KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 20, 2010

Simba yadundwa Rwanda

Na Charles Mganga, Kigali

SIMBA jana ilijiweka kwenye nafasi ngumu ya kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Kagame baada ya kuchapwa bao 1-0 na Sofapaka katika mechi ya kundi C iliyochezwa kwenye uwanja wa Nyamirongo mjini hapa.

Kwa matokeo hayo, Sofapaka imefuzu kucheza robo fainali kwa kuongoza kundi hilo, ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi mbili, ikifuatiwa na Simba yenye pointi tatu. Mechi nyingine ya kundi hili ilitarajiwa kuchezwa jana jioni kati ya URA ya Uganda na Atraco ya Rwanda.

Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo, Simba itacheza mechi yake ya mwisho kesho mchana kwa kumenyana na URA. Iwapo itashinda, itakuwa na nafasi kubwa ya kusonga mbele, lakini kwa kutegemea matokeo ya mechi kati ya Sofapaka na Atraco.

Mchezaji wa zamani wa Yanga, anayechezea Sofapaka, John Barasa
ndiye aliyeiua Simba baada ya kufunga bao hilo na la pekee dakika ya 32 kwa shuti kali lililomshinda kipa Juma Kaseja.

Barasa pia alizitikisa nyavu za Simba dakika ya 16 baada ya kuitoka ngome yake na kufumua shuti lililotinga wavuni, lakini mwamuzi
Mohamed Farah alilikataa kwa madai kuwa mfungaji aliotea.

Sofapaka iliendeleza mshambulizi langoni mwa Simba na kuifanya ngome ya timu hiyo, iliyokuwa chini ya beki Joseph Owino kufanya kazi ya ziada kuokoa mipira ya hatari. Kipa Juma Kaseja mara kadhaa alilazimika kuokoa mashuti ya washambuliaji wa timu pinzani.

Katika dakika 45 za mwanzo, Simba ilizidiwa maarifa na Sofapaka kutokana na sehemu ya kiungo, iliyokuwa chini ya Abdulrahim Humoud na Jerry Santo kuruhusu wapinzani wao kutawala eneo la katikati ya uwanja.

Licha ya kufungwa bao hilo, Simba ilionyesha uhai katika safu ya ushambuliaji, ambapo Mussa Hassan 'Mgosi', Robert Ssentongo na Uhuru Selemani walikuwa tishio kwa kipa, Obungu Wilson.

Kipindi cha pili kilitawaliwa zaidi na Sofapaka, ambayo ilionyesha kiwango cha juu na kuipa wakati mgumu Simba, iliyoshindwa kusawazisha.

Simba: Juma Kaseja, Juma Jabu, Kelvin Yondani, Juma Nyoso, Joseph Owino, Abdulhalim Humoud, Jerry Santo, Uhuru Selemani/Nico Nyagawa, Ramadhani Chombo, Robert Ssentongo na Mussa Mgosi.

Sofapaka: Obungu Wilson, Edger Ochieng, Rashid Idrisa, Anthony Kimani, Hussein Abdulrazak, John Barasa, Hugo Nzoka, Humphrey Ochieng, Bob Mugalia, Thomas Wanyama na James Situma.

No comments:

Post a Comment