KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 14, 2010

Rodrigo: Kombe la Taifa limetusaidia kupata uzoefu

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, Rodrigo Stockler amesema, mashindano ya Kombe la Taifa yamewasaidia vijana wake kuongeza uzoefu.

Rodrigo alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, ushiriki wao katika mashindano hayo utawaweka katika mazingira mazuri zaidi ya kukabiliana na Ivory Coast.

Ngorongoro ilialikwa kushiriki kwenye mashindano ya Kombe la Taifa mwaka huu kwa lengo la kuipa mazoezi, lakini imeshindwa kusonga mbele baada ya kutolewa hatua ya makundi.

Vijana hao walimaliza mechi za kituo cha Dodoma wakiwa nafasi ya tatu baada ya kuambulia pointi mbili, kufuatia kutoka sare na timu za mikoa ya Kigoma na Singida na kufungwa na Dodoma.

Kwa sasa, Ngorongoro inajiandaa kumenyana na Ivory Coast katika mechi ya raundi ya pili ya michuano ya kuwania ubingwa wa Afrika. Ilifuzu kucheza hatua hiyo baada ya kuitoa Malawi kwa jumla ya mabao 5-3.

“Haya mashindano yametusaidia sana, wachezaji wangu hawajaonyesha kwamba wao ni wadogo, walijitahidi kwenda sambamba na wachezaji wa mikoa mingine, ambao ni wakubwa kiumri na wazoefu wa michuano mbalimbali,”alisema Rodrigo.

Kocha huyo kutoka Brazil alisema mechi tatu walizocheza katika mashindano hayo zimewaongezea mbinu mbalimbali vijana wake, ambazo zitawasaidie kukabiliana na Ivory Coast.

Alisema tatizo kubwa lililokuwa likiwasumbua vijana wake ni ubovu wa Uwanja wa Jamhuri na uamuzi mbaya wa waamuzi waliochezesha mechi za kituo hicho.

Rodrigo aliwashutumu waamuzi hao kwa kushindwa kuwalinda vijana wake, ambao ni wadogo kiumri na kuruhusu wachezewe rafu zisizokuwa na ulazima.

Kocha huyo ameamua kuwapumzisha wachezaji wake hadi Julai Mosi mwaka huu watakapoingia kambini kujiandaa kwa pambano lao dhidi ya Ivory Coast.

Ngorongoro na Ivory Coast zinatarajiwa kucheza mechi ya kwanza kati ya Julai 24 na 25 mjini Abidjan na kurudiana kati ya Agosti 7 na 8 mwaka huu mjini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment