KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, October 13, 2011

MAMA MARIA NYERERE ALONGA




SWALI: Oktoba 14 mwaka huu, Tanzania itaadhimisha miaka 12 tangu kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Unapenda kuwaeleza nini Watanzania kuhusu siku hii?

JIBU: Nashukuru sana kwa kuniuliza swali hili, japokuwa majibu yake hayatakuwa kama unavyotarajia, lakini nitajitahidi kadri ninavyoweza. Cha kuwaeleza kwa upande wangu ni vigumu kwa sababu ni matukio yanayoonekana katika vyombo vya habari na wanasoma katika vyombo vya habari na yanatokea katika mawazo mbalimbali ya watu na mazungumzo mitaani. Labda la kuwaeleza kwa upande wangu, ningesema kwamba tunashukuru hii miaka 50 ya uhuru, ni nchi chache ambazo zimeweza kudumisha uhuru na amani kwa muda mrefu kama Tanzania. Nchi zingine zinagombana zenyewe kwa zenyewe kwa kipindi kirefu. Kwa maoni yangu hili jambo ni la kutilia mkazo.
SWALI: Unadhani inatosha kwa Watanzania kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kuwasha Mwenge Butiama ama kuandaa makongamano?
JIBU: Hiyo nayo ni sehemu mojawapo. Naweza kusema huko nako ni sehemu ya kumuenzi Mwalimu Nyerere. Kwenye makongamano ndiko ambako watu wanaweza kuzungumzia tulikotoka, tulipo na tunapokwenda, wanajadiliana, wanasaidiana mawazo. Hivi sasa kuna vipindi vimendaliwa TBC vya miaka 50 ya uhuru, vinamwonyesha rais wa kwanza, wa pili na wa tatu. Sidhani kama kuna ubaya kumuenzi Mwalimu kwa njia hizi.
SWALI: Unayaonaje maisha bila ya kuwa na Mwalimu Nyerere?
JIBU: Kwa maisha ya kawaida, nashukuru kwamba taifa linatuhudumia vizuri. Ninachokikosa ni kutokuwa karibu na mtu niliyemzoea, kila wakati anawaletea jambo jipya. Si kwamba tangu ameondoka hatujafanya mambo mapya, hapana, kiubinadamu tunasema, mwalimu angekuwepo, tungefikia ngazi hii, labda hilo ndilo la maana sana.
SWALI: Ni changamoto zipi ulizowahi kukumbana nazo ukiwa mke wa rais?
JIBU: Kwa bahati nzuri nimekuwa mke wa kwanza wa rais na katika nchi masikini, halafu yenye mapungufu ya elimu na kila hali, ingawa utajiri wa nchi ulikuwa mkubwa, lakini tulikuwa tunaona hakuna kitu kutokana na elimu tuliyokuwa nayo kwa hiyo tulikuwa tunashughulika tu na vikundi vya akina mama, lakini hatukuwa na uwezo mkubwa wa kuweza kuwaendeleza ndugu zetu kama wanavyofanya akina mama hawa wa viongozi wetu hawa wawili, Mama Anna Mkapa na Mama Salma Kikwete.
SWALI: Unadhani ni kwa nini Mwalimu Nyerere aliwalea watoto wake sawa na watoto wengine wa Kitanzania wakati ambapo kwa madaraka aliyokuwa nayo, angeweza kuwapeleka nje kusoma ama wangeishi kifahari sana?
JIBU: Kwa miaka yote niliyoishi naye, alikuwa anasema sisi ni watoto wa masikini, ndiyo misamiati aliyokuwa anatumia. Tumepata bahati tumetumwa na taifa kuongoza, si kwamba sisi ni wafalme, kwa hiyo tulipaswa kuwaona watoto wetu wapo katika ngazi sawa na wengine. Na hata angependa kuwapeleka kusoma nje, hakukuwa na pesa za kuwapeleka huko. Katika awamu ya kwanza, hata pesa za kuendesha serikali ilikuwa matatizo, hivyo hatukuwa na mawazo ya kuwasomesha watoto wetu nje. Tuliona ni vema wapate elimu ya kawaida kama watoto wengine.
SWALI: Ni kwa nini Mwalimu Nyerere hakupenda kabisa kujihusisha na biashara ama kujilimbikizia mali katika kipindi chote alichokuwa madarakani na hata baada ya kustaafu?
JIBU: Kama nilivyojibu swali lililotangulia, pesa hazikuwepo. Hata angetaka kujilimbikizia mali, asingeweza kwa sababu hakukuwa na pesa. Mwalimu alikuwa na majukumu mengi mazito. Mbali ya kuongoza nchi, alikuwa na jukumu la kuhakikisha nchi zote zilizokuwa kusini mwa Afrika zinapata uhuru.Pia tulikuwa na jukumu zito la kulinda mipaka yetu. Pesa kidogo zilizokuwepo wakati huo zilitumika kusomesha madaktari na wataalamu wengine mbalimbali kwa ajili ya kufanyakazi hizo hapa nchini na wakati mwingine tuliomba misaada kwa nchi zilizoendelea, zinawachukua vijana wetu na kwenda kuwasomesha nje.
SWALI: Kwa nini wewe binafsi katika kipindi chote cha uongozi wa Mwalimu Nyerere hukutaka kuanzisha taasisi ya mke wa rais kama ilivyo kwa wake wengine wa marais duniani?
JIBU: Wakati ule na sasa ni tofauti. Nilifanyakazi nyingi za kijamii, lakini hazikuweza kuonekana. Kwa mfano, nilishiriki kuanzisha vijiji vya mfano, lakini kazi hizo kwa wakati ule zilikuwa hazitangazwi. Hatukuona kama kulikuwa na faida kuzitangaza. Zilikuwa hazionekani kama nguo dukani.
