KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 14, 2010

Yanga, Azam kubadilishana Boko na Cannavaro

KLABU ya Yanga imeutaka uongozi wa Azam uwe tayari kubadilishana wachezaji, iwapo inamtaka kwa dhati beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, klabu yake ipo tayari kumruhusu Cannavaro ajiunge na Azam, lakini kwa masharti ya kubadilishana na mshambuliaji John Boko ‘Adebayor’.

Msimamo huo wa Yanga umekuja baada ya kuwepo na taarifa kwamba, Azam inataka kumsajili Cannavaro kwa ajili ya msimu ujao wa ligi na tayari imeshafanya naye mazungumzo ya awali.

Beki huyo kutoka Zanzibar naye ameshauandikia barua uongozi wa Yanga, akiutaka umruhusu aihame klabu hiyo msimu ujao na kujiunga na Azam.

Wakati Azam ikimtaka Cannavaro, Yanga nayo imeshaeleza wazi kuwa, inataka kumsajili Boko, kufuatia mapendekezo yaliyowasilishwa kwa uongozi na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic.

“Sisi hatuna tatizo kumruhusu Cannavaro ajiunge na Azam, lakini sharti letu kubwa ni kwamba na wao waturuhusu kumsajili Boko, vinginevyo tubadilishane wachezaji,”alisema Sendeu.

Ofisa Habari huyo ameutaka uongozi wa Azam uwe tayari kukutana na wenzao wa Yanga ili kuzungumzia kwa undani usajili wa wachezaji hao wawili na kufikia mwafaka.

Katika hatua nyingine, Yanga imesema haitakuwa tayari kumruhusu mshambuliaji wake, Mrisho Ngasa ajiunge na Azam kwa malipo kidogo ya uhamisho.

Sendeu alisema jana kuwa, wamepata taarifa kwamba Ngasa amerejea nchini baada ya Azam kuahidi kumsajili kwa malipo makubwa.

Kwa mujibu wa Sendeu, Ngasa alirejea nchini juzi akitokea Rwanda, alikokwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya APR.

APR ilikuwa tayari kumlipa mchezaji huyo sh. milioni 20, lakini Ngasa alikataa na kutaka aliwe sh. milioni 40 na mshahara wa sh. milioni 1.5 kwa mwezi. Pande hizo mbili zilishindwa kufikia mwafaka.

“Hatuwezi kumfanyia Ngasa mtimanyongo. Tunaikaribisha klabu yoyote ije Jangwani kufanya mazungumzo ya kumnunua, lakini ijiandae kulipa dau kubwa,”alisema.

Hata hivyo, Sendeu hakuwa tayari kutaja kiwango cha fedha, ambacho Yanga inahitaji kulipwa kwa ajili ya mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Tanzania.

"Ni vyema viongozi wa Azam wakaacha kuzungumza na wachezaji wetu pembeni, klabu yetu inafahamika mahali ilipo, waje tuzungumze nao,"alisema Sendeu.

Sendeu alisema wanataka kulipwa dau kubwa kwa ajili ya uhamisho wa Ngasa kwa sababu uwezo wake ni mkubwa na ana uwezo wa kucheza soka ya kulipwa popote duniani.

No comments:

Post a Comment