KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 6, 2010

BYE BYE BENITEZ, ZOLA MANCINI WAKALIA KUTI KAVU

RAFAEL Benitez
ROBERTO MANCINI

GIANFRANCO Zola

LONDON, England
KOCHA Mkuu wa Liverpool, Rafael Benitez amedhihirisha wazi kuwa ataihama klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu baada ya kuishutumu bodi ya wakurugenzi kwa kushindwa kutimiza ahadi walizompa.
Akizungumza mara baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 2-0 na Chelsea mwishoni mwa wiki iliyopita, Benitez alisema ahadi nzuri alizopewa na viongozi wa Liverpool ndizo zilizomshawishi atie saini mkataba mpya mwaka jana.
Benitez alisema huenda mechi kati ya Liverpool na Chelsea itakuwa ya mwisho kwake, akiwa kocha mkuu wa timu hiyo yenye makao makuu yake Anfield.
Liverpool inatarajiwa kucheza mechi yake ya mwisho ya ligi kuu ya England Jumapili kwa kumenyana na Hull City, huku ikiwa imeshapoteza matumaini ya kushika nafasi ya nne. Kocha huyo amekuwa akihusishwa na mipango ya kujiunga na klabu ya Juventus ya Italia.
Benitez amedai kuwa, bodi ya wakurugenzi ya Liverpool imeshindwa kumhakikishia kwamba atapata fungu la kutosha kwa ajili ya kusajili wachezaji wapya, kama ilivyofanya msimu uliopita.
Kocha huyo alisema, anaelewa wazi kwamba, bodi hiyo inataka ajiuzulu ili kukwepa kumlipa fidia ya pauni milioni 16 za Uingereza kwa ajili ya fidia ya kuvunja mkataba wake.
Aliongeza kuwa, bodi hiyo pia inatumia ujanja wa kutaka ilipwe fidia iwapo itapata uthibitisho kwamba, Juventus imekiuka taratibu katika kufanya naye mazungumzo ya kumwajiri.
Hata hivyo, Benitez alisema ana hakika kwamba ataondoka klabu hiyo akiwa msafi, kutokana na kulazimishwa kufanyakazi kinyume na makubaliano kati yake na uongozi wa Liverpool.
“Niliamua kutia saini mkataba mpya kwa sababu kikosi kilikuwa kizuri na fedha za usajili zilikuwepo. Mwishoni, mambo yalibadilika. Tumekuwa na msimu mbovu na natumaini mambo yatakuwa tofauti siku zijazo, lakini kwa sasa naweza kuzungumzia hatma yangu kwa sababu sielewi nini kinachoendelea,”alisema.
“Niliamua kubaki kwa masharti fulani, ambayo yamebadilika. Niliiacha Valencia kwa sababu mazingira yalibadilika. Msimu huu haukuwa mzuri, hilo lipo wazi. Tunaelewa ni kwa nini na kipi kinapaswa kubadilika,”aliongeza.
Benitez alitia saini mkataba mpya wa kuinoa Liverpool mwaka jana. Mkataba huo wa miaka mitano una thamani ya pauni milioni 20.
Kocha huyo alisema, alikuwa na imani kwamba angepata pauni milioni 20 kwa ajili ya usajili wa wachezaji wapya kutokana na fedha za wachezaji aliowauza.
Benitez alipigania kuwa na uamuzi wa mwisho kuhusu masuala ya wachezaji na aliupata baada ya kuondoka kwa mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Rick Parry.
Lakini kuajiriwa kwa mkurugenzi mtendaji mpya, Christian Purslow mwaka jana, kulimuondolea maamuzi hayo baada ya kuishawishi bodi ya wakurugenzi iwe na sauti katika kupanga bajeti na kushiriki katika mazungumzo ya uhamisho.
Liverpool ilitumia fungu kubwa la fedha baada ya kuwaongezea mikataba mipya baadhi ya wachezaji wake nyota kama vile Steven Gerrard, Fernando Torres, Dirk Kuyt, Yossi Benayoun kocha Benitez mwenyewe.
Benitez alisema hakutarajia iwapo kuajiriwa kwa Purslow kungeweza kusababisha matatizo kiasi cha kusababisha uhusiano kati yake na mkurugenzi huyo kukaribia kuvunjika.
Hatma ya Benitez sasa ipo mikononi mwa bodi ya wakurugenzi, ambayo italazimika kuchukua uamuzi haraka baada ya pambano kati ya Liverpool na Hull City, ama isubiri kocha huyo ajiondoe mwenyewe.
Kocha Jose Mourinho wa Inter Milan ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kumrithi Benitez. Makocha wengine wanaopewa nafasi hiyo ni Martin O’Neill, Roy Hodgson na Jesus Jorge wa Benfica ya Ureno.
Juventus ilianza kumuwinda Benitez tangu Januari mwaka huu wakati kocha huyo aliposema, anaona fahari kuhitajiwa na klabu hiyo. Pia aliitaka Inter Milan nayo ifuate nyayo hizo, lakini ilimweka kando na kumuajiri Jose Mourinho.
Katika hatua nyingine, Kocha Roberto Mancini wa Manchester City ameahidi kusajili wachezaji nyota wa dunia, iwapo timu hiyo itapata nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa wa Ulaya msimu ujao.
Miongoni mwa wachezaji, ambao Mancini amepania kuwasajili kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi chake ni pamoja na Fernando Torres wa Liverpool.
Manchester City ipo kwenye kibarua kigumu cha kuwania nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kuu ya England sanjari na Tottenham. Timu hizo zinashika nafasi ya nne na ya tano, zikiwa zinatofautiana kwa pointi moja.
Mancini anaamini kuwa, Manchester City inaweza kushika nafasi hiyo iwapo itaishinda Tottenham katika mechi iliyotarajiwa kuchezwa jana kabla ya kuishinda West Ham Jumapili.
Hata hivyo, Mancini alikiri kuwa, ataweza kumnasa Torres iwapo tu timu hiyo itafuzu kucheza ligi ya mabingwa wa Ulaya.
“Ni jambo la kawaida kwa wachezaji kufikiria jambo hilo. Wachezaji wengi wanataka kucheza ligi ya Ulaya. Ili kukiongezea nguvu kikosi, ni lazima tununue wachezaji wazuri na wachezaji watataka kuja hapa. Lakini hata kama hatutafuzu kucheza ligi ya Ulaya, lazima tununue wachezaji wazuri,”alisema.
Wakati huo huo, Kocha Slaven Bilic wa Croatia ni miongoni mwa wanaopewa nafasi kubwa ya kumrithi Gianfranco Zola katika kibarua cha kuinoa West Ham msimu ujao.
Zola huenda akajiuzulu kuinoa timu hiyo baada ya kuwashutumu waziwazi wamiliki wa klabu hiyo, David Gold and David Sullivan.
Kocha huyo kutoka Italia amekerwa baada ya klabu hiyo kudaiwa kuwa, imetenga pauni milioni nne kwa ajili ya kumsajili kiungo Graham Dorrans kutoka Scotland, ambaye amedai kuwa, kamwe hakuwahi kuzungumza naye.
“Ninapaswa kuwa na sauti kwa wachezaji wanaosajiliwa ama kuuzwa. Mimi ndiye ninayewafundisha wachezaji na nahitaji kuelewa nani ninayemfundisha,”alisema.
“Si sahihi kufikiria kwamba sikutaka nihusishwe katika uhamisho wa wachezaji. Nataka kufahamu watu wanaokuja, nahitaji kuelewa nani ninayehusika naye,”alisema.
Zola (43), analipwa mshahara wa pauni milioni 1.9 kwa mwaka na mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2013.





No comments:

Post a Comment