Tulipopata uhuru, shabaha yetu ya kwanza ilikuwa tujitambue. Na mtu hawezi kujitambua bila kujitegemea. Hilo lilikuwa jukumu letu la kwanza. Ilikuwa ni mazoea wakati ule kumuona mwanamke hawezi kufanyakazi ya aina fulani ama kitu fulani labda mpaka awe waziri. Labda angekwenda vitani akashika bunduki, angeweza kuonekana.
Lakini sasa ni tofauti. Mama Anna Mkapa alikuwa na taasisi yake, amefanyakazi nyingi za kuwainua akina mama na kuwapatia ajira, Mama Salma Kikwete naye anayo taasisi yake, anatoa misaada kwa wanawake na watoto ili waweze kujitegemea, wanasema ukimwelimisha mwanamke, umeelimisha taifa zima na wote wawili wanapata misaada mingi kutoka nje, wamejenge shule, kazi zao zinaonekana kwa sababu zinatangazwa kwenye vyombo vya habari tofauti na wakati ule.
SWALI: Ni jambo lipi lililowahi kumchukiza sana Mwalimu Nyerere katika maisha yake?
JIBU: Swali hilo labda angekuwepo mwenyewe ungemuuliza. Lakini unafikiri ile vita ya Kagera haikumchukiza. Nadhani ilimchukiza sana. Hata matamshi yake kuhusu vita ile yanadhihirisha hilo. Alisema uwezo wa kumpiga tunao, sababu ya kumpiga tunayo na nia ya kumpiga tunayo. SWALI: Na ni tukio lipi, ambalo liliwahi kumfurahisha Mwalimu Nyerere akiwa madarakani au hata baada ya kustaafu?
JIBI: Nadhani ni lile la kumshinda Iddi Amini katika vita vya Kagera.
SWALI: Wewe binafsi ni tukio lipi, ambalo lilikufurahisha sana katika maisha yako?
JIBU: Ni ile siku niliposhuhudia bendera ya Uingereza ikiteremshwa na kupandishwa bendera ya Tanzania. Japokuwa hatukuwa na uelewa wa kutosha, lakini kitendo hicho kilinifurahisha mno.
SWALI: Na ni tukio lipi ambalo lilikuhuzunisha sana katika maisha yako?
JIBU: Ni ule ujinga wangu kwamba Mungu hakustahili kumchukua Mwalimu Nyerere mapema. Hili lilinisikitisha sana kwa sababu ni ujinga kutokubali kwamba Mwenyezi Mungu ana mipango yake.
SWALI: Tanzania Bara inaelekea kutimiza miaka 50 ya Uhuru. Wapo wanasiasa wanaobeza kwamba hakuna chochote kilichofanyika kuiletea nchi maendeleo. Unasemaje kuhusu kauli hizi?
JIBU: Hapa kuna mawili. Lakini tatizo ni msamiati na inategemea ni lugha gani inayotumika. Tungestahili kusema tumepiga hatua, sasa hao wanaosema hakuna kilichofanyika, sijui utabishana nao kitu gani. Kama mtu anasema haoni chochote wakati wewe unaona kuna mabadiliko, ni bora kumwacha kama alivyo. Kwangu mimi nasema tumepiga hatua kubwa sana. Kama ni mapungufu, basi yapo machache sana.
SWALI: Una maoni gani kuhusu suasa ya vyama vingi hapa nchini. Unadhani vinaisaidia serikali katika kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwa watanzania?
JIBU: Ninachoweza kusema ni kwamba, kwa kiasi fulani ama tuseme robo moja wanaisaidia, lakini katika robo zingine tatu zilizobaki wanayumba. Wao wanafikiri wakishika madaraka, kila kitu kitakwenda vizuri ama kuwa sawa. Wakati wa kampeni utawasikia wakisema tutaleta hiki na kile wakati wanajua wazi kwamba haiwezekani. Si kwamba hawaelewi hilo.
SWALI: Nini maoni yako kuhusu matukio ya vurugu, ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani?
JIBU: Mi nadhani haya yote yanatokea kwa sababu ya watu kupewa vijisenti kidogo, sina hakika, lakini nasikia ndio hivyo. Mbona wanapokuwa kwenye michezo hawapigani? Kwa nini wanapigana kwenye siasa? Na kwa nini mtu akubali kupewa pesa ili afanye fujo? Unakwenda kubomoa nyumba ya watu, hapa kuna mawili, na wewe unaweza kuuawa. Hata familia itanyamaza, haiwezi kusema alitumwa na fulani.
SWALI: Tanzania imetoa wanawake wengi katika ngazi za uongozi kitaifa na kimataifa. Unadhani wakati umefika kwa Tanzania kuwa na rais mwanamke?
JIBU: Mimi naona tumechelewa kwa sababu mwamko hivi sasa ni mkubwa, wanawake wengi wana elimu ya kutosha na wana uzoefu wa uongozi. Kwa mfano, marehemu Bibi Titi Mohamed angeweza kuwa rais wakati ule, kwa sasa sidhani kama hilo ni jambo la ajabu, si kama miaka ya zamani. Akinamama wasibweteke. Uwezo tunao.

SWALI: Unatoa mwito gani kwa wanawake wa Tanzania, hasa wale waliojitosa katika masuala ya siasa ama kupewa nafasi za juu za uongozi?
JIBU: Kwa kweli tunapaswa kuwapongeza. Bahati nzuri nimekuwa nikifuatilia sana habari zao na wengine huwa wakija Butiama kunitembelea. Baadhi yao wamepata nafasi hizo kwa shida. Mawazo yao ni mazuri. Nawaomba waongeze bidii kwa sababu wanafanyakazi kubwa.

No comments:

Post a Comment