KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 13, 2011

MAGIGE:SIJUTII MAISHA TULIYOLELEWA NA MWALIMU NYERERE





MAGIGE Kambarage Nyerere ni mtoto wa tatu wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere. Anaishi kijiji cha Mwitongo, jirani na ilipo nyumba ya Mwalimu Nyerere huko Butiama, wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara.
Kielimu, Mzee Magige ni injinia wa masuala ya umeme. Pia ni mpenzi sana wa siasa za ndani na nje ya Tanzania. Anafuatilia na kufahamu vyema uendeshaji wa siasa za vyama vingi hapa nchini pamoja na siasa za baadhi ya nchi kubwa duniani, hasa Marekani.
Anaufahamu kinagauaga mfumo wa uendeshaji wa taifa la Marekani, vyama vya Republican, Democratic , baraza la seneti na baraza la wawakilishi. Huwezi kumdanganya kitu kuhusu taifa hilo.
Unapozungumza na mzee huyu, huwezi kukawia kugundua kwamba ni mweledi wa vitu vingi. Sura yake, uzungumzaji wake, pozi zake na hata uchekaji wake, havina tofauti hata chembe na ilivyokuwa kwa Mwalimu Nyerere.
Wakati tulipobisha hodi nyumbani kwake nikiwa na mwenyeji wangu, Julius Kambare Nyerere, mtoto wa kwanza wa Makongoro Nyerere, tulimkuta akiwa ameketi sebuleni, akitazama televisheni.
Awali alionyesha mshangao mkubwa, hasa baada ya macho yake kukutana na ya kwangu kwa vile hakuwa akinifahamu. Hata hivyo, baada ya kumuona Julius, wasiwasi aliokuwa nao ulionekana kumtoka. Akatukaribisha kwenye makochi, tukaketi.
Baada ya kusalimiana naye, nilijitambulisha kwake na kumueleza madhumuni ya safari yangu. Kwa nukta kadhaa alionekana kama vile anayefikiria kitu fulani kisha akaniuliza ningependa kufahamu nini kutoka kwake. Hivyo ndivyo mazungumzo kati yetu yalivyoanza.
Magige anasema hajutii malezi waliyolelewa na baba yao kwa sababu alikuwa rais wa Watanzania wote, hivyo angewalea tofauti na watoto wengine wa Kitanzania, angepoteza uhalali wa kuwa kiongozi wa nchi.
Anasema bila kuwa baba wa familia yako, ni vigumu kuwa baba wa taifa na kwamba watoto wa rais wanapaswa kuwa sawa na watoto wengine wa Kitanzania, haipaswi kuwepo tofauti.
"Hiyo ndiyo sifa ya uongozi, sio unakuwa rais, lakini maisha ya familia yako yanakuwa ya juu kuliko ya unaowaongoza," anasema mzee huyu mcheshi na anayependa kucheka kila anaposisitiza jambo fulani.
Magige anasema sababu hizo pia ndizo zilizomfanya Mwalimu Nyerere asijihusishe na mambo ya biashara ama kujilimbikizia mali kwa vile angepoteza heshima ya kuwa kiongozi wa nchi.
Anasisitiza: "Mzee Nyerere alikuwa baba wa taifa, sasa ajilimbikizie mali ama kufanya biashara ili iweje?"
Kwa mujibu wa Mzee Magige, siku moja Mwalimu Nyerere aliwaeleza kwamba, gavana wa benki kuu wakati huo, Anthony Nyirabu alikuwa akimzidi mshahara, lakini alikuwa na uwezo kila alipokuwa na shida, kumwelekeza afanye chochote anachokitaka.
Anasema kamwe Mwalimu Nyerere hakuwahi kujiwa na wazo la kufikiria njia za pembeni ili kuongeza mapato. Anasema kwake hilo halikuwa jambo rahisi, licha ya ukweli kwamba, rushwa ilikuwa ngumu kuepukika kwa viongozi wengine wa serikali.
"Kiongozi anayeendekeza mambo haya lazima atambue kwamba ipo siku ataondoka madarakani. Na raslimali za nchi lazima ziendelezwe na mwenye mamlaka ya kuzimilikisha ni rais wa nchi, sasa akiweka mbele maslahi yake ni hatari," anasema Mzee Magige.
"Cheo ni dhamana ya nchi. Unaweza kuamrisha mambo ya ajabu na yakafanyika. Ni makosa makubwa kuchagua viongozi wa aina hii kwa sababu watatupeleka pabaya," anaongeza.
"Mkikosea kuchagua kiongozi, hakuna jinsi, itabidi msubiri muda wake wa uongozi umalizike. Tume huru ya uchaguzi haiwezi kusaidia kupatikana kiongozi mzuri. Rais aliyepo madarakani ndiye anayepaswa kuhakikisha na kusimamia uchaguzi ili uwe huru na wa haki," anasisitiza.
Mzee Magige anasema kiongozi wa nchi anapoondoka madarakani, anapaswa kuwa makini kuhusu mtu anayemwachia madaraka na apatikane kwa njia zinazokubalika badala ya kubebwa ama kupendelewa.
Anasema uchaguzi wa nchi kwenda vizuri unasaidia kuhalalisha mamlaka na wananchi wakiridhika, mambo lazima yaende vizuri. Anasema uwezo wa mtu ni muhimu, lakini mchakato wa kumpata kwake lazima uende vizuri.
Anaongeza kuwa, katika kuadhimisha miaka 12 ya kifo cha Baba wa Taifa na miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika, watanzania wanapaswa kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kuweka utaratibu wa kupatikana kwa viongozi watakaoweka mbele zaidi utaifa badala ya maslahi yao binafsi.
Anasema maadhimisho kama haya yanapaswa kuwakumbusha watanzania umuhimu wa viongozi wa serikali kuweka utaifa mbele, kutambuana na kuwatambua watu wao waliowazunguka.
Pamoja na kuwepo kwa vyama vingi vya kisiasa hapa nchini hivi sasa, Mzee Magige anasema bado watanzania wana umoja na mshikamano na kwamba vyama hivyo vimekuwa vikiisaidia serikali kuzinduka toka usingizini.
Anasema baadhi ya vyama vya siasa kama vile CHADEMA, vinaendesha mambo yake kwa kujifunza kupitia CCM, lakini bado vina safari ndefu ya kutwaa madaraka ya kuongoza nchi. Anasema vyama hivyo pia vinaisaidia CCM kujirekebisha.
"Wapinzani wanaweza kuisumbua CCM kama watakuwa tayari kuungana, vinginvyo bado sana," anasema Mzee Magige.
Hata hivyo, Mzee Magige ameitahadharisha CCM kuwa, inapaswa kuendesha mambo yake kwa uwazi na kuchukua maamuzi mazito badala ya kuwabeba viongozi wake wanaokiuka miiko ya uongozi.
Anasema CCM inapaswa kujifunza kupitia vyama vingine vya siasa vya nchi jirani kama vile Kenya, ambavyo vimepoteza mwelekeo kutokana na kushindwa kukidhi matakwa ya wananchi na pia viongozi wake kuweka mbele zaidi maslahi yao binafsi.
"Chama kinajengwa kwa umoja na mshikamano. Mapungufu yaliyopo sasa yaondoshwe. Viongozi na wanachama wasiogope kuelezana ukweli. Tusitoe nafasi kwa rais wa nchi kudharauliwa, rais anapaswa kuheshimika,"anasema.
"Nguvu ya rais ni chama imara. Kinapaswa kuwa na nguvu na mshikamano. Viongozi wake wanapaswa kuwa na umoja, mwonekano na mwelekeo wa kitaifa. Chama kikiwa legelege, serikali nayo itakuwa legelege,"anaongeza.
Kwa mujibu wa Mzee Magige, tabia ni imani na kwamba kukiwa na umoja, hata yakiwepo makabila zaidi ya 100, hakuna kinachoweza kuwatenganisha.
Mzee huyo anasema pia kuwa, vyombo vya habari vikitumika vizuri, vinaweza kusaidia kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa watanzania, lakini mawaidha yanayotolewa sasa na vyombo hivyo kuhusu siasa, yanatishia amani, umoja na mshikamano wa nchi.
Tofauti na msimamo wa serikali kwamba haina dini, mtazamo wa Mzee Magige ni tofauti. Anasema kauli hiyo si sahihi kwa sababu bila dini, si rahisi kuwepo kwa serikali na kwamba vitu hivyo viwili vinategemeana. Anasema dini ndizo zinazoifanya serikali iwepo madarakani.
"Bila mapadri, watu hawawezi kumkumbuka Yesu. Vivyo hivyo, bila mashehe, watu hawawezi kumkumbuka Mtume Muhammad.

1 comment:

  1. BUSARA NA HEKIMA ZA MWALIMU NYERERE, AMBAYE NI TUZO YA WATANZANIA NA WAAFRIKA WOTE, YATADUMU MILELE, YAKIENEA ZAIDI NA KUSABABISHA MAMBO MAZURI ZAIDI KWA MANUFAA YA JAMII ZETU ZA KIAFRIKA NA DUNIA NZIMA SASA NA SIKU ZIJAZO. Mola amlaze mahali pema peponi shujaa huyu wa Afrika.

    ReplyDelete