KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 13, 2011

MAKOCHA WAIPONDA TAIFA STARS

Kutolewa mapema kwa Taifa Stars katika michuano hiyo, kumeifanya ishindwe kufuzu kucheza fainali hizo kwa mara ya tatu katika kipindi cha miaka sita iliyopita.
Taifa Stars pia ilishindwa kufuzu kucheza fainali za mwaka 2008 zilizofanyika nchini Afrika Kusini na zile za mwaka 2010 zilizofanyika Ghana.
Matokeo hayo yaliifanya Taifa Stars ishike mkia katika kundi D kwa kumaliza mechi zake ikiwa na pointi tano. Morocco imeshika nafasi ya kwanza na kufuzu kucheza fainali hizo, ikifuatiwa na Jamhuri ya Afrika ya Kati na Algeria.
Wakizungumzia mwenendo wa timu hiyo katika michuano ya kimataifa, baadhi ya makocha wa soka nchini wamesema haufurahishi kwa vile imeshindwa kuwapa raha mashabiki wake.
Makocha hao wametaja sababu kadhaa zinazoifanya timu hiyo itolewe mapema katika michuano ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na wachezaji kukosa morari na uwezo mdogo wa Kocha Jan Poulsen.
JOSEPH KANAKAMFUMU
Kocha wa zamani wa Polisi Dodoma, Joseph Kanakamfumu amesema, Taifa Stars imeshindwa kuwika kutokana na mambo kadhaa ya msingi, ikiwa ni pamoja na kushuka kwa morari ya wachezaji.
Kanakamfumu amesema, tangu kuondoka kwa kocha wa zamani wa timu hiyo, Marcio Maximo, timu imekosa mwelekeo na wachezaji hawana ari.
Kocha huyo amesema, awali wachezaji wa timu hiyo pamoja na mashabiki walikuwa wakipata hamasa kubwa kutoka kwa Maximo ndio sababu ilipata mafanikio.
“Serikali nayo ilijitahidi kadri ilivyoweza kuipeleka timu nje kuweka kambi na kuwatembelea wachezaji mara kwa mara kuwahamasisha, lakini hayo yote hayafanyiki hivi sasa,”alisema.
Alisema uamuzi wa viongozi wa serikali kuitembelea timu hiyo, ulichangia kwa kiasi kikubwa kuwapa hamasa wachezaji na kuwafanya wajione wanathaminiwa.
“Katika mazingira hayo, wachezaji walikuwa na kila sababu ya kucheza kwa kujituma na kuonyesha mapenzi kwa timu yao, lakini sasa mambo ni tofauti,”alisema.
Mbali na wachezaji kuvutiwa na timu hiyo, Kanakamfumu alisema hamasa iliyokuwa ikitolewa na viongozi wa serikali na wadhamini ilisababisha ushindani mkubwa wa namba kwa wachezaji kutokana na zawadi walizokuwa wakipewa.
Kanakamfumu alisema inashangaza kuona kuwa, hivi sasa baadhi ya wachezaji wakiitwa kwenye timu hiyo, hupatwa na hofu na kutoa visingizio mbalimbali kwa lengo la kuikwepa.
Kocha huyo pia alilaumu kukosekana kwa mfumo unaoeleweka wa uchezaji, tatizo ambalo alisema linachangiwa kwa kiasi kikubwa na mbinu za ufundishaji.
JOHN TEGETE
Kocha Mkuu wa Toto African na timu ya mkoa wa Mwanza, John Tegete amesema tatizo kubwa analoliona kwa timu hiyo ni uteuzi mbovu wa wachezaji na watanzania kutaka mafanikio ya haraka.
Tegete alisema wachezaji wengi wanaoteuliwa kwenye kikosi hicho wanatoka timu za Simba na Yanga, hata kama uwezo wao ni mdogo ama umeshuka.
Alisema Tanzania inayo hazina kubwa ya wachezaji wenye vipaji, lakini tatizo kubwa lililopo ni kushindwa kubaini vipaji vyao na kuwaendeleza.
Kocha huyo alisema licha ya kuwepo kwa michuano ya vijana na timu za taifa za vijana wa umri mbalimbali, wachezaji hao hawaandaliwi vyema kwa ajili ya kuitumikia Taifa Stars miaka ijayo.
Akitoa mfano, Tegete alisema wakati wa Maximo, alitilia mkazo kuendeleza vipaji vya vijana na kuwapa nafasi kwenye kikosi cha Taifa na hivyo kuwakomaza mapema.
“Maximo alikuwa na sifa zote za kuwa kocha wa Taifa Stars kwa sababu aliwaendeleza vijana, alijenga nidhamu katika timu, wachezaji walijituma na pia alikuwa karibu na wadau wa soka ili kujua nini wanachokitaka,”alisema.
“Lakini tangu kuja kwa Poulsen, hajaweza kuibua mchezaji yeyote kutoka timu za vijana kama alivyokuwa mwenzake, aliyetangulia. Hili ni tatizo,”aliongeza.
Tegete amewataka wadau wa soka nchini kumpa ushirikiano kocha huyo ili aweze kutimiza malengo yake, ikiwa ni pamoja na kupewa nafasi ya kuwatumia wachezaji chipukizi kwenye kikosi chake.
JOHN SIMKOKO
Kocha Mkuu wa Polisi Morogoro, John Simkoko amesema kushindwa kwa Taifa Stars kucheza fainali za 2012, kumewasikitisha wadau wengi wa mchezo huo nchini, lakini hakuna anayepaswa kulaumiwa.
Simkoko amesema jambo la msingi kwa sasa ni Kocha Poulsen kuwasilisha ripoti ya timu yake kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili iweze kufanyiwakazi.
“Ripoti ya Poulsen ndiyo itakayotoa mwelekeo kuhusu nini kimeisibu timu yake na hatua gani zichukuliwe kurekebisha hali hiyo, lakini kwa sasa hatupaswi kulaumiana,”alisema.
Simkoko amewataka viongozi wa klabu za ligi kuu, kuendelea kutilia mkazo timu za vijana kwa lengo la kuibua vipaji vingi zaidi vya soka.
Alisema iwapo klabu za ligi kuu zitaendelea kuwekeza kwenye timu za vijana, itakuwa rahisi kwa vipaji vingi zaidi kuibuliwa na pia kupatikana kwa wachezaji wengi wa timu za taifa za umri mbalimbali.
“Nina imani kupitia mashindano mbalimbali ya vijana, tunaweza kupata wachezaji, ambao wakilelewa vizuri, watakuwa hazina kubwa kwa Taifa Stars miaka ijayo,”alisema.
CHARLES KILINDA
Kocha Mkuu wa JKT Ruvu, Charles Kilinda amesema uteuzi wa timu hiyo unapaswa kutazamwa upya kwa sababu umeegemea zaidi klabu za Simba na Yanga.
Kilinda amesema pia kuwa, baadhi ya wachezaji wanaoteuliwa kuichezea timu hiyo, uwezo wao ni mdogo na wanapaswa kuachwa.
“Nashindwa kuelewa kwa nini wachezaji hawa wamekuwa wakiitwa mara kwa mara wakati kwenye klabu zao wanasugua benchi,”alisema kocha huyo.
Kilinda alisema haiwezekani kwa mchezaji anayewekwa benchi kwenye klabu yake kupewa nafasi kwenye timu ya taifa kwa sababu hawezi kuwa na msaada wowote.
Amelitaja tatizo lingine linalochangia kuifanya timu hiyo ivurunde kuwa ni baadhi ya wachezaji kushindwa kujitambua na kufahamu wajibu wao.
Kocha huyo pia alilaumu tabia ya baadhi ya wachezaji kuchukiana bila sababu za msingi na hivyo kushindwa kuwa na umoja na ushirikiano ndani na nje ya uwanja.
JAMHURI KIHWELO
Kocha Mkuu wa Coastal Union, Jamhuri Kihwelo amesema haoni kama ni sahihi kwa mashabiki kuwatupia lawama wachezaji wa timu hiyo kwa vile hawana makosa.
Kocha huyo maarufu kwa jina la Julio amesema, katika soka kuna kushinda, kushindwa na kutoka sare, hivyo mashabiki wanapaswa kuyakubali matokeo hayo.
“Mimi naamini wachezaji wetu wamekuwa wakicheza kwa kujituma sana, hivyo yaliyopita si ndwele, tugange yajayo, tuache malumbano na kulaumiana, ”alisema.
Julio alisema ni vyema Poulsen aendelee kupewa nafasi ya kukifanyia marekebisho kikosi hicho ili kiwe na mwelekeo anaoutaka badala ya kumlaumu.
Kocha huyo alisema ni vyema pia kwa TFF kuifanyiakazi ripoti ya kocha huyo ili iweze kutafuta kiini cha timu hiyo kuvurunda katika michuano ya kimataifa.
Alisema kuwashutumu wachezaji na kocha wao kunaweza kuwafanya wavunjike nguvu na hivyo kusababisha malengo ya Tanzania kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014 kushindwa kutimia.

No comments:

Post a Comment