'
Friday, May 14, 2010
England yataka uenyeji Kombe la Dunia 2018
ZURICH, Uswisi
MWANASOKA wa kimataifa wa England, David Beckham amekabidhi kitabu chenye kurasa 1,752, ambacho anaamini kitalishawishi Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), kuizawadia England uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018.
Mwenyeji wa fainali hizo mwaka 2018 na 2022 anatarajiwa kutangazwa Desemba 2 mwaka huu.
Mbali na England, nchi nyingine zilizowasilisha maombi ya kuandaa fainali hizo ni Russia na Australia.
“Tuna furaha kubwa; soka ni kitu ambacho kinapita akilini mwetu,”alisema Beckham, ambaye alikabidhi kitabu hicho kwa Rais wa FIFA, Sepp Blatter jana mjini hapa.
Mara baada ya kupokea kitabu hicho, Blatter alidokeza kuwa, alipokea simu kutoka kwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza, David Cameron.
Nchi tisa, zikiwemo Uholanzi na Ubelgiji, zilizoomba kuandaa fainali hizo kwa pamoja, nazo ziliwasilisha maombi yao kwa Blatter jana asubuhi.
Ujumbe wa England ulitambulishwa na Blatter kama unaowakilisha ‘Mama wa soka’.
Beckham aliungana stejini na Makamu wa Pili wa Rais wa FIFA, Geoff Thompson, Msimamizi mkuu wa maombi ya England katika fainali hizo, Andy Anson na Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha England, Lord Trieman, ambaye alimthibitishia Blatter kwamba, England pia ingependa kufikiriwa kuandaa fainali za mwaka 2022.
Katika hotuba yake fupi, Beckham alisema England ina kiu kubwa ya kuandaa fainali hizo kwa sababu soka ina mvuto mkubwa katika nchi hiyo na imejikita akilini mwao.
“Kila timu (itakayoshiriki fainali hizo), itakuwa katika mji wake na kuwa pamoja na mashabiki wake,”alisema Beckham.
Blatter aliushukuru ujumbe wa England kwa kuunga mkono mchezo wa soka, ambao umepata umaarufu mkubwa duniani kabla ya kudokeza kile alichozungumza na Cameron.
“Si tu kwamba alieleza kuunga kwake mkono maombi haya, lakini pia fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010 zitakazofanyika Afrika Kusini,”alisema.
FIFA inatarajia kupata pauni bilioni 2.1 kutokana na matangazo ya televisheni na udhamini katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010 wakati England inakadiria kuongeza mapato hayo kwa robo tatu, kufikia pauni bilioni tatu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment