KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, October 18, 2011

Makumbusho yaliyobeba kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere

Hizi ni baadhi ya zana zilizokuwa zikitumiwa na Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kilimo. Zana hizo zimehifadhiwa kwenye makumbusho yake iliyopo kijiji cha Butiama

Hizi ni viatu vya mvua, vya kawaida na kofia. Vitu hivi vilikuwa vikitumiwa na Mwalimu Nyerere akiwa kwenye shughuli za kilimo.


Hii ni redio iliyokuwa ikitumiwa na Mwalimu Nyerere kusikiliza habari za kimataifa kila alipokwenda Butiama kwa mapumziko.


Hizi ni baadhi ya picha zilizopo kwenye makumbusho ya Mwalimu Nyerere. Picha ya kushoto inamwonyesha Mwalimu Nyerere akiwa na mama yake, Bi Mgaya. Picha ya kulia ni ya baba yake Mwalimu Nyerere, Chifu Burito Nyerere akiwa na mmoja wa wake zake na askari.


Hivi ni vifaa alivyozawadiwa Mwalimu Nyerere baada ya kustaafu urais mwaka 1985. Pia zipo fimbo alizokuwa akipenda kutembea nazo.


Hivi ndivyo makumbusho ya Mwalimu Nyerere inavyoonekana kwa mbele


Hili ni eneo ambalo mizimu ya Muhunda ya Wazanaki huwa ikitokea mara kwa mara kwa ajili ya kuashiria mambo mbalimbali.


Hiki ni kibanda ambacho Mwalimu Nyerere alikuwa akipenda kukitumia kwa ajili ya mazungumzo na wageni mbalimbali waliokuwa wakimtembelea Butiama.



Hili ni eneo ambalo lilikuwa likitumika kuwashia mwenge wa Wazanaki. Eneo hili lipo Mwitongo, jirani na nyumba ya Mwalimu Nyerere.


