KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 21, 2010

Milioni 94 zamng'oa Ngasa Yanga



HATIMAYE timu ya Azam FC imefanikiwa kumng'oa mchezaji Mrisho Ngasa wa Yanga baada ya mazungumzo yaliyofanyika kwa siku mbli kati ya viongozi wa klabu hizo mbili.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya Yanga kimeeleza kuwa, klabu hizo mbili zilikubaliana uhamisho wa mchezaji huyo ugharimu sh. milioni 94 na malipo hayo yalifanyika jana kwenye benki moja iliyopo barabara ya Lumumba, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa habari hizo, kati ya malipo hayo, Ngasa amepata sh. milioni 40 wakati klabu ya Yanga imelipwa sh. milioni 54.

Mwenyekiti wa Yanga, Iman Madega amekiri kufanyika kwa mazungumzo hayo, lakini alikataa kutaja kiasi cha fedha walichokubaliana kwa ajili ya uhamisho wa Ngasa.

Naye Ngasa alipoulizwa alisema, hafahamu lolote kuhusu makubaliano yaliyofikiwa kati ya viongozi wa klabu hizo mbili kwa vile hakuwepo kwenye kikao hicho.

Mchezaji huyo jana mchana alionekana akiwa na Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako na kiongozi mmoja wa Azam wakiingia katika benki moja jijini Dar es Salaam, ambako inasemekana walikwenda kukamilisha malipo hayo.

Taarifa za kuondoka kwa Ngasa zimepokelewa kwa mshutuko mkubwa na mashabiki wa Yanga, kutokana na ukweli kuwa, mchezaji huyo alikuwa tegemeo kubwa la timu hiyo katika safu ya ushambuliaji.

Ngasa, ambaye ni mtoto wa mchezaji wa zamani wa Pamba ya Mwanza na Simba, Khalfan Ngasa, alijiunga na Yanga mwaka 2006 akitokea Kagera Sugar. Aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kwa mara ya kwanza mwaka 2007.

No comments:

Post a Comment