MWENYEKITI mpya wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amesema ajira za watendaji watatu wakuu wa klabu hiyo zitafanyika kwa kufuata taratibu zilizowekwa.
Rage alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, uongozi wake utakutana hivi karibuni kwa ajili ya kupanga taratibu za ajira ya viongozi hao.
Kwa mujibu wa katiba mpya ya Simba, klabu hiyo inapaswa kuajiri katibu mkuu, mhasibu na ofisa habari wa klabu.
Ajira za viongozi hao ni utekelezaji wa maelekezo ya Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), ambalo limezitaka nchi wanachama kuzitaka klabu za ligi kuu ziajiri viongozi hao watatu.
Rage alielezea msimamo huo wa uongozi wake, kufuatia Katibu Mkuu wa zamani wa Simba, Mwina Kaduguda kuomba yeye na viongozi wenzake wa kuajiriwa waliomaliza muda wao, wafikirie kupewa tena ajira hizo.
Mbali na Kaduguda, ambaye kabla ya kupewa ajira hiyo alikuwa katibu mkuu wa kuchaguliwa, wengine ni aliyekuwa mhasibu, Chano Almasi na ofisa habari wa klabu, Clifford Ndimbo.
Rage alisema hata kama ajira hizo zitatolewa tena, ni vigumu kusema iwapo watawarejesha tena viongozi hao wa zamani kwa sababu taratibu za ajira zinafanywa na kamati ya utendaji.
No comments:
Post a Comment