'
Sunday, May 30, 2010
Twiga Stars njia nyeupe kucheza fainali za Afrika
TIMU ya soka ya taifa ya wanawake, Twiga Stars mwishoni mwa wiki iliyopita ilijiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika baada ya kuibugiza Eritrea mabao 8-1 katika mechi ya awali ya raundi ya pili iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Katika makala hii, Mwandishi Wetu RASHID ZAHOR anaelezea kiwango kilichoonyeshwa na Twiga Stars katika mechi hiyo.
Kutokana na ushindi huo, ili ifuzu kucheza fainali hizo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Twiga Stars sasa inahitaji sare ya aina yoyote timu mbili hizo zitakaporudiana wiki mbili zijazo mjini Asmara.
Kwa ushindi huo, hakuna kinachoweza kuizuia Twiga Stars isifuzu kucheza fainali hizo zitakazofanyika mwishoni mwa mwaka huu nchini Afrika Kusini. Labda itokee miujiza kwa Eritrea kuifunga Twiga mabao 8-0.
Lakini iwapo Eritrea itaishinda Twiga mabao yasiyozidi saba katika mechi hiyo, njia itakuwa nyeupe kwa akina dada hao kuweka rekodi ya kuwa timu ya pili ya taifa kufuzu kucheza fainali za Afrika, baada ya Taifa Stars kufanya hivyo mwaka 1980.
Ushindi huo mkubwa kwa Twiga Stars haukupatikana kirahisi ama kwa njia ya mteremko. Ulitokana na kiwango cha juu cha soka kilichoonyeshwa na wachezaji wa timu hiyo na pia kucheza kwa malengo.
Tofauti na walivyocheza katika mechi yao ya marudiano ya raundi ya kwanza dhidi ya Ethiopia na kulazimishwa kutoka nayo sare ya bao
1-1, katika mechi dhidi ya Eritrea, Twiga ilionekana kuwa na mabadiliko makubwa na kuimarika kila idara.
Wachezaji wake walicheza kwa nguvu muda wote wa mchezo bila ya kuonekana kuchoka, walikuwa na stamina na walipeana pasi za uhakika, japokuwa baadhi ya wakati hazikuwa na malengo.
Akina dada hao walicheza mechi hiyo wakiwa chini ya kocha wa muda, Rogasian Kaijage, ambaye alikabidhiwa jukumu hilo baada ya makocha waliopewa dhamana ya kuinoa timu hiyo, Charles Boniface na Mohamed Rishard Adolph kwenda mafunzoni Brazil.
Baadhi ya wadau waliozungumza baada ya mechi hiyo walikiri kuwa, Kaijage ameleta mabadiliko makubwa katika timu hiyo kutokana na wachezaji wake kucheza kwa mfumo unaoeleweka.
“Huyu jamaa bwana (Kaijage) anastahili kukabidhiwa hii timu moja kwa moja kwa sababu ameleta mabadiliko makubwa. Vijana wamecheza mpira unaoeleweka, tofauti na walivyocheza dhidi ya Ethiopia,” alisema Fadhili Hilali, mkazi wa Temeke, Dar es Salaam.
Mwanadada Justina James, mkazi wa Magomeni alisema ilikuwa mara yake ya kwanza kuiona Twiga ikicheza, lakini imemfurahisha kwa sababu ilicheza soka nzuri na kupata ushindi mkubwa.
Katika mechi hiyo, viungo Mwanaidi Abdalla, Fadhila Hamadi na washambuliaji Fatuma Bushiri, Asha Rashid, Eto Mlenzi na Esther Chabruna ndio waliotia fora kwa kugongeana vizuri na kufunga mabao ya kuvutia.
Kwa mfano, bao la pili la Mwanaidi alilifunga kwa shuti la mbali, akiwa amempima kipa Semhar Bekitr wa Eritrea, ambaye alishindwa kulidaka kwa vile alishatoka langoni.
Bao la tatu lililofungwa na Asha nalo lilikuwa la aina yake kwa vile kabla ya kufunga, aliwalamba chenga mabeki wawili pembeni ya uwanja, akaingia na mpira ndani ya mita 18 na kuwalamba tena chenga mabeki wengine wawili kabla ya kuukwamisha mpira wavuni.
Mabeki Sophia Mwasikili, Fatma Khatibu, Pulkeria Charaji na Helen Peter nao walicheza kwa umakini mkubwa, japokuwa baadhi ya wakati walifanya makosa ya kizembe yaliyowawezesha washambuliaji Rahwa Solomon na Tuta Mender kuingia na mpira mara kadhaa kwenye eneo la hatari.
Kilichovutia zaidi, hata wachezaji wa akiba, Fadhila Hamadi na Fatma Mustafa waliongia kipindi cha pili kuchukua nafasi za Mwanahamisi na Esther, walionyesha soka ya kiwango cha juu na hakukuwa na tofauti kati yao na walioanza mchezo huo tangu mwanzo.
Uamuzi wa Kocha Kaijage kufanya mabadiliko ya wachezaji kipindi cha pili ulipokewa kwa furaha kubwa na mashabiki waliohudhuria mechi hiyo, ambao walikuwa na kiu kubwa ya kuona uwezo wa wachezaji wa akiba, ambao hawakupata nafasi katika mechi dhidi ya Ethiopia.
“Hawa watoto waliongia sasa hivi kumbe nao ni wazuri! Mbona hawakucheza katika mechi na Ethiopia,” baadhi ya mashabiki waliohudhuria mechi hiyo walisikika wakisema mara kadhaa.
Kwa jumla, uwezo ulioonyeshwa na Twiga katika mechi hiyo umedhihirisha wazi kwamba, wakipata mafunzo zaidi ya kuwaunganisha vyema, wana uwezo wa kufika mbali zaidi katika michuano hiyo. Kocha Kaijage amedhihirisha kwamba anao uwezo huo.
Pengine ni vyema kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lifikirie kumwongeza Kocha Kaijage katika benchi la ufundi la timu hiyo
kwa sababu inaonekana wachezaji wanamwelewa zaidi na kushika mafunzo yake.
Hii ni kwa sababu, tayari Adolph ni kocha msaidizi wa timu ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 19, Ngorongoro Heroes, hivyo si vyema awe na majukumu mawili kwa wakati mmoja. Nafasi yake ndani ya Twiga apewe Kaijage.
Pamoja na Twiga kujisafishia njia ya kusonga mbele, haipaswi kudharau mechi yao ya marudiano dhidi ya Eritrea kwa sababu hali ya hewa ya nchi hiyo ni baridi kali na inaweza kuwaathiri wachezaji na kuwafanya washindwe kufanya vizuri.
TFF inapaswa kuzingatia ushauri uliotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika wa kuipeleka timu hiyo kuweka kambi kwenye mkoa wenye hali ya hewa inayolingana na Eritrea ili wachezaji wasiathirike.
Lakini kubwa kuliko yote ni kwamba, bado Twiga inahitaji mafunzo zaidi ya kitaalam na pengine ziara waliyoahidiwa ya kwenda Marekani kwa mafunzo ya wiki mbili baada ya kuitoa Eritrea, inaweza kuwa na manufaa zaidi kwa wachezaji.
Ahadi hiyo ya kuipeleka Twiga nchini Marekani, ilitolewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya RBP Oil Industrial Technology Limited, Rahma Al Kharoos, ambaye pia aliipatia timu hiyo sh. milioni 10 kabla ya kupambana na Eritrea kwa lengo la kuwaongezea motisha wachezaji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment