Na Sophia Ashery
KLABU ya Simba imeng'ara katika tuzo za ligi kuu ya soka ya Vodacom msimu huu baada ya kocha wake, Patrick Phiri na wachezaji Juma Kaseja na Mussa Hassan 'Mgosi' kushinda tuzo mbalimbali.
Phiri, raia kutoka Zambia ameibuka kuwa kocha bora wa ligi hiyo baada ya kuiwezesha Simba kutwaa ubingwa kabla ya ligi kumalizika wakati Kaseja na Mgosi walitwaa tuzo za kipa na mfungaji bora.
Kufuatia kunyakua tuzo hizo, Phiri amezawadiwa kitita cha sh. milioni 2.8 wakati Kaseja na Mgosi wamezawadiwa sh. milion mbili kila mmoja.
Mbali ya zawadi hizo, Simba pia imezawadiwa sh. milioni 38 kwa kuibuka mabingwa wapya wa ligi hiyo wakati watani wao wa jadi Yanga wamezawadiwa sh. milioni 15 kwa kushika nafasi ya pili. Azam FC imezawadiwa sh. milioni 10 kwa kushika nafasi ya tatu.
Mshambuliaji Mrisho Ngassa wa Yanga amezawadiwa sh. milioni 2.5 kwa kuibuka kuwa mchezaji bora wa michuano hiyo wakati tuzo ya mwamuzi bora imenyakuliwa na Oden Mbaga kutoka Dar es Salaam, aliyezawadiwa sh. milioni 2.5. African Lyon imezawadiwa sh. milioni 5.5 kwa kuibuka kuwa timu yenye nidhamu.
Akikabidhi zawadi hizo kwa viongozi wa klabu hizo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera alisema Phiri anapaswa kuwa mfano wa kuigwa na makocha wengine kutokana na kuiongoza vyema Simba kutwaa ubingwa.
No comments:
Post a Comment