UKISHAINGIA kwenye geti kubwa la kuingilia nyumbani kwa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, eneo la Mwitongo, Butiama, mbele yako utakutana na kibanda mlimohifadhiwa kaburi lake. Kibanda hicho kilichojengwa kwa matofali, kimenakshiwa kwa milango na madirisha ya vioo na kukifanya kiwe na mvuto wa aina yake.
Mbele ya kibanda hicho ndipo ilipo nyumba kubwa ya Mwalimu Nyerere aliyojengewa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya kustaafu urais na upande wa kushoto ipo nyumba yake ya zamani aliyojengewa na Chama cha Mapinduzi. Nyumba hii imejengwa juu ya vilima vya mawe.
Mita chache kutoka kilipo kibanda mlimohifadhiwa kaburi la Baba wa Taifa, ipo sanamu ya kichwa chake. Nyuma ya sanamu hiyo ndipo palipokuwa na nyumba alimozaliwa, lakini kwa sasa haipo. Ilibomolewa miaka mingi iliyopita na kulifanya eneo hilo liwe wazi.
Nyuma ya sanamu hiyo kuna vilima viwili vya mawe. Kilima cha kwanza ni eneo ulipokuwa ukiwashwa mwenge wa wazanaki na kilima cha pili ni eneo, ambalo mzimu wa Muhunda huwa ukitokea.
Kwa mujibu wa historia ya wazanaki, mzimu huu huwa ukitokea kwa njia tano tofauti. Huweza kutokea kama nyani mkubwa, nyoka, mbuzi, chui na wakati mwingine lundo kubwa la nyuki. Na kila unapotokea, huwa ni ishara ya jambo moja muhimu kwa familia ya Nyerere.
Katika maeneo mengine, ipo nyumba ya zamani ya Chifu Burito Nyerere, ambayo kwa sasa imegeuzwa kuwa ghala la kuhifadhia nafaka, kibanda alichokuwa akitumia Mwalimu Nyerere kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali waliomtembelea, eneo alilopenda kupigia picha na vibanda vidogo vitatu vya kuhifadhia nafaka. Pia kuna banda dogo la kuegeshea magari.
Pembeni ya eneo alilokuwa akiishi Mwalimu Nyerere, zipo nyumba kadhaa za ndugu na familia yake. Ipo nyumba ya mtoto wake wa tatu, Magige Nyerere na pia ya mdogo wake, Josephat Mahunda Nyerere.
Umbali wa mita zipatazo 100 kutoka eneo hilo, lipo jengo dogo, lakini zuri la makumbusho maalumu ya Mwalimu Nyerere. Ndani ya jengo hilo, kumehifadhiwa picha za matukio mbalimbali ya ukumbusho wa Taifa la Tanzania.
Jengo hili limejengwa chini kidogo ya kilima. Wafanyakazi waliomo ndani ya makumbusho hii ni wawili na kazi yao ni kupokea wageni wanaotembelea hapo na kuwaonyesha vitu mbalimbali vya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Ndani ya makumbusho hii, zipo picha mbalimbali zinazomwonyesha Mwalimu Nyerere akiwa katika matukio tofauti wakati alipokuwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanganyika na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Zimo picha alizopiga na viongozi wa nchi mbalimbali duniani walipomtembelea Ikulu mjini Dar es Salaam ama alipokutana nao katika nchi zao. Pia zimo picha za sherehe mbalimbali za kitaifa alizohudhuria akiwa kiongozi mkuu wa nchi na picha alizopiga akiwa na familia yake.
Vilevile zimo picha za baba yake, Chifu Burito Nyerere na baadhi ya wake zake, picha za mama yake, Bi Mgaya na picha za watoto wake wanane tangu walipokuwa wadogo. Picha zote hizo zilipigwa kijijini kwa Mwalimu Nyerere, eneo la Mwitongo.
Ndani ya makumbusho hiyo, vipo vifaa mbalimbali vilivyokuwa vikitumiwa na Mwalimu Nyerere kila alipokwenda Butiama kwa mapumziko. Vifaa hivyo ni pamoja na radio aliyokuwa akitumia kusikiliza habari za kimataifa, viatu vya kulimia, kofia, jembe, shoka, mundu, birika ndogo ya chai na vikombe.
Vifaa vingine ni koti lililotengenezwa kwa kutumia ngozi ya simba dume, nguo alizozawadiwa katika mikoa mbalimbali nchini baada ya kustaafu urais mwaka 1985 na fimbo alizokuwa akitembea nazo, ambazo zilikuwa alama ya utambulisho wake.
Katika eneo moja la makumbusho hiyo, imebandishwa historia ndefu ya Mwalimu Nyerere tangu alipoanza harakati za kuunda Chama cha TANU na hatimaye kugombea uhuru wa Tanganyika. Pia zipo picha za viongozi wa mwanzo wa chama hicho.
Picha zingine zilizomo kwenye makumbusho hiyo ni ya baraza lake la mwisho la mawaziri wakati akielekea kujiuzulu urais mwaka 1985. Pengine picha kubwa na nzuri zaidi ni ile inayomwonyesha akiwa amevaa vazi maalumu, akiwa Ikulu mjini Dar es Salaam.
Picha hii ya aina yake inaacha maswali mengi. Je, Mwalimu Nyerere alibuni vazi hili ili liwe la kitaifa kwa wananchi wa Tanzania? Ama alivutiwa nalo na kuamua kulivaa?
Pengine kwa wakati huu, ambapo wabunifu wa mavazi nchini wakiwa wanahangaika kubuni vazi la kitaifa, watazame picha hii ya Mwalimu Nyerere na kufikiria kulipa nafasi vazi hili vichwani mwao.
Inawezekana kabisa kwamba, Mwalimu Nyerere alishaona mbali na kuamua kubuni vazi hili mapema, isipokuwa watanzania walishindwa kumwelewa. Kazi kwenu wabunifu wa mavazi.

No comments:

Post a Comment