KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 13, 2011

YANGA WAMPIGIA MAGOTI MANJI


UONGOZI wa klabu ya Yanga umeamua kumwangukia mfadhili wa zamani wa klabu hiyo, Yusuf Manji ili aendelee kuisaidia.
Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamefikia uamuzi huo kutokana na klabu kukabiliwa na matatizo makubwa ya kipesa.
Nchunga alisema wamekuwa na majadiliano na Manji kwa siku kadhaa kwa lengo la kumshawishi arejeshe ufadhili wake kwa klabu hiyo.
Manji alikuwa mfadhili mkubwa wa Yanga, kabla ya kuamua kujitoa mwanzoni mwa mwaka huu, kufuatia kutofautiana na baadhi ya viongozi na wanachama.
Kwa mujibu wa Nchunga, kujitoa kwa Manji kuliacha pengo kubwa, ikiwa ni pamoja na klabu kushindwa kuwalipa wachezaji mishahara na kulipa gharama zingine.
Alisema tayari wameshamwandikia barua mfadhili huyo kumuomba arejeshe ufadhili wake kwa lengo la kuinusuru klabu hiyo.
“Tayari Manji ameshajibu barua yetu na ameonyesha kukubali kurejea na kuendelea kuisaidia Yanga,”alisema mwenyekiti huyo.
Hata hivyo, Nchunga alisema kabla ya kutoa uamuzi wake, Manji amepanga kukutana na kuzungumza na wajumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo.
“Ukweli ni kwamba, Manji ameweza kuleta maendeleo makubwa Yanga, kama vile kuleta muafaka, kufanya ukarabati wa uwanja na jengo na pia ameonyesha nia ya kujenga jengo letu la mtaa wa Mafia,”alisema.
Akizungumzia kuhusu mipango ya Yanga kutaka kujitegemea, Nchunga alisema wanatarajia kumtumia Manji kwa vile ana uwezo mkubwa na ushawishi kwa wafanya biashara.
Alisema kukaa pembeni kwa mfadhili huyo, ndiko kulikosababisha Wajapan waliotaka kuwekeza Yanga, kuingia mitini. Alisema ana imani iwapo Manji atarejea, Wajapan hao watafufua mpango wao.
Nchunga alisema bado wanaendelea na mipango yao ya kutumia logo ya klabu kujiongezea mapato na kuongeza kuwa, tayari wameshaingia mkataba na Kampuni ya Nsejjere Sports Wear kwa ajili ya kutengeneza bidhaa zenye nembo ya klabu.
Mwenyekiti huyo wa Yanga amewataka wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi kesho uwanja wa ndege wa Julius Nyerere kumpokea Manji atakapokuwa akirejea nchini kutoka nje.
“Naamini kujitokeza kwetu kwa wingi kutamuhamasisha mfadhili huyo akubali mara moja kurejea Yanga, hivyo nawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi,”alisema.
Wakati huo huo, Nchunga amekiri kuwa, Yanga inadaiwa sh. milioni 14 na hoteli ya Regency ya Dar es Salaam kwa ajili ya malazi ya Kocha Sam Timbe kutoka Uganda.
Mwenyekiti huyo amesema, wamepanga kulipa deni hilo siku chache zijazo. Pia amekanusha madai kuwa, Kocha Timbe amegoma kuinoa timu hiyo.

No comments:

Post a Comment