KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 14, 2010

Makocha wapya Taifa Stars wafanyiwa usaili kwa siri

MAKOCHA watano waliopitishwa kuwania nafasi ya kuinoa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars wamewasili nchini kwa ajili ya kufanyiwa usaili.

Habari zilizonaswa na Burudani jana zimeeleza kuwa, makocha hao waliwasili nchini juzi tayari kwa ajili ya kufanyiwa usaili huo kabla ya kuteuliwa kocha atakayerithi mikoba ya kocha wa sasa, Marcio Maximo.

Usaili wa makocha hao ulianza kufanyika juzi katika hoteli ya New Africa, chini ya usimamizi wa viongozi wa sekretariati ya Shirikikisho la Soka Tanzania (TFF), ikiongozwa na Mkurugenzi wa Ufundi,
Sunday Kayuni.

Makocha waliofanyiwa usaili huo wanatoka katika nchi za Bulgaria, Serbia, Denmark, Poland na Ureno.

Juhudi za gazeti hili kupata majina ya makocha hao zilishindwa kufanikiwa kwa vile usaili huo ulifanyika kwa siri kubwa na chini ya ulinzi na haikuruhusiwa kwa waandishi wa habari kuingia kwenye ukumbi wa hoteli hiyo.

Hata hivyo, habari kutoka ndani ya TFF zimeeleza kuwa, makocha hao watafanyiwa usaili kwa muda wa siku tatu kabla ya kutangazwa kwa mshindi.

Chanzo chetu cha habari kilidokeza kuwa, usaili wa makocha hao umefanywa kuwa siri kubwa ili kuepuka kuvuja kwa majina yao kabla ya kuchaguliwa mmoja wao, atakayefaulu usaili huo.

Imeelezwa kuwa, mara baada ya usaili huo, jina la kocha atakayepitishwa litatangazwa kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Maximo, ambaye anamaliza mkataba wake Julai 28 mwaka huu.

Katika hatua nyingine, timu ya soka ya taifa ya wanawake, Twiga Stars inatarajiwa kuingia kambini leo kujiandaa kwa pambano lake dhidi ya Eritrea.

Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Twiga Stars itaweka kambi kwenye hoteli ya FNG Annex iliyopo Msasani.

Twiga Stars inatarajiwa kuvaana na Eritrea katika pambano la awali la raundi ya pili ya michuano ya Afrika, litakalochezwa Mei 22 mwaka huu mjini Dar es Salaam kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye mjini Asmara.

No comments:

Post a Comment