KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, May 30, 2010

Manji kumrejesha Ngasa Yanga

Na Emmanuel Ndege

MFADHILI Mkuu wa klabu ya Yanga, Yussuf Manji ameapa kuwa, atamrejesha mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Mrisho Ngasa aliyejiunga na klabu ya Azam hivi karibuni.

Akizungumza mjini Dar es Salaam jana, Manji alisema atafanya hivyo wakati wa usajili wa dirisha dogo.

Manji alisema amefikia uamuzi wa kumrejesha Ngassa kwenye klabu hiyo kutokana na uongozi kutomshirikisha wakati wa kumuuza.

Mfadhili huyo alisema ameshangazwa na kitendo cha Mwenyekiti wa Yanga, Iman Madega kufanya mazungumzo na viongozi wa Azam kuhusu Ngasa bila kumshirikisha.

Alisema kuuzwa kwa Ngasa kumemfedhehesha yeye binafsi kwa sababu baadhi ya wanachama wameanza kumuona kama vile ameishiwa kifedha.

“Mimi ndiye niliyekuwa nikimlipa Ngasa fedha zote za usajili pamoja na mshahara, nilikuwa na haki ya kufahamishwa kuhusu mipango ya kumuuza Azam,”alisema.

“Matokeo yake ni kwamba, sasa nachekwa na baadhi ya wanachama pamoja na watani wetu Simba kwamba nimefulia. Siwezi kukubali kitu hiki kitokee, nitamrejesha Ngasa kwa gharama zozote,”aliongeza.

Mfadhili huyo alisema kama aliweza kununua mechi ya Yanga na Etoile Sahel ya Tunisia miaka minne iliyopita kwa kulilipa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), sh. milioni 100 na kuruhusu mashabiki waingie uwanjani bure, haoni kwa nini ashindwe kumrejesha Ngasa.

Ngasa amenunuliwa na Azam kwa kitita cha sh. milioni 98. Kati ya fedha hizo, Ngasa alilipwa sh. milioni 40 wakati klabu ya Yanga ilipata sh. milioni 58.

“Nimekuwa nikitumia fedha nyingi kuigharamia Yanga, siwezi kushindwa kuirejeshea Azam fedha ilizotumia kumnunua na nitafanya hivyo wakati wa usajili wa dirisha dogo,” alisisitiza.

Alipoulizwa jana iwapo yupo tayari kurejea Yanga, Ngasa alisema hakuna tatizo kwa vile suala la msingi ni fedha.

“Kama Manji amesema atairejeshea Azam fedha ilizoilipa Yanga wakati wa usajili wa dirisha dogo, mimi sina kinyongo nipo tayari kurudi,”alisema Ngasa.

Wakati huo huo, Manji ameahidi kugharamia uchaguzi mkuu wa klabu ya Yanga unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni mjini Dar es Salaam.

Manji alisema jana kuwa, atawaandalia chakula na usafiri wanachama wote wa Yanga wakati wa uchaguzi huo ili uweze kufanyika kwa ufanisi.

“Nimesikia wenzetu Simba walifanya uchaguzi, lakini hakukuwa na chakula kwa wanachama waliopiga kura, mimi nawaahidi wanachama kwamba watapata chakula safi siku hiyo,”alisema.

Uchaguzi mkuu wa Yanga, utatanguliwa na mkutano mkuu wa kujadili katiba mpya ya klabu hiyo, unaotarajiwa kufanyika Juni 6 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment