'
Friday, May 7, 2010
Posho wa Maisha Plus aja na mduara
Na Badru Kimwaga
MSHINDI wa nne wa Shindano la Maisha Plus 2010, Leonard Erasmos Komba 'Ponyo', yupo mbioni kuachia kibao kipya cha muziki kiitwacho Pwani, kitakachokuwa katika miondoko ya mduara.
Ponyo, maarufu pia kama Man, aliyewahi kuliimbia kundi la Migo Massive, alisema baada ya ukimya wa muda mrefu katika fani ya muziki, ameamua kutoka na kibao hicho kwa nia ya kutambulisha ujio wa albamu yake na kuthibitisha kuwa bado wamo kwenye 'gemu' hiyo.
Msanii huyo anayeigiza pia filamu na kuchonga vinyago, alisema kibao hicho cha Pwani anachotarajiwa kukiingiza studio hivi karibuni atakiimba na msanii nyota wa kundi la Tip Top Connection, Tundaman.
Alisema kibao hicho ni kati ya vibao nane vitakavyokuwa katika albamu yake mpya na ya kwanza itakayokuwa na miondoko tofauti kuanzia reggae, mduara, R&B na Zouk.
"Baada ya ukimya mrefu kutokana na kujitumbukiza kwenye filamu, nimepanga kurejea tena na safari hii najiandaa kuachia Mduara utakaoenda kwa jina la Pwani utakaotambulisha albamu yangu ijayo," alisema Ponyo.
Ponyo, aliyetamba kwenye Maisha Plus na kibuyu chake cha ajabu, alisema albamu hiyo ijayo na ya kwanza kwake itakuwa na nyimbo nane, baadhi ikiwa ni Pwani, Mzuka, Tobi na Nini Unataka.
Aliongeza kwa sasa anahaha kusaka watu wa kumpiga tafu kuweza kufanikisha mipango ya kuachia albamu hiyo mapema kabla ya kufika mwezi Agosti.
"Tatizo linalonikwamisha kwa sasa ni mshiko wa kukamilisha kazi hii, hivyo kama kutakuwa na wenye uwezo wajitokeza kunisaidia," alisema Ponyo.
Akiwa na Migo Massive lililokuwa likiundwa na wasanii wengine kama Luga Chriss na Bob Lee, Ponyo na wenzake walitamba na vibao kama Sitaki Demu na Summer Party kilichowafanya washiriki tamasha la Fiesta la mwanzoni mwa 2000.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment