KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 13, 2011

MWALIMU NYERERE HAKUPENDA KUWA TAJIRI-MAHUNDA





UKUTANAPO na Mzee Josephat Mahunda Nyerere kwa mara ya kwanza, huwezi kuamini kuwa ni mdogo wake, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere. Sura zao hazifanani sana kama ilivyokuwa kwa marehemu Joseph Nyerere ama watoto wengine wa Chifu Burito Nyerere.
Ni mrefu na mwembamba. Uso wake si mpana na rangi ya sura yake imechanganyika weusi na weupe kidogo. Pengine ni kwa sababu ya umri wake. Tofauti ya umri kati yake na Mwalimu Nyerere ilikuwa miaka sita.
Siku tulipokutana, alikuwa amevalia suruali ya bluu na shati jeupe la mikono mirefu. Chini alivalia viatu vyeusi vya ngozi. Nywele zake alizichana kwa mtindo unaofanana na ule aliokuwa akitumia Rais wa zamani wa Uganda, hayati Milton Obote.
Alikuwa ameketi kwenye kigoda kidogo, chini ya mti, mbele tu kidogo ya nyumba yake. Pembeni yake walikuwepo watoto wadogo watatu, mmoja akiwa anapika ugali kwa ajili ya chakula chao cha mchana. Nilikuja kubaini baadaye kuwa, watoto hao ni wajukuu zake.
Nyumba anayoishi Mzee Josephat ni ya kawaida. Ni nyumba ndogo iliyojengwa kwa mawe, yenye vyumba visivyozidi vinne. Nyumba hiyo ipo kando ya geti la kuingilia nyumbani kwa Mwalimu Nyerere eneo la Mwitongo.
Josephat ndiye mtoto pekee wa Chifu Burito Nyerere aliyebaki hai hadi sasa. Alizaliwa mwaka 1928 wakati Baba wa Taifa alizaliwa mwaka 1922. Yeye na Mwalimu Nyerere wamechangia baba, lakini mama zao ni tofauti.
Sura ya Mzee Josephat haionyeshi furaha hata chembe. Ni mtu anayeonekana kujawa na mawazo muda wote. Anaonyesha dhahiri kukosa kitu fulani adimu na muhimu katika maisha yake. Je, ni kwa nini mzee huyu yupo hivi? Na ni kitu gani kinachomkera na kumfanya asiwe na furaha? Hayo ni baadhi tu ya maswali niliyoanza kujiuliza wakati huo huku nikiwa na hamu kubwa ya kupata majibu kutoka kwake.
Mzee Josephat hafichi kusema ukweli. Anasema wazi kuwa, kifo cha Mwalimu Nyerere kimeacha ukiwa mkubwa kwa familia yake kwa sababu alikuwa ndiye baba wa familia yote.
"Kwa sasa, familia ya Mwalimu Nyerere inaishi kwa shida. Alipokuwa hai, alikuwa ameshikilia kila kitu. Alikuwa kichwa cha familia,"anasema mzee huyo mwenye umri wa miaka 83 hivi sasa.
"Hivi sasa hatupati huduma kubwa kutoka serikalini. Tunaishi kwa kujitegemea sisi wenyewe. Kiongozi wetu tuliyemzoea hayupo tena, tumebaki wakiwa,"anasema.
Mzee huyu anasema binafsi alikuwa karibu sana na Mwalimu Nyerere wakati akiwa madarakani na hata baada ya kustaafu urais na kila alipokuwa akienda Butiama kwa mapumziko, alikuwa akipenda kumtembelea nyumbani kwake.
"Maisha aliyokuwa akiishi Mwalimu Nyerere yalikuwa ya ajabu. Yalikuwa maisha ya kawaida. Hakuwa akipenda kujiweka kimbelembele. Ndivyo hulka yake ilivyokuwa. Hakuna anayefahamu ni kwa nini alikuwa mtu wa aina hiyo," anasema.
"Hata maisha ya watoto wake yalikuwa ya kawaida. Yalikuwa sawa na maisha ya watoto wengine wa Tanzania. Hakupenda kuwadekeza watoto wake. Pia hakupenda kujilimbikizia mali. Hiyo ilikuwa sumu kwake.
"Kusema nataka niishi hivi au vile (kifahari), jambo hilo halikuwepo kabisa kichwani mwake. Alikuwa mtu wa ajabu. Hakuwahi kuwa na mradi wowote ama kufanya biashara. Alitegemea zaidi nafasi yake ya urais na kilimo,"anasema.
"Na hata alipokuwa akirejea Butiama kwa mapumziko, shughuli yake kubwa ilikuwa kilimo. Alipenda sana kulima. Alikuwa na shamba kubwa sana," anaongeza mzee huyo mwenye watoto 18.
Mbali na kulima, Josephat anasema Mwalimu Nyerere alikuwa akipenda kushiriki kucheza bao na kujumuika na wazee kwa ajili ya kuzungumza mambo mbalimbali. Pia alipenda kupumzika katika baadhi ya maeneo ya nje ya nyumba yake.
Mzee huyo anasema, tangu akiwa mdogo, Mwalimu Nyerere alikuwa akipenda sana kusoma. Anasema aliondoka Butiama akiwa na umri wa miaka 12 na kwenda kusoma shule ya msingi ya Mwisenge iliyopo Musoma.
Anasema baada ya kumaliza masomo yake, Mwalimu Nyerere alikuwa na ndoto kubwa ya kupigania uhuru wa Tanganyika wakati huo kwa sababu hakuwa akipenda kuona watanzania wakiendelea kukandamizwa na kunyonywa na wakoloni. Hata hivyo, mzee huyo hakuwa akivutiwa na mambo ya siasa. Wala hakushiriki kupigania uhuru wa Tanganyika. Anasema hakuwa akivutiwa na mambo hayo katika maisha yake.
Kwa mujibu wa Josephat, Mwalimu Nyerere na Mama Maria Nyerere walifanikiwa kupata watoto wanane. Aliwataja kwa majina kuanzia wa kwanza kuwa ni Andrew, Watiku, Magige, John, Makongoro, Madaraka, Rosemary na Pauletta.
Anasema kati ya watoto hao wanane, ni watatu pekee waliowahi kujitumbukiza katika ulingo wa siasa. Hao ni Makongoro, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara, Rosemary, ambaye aliwahi kuwa mbunge wa viti maalumu na Magige.
Mzee Josephat hapendi mambo ya siasa, hivyo hataki kabisa kuzungumzia masuala ya siasa ya vyama vingi hapa nchini na pia mustakabali wa taifa hili baada ya kufariki kwa mwasisi wake, Mwalimu Nyerere.
Vilevile hapendi kuzungumzia maisha ya watu wengine ama jamii inayomzunguka. Mapenzi yake kwa kaka yake, Mwalimu Nyerere yalikuwa makubwa pengine kuliko kitu chochote kingine katika maisha yake. Simanzi aliyonayo kwa kumkosa haielezeki.
Isipokuwa ametoa mwito maalumu kwa wananchi wa Tanzania, ambapo amewataka kudumisha amani, umoja na mshikamano, mambo yaliyoasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Anasema hiyo ndiyo njia pekee nzuri ya kumuenzi na kuonyesha heshima na upendo kwake.

No comments:

Post a Comment