KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 6, 2010

MANJI APASUA BOMU YANGA



Na Emmanuel Ndege
MFADHILI mkuu wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji amekanusha madai kuwa, aliihujumu timu hiyo ilipocheza na Simba katika mechi ya mzunguko wa pili wa michuano ya soka ya ligi kuu ya Vodacom.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam juzi, Manji alisema asingeweza kufanya kitu kama hicho kwa sababu ana mapenzi makubwa na Yanga na amekuwa akiifadhili kwa mamilioni ya fedha.
Katika mechi hiyo, iliyochezwa Aprili 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilipigwa mweleka wa mabao 4-3 na Simba.
Manji alisema wanachama wa Yanga waliotoa madai hayo kwenye vyombo vya habari, hawana shukurani kwa sababu haiingii akilini ni vipi anaweza kufanya hivyo kwa timu, ambayo amekuwa akitumia fedha zake nyingi kuisaidia.
“Mimi naipenda sana Yanga, siwezi na sintaweza kuihujumu kwa sababu yoyote ile,” alisema Manji.
Aliongeza kuwa, tangu alipojiunga na klabu hiyo, amefanikiwa kurejesha amani na mshikamano baada ya kumaliza tofauti zilizokuwa zimejitokeza kati ya makundi mawili yaliyokuwa yakipingana ya Yanga Asili na Yanga Kampuni na kuifanya Yanga iwe moja.
“Tazama, nimekarabati jengo la Yanga kwa fedha nyingi, nimetengeneza eneo la kuchezea soka, nimetumia fedha nyingi kusajili wachezaji wa ndani na kutoka nje ya nchi, sasa iweje baadhi ya wanachama wanadai kuwa nimeichoka Yanga!”Alihoji.
“Wanaosema nimeihujumu Yanga, nawauliza nifanye hivyo ili iweje? Ili nipate nini? Nitumie mamilioni ya pesa zangu kuisaidia, halafu eti niihujumu!” Alisema mfadhili huyo huku akionyesha uso wa masikitiko.
Manji alisema chini yake, ameiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa ligi kuu mara mbili mfululizo pamoja na Kombe la Tusker, hivyo haoni kitu gani kinachoweza kumfanya ageuke na kuihujumu.
“Hizi ni kauli zisizo na msingi wowote. Wanachama wanaosema maneno hayo, hawana shukurani kabisa,”alisema.
Manji alisema milango ipo wazi kwa mtu yeyote anayetaka kuifadhili Yanga ajitokeze. Lakini alisisitiza kuwa, hatoweza kutokea mfadhili atakayeweza kufanya mambo aliyoyafanya ndani ya klabu hiyo.
Mfadhili huyo amewataka wanachama wa Yanga wawe makini na watulivu katika kipindi hiki, ambacho klabu hiyo inaelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Alionya kuwa, iwapo wanachama wataanza kutofautiana na kutoa kauli za uchochezi, upo uwezekano mkubwa wa kuibuka kwa mgogoro mwingine unaoweza kusababisha klabu irejee ilikotoka.
Akizungumzia usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa ligi, Manji alisema kazi hiyo amemkabidhi Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic kutoka Serbia.
“Masuala yote ya usajili yapo chini ya Papic kwa sababu yeye ndiye anayejua nani anahitajika na nani hahitajiki ndani ya Yanga. Mimi kazi yangu ni kutoa pesa tu,”alisema.
Alizionya klabu za ligi kuu kuepuka kugombea wachezaji wakati wa kipindi cha usajili, badala yake zifanye majadiliano iwapo klabu moja inataka mchezaji kutoka klabu nyingine.
“Kama kuna klabu yoyote itakayofanya umafia Yanga, itakiona cha moto. Nitajibu mapigo kwa nguvu zote,”alijigamba,

No comments:

Post a Comment