokana na uzuri wa sura yake.
Van Vicker alisema alianza kucheza filamu za Kinigeria baada ya kushirikishwa katika filamu moja iliyochezwa kwa ushirikiano kati ya waigizaji wan chi hizo mbili.
Kwa mujibu wa mcheza filamu huyo, alijitosa katika fani hiyo miaka sita iliyopita baada ya mtayarishaji mmoja wa filamu nchini Ghana kuvutiwa na mwonekano wake. Awali, alikuwa mtangazaji wa radio na televisheni.
“Sidhani iwapo mwonekano wangu ndio ulioniwezesha nipate nafasi ya kucheza filamu. Walikuwa wakihitaji mtu makini na mwenye kujiamini. Binafsi ninajiamini na Mungu amenijalia kuwa na sura nziri,”alisema.
Van Vicker alisema si kweli kwamba kufanana kwake na Ramsey Noah ndiko kulikochangia kumfanya awe maarufu. Alisema yeye na Ramsey ni waigizaji wenye mwonekano na mambo tofauti.
Licha ya kupendwa na wanawake wengi, Van Vicker alisema anampenda na kumheshimu mke wake, ambaye walifunga ndoa miaka minane iliyopita.
Mcheza filamu huyo alisema, alifunga ndoa na mkewe wakati akiwa na umri wa miaka 26 na kuongeza kuwa, alifanya hivyo kwa sababu wakati ulikuwa umewadia na alimpata mwanamke anayependeka.
Van Vcker alikiri kuwa, Nigeria imepata mafanikio makubwa katika fani ya filamu, ikilinganishwa na Ghana, kwa sababu ilianza mapema zaidi. Alisema ana hakika tofauti hiyo itapungua hivi karibuni.
Alisema haelewi ni kwa nini watayarishaji wengi wa filamu nchini Nigeria, hupenda kumpa nafasi kwenye filamu za mapenzi. Alisema sababu hiyo ndiyo iliyomfanya aamue kuandaa filamu yake, atakayocheza nafasi tofauti.
Baadhi ya filamu za Ghana alizoshiriki kucheza ni pamoja na Divine love, Darkness for sorrow na Beyonce Mummy wakati zile za Kinigeria ni Woman’s Hour, Total Love, ‘One More Kiss na Opposite Attraction.

Simba yapania kumiliki TV na redio


Mkakati ni kuwa na wanachama milioni moja

Yatamba falsafa yake ni kuwa kama Barcelona

Na Ezekiel Kamwaga

MPAKA wakati huu ninapoandika makala hii, Simba inaongoza ligi kuu ya Tanzania Bara ikiwa na pointi 27 baada ya kucheza mechi 11. Pia inaongoza kwa kufunga mabao 18 na ni timu pekee iliyofungwa mabao machache.
Simba pia ina wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa. Tofauti ya mabao yake ya kufunga na kufungwa ni 14 na ina idadi nzuri ya wachezaji waliofunga mabao kwenye mechi za ligi.
Kwa kawaida, timu inayochukua ubingwa ni ile ambayo haitegemei mtu mmoja kufunga. Unahitaji kuwa na wachezaji takribani watatu wanaopachika mabao ili uwe na uhakika wa kutwaa ubingwa.
Simba inao wachezaji wanne katika orodha ya wafungaji kumi wanaoongoza katika ligi kuu. Kuna Emmanuel Okwi, Patrick Mafisango, Felix Sunzu na Gervais Kago.
Haina tofauti na Barcelona ya Hispania, ambayo baada ya mechi nane za La Liga, inao wachezaji wanne katika orodha ya wafungaji wanaoongoza nchini humo; Lionel Messi, Cesc Fabregas, David Villa na Xavi Alonso.
Simba pia kwa sasa ina kikosi bora zaidi cha vijana wa chini ya miaka 20 katika timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu. Humo ndipo wachezaji kama Frank ‘Nteze John’ Sekule, Abdallah Seseme, Hassan Khatib, Ramadhan Salum na Ramadhani Singano (Messi) wanapopikwa.
Vijana hawa wanatengenezwa na gwiji wa zamani wa Simba, Selemani ‘Veron’ Matola, akishirikiana na Amri ‘Stam’ Said. Lakini pia kuna kikosi cha vijana wa chini ya miaka 17 na kile cha chini ya miaka 14 kinachofundishwa na Maka Malwisi.
Hakuna wasiwasi kuwa, Simba ndiyo timu pekee hapa nchini yenye timu zisizo za ubabaishaji za vijana. Hii ina maana kuwa, katika kipindi kifupi kijacho, ‘Lunyasi’ itakuwa ikitengeneza wachezaji wake wenyewe kama ilivyo kwa Barcelona.
Klabu zote kubwa duniani hujitambulisha kwa falsafa fulani. Simba inajulikana kuwa falsafa yake ni mpira wa chini, wenye pasi na ufundi mkubwa. Ndiyo maana wengi wa mashabiki wa Simba hupenda pia soka ya Barcelona. Ni kwa sababu ya falsafa tu.
Katika mazoezi ya timu zetu za vijana, akina Matola na Maka husimamisha mpira wakati mchezaji anapobutua mpira mbele. Hiyo si falsafa ya Simba. Inacheza mpira na si kubutua. Vijana hawa wakiwa wakubwa, watajua wanachezea timu gani. Wanajengwa wangali vijana kuchezea Simba ikiwa ni pamoja na kuijua falsafa yake.
Kubwa kuliko yote, nje ya uwanja kuna umoja na mshikamano mkubwa baina ya viongozi na wanachama. Hakuna tena masuala ya mapinduzi, migogoro na rabsha, ambazo zilizoeleka miaka ya nyuma.
Amani na utulivu uliopo umewezesha timu kuendeshwa kisasa zaidi na pengine ni miongoni mwa klabu chache katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ambazo walau zinaendeshwa katika mfumo wa kisasa.
Mchakato wa ujenzi wa uwanja wa kisasa katika eneo la Bunju jijini Dar es Salaam umeanza. Simba itakuwa na uwanja wake yenyewe kwa ajili ya mechi na mazoezi.
Kama mipango yote itakwenda kama ilivyopangwa, Simba inaweza kuwa klabu ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kuwa na uwanja wake wenye uwezo wa kubeba watu takribani 30,000.
Uwanja huo utakuwa miongoni mwa vyanzo vikubwa vya mapato kwa klabu. La kufahamu ni kuwa, mchakato wa kujenga uwanja ni suala lenye kuhitaji subira ya hali ya juu.
Simba pia imeingia katika mkakati kabambe wa kuongeza idadi ya wanachama wake. Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, maelfu ya mashabiki wa klabu wamefikiwa katika juhudi za kutaka kuongeza wanachama.
Matawi mapya yamefunguliwa. Kupitia kauli mbiu ya mwaka huu ya Siku ya Simba (Simba Day) iliyosema; Simba ni Matawi, Simba ni Wanachama, idadi ya wanachama wapya imeongezeka na wengi wanazidi na kutaka kujiunga.
Klabu kuwa na wanachama wengi ni suala la siha. Klabu kama Real Madrid ya Hispania (nasikia ipo ya Mbezi kwa Musuguri) ina nguvu kubwa kwa sababu ya kuwa na wanachama wengi.
Ada ya mwaka kwa mwanachama mmoja wa Simba ni Sh. 12,000. Kama timu ikiwa na wanachama milioni moja tu ( Lunyasi ina wapenzi zaidi ya milioni 10), klabu ina uwezo wa kukusanya kiasi cha Sh. bilioni moja kwa mwezi. Hii maana yake ni Sh bilioni 12 kwa mwaka mmoja tu.
Fedha hizi ni mara kumi ya zile zinazotolewa na wadhamini wa Ligi Kuu ya Tanzania (Vodacom) kwa timu zote zinazoshiriki ligi hiyo kwa mwaka mzima.
Fedha hizo zinamaanisha kuwa, Simba itakuwa na uwezo wa kumaliza ujenzi wa uwanja wake kwa kasi, kusajili wachezaji wa kiwango cha juu, kuongeza thamani yake kwa wadhamini na kushindana katika hadhi ya kimataifa.
Ndiyo maana, ni jambo la kheri kuwa idadi ya wanachama inaongezeka kila kukicha. Chini ya uongozi wa Mwenyekiti, Ismail Aden Rage (Mb) na Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, suala la kuongeza idadi ya wanachama ni kipaumbele.
Si kitu ambacho wengi wanakifahamu, lakini Simba iko mbioni kuanzisha kituo chake cha televisheni (Simba TV). Katika muda si mrefu ujao, Simba itakuwa na kituo chake chenyewe cha runinga, gazeti na jarida. Tayari tovuti ya klabu imeanza, ingawa bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Iwapo mipango yote hiyo ya vyombo vya habari itakamilika kama ilivyopangwa, klabu itazidi kupiga hatua kubwa. Wapenzi, wanachama, wadhamini na wadau wengine watapata fursa ya kupata habari zote za klabu na kubadilishana taarifa kila wakati. Hili ni jambo muhimu sana katika maendeleo ya klabu.
Zaidi ya kuwa na vyanzo vya habari, vyombo hivi pia vinaweza kuwa vyanzo vizuri vya mapato. Hivyo mipango hii inamaanisha kuwa, wakati wapenzi wakiwa wanapata taarifa, klabu pia itakuwa inaongeza mapato yake.
Klabu ya Simba pia inafanyakazi kwa karibu na Kampuni ya Push Mobile. Kupitia ushirikiano huu, wapenzi takribani 34,000 wa Simba wanapata taarifa za kila siku za klabu kupitia simu zao za mkononi.
Simba imekuwa klabu ya kwanza Afrika Mashariki kuwa na utaratibu huu. Ni utaratibu, ambao unahakikisha wapenzi wake wanapata taarifa kabla ya wananchi wengine kuhusu klabu yao, lakini umesaidia pia kuongeza mapato ya klabu.
Changamoto ziko nyingi na kadri tuendavyo mbele, kuna changamoto zaidi zitakuja. Lakini jambo moja la msingi ni kwamba, Simba inaanza kwenda mbele kwa kasi sana. Na mwendo huo unahusisha masuala ya nje na ndani ya uwanja.
Siku moja, miaka mingi ijayo, watu watazungumzia kipindi hiki kuwa ndipo haswa Simba ilipoanza harakati za kufika pale itakapokuwa wakati huo.


Mwandishi wa makala hii ni Ofisa Habari wa klabu ya Simba na pia mwandishi wa habari.

SIMBA, YANGA NGOMA INOGILE

Kikosi cha Yanga

Kikosi cha Simba


Okwi, Boban, Sunzu wapania kupeleka kilio Jangwani

Tegete, Asamoah, Gumbo kukata ngebe za mnyama?

Papic, Basena watamba kuwapa raha mashabiki wao


MIAMBA ya soka nchini, Simba na Yanga inakutana kwa mara ya kwanza msimu huu keshokutwa Jumamosi katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa. Dar es Salaam.
Hii ni mara ya tatu kwa Simba na Yanga kukutana katika kipindi cha miezi minne iliyopita. Zilipokutana Julai 10 mwaka huu katika mechi ya fainali ya Kombe la Kagame, iliyochezwa kwenye uwanja huo, Simba ilipigwa mweleka wa bao 1-0.
Yanga ilipata bao hilo la pekee na la ushindi kupitia kwa mshambuliaji wake wa kimataifa kutoka Ghana, Kenneth Asamoah dakika ya 108. Mshindi ilibidi apatikane dakika za nyongeza baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa suluhu.
Asamoah alifunga bao hilo kwa kichwa, akiunganisha mpira wa krosi uliochongwa na kiungo wa zamani wa wapinzani wao hao, Rashid Gumbo aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Godfrey Taita aliyeumia.
Gumbo aliambaa na mpira wingi ya kushoto na kuwatoka mlinzi Nassor Said ‘Chollo’ na kumimina krosi ambayo ingeweza kuokolewa na mlinzi Kelvin Yondani, lakini katika harakati za kufanya hivyo, aliteleza na kuanguka na mpira kumkuta mfungaji, aliyekuwa nyuma yake na kugonga kichwa ambacho kilijaa wavuni na kumwacha kipa Juma Kaseja akiwa hana la kufanya.
Watani hao wa jadi wa soka nchini walikutana tena Agosti 12 mwaka huu katika mechi ya kuwania Ngao ya Hisani, maalumu kwa ajili ya ufunguzi wa ligi. Katika mechi hiyo, iliyopigwa tena kwenye uwanja huo, Simba ililipa kisasi baada ya kuichapa Yanga mabao 2-0.
Mabao yote mawili ya Simba yalipachikwa wavuni katika kipindi cha kwanza. Bao la kwanza lilifungwa dakika ya 16 na Haruna Moshi 'Boban' wakati la pili liliwekwa kimiani dakika ya 37 kwa njia ya penalti na Mzambia, Felix Sunzu.
Je, ni Simba au Yanga itakayotoka uwanjani na ushindi keshokutwa kwa kuchukua pointi zote tatu na kuwapa raha mashabiki wake?
Swali hilo ndilo linaloelekea kuviumiza vichwa vya mashabiki wa soka nchini, ambao mojawapo kati ya timu hizo ikifungwa, hutawaliwa na simanzi zito huku wale walioshinda wakisherehekea ushindi kwa mbwembwe za aina zote.
Tayari presha imeshaanza kuwa juu kwa viongozi, wanachama na mashabiki wa klabu hizo huku kukiwa na taarifa kwamba, Yanga ilipanga kwenda kuweka kambi nchini Msumbiji kwa ajili ya kujiandaa na pambano hilo, lakini baadaye ilifuta mpango huo na kuamua kwenda kuweka makazi Mwanza.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kambi hiyo ya Yanga imegharamiwa na mfadhili wao, Yussuf Manji, ambaye amekubali kurejea kuifadhili timu hiyo baada ya kuombwa kufanya hivyo na uongozi, chini ya Mwenyekiti, Lloyd Nchunga.
PAPIC AREJESHWA
Pia kuna habari kuwa, Yanga itacheza mechi hiyo ikiwa chini ya kocha wake wa zamani, Kostadin Papic, ambaye ameingia mkataba wa miaka miwili wa kuinoa timu hiyo baada ya Sam Timbe kutoka Uganda kumaliza mkataba wake.
Hata hivyo, uamuzi wa Yanga kumrejesha Papic umeonekana kuwakera wachezaji wa timu hiyo kwa madai kuwa, kocha huyo alikuwa akiwagawa wachezaji wake na pia alikula pesa za usajili za baadhi ya wachezaji.
Papic, ambaye ni raia wa Serbia, alijiunga na Yanga kwa mara ya kwanza Oktoba mwaka 2009, akirithi mikoba ya Mserbia mwenzake, Profesa Dusan Kondic. Papic alitua Yanga akitokea Hearts of Oak ya Ghana, ambako alitumuliwa kwa sababu ya matokeo mabaya.
Kocha huyo, aliyewahi kuzinoa timu za Orlando Pirates, Kaizer Chiefs, Martzburg United za Afrika Kusini, Enyimba, Kwara United na Lobi Stars za Nigeria, alitupiwa virago Februari mwaka huu na nafasi yake kuchukuliwa na Timbe.
Timbe alikaririwa juzi akisema kuwa, mkataba wake na Yanga unatarajiwa kumalizika Mei mwakani, hivyo anashangazwa na taarifa zinazoripotiwa kuwa, mkataba wake umemalizika. Alisema bado uongozi haujampa taarifa yoyote kuhusu kusitisha mkataba wake.
"Mimi sina tatizo la kukatisha mkataba wangu, cha msingi ni kwamba nataka wanilipe haki zangu zote,"alisema kocha huyo.
Timbe alileta heshima kubwa Yanga msimu uliopita baada ya kuiwezesha kutwaa ubingwa wa ligi kuu na ule wa Kombe la Kagame. Tatizo kubwa lililosababisha Timbe aondolewe ni madai kuwa, amekuwa akikataa kutekeleza ushauri wa mabosi wake.
Papic alikuwepo uwanjani, akiwa ameketi jukwaani wakati Yanga ilipocheza na JKT Oljorokwenye uwanja wa Chamazi. Wakati wa mechi hiyo, kocha huyo aliwaeleza waandishi wa habari kwamba, ameshafanya mazungumzo ya awali na uongozi wa Yanga ili ainoe kwa mkataba wa muda mfupi.
Mserbia huyo alijigamba kuwa, hana wasiwasi na Simba kwa vile anaifahamu vyema na ameahidi kuwapa raha mashabiki wa Yanga kwa madai kuwa, anayo dawa ya kuwafunga wapinzani wao.
Pamoja na majigambo yake hayo, Papic ameshaonja ladha ya vipigo viwili kutoka kwa Simba. Mara ya kwanza ilikuwa Oktoba 31, 2009 wakati Yanga ilipochapwa bao 1-0 na Simba. Bao hilo la pekee lilifungwa na Mussa Hassan 'Mgosi'.
Papic aliendelea kuonjeshwa ladha nyingine ya kipigo Aprili 18 mwaka jana wakati Yanga ilipochapwa mabao 4-3 na wapinzani wao hao, mabao ya Simba yakifungwa na Uhuru Selemani, Mgosi aliyefunga mawili na Hillary Echessa. Mabao ya Yanga yalifungwa na Athumani Iddi 'Chuji' na Jerry Tegete, aliyefunga mawili.
Kocha huyo aliweza kuiongoza Yanga kushinda dhidi ya Simba katika mechi ya kwanza ya ligi iliyochezwa Oktoba 16 mwaka jana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza. Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda bao 1-0, lililowekwa kimiani na Jerry Tegete dakika ya 70.
Papic pia aliiwezesha Yanga kuifunga Simba mabao 2-1 katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Tusker na baadaye kuwalaza watani wao hao kwa penalti 3-1 katika mechi ya kuwania Ngao ya Hisani msimu uliopita.
Kwa upande wa Simba, hali inaonekana kuwa shwari huku kocha wake, Moses Basena kutoka Uganda akijigamba kuwa, wataendeleza ubabe kwa watani wao hao. Basena anajivunia kikosi chake kwa madai kuwa, hivi sasa kimeanza kushika maelekezo yake.
Basena alisema timu yake ilikuwa ikiibuka na ushindi kiduchu katika mechi za awali za ligi hiyo kutokana na washambuliaji wake kuwa na papara kila wanapokaribia lango la timu pinzani. Alisema tayari ameshalirekebisha tatizo hilo na ndio sababu waliweza kushinda mechi za hivi karibuni kwa mabao mengi.
Hata hivyo, Basena alikiri kuwa kwa kawaida mechi kati ya Simba na Yanga huwa hazitabiriki, lakini kwa jinsi alivyowaona mahasimu wao katika siku za hivi karibuni, uhakika wa ushindi kwa timu yake ni mkubwa.
MSIMAMO WA LIGI
Timu hizo mbili zinaingia uwanjani huku Simba ikiwa inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi sit kati yake na Yanga, inayoshika nafasi ya tatu. Simba inazo pointi 27 baada ya kucheza mechi 11 wakati Yanga imeambulia pointi 21 kutokana na idadi hiyo ya michezo.
Simba ilianza ligi hiyo kwa kuichapa JKT Oljoro mabao 2-0 mjini Arusha, ikaichapa Coastal Union bao 1-0 mjini Tanga, iliilaza idadi hiyo ya bao Villa Squad mjini Dar es Salaam,ikatoka suluhu na Azam kabla ya kuichapa Polisi Dodoma bao 1-0 mjini Dar es Salaam.
Katika mechi zingine, Simba ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar mjini Bukoba, ikatoka sare ya mabao 3-3 na Toto African mjini Mwanza, iliichapa Mtibwa Sugar bao 1-0 mjini Dar es Salaam, iliicharaza African Lyon mabao 4-0, iliichapa Ruvu Shooting mabao 2-0 kabla ya kuifunga JKT Ruvu idadi hiyo ya mabao.
Watani wao wa jadi Yanga walianza ligi hiyo vibaya baada ya kuchapwa bao 1-0 na JKT Ruvu mjini Dar es Salaam, wakalazimishwa sare ya bao 1-1 na Moro United, walitoka suluhu na Mtibwa Sugar mjini Morogoro, walilazimishwa sare ya bao 1-1 na Ruvu Shooting kabla ya kuzinduka na kuichapa African Lyon mabao 2-1 mjini Dar es Salaam.
Katika mechi zingine, Yanga ilikwaa kisiki kwa Azam baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0, ikaibwaga Villa Squad mabao 3-2, ikaibamiza Coastal Union mabao 5-0, iliichapa Kagera Sugar bao 1-0, iliicharaza Toto African mabao 4-2 kabla ya kuichapa JKT Oljoro bao 1-0. Mechi zote hizo zilichezwa mjini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa takwimu, safu za ushambuliaji za Simba na Yanga zinaonekana kuwa na ukali unaolingana baada ya kila timu kufunga mabao 18 katika mechi 11. Hata hivyo, safu ya ulinzi ya Yanga imeruhusu nyavu zake kutikisika mara tisa wake ile ya Simba imeruhusu mabao manne.
Mshambuliaji Kenneth Asamoah ndiye anayeongoza kwa kuifungia Yanga mabao saba wakati Emmanuel Okwi wa Simba anaongoza kwa kuifungia timu yake mabao matano.
JINO KWA JINO
Vikosi vyote viwili vitashuka dimbani huku vikiwa havina majeruhi. Kocha Basena alisema anashukuru kwamba, wachezaji wake, Mwinyi Kazimoto na Machaku Salum, ambao walikuwa majeruhi, wamepona. Isipokuwa bado ana wasiwasi na hali za afya za mabeki Victor Costa na Amir Maftah.
Costa aliumia wakati akiwa kwenye mazoezi ya timu ya Taifa, Taifa Stars iliyokuwa ikijiandaa kwa pambano lake la mwisho la michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika dhidi ya Morocco wakati Maftah aliumia katika mechi ya ligi dhidi ya Kagera Sugar.
Katika mechi za hivi karibuni, Basena amekuwa akiwatumia zaidi Nassoro Cholo, Juma Jabu, Juma Nyosso na Obadia Mungusa katika safu ya ulinzi, wakiongozwa na kipa Juma Kaseja. Katika kiungo, amekuwa akiwachezesha zaidi Jerry Santo, Shomari Kapombe na washambuliaji ni Gervas Kago, Haruna Moshi, Felix Sunzu, Uhuru na Machaku.
Kwa upande wa Yanga, wachezaji wake Shadrack Nsajigwa, Nurdin Bakari, Stephano Mwasika, Davis Mwape na Idrisa Rashid, ambao nao walikuwa majeruhi, wameripotiwa kuwa fiti baada ya kupona.
Kupona kwa Mwasika kumeipa ahueni kubwa Yanga kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi ya beki wa kushoto huku akipanda mbele kusaidia mashambulizi. Nafasi yake ilikuwa ikizibwa na Oscar Joshua.
Kocha Timbe alikuwa akiwatumia zaidi kipa Yaw Berko, Godfrey Taita, Joshua, Bakari Mbegu na Nadir Haroub kucheza safu ya ulinzi huku viungo akiwachezesha Juma Seif, Rashid Gumbo na Haruna Niyozima. Safu ya ushambuliaji inaundwa na Tegete, Hamiza Kiiza, Asamoah na Pius Kisambale.
MSIMAMO WA LIGI KUU TANZANIA BARA
P W D L GF GA PTS

Simba SC 11 8 3 0 18 4 27 2

Young Africans 11 6 3 2 18 9 21 3

Azam 10 6 3 1 11 3 21 4

JKT Oljoro 11 5 4 2 9 6 19 5

Mtibwa Sugar 10 4 3 3 11 9 15 6

JKT Ruvu 11 3 6 2 13 12 15 11

African Lyon 11 3 3 5 8 15 12 7

Kagera Sugar 10 2 5 3 11 11 11 8

Ruvu Shooting 10 2 5 3 8 9 11 9

Toto African 10 2 4 4 12 14 10 10

Moro United 10 2 4 4 13 17 10 13

Coastal Union 11 3 1 7 11 17 10 12

Polisi Dodoma 11 1 5 5 10 14 8 14

Villa Squad 11 1 3 7 9 23 6

Wednesday, October 26, 2011

Mussa Kijoti afunika uzinduzi wa Five Stars

Mussa Kijoti

Mariam Mohamed

Mwamvita Shaibu


MWIMBAJI anayechipukia kwa kasi katika muziki wa taarab nchini, Mussa Ally 'Kijoti' ametamba kuwa, atahakikisha analiziba vyema pengo lililoachwa na marehemu kaka yake, Issa Kijoti.
Mussa alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa uzinduzi wa kundi la Five Stars Modern Taarab 'Watoto wa Bongo' uliofanyika kwenye ukumbi wa Travertine, Magomeni, Dar es Salaam.
Issa, ambaye alijizolea sifa kemkem kutokana na uimbaji wake wa kuvutia, alifariki dunia Machi 13 pamoja na wasanii wengine 13 wa kundi hilo katika ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Mikumi mkoani Morogoro.
Wasanii hao walifariki dunia baada ya basi dogo aina ya Toyota Coaster walilokuwa wakisafiria kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam, kulivaa lori lililokuwa limeegeshwa pembeni ya barabara na baadaye kupinduka.
Mussa, ambaye kwa sasa anaimba nyimbo zote zilizokuwa zikiimbwa na marehemu kaka yake, ameanza kugusa hisia za mashabiki wengi kutokana na uimbaji wake kushabihiana na marehemu kaka yake.
Mwimbaji huyo alionyesha cheche zake na kuwaacha hoi mashabiki baada ya kuimba kwa ukamilifu wimbo wa 'Wapambe msitujadili', uliompatia umaarufu mkubwa kaka yake.
Mussa alipanda jukwaani kwa mara ya kwanza katika uzinduzi wa albamu mpya ya ‘Mwenye hila habebeki’, uliokwenda sambamba na uzinduzi wa kundi hilo. Uzinduzi huo ulihudhuriwa na umati mkubwa wa mashabiki.
Akiwa amevaa suruali nyeupe, shati jeusi, koti jeupe na viatu vyeusi, Mussa alionekana lulu kutokana na uwezo mkubwa wa uimbaji aliouonyesha.
Kupanda jukwaani kwa mwimbaji huyo chipukizi kuliufanya ukumbi ulipuke mayowe ya kumshangilia huku baadhi ya mashabiki wakijimwaga stejini kucheza.
Akizungumza na Burudani wakati wa onyesho hilo, Mussa alisema lengo lake ni kuwa mwimbaji maarufu ndani na nje ya nchi na kusisitiza kuwa, hilo linawezekana.
Alisema akiwa katika kundi hilo, atahakikisha anakitumia kipaji chake ili kufikia malengo aliyojiwekea, ambayo ni kuwa mwimbaji nyota katika tasnia ya muziki wa taarab.
"Nitahakikisha ninatumia kipaji nilichojaaliwa na Mungu kufikia malengo yangu. Ninawaomba wapenzi na mashabiki wangu wazidi kuniunga mkono," alisema.
Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 19, aliyemaliza darasa la saba mwaka 2008 alisema, anaushukuru uongozi wa kundi hilo kwa kumpa ushirikiano mzuri na ameahidi kufanya mambo makubwa zaidi.
Mbali na Mussa, wasanii wengine waliong’ara wakati wa onyesho hilo ni mpiga gita maarufu, ambaye alijiunga na kundi hilo hivi karibuni, Shaban Mafloo, aliyeonekana kugusa hisia za mashabiki wengi kutokana na kulikung'uta kwa umahiri mkubwa.
Kutokana na umahiri wake huo, baadhi ya mashabiki walishindwa kujizuia na kuanza kumzunguka huku wakimshangilia na kumtunza pesa.
Waimbaji wengine waliotia ni Zena Mohammed, aliyeimba kibao cha ‘Watu na tabia zao’ kilichowafanya mashabiki kuviacha viti vyao kwa muda na kujitosa jukwaani kucheza.
Naye Mariam Mohamed, mshindi wa shindano la BSS mwaka jana, aliwateka mashabiki kwa kibao chake cha ‘Mwenye hila habebeki’ wakati Saidi Yussuf aling’ara kwa kibao chake cha ‘One mistake, one goal’ akishirikiana na Mwamvita Shaibu.
Mpiga kinanda wa kundi hilo, Ally J kama ilivyo kawaida yake, alifanikiwa kuwateka mashabiki kutokana na kuipapasa ala hiyo kwa ufundi wa hali ya juu.
Uzinduzi wa kundi hilo ulipambwa na bendi ya muziki wa dansi ya Mapacha Watutu, inayoundwa na wanamuziki Jose Mara, Khalid Chokoraa na Kalala Junior.

Thursday, October 20, 2011

Salha amuasili mtoto yatima Dar






MREMBO wa Tanzania wa mwaka 2011, Salha Israel ameamua kumuasili mtoto mchanga mwenye umri wa mwezi mmoja, aliyelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
Salha alitangaza uamuzi wake huo mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kuelezwa mazingira yaliyosababisha mtoto huyo alazwe kwenye hospitali hiyo.
Mrembo huyo wa Tanzania, alifanya ziara kwenye hospitali hiyo, akiwa amefuatana na waandaaji wa kipindi cha Njia Panda, kinachorushwa hewani na kituo cha Radio cha Clouds FM.
Mtoto huyo, ambaye Salha ameamua kumpa jina lake, alikutwa ametupwa vichakani na kuokotwa na wasamaria wema, ambao ndio waliomfikisha Muhimbili.
Salha aliwaeleza wauguzi wa hospitali hiyo kwamba, atahakikisha anamlea mtoto huyo katika maisha yake yote.Mtoto huyo yatima, amelazwa wodi namba 36, ambayo ni maalumu kwa watoto wachanga.
Mlimbwende huyo amesema, katika kipindi chote atakachokuwa akilitumikia taji lake, atajikita zaidi katika harakati za kutetea haki za watoto wachanga.
"Watoto hawa wamekuwa wakisahauliwa kwa kiasi kikubwa. Watu wanakumbuka kuwasaidia watoto kuanzia miaka mitano na kuendelea na kukimbilia kutoa vyandarua na vitu vingine, lakini ukweli ni kwamba kundi la watoto hawa limesahaulika mno, “alisema mrembo huyo.
Mbali na kumuasili mtoto huyo, Salha aliitumia ziara yake katika hospitali hiyo kutoa misaada mbalimbali kwa watoto waliolazwa kwenye wodi hiyo. Misaada iliyotolewa na mrembo huyo ni sabuni za kufulia, maji na mashuka.
“Huu ni mwanzo tu wa kampeni hii, nitakaporudi kwenye mashindano ya dunia, mimi pamoja na wadau wengine wa urembo, tutahakikisha tunafanya kampeni kubwa ya kuihamasisha na kuielimisha jamii katika suala zima la kuwasaidia watoto hawa, ambao baadhi yao hutelekezwa na wazazi wao kutokana na kuwa na matatizo mbalimbali wangali wachanga,” alisema.
Naye Mkuu wa Itifaki wa Kamati ya Miss Tanzania,Albert Makoye aliushukuru uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kuwapa sapoti ya kutosha katika kutekeleza mpango wa kuwasaidia watoto waliolazwa kwenye hospitali hiyo.
Makoye alisema watoto wanaotupwa na wazazi wao kutokana na matatizo mbalimbali, wanastahili kusaidiwa kwa vile wanazo haki zote za kuishi kama watoto wengine.
Wakati huo huo, Salha anatarajiwa kuondoka nchini leo kwenda London, Uingereza kwa ajili ya kushiriki katika fainali za kumsaka mrembo wa dunia. Shindano hilo limepangwa kufanyika Novemba 8 mwaka huu.
Salha aliagwa rasmi juzi na Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, Athumani Mfutakamba, ambaye alimtaka mrembo huyo kuyatumia mashindano hayo kutangaza vivutio vya nchi. Salha alikabidhiwa fedha taslim sh. milioni tisa kutoka kwa wafanyakazi wa wizara hiyo na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

ASLAY: Chipukizi anayetamba na kibao cha Nitakusemea




KWA umri, msanii Aslay Isihaka bado ni kijana mdogo. Ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Tandika, Dar es Salaam. Umri wake ni miaka 15.
Aslay ni mmoja wa watoto wanaolelewa katika kituo cha Mkubwa na Wanawe, kinachomilikiwa na Saidi Fela, mmiliki wa kikundi cha TMK Wanaume Family. Kituo hiki kipo maeneo ya Temeke-Mwembe Yanga, Dar es Salaam.
Fela ameanzisha kikundi hiki kwa lengo la kuibua na kuendeleza vipaji vya wasanii chipukizi. Amekusanya vijana wadogo kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, hasa Temeke na wengine kutoka mikoani.
Katika kituo hicho, mbali na kufundishwa muziki, watoto hao pia hufundishwa masomo mbalimbali ya darasani. Mwalimu wao wa muziki ni msanii, Mheshimiwa Temba.
Tangu alipojiunga na kituo hicho kwa ridhaa ya wazazi wake, Aslay amedhihirisha wazi kuwa muziki upo kwenye damu yake na ni kipaji alichozaliwa nacho.
Kibao chake cha ‘Nitakusemea’, ambacho amekirekodi chini ya usimamizi wa Fela, ni uthibitisho wa wazi kuwa, kijana huyu amejaliwa sauti murua, inayoweza kumshawishi na kumvuta mtu yeyote kuisikiliza.
Kwa sasa, kibao hicho kimekuwa kikitamba kwenye vituo mbalimbali vya radio na televisheni nchini. Pia kinapendwa sana na watoto wa umri wake na hata watu wazima, hasa kina mama.
Video ya wimbo huo imenakshiwa zaidi na msanii wa maigizo, maarufu kwa jina la Pembe, ambaye ameigiza kama baba yake Aslay. Lakini sauti halisi ya maneno yanayotamkwa na Pembe ni ya Fela.
Akihojiwa katika kipindi cha Jambo, kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha TBC 1 hivi karibuni, Aslay alikiri kuwa, kibao hicho kimemfanya awe maarufu.
“Kuna siku nilipokwenda shule, mwalimu wangu alinitizama kisha akaniuliza, ‘kumbe wewe unaweza kuimba’,” alisema Aslay.
“Lakini kwangu mimi, umaarufu huo unazidi kuniongezea hamasa ya kufanya vizuri zaidi. Watu wengi wananiunga mkono, hasa akina mama, ambao wimbo huo ni kama vile unawatetea.
“Baadhi ya akina mama wamesema nimeimba vizuri, lakini kwa wanaume, wanaona kama vile nimewaharibia. Baadhi yao wamekuwa wakinilaumu kwa kuimba wimbo huo,”aliongeza.
Kwa mujibu wa Aslay, anatarajia kurekodi albamu yake ya kwanza mwezi ujao na itakuwa na vibao 10. Alisema lengo lake ni kurekodi vibao vikali vitupu badala ya vile vya kujazia albamu.
Aliwataja baadhi ya wasanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya aliowashirikisha kurekodi nyimbo zake kuwa ni pamoja na Saidi Chege, Diamond, Mheshimiwa Temba, Zahir Ally Zorro na Linah.
Aslay alitamba kuwa, licha ya kuwepo wasanii wengi wazuri wa umri wake kama vile Dogo Janja na Young D, hawana uwezo wa kumfikia kimuziki.
“Hawa madogo wote ni watoto kwangu. Wao wanachana, mimi naimba,”alisema Aslay.
“Dogo Janja amekuwa akiongea sana kuhusu mimi, lakini bado sana, haniwezi,”aliongeza.
Hata hivyo, Aslay amekiri kuwa, bado ni mapema kwake kupata manufaa kutokana na muziki, lakini wazazi na ndugu zake wameyafurahia mafanikio yake.
Alisema anachokipata kwa sasa ni pesa ndogo ndogo kwa matumizi yake ya shule. Alisema huduma ya malazi na chakula anaipata katika kituo anachoishi.
Aslay anamzimia sana msanii mwenzake wa kituo hicho anayejulikana kwa jia la Dula, ambaye amemwelezea kuwa ni mkali wa kuimba na ana kipaji cha aina yake.
Msanii huyu pia ni shabiki mkubwa wa soka. Kwa timu za hapa nchini, anavutiwa sana na Simba na kwa timu za nje, anaishabikia zaidi Chelsea.
Lengo la Aslay ni kuwa mwanamuziki wa kimataifa. Anapenda kuwa maarufu duniani, kama ilivyokuwa kwa nyota wa pop nchini Marekani, marehemu Michael Jackson.

Mtanzania anayekipiga Chelsea, ruksa kuichezea Taifa Stars


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema, milango ipo wazi kwa mchezaji chipukizi, Adam Nditi, anayecheza soka ya kulipwa England, kuichezea timu ya Taifa, Taifa Stars.
Nditi ni mmoja wa wachezaji wanaounda timu ya vijana wa chini ya umri wa miaka 21 ya Chelsea na umahiri wake katika kuwazuia washambuliaji wa timu pinzani umempatia sifa lukuki.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, mwenye jukumu la kumwita mchezaji huyo ni Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen.
“Kwa taratibu zilivyo, mwenye jukumu la kuteua wachezaji wa Taifa Stars ni kocha,”alisema ofisa huyo wa TFF.
“Baada ya uteuzi, inachokifanya TFF ni kuhakikisha wachezaji walioteuliwa wanapatikana. Poulsen hajawahi kumteua Nditi,”aliongeza.
Kocha Mkuu mpya wa Chelsea, Villas-Boas hivi karibuni alimpandisha Nditi kutoka kwenye kikosi cha vijana wa chini ya miaka 18 kwenda cha vijana wa chini ya miaka 21.
Jina la mchezaji huyo limo kwenye orodha ya wachezaji wa timu hiyo ya Chelsea, iliyowasilishwa kwenye Chama cha Soka cha England.
Kupandishwa daraja kwa mchezaji huyo wa Kitanzania kunamaanisha kwamba, anaendelea vizuri katika klabu hiyo tajiri ya England.
Nditi alianza kucheza soka katika chuo cha kukuza vipaji cha klabu hiyo, ambapo amekuwa mchezaji wa kutumainiwa katika kikosi cha vijana wa chini ya miaka 18 kwa zaidi ya misimu mitatu.
Akiwa katika chuo hicho, Nditi alikuwa chini ya kocha Muingereza, Neil Bath, lakini baada ya kupandishwa, sasa atakuwa chini ya kocha mwingine, Muingereza Adrian Viveash.
Nditi alizaliwa Septemba 18, 1994 huko Kikwajuni, Zanzibar kabla ya kwenda Uingereza, ambako alijiunga na chuo cha soka cha Chelsea.
Hata hivyo, kumezuka wasiwasi iwapo Nditi anaweza kuichezea Taifa Stars baada ya kuwepo taarifa kwamba, tayari kijana huyo ameshapara uraia wa Uingereza.
Sheria zilizopo sasa hapa nchini haziruhusu Mtanzania kuwa na uraia wa nchi mbili. Marekebisho ya sheria hiyo bado yanaendelea kufanyika kwa lengo la kuruhusu watanzania kuwa na uraia wa nchi mbili.
Marekebisho hayo yamelenga kuwawezesha watanzania waliopo nje, kuwekeza hapa nchini kwa lengo la kukuza uchumi.
Nditi amejipatia umaarufu mkubwa kwa klabu ya Chelsea kutokana na kuimudu vyema nafasi ya beki wa kushoto na kiungo mshambuliaji. Alijiunga na Chelsea mwaka 2008.
Alianza kuichezea timu ya chuo cha soka cha Chelsea msimu wa 2010/11 katika mechi dhidi ya Tottenham. Akiwa kwenye kikosi hicho, alicheza zaidi nafasi ya beki wa kushoto.
Alifunga bao lake la kwanza Aprili mwaka 2011 wakati timu ya chuo hicho ya Chelsea ilipomenyana na Norwich.
Nditi pia alikuwemo kwenye kikosi cha vijana cha Chelsea kilichomenyana na Arsenal Januari 20 mwaka huu katika mechi ya Kombe la FA la vijana na kutoka sare ya bao 1-1. Mechi hiyo ilipigwa kwenye uwanja wa Stamford Bridge.
Majina yake halisi ni Adam Eric Richard Nditi.

NCHUNGA: Tutawekeana mipaka na Manji


SWALI: Tunaomba ufafanuzi kutoka kwako, je ni kweli mmemuomba mfadhili wa zamani wa Yanga, Yusuf Manji kurejea kuisaidia klabu yenu?
JIBU: Ni kweli tumefanya hivyo na tumewahi kuwa na mazungumzo naye kabla hajasafiri kwenda nje ya nchi kwa shughuli zake za biashara na sasa tayari amerejea na wakati wowote tutafanya naye kikao kingine.
Pamoja na ukweli wa jambo hilo, tumeangalia kwa kina sababu, ambazo awali zilimfanya ajiweke pembeni kuisaidia klabu yetu na timu kwa jumla.
Sio siri kwamba, klabu yetu kwa sasa ina hali mbaya sana, hivyo tumeona kuna umuhimu wa kumuomba mfadhili huyo arejee kuisaidia klabu kwa moyo wake wote.
SWALI: Binafsi unadhani ni sababu zipi zilizochangia kumfanya Manji ajiweke pembeni? Inawezekana ni lugha chafu kutoka kwa baadhi ya wanachama au kuna mambo mengine?
JIBU: Kwa kweli yapo mambo mengi, yakiwemo hayo uliyoyataja.Wapo baadhi ya wanachama walifikia hatua ya kutoa lugha chafu kwake wakati yeye ndiye anayetoa pesa zake wakati wanachama hao wamekuwa wakishindwa kuchangia hata shilingi mia tano kwa ajili ya maji ya kunywa ya wachezaji.
Ulifika wakati uongozi ukaona kwamba, ni vyema tumuombe Manji arejee kutusaidia kuiendesha Yanga kwa sababu klabu hii ni mali ya watanzania wengi, matajiri na masikini. Hao wanachama wachache wenye upeo mdogo wa kuelewa mambo, tutawadhibiti, hatuwezi kuwaacha watuyumbishe.
Vilevile tupo mbioni kufanya mambo mengi muhimu ili kuhakikisha wanachama wakorofi hawapati nafasi ya kufanya ama kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu kwa watu, ambao wamekuwa wakijitolea pesa zao kuisaidia Yanga. Tunataka kuona Yanga ikipata mafanikio.
Hebu fikiria, Manji alishafanya mazungumzo na baadhi ya wafadhili wa ndani na nje ya nchi wakiwemo Wajapan kwa ajili ya kuwekeza Yanga. Lakini baada ya kujiengua kwa sababu ya kashfa za hawa wanachama, mpango huo ulikufa.
Hatupendi kuona hili likitokea tena. Tutajipanga vizuri kushirikiana naye ili tuweze kupata watu watakaoisaidia Yanga na kuiwezesha kuwa klabu ya kimataifa.
SWALI: Moja ya malalamiko yaliyokuwepo huko nyuma ni kwamba, Manji alikuwa akiingilia madaraka ya uongozi. Je, mna mpango wowote wa kuweka mipaka ya utendaji kati ya uongozi na mfadhili huyo endapo atakubali kuisaidia tena klabu yenu?
JIBU: Kwa kweli jambo hilo tumeliangalia kwa umakini mkubwa, ndio maana kabla ya kuingia naye mkataba mpya wa kuisaidia klabu yetu, itabidi akutane na kamati ya utendaji ya Yanga.
Hapo tutaweza kumpa nafasi na kumueleza kazi zake ndani ya klabu na mipaka yake na sisi viongozi tutafahamishana mipaka kati yetu na mfadhili huyo.
Hili jambo litasaidia sana kuondosha mkanganyiko wa kiutendaji na kujenga Yanga imara na yenye umoja badala ya kuendelea kuwepo utengano.
Unajua mwakani tunaiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa, hivyo tunahitaji utulivu ili tuweze kuifanya Yanga ifanye vizuri katika michuano ya klabu bingwa Afrika.
Nina imani Manji ataweza kutoa mchango mkubwa kuhakikisha ndoto yetu inatimia bila ya hofu yoyote, ikiwemo kutuwezesha kwenda nje ya nchi kucheza michezo kadhaa ya kirafiki na kuwapa uzoefu zaidi wachezaji wetu.
SWALI: Vipi kuhusu mipango yenu ya kutaka kujitegemea zaidi kwa sababu Manji ni binadamu, anaweza kuwepo au asiwepo, sasa mmepanga kufanya nini?
JIBU: Tumeanza kujipanga kuandaa hafla ya chakula cha usiku kwa ajili ya kuichangia klabu. Tayari tumemwandia barua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ili awe mgeni rasmi katika hafla hiyo. Tunasubiri kujibiwa na Ikulu. Baada ya majibu hayo, ndipo tutapanga tarehe ya kuandaa chakula hicho. Nina hakika tutaweza kuchangiwa pesa nyingi tu.
Kwa hesabu za haraka haraka, tunahitaji karibu shilingi bilioni sita ili tuweze kukamilisha programu zetu za ujenzi wa uwanja, jengo la Mafia na mambo mengine.
SWALI: Unapenda kuwaeleza nini wanachama na wapenzi wa klabu ya Yanga?
JIBU: Kwanza kabisa nawaomba manachama na wapenzi wa Yanga tuwe kitu kimoja ili tuweze kushirikiana na Manji na watu wengine wenye nia ya kutaka kuisaidia klabu yetu. Tusiwape nafasi watu wenye nia ya kutaka kutuvuruga.
Ni vyema wale wote wenye kuitakia mabaya Yanga katika kipindi hiki, wakae pembeni, waache uongozi na wanachama wenye nia ya kuiendeleza Yanga wafanye kazi zao, hatutaki kuona wanatuchanganya, tuna mambo mengi ya kufanya.

Mapacha wa Mariah Carey hadharani


NEW YORK, Marekani
MWANAMUZIKI nyota wa Marekani, Mariah Carey na mumewe Nick Cannon, wamewatoa hadharani watoto wao mapacha, Monroe na Moroccan.
Hii ni mara ya kwanza kwa Mariah na mumewe kuwaonyesha watoto hao hadharani, tangu walipozaliwa Aprili 30 mwaka huu.
Mariah (41) na Cannon walikwenda na watoto wao kwenye mahojiano maalumu yaliyofanyika katika kipindi na mtangazaji, Barbara Walters kuhusiana na ndoa yao.
Wakati wote wa mahojiano hayo, Monroe na Moroccan walionyesha uchangamfu.
Monroe, ambaye ni msichana, alibebwa na mama yake na Moroccan muda mwingi alikuwa kwa baba yake. Mariah alisema mapacha hao wamewapa majina ya utani ya 'Roc na Roe'.
"Mwili wangu ulikuwa mkubwa sana. Kuwatunza watoto wawili mapacha muda mrefu, si jambo dogo, lakini imewezekana. Kimsingi ilikuwa ni hatari," alisema Mariah.
Cannon alisema mtoto wake wa kike Monroe amefanana na mama yake Mariah.
"Watoto wetu ni wachangamfu, kila asubuhi wanapoamka, huonyesha sura za tabasamu, kama wana njaa utawabaini," alidokeza muigizaji huyo.

Van Persie aipa kiwewe Arsenal


LONDON, England
KLABU ya Arsenal ya England inakabiliwa na mtihani mgumu wa kumzuia nahodha wake, Robin va Persie baada Real Madrid ya Hispania kutenga pauni milioni 30 (sh. bilioni 69) kwa ajili ya kumsajili.
Kocha Mkuu wa Real Madrid, Jose Mourinho ametumia uamuzi wa Van Persie kuuza nyumba yake mjini London kumzengea wakati wa usajili wa dirisha dogo Januari mwakani.
Mholanzi huyo amebakiza miezi sita kabla ya mkataba wake na Arsenal kumalizika, ambapo atakuwa mchezaji huru na Mourinho amepanga kumng'oa kwa dau kubwa ili kujenga kikosi imara.
Mourinho, aliyeiongoza Real Madrid kuilaza Lyon mabao 4-0 katika ligi ya mabingwa wa Ulaya juzi, anataka kujenga safu imara ya ushambuliaji licha ya kuwa na Cristiano Ronaldo na Karim Benzema.
Hata hivyo, Mourinho atakuwa na kazi ngumu ya kumsajili Van Persie kutokana na ukweli kuwa ndio lulu ya kocha Arsene Wenger kwa ufungaji mabao.
Wenger alimpa unahodha Van Persie baada ya kuondoka Cesc Fabregas msimu uliopita, aliyetimkia Barcelona.
Wachezaji wengine walioihama klabu hiyo majira ya kiangazi ni Gael Clichy na Samir Nasri waliotua Manchester City.
Katika hatua nyingine, Wenger amesisitiza kuwa hana mpango wa kuondoka Arsenal kwa sasa.
Wenger ameelezea msimamo wake huo juzi, siku moja baada kuripotiwa kuwa, ameamua kuondoka klabu hiyo kabla ya mkataba wake kumalizika.
Kuna habari kuwa, tayari klabu ya PSG ya Ufaransa ilishaanza kujiandaa kumnyakua kocha huyo kwa kumfanya mkurugenzi wa michezo.
“Nimesaliwa na miaka mitatu kwenye mkataba wangu na Arsenal na siku zote nauheshimu mkataba wangu,”alisema kocha huyo.

GERRARD: Sikutegemea


LONDON, England
NAHODHA wa timu ya soka ya Liverpool ya England, Steven Gerrard, amesema hakutarajia kurejea kwenye kiwango bora baada ya kuwa nje ya uwanja kwa miezi sita.
Gerrard alirejea uwanjani kwa mara ya kwanza mwishoni mwa wiki iliyopita wakati Liverpool ilipomenyana na Manchester United katika ligi kuu ya England na kutoka sare ya bao 1-1.
Nahodha huyo wa Liverpool alifanyiwa upasuaji wa ngiri na kumfanya ashindwe kucheza soka kwa muda mrefu.
Gerrard alisema alipokuwa akiuguza majereha hayo, alidhani ungekuwa mwisho wake wa kucheza, soka lakini baada ya kucheza kwa ustadi dhidi ya United, anajiona ni mchezaji mpya.
"Nimepitia kipindi kigumu sana, miezi sita nje ya uwanja ni mingi na nilidhani nimekwisha. Lakini naendelea kurejea katika hali yangu ya kawaida siku hadi siku," alisema mchezaji huyo.
Gerrard (31) alidokeza kuwa, kabla ya kufanyiwa upasuaji, alikuwa akipigwa sindano za maumivu ili acheze baadhi ya mechi, hatua ambayo alidai haikuwa sahihi, lakini alilazimika kufanya hivyo ili kuokoa jahazi Liverpool.
Aliongeza kuwa, alilazimika kutumia muda mfupi kufanya mazoezi msimu uliopita kwa hofu ya kujitonesha.
“Miezi sita iliyopita ilikuwa kipindi kigumu kwangu katika maisha yangu kisoka,”alisema nguli huyo.
Mchezaji huyo ndiye injini ya Liverpool na amekuwa akitoa mchango mkubwa katika kikosi hicho.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kenny 'King' Dalglish amesema Gerrard atakuwa nahodha wa muda mrefu.

Asamoah kuuzwa kwa mkopo Moro United


KAMATI ya Usajili ya klabu ya Yanga imeanza mchakati wa kuongeza nguvu kwenye kikosi cha timu hiyo ikiwa ni pamoja na kuwauza baadhi ya wachezaji wake.
Habari zilizopatikana jana kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, kwa kuanzia, kamati hiyo imeamua kumuuza kwa mkopo mshambuliaji wake, Kenneth Asamoah kwa klabu ya Moro United.
Kwa mujibu wa habari hizo, Asamoah huenda akauzwa kwa Moro United wakati wa usajili wa dirisha dogo unaotarajiwa kufanyika Januari mwakani.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo alilieleza gazeti la Burudani kuwa, uamuzi wa kumuuza Asamoah umefikiwa kutokana na kiwango chake kushuka.
Mjumbe huyo alisema, kamati yake imekuwa ikiandaa ripoti ya kila mchezaji ili iwe rahisi kujua uwezo wao na nafasi yao kwa Yanga.
“Lengo letu ni kujenga timu imara kwa ajili ya michuano ya klabu bingwa Afrika mwakani,”alisema mjumbe huyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Hatua hiyo ya Yanga imekuja siku chache baada ya mfadhili wa zamani wa klabu hiyo, Yussuf Manji kuushutumu uongozi kwa kusajili wachezaji wengi wasiokuwa na uwezo, wakiwemo kutoka nje ya nchi.
Wachezaji wengine, ambao wapo njia panda kuuzwa na klabu hiyo ni pamoja na Pius Kisambale na Godfrey Bonny.

Simba yambania Jerry Santo


UONGOZI wa klabu ya Simba umesema hauna mpango wa kumuuza kiungo wake, Jerry Santo kwa klabu nyingine.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, Santo bado ni mchezaji halali wa klabu hiyo. Kamwaga alisema wameshafanya mazungumzo ya awali na Santo ili aweze kuongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo.
Kwa mujibu wa Kamwaga, uamuzi wa kumuongezea mkataba Santo umefikiwa na benchi la ufundi la timu hiyo kutokana na kuridhika na uwezo wake.
“Jambo la msingi ni kwamba hatuna mpango wa kumwachia Santo akajiunge na klabu nyingine kwa sababu bado tunamuhitaji,”alisema.
Simba imeelezea msimamo wake huo baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuripoti hivi karibuni kuwa, mchezaji huyo anatarajiwa kwenda kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi.
Vyombo hivyo vya habari vilieleza kuwa, Santo amepanga kwenda nje baada ya mkataba wake na Simba kumalizika mwishoni mwa mwaka huu.

Wachezaji Yanga wapigwa mkwara



UONGOZI wa klabu ya Yanga umewapiga marufuku wachezaji wake kutoka nje ya kambi ya timu hiyo bila idhini ya uongozi.
Agizo hilo limekuja baada ya baadhi ya wachezaji wa timu hiyo kukutwa wakitanua katika maonyesho ya muziki wa dansi ya bendi za FM Academia na Twanga Pepeta International yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, wachezaji hao walikutwa wakitanua kwenye kumbi za klabu ya TCC, Chang’ombe na Msasani Beach huku baadhi yao wakiwa wamelewa chakari.
Kutokana na kukutwa katika maeneo hayo, baadhi ya wanachama waliamua kuwasilisha majina ya wachezaji hao kwa uongozi na Kocha Sam Timbe ili waweze kuchukuliwa hatua.
Kwa mujibu wa habari hizo, timu hiyo sasa imeingia rasmi kambini juzi makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
“Ni kutokana na matukio hayo, uongozi sasa umeamua timu iingie kambini mara moja na kuwapiga marufuku wachezaji kutoka nje ya kambi bila ruhusa ya uongozi,” kimesema chanzo cha habari.
Wakati huo huo, mabingwa hao watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, leo wanatarajiwa kushuka dimbani kumenyana na Toto African katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pambano hilo linatarajiwa kuwa kali na la kusisimua kwa vile kila timu itapania kushinda ili kutoka uwanjani na pointi zote tatu.
Yanga inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi tisa wakati Toto African ni ya tisa ikiwa na pointi 10 kutokana na idadi hiyo ya mechi.
Kocha Mkuu wa Yanga, Sam Timbe alisema juzi kuwa, wanaipa mechi hiyo umuhimu mkubwa kwa vile wamepania kushinda mechi zao zote zilizosalia za mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.
“Kwa kweli sitaki kuona tunapoteza mechi yoyote ya mzunguko wa kwanza, na tutaanzia kwa Toto African,”alisema kocha huyo raia wa Uganda. Kwa upande wake, Kocha John Tegete wa Toto African amejigamba kuwa, kikosi chake kimejiandaa vyema kwa ajili ya kukabiliana na Yanga.
Tegete aliwaonya mashabiki wa Yanga kuwa, wasitarajie kupata mteremko katika mechi hiyo kwa vile wana uhakika mkubwa wa kufanya vizuri.

Isha Mashauzi amuangukia Mzee Yussuf


MSANII nyota wa muziki wa taarab nchini, Isha Ramadhani 'Mashauzi' ametamka hadharani kwamba, alifanya kosa kubwa kuondoka katika kikundi cha Jahazi.
Isha alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati kundi la Jahazi, chini ya mkurugenzi wake, Mzee Yussuf lilipofanya onyesho kwenye ukumbi wa Travertine, Magomeni, Dar es Salaam.
Mwanamama huyo mwenye mbwembwe na madaha awapo jukwaani, alikuwa mwimbaji nguli katika kundi hilo na kujipatia umaarufu mkubwa kutokana na tungo zake kukubalika na mashabiki wengi.
Baada ya kuondoka katika kundi hilo, msanii huyo aliamua kuanzisha kundi lake la Mashauzi Classic na tangu hapo alikuwa haonekani katika maonyesho ya Jahazi.
Kuondoka kwa mwimbaji huyo katika kundi la Jahazi, kuliibua maswali mengi na baadhi ya mashabiki walijenga hisia kwamba, huenda alikuwa na ugomvi na Yussuf.
Lakini Isha aliamua kuvunja ukimya mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kusema kuwa, kitendo alichofanya hakikuwa cha kiungwana.
Isha alitumia fursa hiyo kumuomba radhi Yussuf pamoja na wasanii wengine wa kundi la Jahazi, kauli iliyopokelewa kwa shangwe nyingi na mashabiki waliohudhuria onyesho hilo.
Mbali ya kuomba radhi, Isha alipanda jukwaani wakati wa onyesho hilo na kuimba moja ya vibao vyake vya zamani, alipokuwa Jahazi.
Tukio hilo liliwafanya mashabiki na wapenzi wa muziki huo kumpongeza Isha kwa kitendo chake hicho cha kiungwana cha kuomba radhi baada ya kutambua amefanya kosa.
Isha alisema si vyema kwa sasa kuendeleza malumbano na kujengeana chuki baina ya wasanii kwa vile kufanya hivyo hakuna faida yoyote kwao zaidi ya kudumaza soko la muziki huo na maendeleo yake.

Simba yazidi kupaa

Emmanuel Okwi

Haruna Moshi 'Boban'


SIMBA jana iliendelea kupaa katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara, baada ya kuicharaza Ruvu Shooting mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Ushindi huo ulikuwa wa saba kwa Simba katika ligi hiyo na uliiwezesha kuwa na pointi 24 baada ya kucheza mechi 10. Ruvu Shooting ni ya nane ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza idadi hiyo ya mechi.
Pambano hilo lilianza kwa kasi huku wachezaji wa Simba wakigongeana pasi fupi fupi wakati Ruvu Shooting walitumia pasi ndefu na kucheza kwa kutumia nguvu zaidi.
Simba ilikuwa ya kwanza kubisha hodi kwenye lango la Ruvu Shooting dakika ya 26 wakati kipa Benjamin Haule wa Ruvu Shooting alipoutema mpira na kumkuta Uhuru Selemani, lakini shuti lake liligonga mwamba wa goli na mpira kuokolewa.
Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu katika kipindi cha kwanza, lakini umaliziaji mbovu wa washambuliaji wake ulikuwa kikwazo kupata mabao. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu. Simba ilikianza kipindi cha pili kwa kumpumzisha Uhuru Selemani na kumwingiza Haruna Moshi, ambaye aliongeza uhai kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Bao la kwanza la Simba lilifungwa na Emmanuel Okwi dakika ya 47, kufuatia gonga safi kati yake na Haruna Moshi ‘Boban’. Kipa Benjamin Haule wa Ruvu Shooting alishindwa kuokoa shuti hilo.
Boban aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 53 baada ya kugongeana vizuri na Okwi. Kabla ya kufunga bao hilo zuri na la aina yake, Okwi alimchungulia kipa Haule na kuukwamisha mpira wavuni.
Simba sasa imesaliwa na mechi tatu dhidi ya JKT Ruvu, Yanga na Moro United kabla ya kukamilisha mechi za mzunguko wa kwanza.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo wakati mabingwa watetezi Yanga watakapomenyana na Toto African kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kesho Azam itavaana na Polisi Dodoma kwenye uwanja wa Chamazi.
Simba: Juma Kaseja, Saidi Cholo, Juma Jabu, Juma Nyoso, Obadia Mungusa, Patrick Mafisango/Shomari Kapombe, Jerry Santo, Ulimboka Mwakingwe, Emmanuel Okwi, Felix Sunzu, Uhuru Selemani/Haruna Moshi.
Ruvu Shooting: Benjamin Haule, Michael Pius, Paul Ngalema, George Michael, Shabani Zuzan, Iddi Nyambiso, Ayoub Kitala, Hassan Dilunga, Abdalla Juma/Abdalla Abdulrahman, Kassim Linde, Raphael Keyala.

Tuesday, October 18, 2011

MAKONGORO: Viongozi waache tamaa ya utajiri

Makongoro Nyerere (kushoto) akizungumza na mmiliki wa blogu hii, Rashid Zahor ofisini kwake Musoma mkoani Mara



UNAPOTAJA majina ya watoto wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jina linaloweza kutambulika kirahisi zaidi kutokana na umaarufu wake ni la Makongoro Nyerere.
Umaarufu wa Makongoro unatokana na mambo mengi, lakini yaliyo makubwa ni kujihusisha kwake na masuala ya siasa na pia kupenda kujichanganya na watu mbalimbali kwa ajili ya kubadilishana mawazo na kupata kinywaji kidogo.
Makongoro, ambaye ni mtoto wa tano wa Baba wa Taifa, aliwahi kuwa mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi mwaka 1995 na aliwahi kumtembelea baba yake Butiama akiwa na viongozi wenzake wa chama hicho.
Hata hivyo, Makongoro hakuweza kudumu kwenye ubunge kwa muda mrefu. Aliondolewa kwenye nafasi hiyo kwa uamuzi wa mahakama, kufuatia kesi iliyofunguliwa ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo.
Miaka michache baadaye, Makongoro alirejea CCM na miaka ya hivi karibuni, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama mkoa wa Mara, wadhifa anaoendelea kuushikilia hadi sasa.
Makongoro ni mwanasiasa mzuri. Licha ya kuijua vyema historia ya TANU, CCM, mapambano ya kugombea uhuru wa Tanganyika na siasa za vyama vingi, ni mtu mwenye ushawishi na uelewa mkubwa juu ya mambo mbalimbali.
Hayo yalijidhihirisha wakati nilipobahatika kuzungumza na mwanasiasa huyu kwenye ofisi za CCM mkoa wa Mara baada ya kumkosa nyumbani kwake kijiji cha Butiama kilichopo wilaya ya Musoma Mjini.
Katika mazungumzo hayo, ambayo yalilenga maadhimisho ya miaka 12 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa na miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika, Makongoro alisema njia pekee nzuri ya kumuenzi Mwalimu Nyerere ni kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa watanzania.
Makongoro alisema Mwalimu Nyerere na wazee wenzake, akiwemo hayati Abeid Amaan Karume, kwa makusudi walifanya juhudi za kisayansi kuwaunganisha watanzania kuwa wamoja baada ya kugundua kwamba, wakoloni waliokuwa wakiwatawala, hawakuwa wengi na walitumia mbinu kuwagawa.
“Walichofanya ni kuchukua hatua mbalimbali kuleta umoja kabla ya uhuru na miaka 10 baada ya uhuru. Umoja huu bado upo, lakini unaweza kuyumba kutokana na maongozi ya kisiasa ya vyama vingi, halafu tukawaambukiza wananchi,”alisema.
Mwanasiasa huyo machachari alisema, watanzania bado wana umoja, lakini vyama vya siasa vinaweza vikaanzisha makundi ndani ya vyama vyenyewe na kisha makundi hayo kuhamia kwa wananchi.
“Hivyo kwangu mimi, njia pekee nzuri kwa wananchi kumuenzi Baba wa Taifa na viongozi wenzake wa wakati huo ni kudumisha amani na umoja, vilivyodumu wakati wao hadi walipotuachia uongozi,”alisema.
Akizungumzia uwepo wa vyama vingi vya siasa nchini, Makongoro alisema bado unakwenda kama ulivyoachwa na Mwalimu Nyerere, isipokuwa zipo dosari chache, lakini haziwezi kutishia amani iliyopo nchini.
Alisema uhuru ni jambo jema, lakini uhuru usio na nidhamu ni haramu. Alisema iwapo inatokea watu wanakwenda kufanya vurugu mahali kwa mtu, ambaye ni mwanasiasa ama si mwanasiasa, huo ni uhuni na inatakiwa waadhibiwe.
Alisema matukio ya aina hiyo yanaweza kutokea nchi yoyote,wakati wowote na kufanywa na mtu yeyote, lakini hayamaanishi kwamba amani inatoweka. Alisisitiza kuwa, amani bado ipo nchini.
Alitoa mfano wa uchaguzi mdogo wa jimbo la Tarime, kufuatia kifo cha mbunge wake, Chacha Wangwe, ambapo baadhi ya wananchi walikatwa mapanga na mbunge mmoja kupiga risasi hewani ili kujitetea.
Mfano mwingine uliotolewa na Makongoro ni ule wa wafuasi wa CHADEMA kumvisha mbwa fulana yenye nembo ya CCM na watu kumkatakata mapanga.
“Huyu ni mnyama masikini, hajui lolote na kwa mazingira ya Tarime yalivyo, pengine aliona wamemsitiri kwa baridi, kumbe kuna watu wengine wamekerwa na kitendo kile,”alisema.
“Vyama vina matatizo. Palipo na haki pana wajibu. Huwezi kutaka haki ya kuwa huru, lakini hutaki kuwajibika na kuwa na nidhamu. Uhuru wako utakuwa mchezo wa kuigiza,”aliongeza.
Makongoro alisema, kutokana na tukio hilo, CCM ingeweza kulalamika kwa tume ya taifa nay eye alikuwa mwenyekiti, lakini hakupelekewa malalamiko hayo zaidi ya kupewa taarifa ya tukio na kuelezwa kwamba mbwa huyo ameshashughulikiwa.
“Unaweza kuita ni uvunjifu wa amani, lakini hapana, huu ni ushabiki uliovuka mpaka. Wangeweza kuniita na kunieleza. Tume ya uchaguzi inapaswa kukemea. Haiwezekani kila tunapoingia kwenye uchaguzi mdogo, watu wakatane mapanga,”alisema Makongoro.
Aliongeza kuwa, watu wanaofanya vurugu wakati wa uchaguzi mdogo wanajulikana vyema, hivyo wakati umefika kwa bunge kutunga sheria ya kuwadhibiti ili kukomesha vitendo hivyo.
Makongoro alisema vyama vingi vya siasa vilivyopo sasa, Baba wa Taifa aliviacha na kama ni kuongezeka, huenda ni kimoja ama viwili. Alisema Mwalimu Nyerere ni mmoja wa waasisi wa siasa ya vyama vingi nchini baada ya kura ya maoni.
Alisema katika upigaji huo wa kura ya maoni, asimilia 80 ya watanzania hawakutaka vyama vingi wakati asilimia 20 ndio waliotaka na kwamba kwa kuzingatia idadi hiyo, kulikuwa hakuna haja ya kuwaunga mkono watu wachache.
“Lakini mwalimu siku zote alikuwa anaona mbali. Alisema kama unataka kudumisha amani, kungali mapema tusifanye kosa hilo. Hao wachache nao tuwaingize kwenye taratibu za nchi. Alitoa ushauri, anaheshimika, CCM na serikali ikakubali ushauri wake, katiba ya nchi ikabadilishwa,”alisema.
Makongoro alisema kwa sasa, hakuna juhudi za kutosha za kutoa raslimali kwa wasiokuwa nacho na kuongeza kuwa, wakati wa Mwalimu Nyerere, raslimali zilikuwepo, lakini ziligawiwa sawa na kasi ya waliotajirika haikuwa kubwa kama hivi sasa.
Alisema kasi hiyo kwa sasa imeongezeka, wasiokuwa nacho wamebaki hivyo na waliofaidika nazo, wameendelea kutajirika zaidi na kufanya tofauti kati yao iwe kubwa.
Makongoro pia alilalamikia kukiukwa kwa miiko ya uongozi, ambapo alisema jambo hilo limekuwa likisababisha matatizo makubwa katika jamii. Alisema serikali ilifanya kosa kubwa kutenganisha miiko ya uongozi na maadili ya uongozi.
“Viongozi wakati wa historia yetu, walipunguza masharti ya Azimio la Arusha yaliyokuwa yakiwabana, pengine kwa nia nzuri. Kuna viongozi hawakuruhusiwa kufanyakazi zingine, hali zao ni mbaya.
“Tunayo mifano hai ya viongozi, ambao wameruhusiwa kufanya shughuli zingine, wamestaafu, lakini hali zao ni ahueni kidogo. Lakini haina maana kwamba mwanya huu hautumiki na wengine, ambao wapo madarakani na wengine wamestaafu, kujitajirisha kupita kiwango,”alisema.
“Wakikurupuka na Azimio la Zanzibar ghafla, unaweza kufumba macho yako kuona mambo, ambayo ni kweli yapo sasa hivi. Tunao viongozi pengine aliwahi kuwa katibu mkuu wa CCM akastaafu, ukienda kumuona hali yake, bado yupo hai, hali yake ni mbaya kwa sababu alikuwa mwadilifu. Pengine azimio hilo lilimlenga mtu kama huyu,”aliongeza.
“Wapo wengine, ambao walijiangalia tu vizuri kwa nafasi zao, iwe waziri au yeyote, walitumia vizuri fursa hizo, waliishi vizuri na watoto wao kuwafikisha mahali wanajitegemea. Wengine walitumia mwanya huo kufanya balaa,” alisema.
“Mwalimu alikuwa anaishi kwa kufundisha kwa vitendo maisha yake yote. Usichanganye bahati aliyopata yeye ya kupendwa na kuhesimiwa na wananchi baada ya kifo chake kutokana na matendo yake na alivyojiweka.
“Waswahili wanasema imani huzaa imani, chuki huzaa chuki na upendo huzaa upendo. Yeye alipata bahati hiyo, wenzake aliowaachia walipanga utaratibu wa kumuenzi, si kila nchi inapanga hivyo, ilikuja kutokana na tabia zake.
“Mwalimu amepata bahati, nchi hii imeendelea kumpenda hadi sasa na nchi hii inamtunza mjane wake, haitunzi wanawe, ni bahati kwamba heshima yake ni nzuri na mazingira yanaonyesha hiyo ni kamali mbaya, angeweza kuondoka hana nyumba.
“Ameacha nyumba mbili, moja kajengewa na chama kwa lazima, nyingine alijengewa na jeshi, angebaki na nyumba yake binafsi ya Butiama, hali ingekuwa mbaya.
“Tusimsifu mwalimu kwa kuwa ameondoka, alikuwa mwadilifu. Huyo mwingine umemtayarishia utaratibu gani? Mwalimu alifanya hivyo kwa sababu aliishi kwa imani na watanzania wanamrudishia imani hiyo,”alisema Makongoro.
Makongoro alisema kwa mazingira ya Tanzania, historia imebadilika na kwamba, serikali iliyotawaliwa na ufisadi, haiwezi kuwa na usalama popote. Alisema nchi inapaswa kupata mwongozo kwa watu wenye kipato cha chini kutazamwa upya.
Amewaonya watu wanaojiona matajiri kwamba wanajidanganya kwa kudhani watanunua chama na heshima. Alisisitiza kuwa, kamwe hilo haliwezekani, isipokuwa linatokea kutokana na mazingira ya nchi kuwa maskini.

Makumbusho yaliyobeba kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere

Hizi ni baadhi ya zana zilizokuwa zikitumiwa na Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kilimo. Zana hizo zimehifadhiwa kwenye makumbusho yake iliyopo kijiji cha Butiama

Hizi ni viatu vya mvua, vya kawaida na kofia. Vitu hivi vilikuwa vikitumiwa na Mwalimu Nyerere akiwa kwenye shughuli za kilimo.


Hii ni redio iliyokuwa ikitumiwa na Mwalimu Nyerere kusikiliza habari za kimataifa kila alipokwenda Butiama kwa mapumziko.


Hizi ni baadhi ya picha zilizopo kwenye makumbusho ya Mwalimu Nyerere. Picha ya kushoto inamwonyesha Mwalimu Nyerere akiwa na mama yake, Bi Mgaya. Picha ya kulia ni ya baba yake Mwalimu Nyerere, Chifu Burito Nyerere akiwa na mmoja wa wake zake na askari.


Hivi ni vifaa alivyozawadiwa Mwalimu Nyerere baada ya kustaafu urais mwaka 1985. Pia zipo fimbo alizokuwa akipenda kutembea nazo.


Hivi ndivyo makumbusho ya Mwalimu Nyerere inavyoonekana kwa mbele


Hili ni eneo ambalo mizimu ya Muhunda ya Wazanaki huwa ikitokea mara kwa mara kwa ajili ya kuashiria mambo mbalimbali.


Hiki ni kibanda ambacho Mwalimu Nyerere alikuwa akipenda kukitumia kwa ajili ya mazungumzo na wageni mbalimbali waliokuwa wakimtembelea Butiama.



Hili ni eneo ambalo lilikuwa likitumika kuwashia mwenge wa Wazanaki. Eneo hili lipo Mwitongo, jirani na nyumba ya Mwalimu Nyerere.


UKISHAINGIA kwenye geti kubwa la kuingilia nyumbani kwa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, eneo la Mwitongo, Butiama, mbele yako utakutana na kibanda mlimohifadhiwa kaburi lake. Kibanda hicho kilichojengwa kwa matofali, kimenakshiwa kwa milango na madirisha ya vioo na kukifanya kiwe na mvuto wa aina yake.
Mbele ya kibanda hicho ndipo ilipo nyumba kubwa ya Mwalimu Nyerere aliyojengewa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya kustaafu urais na upande wa kushoto ipo nyumba yake ya zamani aliyojengewa na Chama cha Mapinduzi. Nyumba hii imejengwa juu ya vilima vya mawe.
Mita chache kutoka kilipo kibanda mlimohifadhiwa kaburi la Baba wa Taifa, ipo sanamu ya kichwa chake. Nyuma ya sanamu hiyo ndipo palipokuwa na nyumba alimozaliwa, lakini kwa sasa haipo. Ilibomolewa miaka mingi iliyopita na kulifanya eneo hilo liwe wazi.
Nyuma ya sanamu hiyo kuna vilima viwili vya mawe. Kilima cha kwanza ni eneo ulipokuwa ukiwashwa mwenge wa wazanaki na kilima cha pili ni eneo, ambalo mzimu wa Muhunda huwa ukitokea.
Kwa mujibu wa historia ya wazanaki, mzimu huu huwa ukitokea kwa njia tano tofauti. Huweza kutokea kama nyani mkubwa, nyoka, mbuzi, chui na wakati mwingine lundo kubwa la nyuki. Na kila unapotokea, huwa ni ishara ya jambo moja muhimu kwa familia ya Nyerere.
Katika maeneo mengine, ipo nyumba ya zamani ya Chifu Burito Nyerere, ambayo kwa sasa imegeuzwa kuwa ghala la kuhifadhia nafaka, kibanda alichokuwa akitumia Mwalimu Nyerere kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali waliomtembelea, eneo alilopenda kupigia picha na vibanda vidogo vitatu vya kuhifadhia nafaka. Pia kuna banda dogo la kuegeshea magari.
Pembeni ya eneo alilokuwa akiishi Mwalimu Nyerere, zipo nyumba kadhaa za ndugu na familia yake. Ipo nyumba ya mtoto wake wa tatu, Magige Nyerere na pia ya mdogo wake, Josephat Mahunda Nyerere.
Umbali wa mita zipatazo 100 kutoka eneo hilo, lipo jengo dogo, lakini zuri la makumbusho maalumu ya Mwalimu Nyerere. Ndani ya jengo hilo, kumehifadhiwa picha za matukio mbalimbali ya ukumbusho wa Taifa la Tanzania.
Jengo hili limejengwa chini kidogo ya kilima. Wafanyakazi waliomo ndani ya makumbusho hii ni wawili na kazi yao ni kupokea wageni wanaotembelea hapo na kuwaonyesha vitu mbalimbali vya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Ndani ya makumbusho hii, zipo picha mbalimbali zinazomwonyesha Mwalimu Nyerere akiwa katika matukio tofauti wakati alipokuwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanganyika na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Zimo picha alizopiga na viongozi wa nchi mbalimbali duniani walipomtembelea Ikulu mjini Dar es Salaam ama alipokutana nao katika nchi zao. Pia zimo picha za sherehe mbalimbali za kitaifa alizohudhuria akiwa kiongozi mkuu wa nchi na picha alizopiga akiwa na familia yake.
Vilevile zimo picha za baba yake, Chifu Burito Nyerere na baadhi ya wake zake, picha za mama yake, Bi Mgaya na picha za watoto wake wanane tangu walipokuwa wadogo. Picha zote hizo zilipigwa kijijini kwa Mwalimu Nyerere, eneo la Mwitongo.
Ndani ya makumbusho hiyo, vipo vifaa mbalimbali vilivyokuwa vikitumiwa na Mwalimu Nyerere kila alipokwenda Butiama kwa mapumziko. Vifaa hivyo ni pamoja na radio aliyokuwa akitumia kusikiliza habari za kimataifa, viatu vya kulimia, kofia, jembe, shoka, mundu, birika ndogo ya chai na vikombe.
Vifaa vingine ni koti lililotengenezwa kwa kutumia ngozi ya simba dume, nguo alizozawadiwa katika mikoa mbalimbali nchini baada ya kustaafu urais mwaka 1985 na fimbo alizokuwa akitembea nazo, ambazo zilikuwa alama ya utambulisho wake.
Katika eneo moja la makumbusho hiyo, imebandishwa historia ndefu ya Mwalimu Nyerere tangu alipoanza harakati za kuunda Chama cha TANU na hatimaye kugombea uhuru wa Tanganyika. Pia zipo picha za viongozi wa mwanzo wa chama hicho.
Picha zingine zilizomo kwenye makumbusho hiyo ni ya baraza lake la mwisho la mawaziri wakati akielekea kujiuzulu urais mwaka 1985. Pengine picha kubwa na nzuri zaidi ni ile inayomwonyesha akiwa amevaa vazi maalumu, akiwa Ikulu mjini Dar es Salaam.
Picha hii ya aina yake inaacha maswali mengi. Je, Mwalimu Nyerere alibuni vazi hili ili liwe la kitaifa kwa wananchi wa Tanzania? Ama alivutiwa nalo na kuamua kulivaa?
Pengine kwa wakati huu, ambapo wabunifu wa mavazi nchini wakiwa wanahangaika kubuni vazi la kitaifa, watazame picha hii ya Mwalimu Nyerere na kufikiria kulipa nafasi vazi hili vichwani mwao.
Inawezekana kabisa kwamba, Mwalimu Nyerere alishaona mbali na kuamua kubuni vazi hili mapema, isipokuwa watanzania walishindwa kumwelewa. Kazi kwenu wabunifu wa mavazi.