KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 13, 2011

CHIFU WANZAGI, KIJANA ALIYEBEBA SIRI NZITO ZA MWALIMU NYERERE



CHIFU Japhet Wanzagi ndiye msemaji mkuu wa familia ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Ndiye kiongozi mkuu wa kabila la Wazanaki, ambalo makao yake makuu ni katika kijiji cha Butiama kilichopo wilayani Musoma Vijijini mkoani Mara.


Jina lake halisi ni Japhet Kizulila Wanzagi. Alirithi cheo cha uchifu wa kabila hilo Machi mwaka 1997, baada ya kufariki kwa baba yake, Chifu Edward Wanzagi Nyerere, ambaye alikuwa kaka mkubwa wa Mwalimu Nyerere. Ni mtoto wa 37 kati ya watoto 57 wa Chifu Edward Wanzagi, ambaye naye alirithi cheo hicho kutoka kwa baba yake Nyerere, Chifu Burito Nyerere.


Mbali ya wadhifa huo, Chifu Japhet Wanzagi pia ni Askofu Mkuu wa kanisa la Last Church of God Tanzania, cheo alichokipata mwaka 2007 na hivi karibuni alikuwepo mjini Mbeya kwa ajili ya shughuli za kidini za kanisa hilo.


Huyu ndiye aliyeachiwa siri nzito na Mwalimu Nyerere, siku chache kabla hajaondoka kwenda nchini Uingereza kwa ajili ya kupatiwa matibabu na hatimaye kufariki dunia Oktoba 14 mwaka 1999.Inasemekana kuwa Mwalimu Nyerere alimweleza Chifu Wanzagi siri nzito kuhusu wanasiasa na viongozi wa serikali ya Tanzania wakati huo.


Katika hilo, inasemakana Mwalimu Nyerere alimtajia Chifu Wanzagi majina ya wanasiasa na viongozi, ambao hawafai kupewa madaraka ya kuiongoza Tanzania.Mbali na hilo, inasemekana pia kuwa, Mwalimu Nyerere alimweleza kiongozi huyo wa Wazanaki ni kwa njia zipi Tanzania itaweza kuendesha siasa ya vyama vingi bila kuvuruga amani, umoja na mshikamano uliopo miongoni mwa Watanzania, mambo aliyoyaasisi kwa kushirikiana na Rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume.


Alimweleza siri hizo kwa sababu alimwamini zaidi, pengine kuliko hata familia yake au pengine kutokana na wadhifa alionao katika jamii ya Wazanaki. Pia inawezekana ni kwa sababu Chifu Wanzagi ni msomi mzuri, mwona mbali na muelewa wa mambo mengi.


Dalili hizo zinajionyesha wazi kutokana na kauli zake, matendo yake na uongozi wake. Wazee na vijana wengi wa Butiama wanampenda na mara nyingi huenda nyumbani kwake kwa lengo la kupata ushauri wake juu ya mambo mbalimbali yanayowahusu.


Hata hivyo, Chifu Wanzagi hayupo tayari kueleza siri hiyo nzito aliyoachiwa na Mwalimu Nyerere. Sababu kubwa anayoitoa ni kwamba, siasa ya Tanzania kwa sasa imekaa pabaya.

Akizungumza na Uhuru hivi karibuni, Chifu Wanzagi alisema si viongozi na wanasiasa wote wa Tanzania waliopenda mawazo ya Mwalimu Nyerere. Alisema baadhi ya wanasiasa hao wamediriki kutamka waziwazi kwamba Mwalimu Nyerere aliwaonea.


“Alikuwa mwalimu kwa watu wengine, hasa wale waliomzunguka kama jina lake lilivyokuwa. Lakini kwa wakati huu tulionao, ukiwafundisha wenzako kupitia mafundisho yake (Mwalimu Nyerere), utaonekana hujui kitu. Pia unaweza kusababisha matatizo makubwa, ndio sababu sipendi kuzungumza lolote kuhusu wosia nilioachiwa na Mwalimu,”anasema.


Chifu huyo wa Wazanaki alisema anasikitika kuona viongozi wengi wa serikali wameacha kufuata mstari wa uadilifu aliochora Mwalimu Nyerere, badala yake wamekuwa wakinyakua raslimali za nchi kwa maslahi yao binafsi.


Kutokana na kasoro hiyo, amewashauri viongozi wa serikali kutumia siku ya kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere kutafakari ni jambo lipi wanaweza kujisifu kwamba wamelifanya kwa lengo la kumuenzi mwasisi huyo.


“Hii ni siku muhimu sana kwa watanzania kumkumbuka kiongozi wao wa kwanza. Kila mtanzania, mzalendo na anayeipenda nchi yake, anapaswa kutafakari na kujiuliza amefanya kitu gani kumuenzi kiongozi huyu. Lazima kuwe na kitu kwamba bila yeye, kisingekuwepo na je hicho kitu bado kipo na kina hali gani?” anasema.


Chifu Wanzagi alisema uamuzi wa serikali kuwasha mwenge wa Uhuru leo katika kijiji cha Butiama, alikozaliwa Mwalimu Nyerere, inaweza kuwa ishara ya nzuri ya kumkumbuka Baba wa Taifa, lakini lazima uwepo ujumbe maalumu kwa Watanzania.\


“Mimi naamini ujumbe upo. Kwa maoni yangu, ujumbe huo unapaswa kulenga kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa watanzania. Tunapaswa kuendelea kuwa wamoja na kudumisha uhusiano mwema na jirani zetu,”anasema.


Chifu Wanzagi alisema pia kuwa, katika kuadhimisha miaka 12 tangu Mwalimu Nyerere alipofariki dunia na miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara, watanzania wanapaswa kumuenzi kwa vitendo badala ya maneno na kupiga vita rushwa kwa nguvu zote.


Alisema vitendo vya kutoa na kupokea rushwa kwa sasa vimekithiri na kuota mizizi na vinaipeleka nchi pabaya na kwamba kinachosikitisha ni kuona kuwa, hakuna wa kukemea vitendo hivi.Alisema mbaya zaidi ni kuona kuwa, baadhi ya viongozi wa serikali wamevikumbatia zaidi vitendo hivyo badala ya kuvikemea na hivyo kuvifanya vionekane ni jambo la kawaida.


“Nina hakina kama Baba wa Taifa angependa rushwa, familia yake ingekuwa mbali sana. Na hata sisi tunaomzunguka, tungekuwa tunaishi kivingine kabisa,”anasema.


Alisema mapenzi kwa nchi yake na taifa lake, ndivyo vitu vilivyomfanya Mwalimu Nyerere aishi maisha ya kawaida na familia yake na alifanya hivyo kutokana na kuona mbali.Alisema hakuna kiongozi mwingine wa wakati huo duniani na hata hivi sasa, ambaye angeweza kuishi maisha aliyokuwa akiishi Baba wa Taifa kutokana na wadhifa aliokuwa nao.


“Lakini kutokana na nafasi yake, aliona isingekuwa vyema kuishi maisha ya kifahari na hata watoto wake waliridhika. Alikuwa na dhamana ya nchi, hivyo asingeweza kufanya hivyo,”anasema.


“Ukishakuwa kiongozi wan chi, hupaswi kufanya biashara na kujilimbikizia mali. Ukiwa mtu wa aina hiyo, ni rahisi kununuliwa. Ukiwa kiongozi wa nchi, unapaswa kufanana na Mwalimu. Hakutaka hata ndugu zake wajihusishe na biashara,”anasema.


Akitoa mfano, alisema miaka sita baada ya nchi kupata uhuru kutoka kwa Waingereza, Mwalimu Nyerere alifika nyumbani kwa baba yake (Chifu Edward Wanzagi), aliyekuwa na nyumba ndogo Musoma na kumshawishi aiuze ili kutekeleza kwa vitendo Azimio la Arusha.Alisema nyumba hiyo iliyokuwa katikati ya mji, iliuzwa kwa sh. 8,000 kwa mfanyabiashara mmoja mwenye asili ya kiasia, aliyejulikana kwa jina la Guru na kuongeza kuwa, kwa sasa eneo hilo kumejengwa gereji kubwa ya magari. Alisema watu wengi walikuwa wahanga wa siasa ya Mwalimu.


“Hivyo tunapaswa kumuenzi Mwalimu kwa kuchukia rushwa na kuifanya ionekane kuwa adui wa kwanza mbaya kwa watanzania kuliko maradhi na umaskini. Hawa maadui wengine wawili wanapaswa kufuata baadaye,”anaongeza.


Chifu Wanzagi alisema wapo baadhi ya viongozi wa serikali wanaojaribu kukemea rushwa, lakini walio wengi hawafahamu wajibu wao kwa wananchi ndio sababu wanakumbatia vitendo hivyo na kuviona vya kawaida.


Kiongozi huyo wa Wazanaki pia alieleza kusikitishwa kwake na tabia ya viongozi wa siasa kulindana baada ya kufanya makosa. Alisema watu wanafanya makosa na kukabiliwa na tuhuma nyingi, lakini wanalindwa na kuendelea na kazi zao bila wasiwasi.


"Enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere, watu wa aina hii wasingevumiliwa, angewatoa. Hakuwa anamwacha mtu anayetuhumiwa kuendelea kukalia ofisi wakati anachunguzwa. Hali ya sasa inasikitisha sana," anasema Chifu Wanzagi.


Chifu huyo alisema Mwalimu Nyerere alikuwa akiona mbali ndio sababu hotuba alizozitoa wakati nchini ilipopata uhuru hazichuji na kwamba mambo mengi aliyoyatabiri wakati huo ndio yanayotokea hivi sasa.


Akizungumzia siasa ya vyama vingi nchini, Chifu Wanzagi alisema wakati ilipoanzishwa, watu wengi hawakuwa wakifahamu iwapo itasababisha wananchi wasigane na kutokea matukio ya kuhatarisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwao.


“Wengi wetu tumesikitishwa sana na yale yaliyotokea wakati wa uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga. Uchaguzi huo ni kioo cha kuonyesha kule tunakokwenda. Watu wameumbuana waziwazi na kujiweka uchi hadharani. Ni hali ya kusikitisha sana,”anasema.


“Sidhani kama Mwalimu angekuwepo, yangetokea yale yote yaliyotokea Igunga. Angekuwa anakemea. Alikuwa na kauli na watu walimuheshimu,” aliongeza.

No comments:

Post a Comment