'
Sunday, May 9, 2010
RAGE BOSI MPYA SIMBA
ALIYEKUWA Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ismail Rage amechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa klabu ya Simba.
Rage alichaguliwa kushika wadhifa huo juzi baada ya kumbwaga Hassan Othman 'Hassanoo' katika uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa bwalo la maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.
Katika uchaguzi huo, Rage alipata kura 785 wakati Hassanoo alipata kura 435. Idadi ya kura zilizopigwa ni 1, 437 wakati kura 127 ziliharibika.
Nafasi ya makamu mwenyekiti ilichukuliwa na Godfrey Nyange 'Kaburu, ambaye hakuwa na mpinzani. Alipata kura 1,359 sawa na asilimia 80.5.
Waliochaguliwa kuunda safu ya wajumbe wa kamati ya utendaji, idadi ya kura zikiwa kwenye mabano ni Joseph Kinesi (991), Mkwabi Sued (823), Damian Manembe (725), Saidi Pamba (793), Francis Waya (695) na Ibrahim Masoud (638).
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Rage alisema huu ni wakati mwafaka kwa wana-Simba kuendeleza amani na utulivu uliopo klabuni. Pia aliwataka wanachama kuungana na kuijenga upya Simba.
Rage alisema jukumu lililo mbele yake ni zito kwa sababu anapaswa kuhakikisha Simba inapata maendeleo makubwa zaidi kuanzia klabu hadi kwenye timu, lengo likiwa ni kuweka historia mpya.
Alisema kutokana na ukongwe wake, Simba inapaswa kuwa klabu ya kupigiwa mfano katika mashindano ya kimataifa na kurejesha rekodi yake iliyopotea muda mrefu.
Rage alisema kinachotakiwa kwa sasa ni viongozi na wanachama kushirikiana, kuheshimiana na kutambua mipaka ya kazi, jambo ambalo litaifanya klabu hiyo kuwa na taratibu nzuri za uongozi.
Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Hassan Dalali alisema anajivunia kwamba anaondoka Simba akiwa ameiacha klabu ikiwa na amani na utulivu. Alisema angependa kuona mambo hayo yanaendelezwa katika kipindi cha uongozi mpya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment