KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, April 29, 2017

SIMBA YATINGA FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO, YAICHAPA AZAM 1-0


SIMBA leo imekata tiketi ya kucheza fainali ya michuano ya soka ya Kombe la Azam, maarufu kama Kombe la Shirikisho, baada ya kuichapa Azam bao 1-0.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilijipatia bao hilo la pekee na la ushindi dakika ya 48 kupitia kwa mshambuliaji Mohamed Ibrahim.

Hata hivyo, Mohamed alishindwa kumaliza mchezo huo baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 74 kwa kucheza rafu mbaya.

Awali, Azam nayo ilipata pigo baada ya kiungo wake, Salum Abubakar kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Mathew Akrama kutoka Mwanza dakika ya 15 kwa kosa la kumkwatua kwa nyuma Ibrahim Ajib wa Simba.

Simba sasa inasubiri mshindi wa pambano lingine la nusu fainali kati ya Yanga na Mbao FC litakalochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.

Wednesday, April 26, 2017

CAF YATOA RATIBA YA MAKUNDI YA KLABU BINGWA NA KOMBE LA SHIRIKISHO.

Shirikisho la Mpira barani Afrika CAF limetangaza makundi ya Michuano ya klabu bingwa pamoja na kombe la Shirikisho hatua ya 16 huku yakigawanywa katika makundi manne na kila kundi litatoa timu mbili ambazo zitafuzu kuingia hatua ya Robo Fainali.

Makundi Ligi ya Mabingwa kama ifuatavyo:


MBAO FC YATAMBA KUISHIKISHA ADABU YANGA



Kikosi cha Mbao FC cha mkoani Mwanza kina imani ya kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho kwa kuing’oa na kuivua ubingwa Yanga.
Mbao FC wanajiamini kutokana na safu nzuri ya ushambuliaji, lakini wameandaa safu yao ya ulinzi kikamilifu kuwadhibiti Simon Msuva na Amissi Tambwe, kuhakikisha hawapati nafasi ya kufunga.
Mbao inatarajia kukutana na Yanga Jumapili katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA ambapo hadi sasa ni timu nne tu ndizo zilizobakia.
Msemaji wa Mbao FC, Chrisant Malinzi, amesema kuwa, walikuwa na hamu kubwa ya kukutana na Yanga kwenye FA na kudai kuwa wameiandaa ipasavyo safu yao ya ulinzi kuhakikisha wanatoa upinzani mkubwa kwa Msuva na Tambwe ili wasipate nafasi ya kufunga kwa kuwa wanahitaji kutinga fainali.
“Tulianza mipango yetu siku nyingi ya kujiandaa katika michuano ya Kombe la FA na tulikuwa tukisubiria tu timu ya kupangwa nayo, tulikuwa na kiu ya kucheza na Yanga, kwani tupo tayari kwa mchezo huo na wala hatuhofii safu ya ushambuliaji ya Yanga kwani na sisi tuna safu nzuri ya ulinzi ya kuweza kuwazuia Msuva na Tambwe, tumejipanga vyema kuhakikisha tunapata nafasi ya kuingia fainali.
 “Kikosi chetu kipo vizuri na hadi tunafikia hapa ni juhudi za wachezaji hivyo nina imani tutafanikiwa kufanya vyema na hatimaye kuingia fainali kwani lengo letu ni kuona tunafanikiwa kutwaa taji ili kuwakilisha nchi kimataifa,” alisema Malinzi.

HIMIDI MAO AICHIMBIA MKWARA SIMBA



NAHODHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, ameweka wazi kuwa wana morali kubwa ya kupata matokeo mazuri kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Sports) dhidi ya Simba Jumamosi ijayo.

Kikosi cha Azam FC kipo kwenye maandalizi makali kuelekea mchezo huo, ambapo tayari kimeshaingia kambini tokea jana katika makao makuu ya klabu hiyo ndani ya viunga vya Azam Complex kujiandaa na mchezo.

Himid ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa kikosi hicho kipo vizuri na watanufaika na urejeo wa wachezaji wao muhimu waliokuwa majeruhi.

“Morali iko juu, timu ipo vizuri bahati nzuri wachezaji wenzetu karibia asilimia 90 wapo vizuri na wapo fiti na wako tayari kwa mchezo na naamini kocha atakuwa na nafasi nzuri ya kuchagua timu yake ya kwenda kucheza mchezo huo,” alisema.

Kiungo huyo anayesifika kwa ukabaji na mwenye mashuti makali, aliongeza kuwa mchezo huo utakuwa mgumu licha ya kufanikiwa kuwafunga mara mbili katika mechi mbili zilizopita.

“Usidhani kama mchezo huu wa tatu utakuwa mrahisi kama mara mbili zilizopita tulizoshinda, kwani Simba nayo inajipanga, lakini naamini sisi tutajipanga vizuri zaidi ili kuweza kushinda mechi hiyo inayokuja,” alisema.

Himid ambaye amekulia kwenye timu hiyo kwa takribani miaka tisa sasa, alitoa wito kwa mashabiki wa Azam FC kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo huo ili kuwapa sapoti kwani wao ni sehemu muhimu sana katika timu na uwepo wao utawaongezea nguvu zaidi uwanjani ya kuibuka kidedea.

SERENGETI BOYS YAIONYESHA TENA UBABE GABON




Na Mwandishi Wetu, RABAT
TIMU ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys leo imedhihirisha ubabe wake kwa wenyeji wa fainali za U-17 Afrika mwaka huu, Gabon baada ya kuwafunga tena 2-1 katika mchezo wa kirafiki mjini Rabat.
Mabao ya Serengeti Boys leo yamefungwa na Assad Juma na Abdul Hussein na hicho kinakuwa kipigo cha pili mfululizo vijana wa Tanzania wanawapa wavulana w Gabon, baada ya Aprili 22 kuwafunga pia 2-1, mabao ya Kelvin Nashon Naftali dakika ya 18 na Ibrahim Abdallah Ally dakika ya 75.
Serengeti Boys imeweka kambi ya mwezi mmoja nchini Morocco kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, zinazotarajiwa kuanza Mei 14 hadi 28, mwaka huu nchini Gabon.
Kwa ujumla huo unakuwa mchezo wa tano wa maandalizi kwa Serengeti kujiandaa fainali za Gabon, baada ya awali kuifunga Burundi mara mbili, Machi 30 mabao 3-0 na Aprili 1 mabao 2-0, mechi zote mbili zikipigwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, kabla ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Ghana ‘Black Starlets’ Aprili 3 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Serengeti Boys itakuwa kambini mjini Rabat hadi Mei 1, mwaka huu itakapowenda Younde, Cameroon kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya wenyeji Mei 3 na 6, mwaka huu.
Mei 7 timu hiyo itakwenda Gabon ambako imepangwa kundi B pamoja na timu za Mali, Niger na Angola, wakati Kundi A lina timu za wenyeji, Gabon, Guinea, Cameroon na Ghana.
HABARI KWA HISANI YA BLOGU YA BINZUBEIRY

Tuesday, April 25, 2017

HAYA NDIO MAJIBU NA MAELEZO YA HAJI MANARA BAADA YA KUFUNGIWA NA TFF


“Namshukuru Mungu kwa sasa masuala yangu binafsi ya kifamilia nimeyamaliza na naweza sema kitu, kwanza niwape pole nyie kwa haya yaliyonitokea, mimi sio mtu ninayeamini uonevu sio mtu ninayeweza kunyamaza nikiona haki inaporwa, sio mtu mwenye moyo dhaifu wa kuogopa kukosoa pale panapopaswa kurekebishwa”

“Always nitabaki hivyo juzi Ijumaa jioni niliambiwa na ofisi yangu imekuja barua toka TFF, ikiniharifu kuna wito wa kunitaka nifike Karume kusikiliza mashitaka dhidi yangu Jumapili ya jana asubuhi, wakati huo nikiwa Zanzibar kwa masuala yangu ya kifamilia na ofisi ikaiandikia TFF barua ya kuomba kusogezwa mbele kwa shauri hili hadi Jumanne ya kesho kwa kuwa nitakuwa nipo Dar es Salaam”


“Barua iliwafikia na binafsi nikaongea na Afred lucas msemaji wao na akanijibu ameipokea yeye na imegongwa muhuri na katibu Mkuu wa TFF keshaipata, kumbuka hiyo ni jioni ya Ijumaa, Jumamosi nikampigia Alfred kuulizia kikao hicho cha kamati kimepangwa lini, akanijibu Jumatatu ya leo atanijibu, jana tena mkasikia mliyosikia ni uharaka upi ilionao TFF wa kushindwa kunipa haki ya kusikilizwa?”

“Natural justice nchi hii haitambuliki!! wahaini na wauaji nao pia husikilizwa iweje kwa mtuhumiwa ambae anapigia kelele haki ya mwajiri wake? kuna hoja dhaifu inajengwa kuwa nilipaswa nijibu bnafsi barua ya TFF, hivi ningewezaje kuijibu barua wakati sikuwepo Dar es Salaam na sikuwa nimeiona na vipi klabu yangu isiwe na haki ya kunijibia barua, wakati leo imepokwa haki ya kutokuwa na msemaji?”

“Hivi TFF hawajui kuwa mimi nilikuwa naongea kwa niaba ya ofisi na klabu yangu? nikija sababu za kunifungia nimejiuliza ni kaka yangu huyu Msemwa aliyekuwa anasoma hii hukumu? nimemuona kwa Millard Ayo, anasoma hukumu ilio kinyume na hati ya mashtaka”

“Hati yao ina makosa mengine na hukumu pia nyingine ni aina ya hukumu katili zaidi kwa viwango vya mpira wetu ila nawaambia TFF Haji hajawahi kuwa dhaifu wa moyo, anaweza kuwa dhaifu wa kiwiliwili lakini nina moyo wa Simba, nitapambana kwa kiwango cha juu sana”

“Nitadai haki yangu na mwajiri wangu kwa viwango na nitaziomba kamati zao zipokee rufaa yangu na kukaa kwa uharaka huu walionifanyia na nipewe haki ya kusikilizwa, nisihukumiwe kishabiki wala kwa chuki na nawahakikishia kikao kitakachokaa”

Sunday, April 23, 2017

BMT YATOA MAAGIZO YA KUMALIZA MZOZO WA TFF NA SIMBA



SIMBA KUVAANA NA AZAM; YANGA NA MBAO FC KOMBE LA SHIRIKISHO


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), leo limetangaza ratiba ya mechi za nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho, maarufu kama Azam Sports Federation Cup.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, iliyopangwa na kutangazwa leo, mabingwa watetezi Yanga wamepangwa kumenyana na Mbao FC, katika mechi itakayopigwa Aprili 30, mwaka huu, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Ratiba hiyo inayonyesha kuwa, mabingwa wa mwaka juzi, Azam watacheza mechi hiyo kwa kuumana na wakongwe Simba. Mechi hiyo itapigwa Aprili 29, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

SIMBA YAPOKWA POINTI TATU ZA KAGERA SUGAR


KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imeamua kuipokonya Simba pointi tatu ilizopewa na Kamati ya Saa 72,  baada ya kubainika kuwa, Kagera Sugar ilimchezesha mchezaji Mohamed Fakhi akiwa na kadi tatu za njano.

Akisoma maamuzi ya kamati hiyo leo, Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa, amesema Kamati ya Saa 72 ilikosa uhalali wa kusikiliza rufani ya Simba kutokana na kikao chake kuwashirikisha baadhi ya wajumbe wasiohusika.

Aidha, Mwesiga alisema Kamati ya Nidhamu imebaini kuwa, rufani ya Simba ilikosa uhalali wa kusikilizwa kutokana na walalamikaji kutokana rufani na pia kushindwa kulipia ada ya sh. 300,000.

Licha ya Simba kupokwa pointi hizo, bado inaongoza ligi kwa kuwa na pointi 59, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 56, lakini ikiwa na mechi mbili mkononi, hivyo kuwepo na uwezekano mkubwa wa kutwaa ubingwa.

HAJI MANARA ATUPWA JELA YA SOKA MWAKA MMOJA, ATOZWA FAINI MILIONI MOJA


 
MKUU wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara, amefungiwa kujihusisha na soka kwa mwaka mmoja, kutokana na kutoa lugha chafu kwa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Aidha,  Manara, ambaye alishindwa kuhudhuria kikao cha Kamati ya Nidhamu ya TFF, kilichotoa adhabu hiyo leo, ametozwa faini ya sh. milioni moja baada ya kupatikana na hatia ya makosa matatu.

Manara alishindwa kuhudhuria kikao hicho kwa madai ya kupata dharura, lakini anayo nafasi ya kukata rufani.

Saa kadhaa baada ya Kamati ya Nidhamu ya TFF kutangaza kumfungia Manara, Ofisa Habari wa zamani wa Yanga, ambaye naye alifungiwa mwaka mmoja, Jerry Muro, ametumia ukurasa wake wa instagram kuandika alivyoupokea uamuzi huo.

“Mtuache sasa tupumzike, tuliyofanya kwa taifa hili haswa kwenye mpira nadhani yametosha, swahiba karibu kijiweni @hajismanara.“

DK MWAKYEMBA AKUTANA NA KUTETA NA VIONGOZI WA SIMBA





Picha na Kitengo cha Mawasiliano WHUSM Dodoma.

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe amekutana na na uongozi wa klabu ya Simba ukiongozwa na Rais wake Bw. Evans Aveva kwenye Ofisi zake Mjini Dodoma.

Uongozi wa Simba umeitikia wito wa Mhe. Mwakyembe wa kukutana naye na kujadili masuala mbalimbali ya mpira wa Miguu zikiwemo fursa na changamoto katika mabadiliko na maedneleo ya uendeshaji wa timu.

Aidha  Mhe. Mwakyembe  amepokea maoni ya Uongozi wa samba na kusahauri kuendelea kutoa ushirikiano na wadau wa mpira wa miguu nchini.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa  na Katibu Mkuu Wizara husika prof Elisante Ole Gabriel, Mkurugenzi wa Michezo Yusufu Omary, Katibu Mkuu wa BMT Mohamed Kiganja, na Msajili wa Vilabu na Vyama nchini.

YANGA YAZIFUATA SIMBA, AZAM NUSU FAINALI KOMBE LA FA



Mabingwa wa tetezi wa Kombe la Shirikisho, Yanga wametinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tanzania Prisons.

Mchezo huo wa robo fainali ulifanyika jana, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo Yanga sasa inaungana na mahasimu wao Simba, Azam na Mbao FC katika hatua inayofuata ya nusu fainali.

Yanga ilipata magoli yake kupitia kwa Amissi Tambwe aliyefunga dakika ya 16 ya mchezo, Obrey Chirwa aliyefunga bao la pili dakika ya 41. Yanga ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Simon Msuva aliifungia Yanga bao la tatu dakika ya 46 na kuihakikishia ushindi. Mechi hiyo haikuwa na mvuto kutokana na kunyesha kwa mvua kubwa.

Prisons nusura wapate bao la kufutia machozi baada ya kupata penalti dakika ya 54, lakini mpigaji Victor Hangaya aligongesha mwamba.

Ratiba ya mechi za nusu fainali inatarajiwa kupangwa leo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Friday, April 21, 2017

TFF YAMPELEKA HAJJI MANARA KAMATI YA MAADILI



Kwa mujibu wa Katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kila mwanafamilia wa mpira wa miguu Tanzania analazimika kuheshimu na kufuata kanuni za maadili za shirikisho kama zilivyoainishwa kwenye kanuni zake mbali mbali.

Wanafamilia wa mpira wa miguu ni pamoja na wachezaji, makocha, waamuzi, viongozi wa mpira wa ngazi zote na waajiriwa wa taasisi ambazo ni wanachama wa TFF wa ngazi mbalimbali.

Ili kutunza heshima ya mpira wa miguu Tanzania, wanafamilia wa mchezo huo katika kutimiza masharti ya kanuni za maadili za TFF, hawana budi kuheshimu na kufuata taratibu zote hizo ndani na nje ya uwanja.

Taswira njema ya shirikisho inajenga imani ya wadau wakiwamo serikali, mashirika mbalimbali ya umma na binafsi, vyombo vya habari, vyama vya mpira vya kimataifa, NGO’s na watu binafsi kwa taasisi (TFF). Kinyume chake ni kulibomoa shirikisho.

Dhima ya uongozi wa TFF ni pamoja na kulinda na kutunza heshima hii. Hivyo vitendo vyovyote vyenye viashiria vya uvunjaji wa maadili havitavumiliwa, na vikitokea hatua zitachukulia.

Na kwa muktadha huu Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania, limemfungulia mashtaka ya kinidhamu Msemaji wa Simba Bw. Hajji Manara kwenye Kamati ya Maadili. Leo hii Aprili 21, 2017 atapewa mashtaka yake na kujulishwa lini na wapi yatasikilizwa.

TFF inaendelea kutoa rai kwa wadau wa mpira kuwa pamoja ni kwamba ni haki yao kushauri, kupendekeza, kukosoa lakini yote haya yafanyike kwa staha ili kutunza heshima ya mpira wetu.

YOUNG AFRICANS, TANZANIA PRISONS KUMALIZIA ROBO FAINALI ASFC


 Mchezo wa Robo Fainali ya Nne ya Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup 2016/2017), kati ya Young Africans na Tanzania Prisons FC utafanyika kesho Aprili 22, 2017 saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo utatoa mshindi ambaye ataungana na timu nyingine tatu ambazo tayari zimefuzu kwa hatua ya Nusu Fainali. Timu zilizotangulia Nusu Fainali ya ASFC ni za Mbao FC, Simba SC na Azam FC.

Jumapili Aprili 23, mwaka huu kutakuwa na droo ya wazi kwa timu nne zitakazokuwa zimefuzu kwa hatua ya Nusu Fainali ya ASFC, itakayofanyika Kituo cha Televisheni cha Azam ambao ni wadhamini wakuu wa jina la michuano na haki ya kuonesha mubashara michuano hii ambayo inafanyika kwa msimu wa pili mfululizo.

Azam FC ilikata tiketi ya kucheza Nusu Fainali ya ASFC baada ya kuifunga Ndanda FC mabao 3-1, kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam Aprili 5, 2017 ikitanguliwa na Mbao iliyoishinda Kagera Sugar mabao 2-1 katika mchezo ulifanyika Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera Machi 18, 2017 ilihali Machi 19, mwaka huu Simba iliwatoa Madini ya Arusha kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Nusu Fainali inatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, kabla ya fainali ambako Bingwa wa michuano hii ambayo msimu huu ilishirikisha timu 86 ikiwa ni pamoja na za Ligi Kuu ya Vodacom (timu 16); Ligi Daraja la Kwanza (timu 24); Ligi Daraja la Pili (timu 24) na mabingwa wa mikoa timu 22, atazawadiwa Sh. 50 milioni na kupata tiketi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho - CAF.

WAINGIZAJI, WASAMBAZAJI FILAMU WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA



Na: Abuu Kimario – BODI YA FILAMU

Waingizaji na Wasambazaji wa Filamu za nje watakiwa kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamia sekta ya filamu nchi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda wakati akizungumza na wadau wa Sekta ya filamu nchini mara baada ya kupokea maandamano ya Amani ya waigizaji wa Filamu za Kitanzania (Bongo Movie) katika makutano ya mtaa wa Magira na Lukoma, Kariakoo Jijini Dar es Salaam leo.

Makonda amesema kuwa lengo la Serikali siyo kuwazuia wafanyabiashara hao, bali inawataka wafuate sheria na taratibu zinazosimamia sekta hiyo muhimu katika maendeleo ya taifa letu.

“Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam haitawaonea haya wafanyabiashara wote wanaouza kazi za wasanii wa muziki na filamu ambao hawazingatii sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia sekta hizo kwani kufanya hivyo kunalikosesha taifa mapato yatokanayo na Kodi na kusababisha kukosekana kwa uwiano kwenye ushindani wa kibishara kati ya filamu za ndani na filamu kutoka nje ya nchi,” alisema Makonda.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nuru Millao akiwasilisha salamu za Waziri wa Wizara hiyo alisema kuwa, Waziri Mwakyembe anasikitishwa na uharamia unaofanywa na wafanyabishara wasiokuwa waaminifu na kusababisha kudumaza kazi za wasanii wazawa.

Aliongeza kuwa Serikali haitaishia kufanya operesheni za kushtukiza pekee, badala yake Serikali imeendelea kufanya maboresho ya Sera na Sheria zinazosimamia kazi za wasanii nchini ili ziendane na wakati.

Awali akitoa ufafanuzi kuhusu sheria Na.4 ya mwaka 1976 ya Filamu na Michezo ya kuigiza nchini alisema kuwa waingizaji na wasambazaji wa filamu za kutoka nje nchi wanao wajibu kisheria kuwasilisha kazi zao katika ofisi zake kwa ajili ya ukaguzi ili kujiridhisha kama kazi hizo zinakidhi vigezo vya kisheria ikiwemo maudhui na maadili, kisha zinapangiwa madaraja kulingana na maudhui yake.

Fissoo alisema kuwa sheria pamoja na kanuni zake hazihishii tu kwa watengenezaji na wasambazaji wa filamu za ndani, hivyo ni vyema wafanyabiashara wanaofanya biashara hiyo wakazingatia sheria hiyo na kanuni zake, kinyume chake ni uvunjifu wa sheria kwa makusudi.

“Niseme tu kuwa lengo la Serikali sio kuwazuia kufanya biashara yenu ya uingizaji na usambazaji wa filamu za nje, kinachofanyika ni kuhakikisha mnafuata sheria na taratibu kama wafanyabiashara wengine ili kuleta usawa kwenye ushindani wa kibiashara”, alisema Fissoo.

Kwa muda sasa Serikali imekuwa ikihamasisha wafanyabiashara wa kazi za Muziki na Filamu kuzingatia sheria ili kulinda maslahi ya pande zote. Kikao cha leo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na viongozi wa Wizara na taasisi zinazosimamia kazi za wasanii nchini ni juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha inatekeleza ahadi yake ya kuinua hadhi na maslahi ya wasanii.

Sunday, April 16, 2017

SAFARI YA YANGA KIMATAIFA YAFIKIA TAMATI


UNAWEZA kusema kuwa safari ya Yanga katika michuano ya Afrika mwaka huu imefikia ukingoni baada ya kupigwa mweleka wa mabao 4-0 na MC Alger ya Algeria.

Kipigo hicho kwa Yanga, ilichokipata katika mechi ya marudiano iliyochezwa jana mjini Algiers, kimeifanya itolewe kwa jumla ya mabao 4-1, baada ya kushinda mechi ya awali mjini Dar es Salaam kwa bao 1-0.

Yanga iliangukia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa raundi ya pili na Zanaco ya Zambia kwa faida ya bao la ugenini, baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya bao 1-1.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na waamuzi kutoka  Guinea, Yanga ilikwenda mapumziko ikiwa imeshakubali kipigo cha mabao 2-0.

Dalili za Yanga kupoteza mchezo huo zilionekana mapema kutokana na kuibuka migogoro baina ya wachezaji na viongozi kabla ya safari ya kuanza safari ya Algeria

Wachezaji Vincent Bossou kutoka Togo na Obrey Chirwa kutoka Zambia, waligoma kusafiri na timu kwa sababu ya madai ya mishahara yao ya miezi mitatu.

SIMBA YAKWAA KISIKI KWA TOTO AFRICAN


MATUMAINI ya Simba kutwaa taji la ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, jana yaliota mbawa baada ya kulazimishwa kutoka suluhu na Toto African katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.

Sare hiyo imeifanya Simba iendelee kuongoza ligi ikiwa na pointi 62 baada ya kucheza mechi 26, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 56 huku ikiwa na mechi mbili za viporo mkononi.

Iwapo Yanga itashinda mechi hizo mbili, itafikisha pointi 62, sawa na Simba, hivyo kufanya ushindani wa kuwania ubingwa kuamuliwa kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Jacob Adongo wa Mara, timu zote mbili zilishambuliana kwa zamu muda wote wa dakika 90, lakini hakuna iliyoweza kupata bao.

Saturday, April 15, 2017

MAJALIWA YA YANGA KOMBE LA SHIRIKISHO MIKONONI MWA MC ALGER



INAWEZEKANA ukawa mwisho wa safari ya Yanga katika michuano ya Afrika mwaka huu, au ukawa ni mwendelezo wa kufuzu kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.

Jibu hilo litapatikana leo wakati mabingwa hao wa Tanzania Bara, waliotolewa katika michuano ya ligi ya mabingwa Afrika, watakaporudiana na MC Alger ya Algeria mjini Algiers.

Mechi hiyo ni ya marudiano kati ya timu hizo. Katika mechi ya awali, iliyochezwa wiki iliyopita mjini Dar es Salaam, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Ili iweze kusonga mbele, Yanga inahitaji kushinda mechi hiyo au kupata sare ya aina yoyote wakati wapinzani wao watalazimika kushinda kwa mabao 2-0.

Kwa mujibu wa ratiba, mechi hiyo imepangwa kuanza saa mbili usiku kwa saa za Afrika Mashariki, lakini bado haijafahamika iwapo utaonyeshwa moja kwa moja na televisheni za hapa nchini.

Katika mechi hiyo, Yanga itamkosa mshambuliaji wake wa kulipwa, Obrey Chirwa kutoka Zambia, ambaye hakusafiri na timu hiyo kwenda Algeria, kwa kile kinachodaiwa kuwa ameweka mgomo baridi kutokana na kutolipwa mishahara kwa miezi mitatu.

Pengine tegemeo kubwa kwa timu hiyo litakuwa kwa washambuliaji wake nyota, Amissi Tambwe na Mzimbabwe, Donald Ngoma, waliokuwa majeruhi kwa muda mrefu.

KAGERA SUGAR YAPINGA USHINDI WA MEZANI WA SIMBA


SIMBA, TOTO HATUMWI MTOTO DUKANI LEO


VINARA wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba leo wanateremka dimbani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, kumenyana na Toto Africans.

Simba inashuka dimbani kucheza mechi hiyo, ikiwa ni siku chache baada ya kuichapa Mbao FC mabao 3-2 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja huo Jumatano iliyopita.

Kabla ya kucheza na Mbao, Simba ilikuwepo mjini Bukoba, ambako ilimenyana na Kagera Sugar na kuchapwa mabao 2-1, lakini ikaambulia ushindi wa mezani baada ya kubainika kuwa, wapinzani wao walimchezesha mchezaji aliyekuwa na kadi tatu za njano.

Katika mechi ya leo, Simba imepania kuifunga Toto African ili kujiimarisha zaidi kileleni mwa ligi hiyo na hivyo kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa, ambao imekuwa ikiukosa kwa miaka mitatu sasa.

Hata hivyo, mechi hiyo haitarajiwi kuwa nyepesi kwa Simba kwa vile Toto African nayo itacheza kufa na kupona ili kujinasua katika janga la kushuka daraja.

Katika mechi ya awali iliyochezwa Oktoba, mwaka jana, mjini Dar es Salaam, Simba iliinyuka Toto mabao 3-0.

Simba inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 61, baada ya kucheza mechi 26, ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 56 baada ya kucheza mechi 25.

KAMATI YA SAA 72 YAIPA SIMBA USHINDI WA POINTI TATU DHIDI YA KAGERA SUGAR

HATIMAYE hayawi hayawi yamekuwa. Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, 'Kamati ya Saa 72', imefikia uamuzi wa kuipa Simba pointi tatu na mabao matatu kutokana na rufaa waliyoikatia Kagera Sugar.

Simba iliikatia rufaa Kagera Sugar kwa kumtumia beki Mohammed Fakhi huku akiwa na kadi tatu za njano, wakati timu hizo zilipomenyana katika mechi baina ya timu hizo iliyochezwa Aprili 2, mwaka huu.

Katika mchezo huo, Kagera Sugar iliichapa Simba mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.

Ilidaiwa kuwa, Kagera Sugar ilikiuka kanuni za ligi kwa kumchezesha Fakhi, beki wa zamani wa Simba huku akiwa anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Ahmed Yahya, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, kamati yake ilibaini ni kweli Kagera Sugar walifanya kosa hilo la kikanuni na adhabu yake ni kupokonywa ushindi.

Kutokana na kupewa pointi hizo, Simba sasa inaongoza ligi kwa kuwa na pointi 61 baada ya kucheza mechi 26, ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 56 kutokana na mechi 25 walizocheza hadi sasa.

Tuesday, April 11, 2017

SARAH SOLO; MWANAMUZIKI NYOTA WA KIKE ANAYETIKISA DRC





WASWAHILI wana msemo unaosema, nyota njema huonekana asubuhi. Hivyo ndivyo ilivyojidhihirisha kwa mwanamuziki mpya wa kundi la Wenge Musica Maison Mere, Lisungi Kabedi Sarah Urielle, maarufu kwa jina la Sarah Solo.

Mwanadada huyo ametokea kuwa maarufu baada ya kufuzu majaribio aliyofanyiwa na kundi la Wenge Musica Maison Mere na kutambulishwa mbele ya mashabiki, katika onyesho lililofanyika hivi karibuni, kwenye ukumbi wa Zamba Playa.

Ukumbi huo ulioko mjini Kinshasa, ndio unaotumiwa na kundi hilo kufanya mazoezi na pia ndio uliotumika kumtambulisha Sarah Solo, ambaye aliwahi kufanya shughuli za muziki nchini Ivory Coast, kwa miaka kadhaa, akiwa mwanamuziki wa kujitegemea.

Katika onyesho hilo, Werrason alitumia dakika kama 10, kumtambulisha Sarah, akielezea uwezo na umahiri wake wa kupiga gita la solo na kuimba huku mashabiki wakimsikiliza kwa makini.

Baadaye Werrason alimpa nafasi mwanamama huyo ya kuwasalimia mashabiki. Akazungumza maneno machache kisha akalifuata gita la solo mahali lilipokuwa, akalivaa mwilini huku akilitazama kwa makini kama mtu anayeajabia kitu fulani.

Werrason akamtazama binti huyo kwa makini kisha akatabasamu na kutamka neno moja 'solo'. Sarah akaitikia kwa kupiga mdonoo mmoja wa gita. Werrason akaita tena kwa mara ya pili 'solo'. Sarah akajibu kwa kupiga mdonoo wa pili wa gita.

Ni kuanzia hapo mashabiki wakaanza kulipuka mayowe ya kumshangilia. Kuona hivyo, Werrason akawauliza wanataka mipigo gani ya solo kutoka kwa Sarah. Bila kumung'unya maneno wakamjibu kwa pamoja 'Sebene'.

Hapo ndipo Sarah alipoanza kuonyesha kuwa sio wa mchezo mchezo. Akaanza kufanya mavitu yake kwa kulipiga gita hilo kwa umahiri mkubwa na kuwafanya mashabiki wapagawe.

Katika onyesho hilo la utambulisho, mwanadada huyo alipiga gita hilo kwa
kunakili nyimbo zilizopigwa na wacharaza magita wa bendi hiyo, ambao aidha bado wanaitumikia ama walishaondoka, kama vile Flammi Kapaya, Kimbangu, Burkina Wasewa ‘Mbokalia’ na wengineo.

Ilikuwa raha iliyoje kumshuhudia mwanamama huyo akilidonoa gita hilo kwa staili za kuvutia huku baadhi ya mashabiki wakiufananisha umahiri wake huo na ule waliokuwa nao wakongwe Diblo Dibala, Dally Kimoko na Nene Tchakou.

Sarah, aliyekuwa amevalia blauzi iliyoungana na kaptula ya rangi ya kahawia, na ambaye hupenda kusuka nywele zake kwa staili ya mabutu, alikoleza starahamu ukumbini kwa kupiga gita hilo huku akiwa anayumba stejini, mithili ya mtu aliyetaka kuanguka.

Werrason akatoa ishara ya kusimamisha muziki kisha akaanza kuimba kibwagizo cha moja ya nyimbo zake maarufu. Baadaye akatoa ishara ya muziki kuendelea. Sarah akaendelea kufanya mavitu huku akitikisa kichwa chake na kurusha miguu yake huku na huko.

Baadhi ya mashabiki walishindwa kuvumilia, wakavamia stejini na kuanza kumtuza fedha lukuki huku wengine wakicheza kwa kufuatisha mapigo ya ala na kumshangilia kwa nguvu.

Wapiga picha nao wakawa wakipigana vikumbo stejini ili kupata picha nzuri za mwanamama huyo akiwa anacharaza gita la solo. Kwa hakika ilifurahisha kumkodolea macho.

Ili kudhihirisha kwamba Sarah hakuwa wa kawaida, Werrason akampa nafasi ya kuonyesha uwezo wake wa kuimba na kupiga gita. Naye hakufanya ajizi. Akawaongoza wanamuziki wenzake kupiga kibao cha Nakei Nairobi cha kundi la Afrisa International, kilichoimbwa na mkongwe Mbilia Bel.

Mshangao waliokuwa nao mashabiki kwa Sarah, pia ndio waliokuwa nao wanamuziki wa Wenge Musica Maison Mere. Baadhi ya wakati wanamuziki hao walijikuta wakimkodolea macho mwanadada huyo mithili ya watu waliokuwa wakistaajabu kumuomba kiumbe mpya aliyeteremshwa na Mola moja kwa moja kutoka mbinguni.

Sarah alizaliwa katika Jiji la Kinshasa na kuanza shughuli za muziki akiwa na umri wa miaka 12. Bendi yake ya kwanza ilikuwa Lavoniora Esthetique, iliyokuwa ikiongozwa na Dakumuda New Man.

Baada ya kudumu kwenye bendi hiyo kwa miaka saba, alijiunga na bendi ya Bana Ok inayoongozwa na mkongwe, Lutumba Simaro hadi mwaka 2012, alipoamua kuhamia nchini Ivory Coast kwa lengo la kusaka mafanikio zaidi.

Akiwa nchini humo, Sarah aliamua kuwa mwanamuziki wa kujitegemea, akirekodi na wanamuziki mbalimbali wa DRC waliokwenda huko kufanya maonyesho ya muziki.

Akimuelezea mwanadada huyo, Lutumba alisema ni mwenye uwezo wa kuelewa mafundisho kwa haraka na pia msikivu na mwenye adabu na tabia njema.

Sunday, April 9, 2017

HATIMAYE ROMA MKATOLIKI APATIKANA AKIWA MZIMA WA AFYA


HATIMAYE kitendawili cha kutekwa kwa msanii nyota wa muziki za bongo fleva, Ibrahim Mussa, maarufu kwa jina la Roma Mkatoliki kimeteguliwa baada ya jana kuonekana katika kituo cha polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam.

Roma na wenzake wawili, waliodaiwa kutekwa hivi katibuni, walionekana kituoni hapo wakihojiwa na polisi kuhusu kutoonekana kwao kwa zaidi ya siku tano.

Madai ya kutekwa kwa wasanii hao, ambayo yalitapakaa kila kona ya nchi na kuzua taharuki miongoni mwa mashabiki, yalisababisha baadhi ya wasanii kupatwa na wasiwasi kuhusu hatma ya maisha yao na kulitaka Jeshi la Polisi kuwatafuta kwa udi na uvumba.

Chanzo cha kuaminika kutoka kwenye kituo hicho cha polisi kilieleza kuwa, Roma na wenzake hao walifikishwa kituoni hapo asubuhi. Hata hivyo, hakikueleza walifikishwa kituoni hapo kwa tuhuma zipi.

" Ni kweli kuwa Roma na wenzake wapo hapa na wapo katika hali nzuri. Kinachofanyika sasa ni kuwahoji ili kujua walikuwa wapi na kama ni kweli walitekwa na hao waliowateka ni kina nani,"kilisema chanzo hicho.

Hadi ilipofika saa 11 jioni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Suzan Kaganda hakuweza kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo.

Roma na wenzake wanadaiwa kutekwa nyara wakati walipokuwa kwenye studio za Tongwa Records, Dar es Salaa, Ilidaiwa kuwa, watu waliowateka pia waliondoka na kompyuta na seti ya televisheni ya studio hiyo.


YANGA YAPATA USHINDI MWEMBAMBA KWA WAALGERIA


BAO lililofungwa na kiungo Thabani Kamusoko jana liliiwezesha Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya MC  Alger ya Algeria katika mechi ya awali ya hatua ya mtoano ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Kamusoko alifunga bao hilo dakika ya 61 kwa shuti kali baada ya gonga safi kati yake, Haruna Niyonzima na Simon Msuva.

Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa inahitaji sare ya aina yoyote timu hizo zitakaporudiana wiki ijayo mjini Algiers.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa soka wameilaumu Yanga kwa kushindwa kuondoka uwanjani na ushindi mkubwa wa mabao kwa vile wapinzani wao walicheza kwa kasi ndogo huku wakionekana dhahiri kutafuta sare.

Katika mechi hiyo iliyohudhuriwa na mashabiki wachache, Yanga ilipata nafasi nzuri kadhaa za kufunga mabao, lakini zilipotezwa na washambuliaji wake, Obrey Chirwa, Deus Kaseka na Msuva kutokana na kukosa umakini kila walipolikaribia lango la wapinzani wao.

MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AWAALIKA SERENGETI BOYS NYUMBANI KWAKE KWA AJILI YA CHAKULA USIKU












Monday, April 3, 2017

SIMBA YAPIGWA MWELEKA 2-1 NA KAGERA SUGAR


MATUMAINI ya Simba kutwaa taji la ligi kuu ya Tanzania Bara yameanza kuota mbawa baada ya kupigwa mweleka wa mabao 2-1 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Kipigo hicho kimeifanya Simba iendelee kushika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 55, nyuma ya mabingwa watetezi Yanga wanaoongoza kwa kuwa na pointi 56.

Washambuliaji wa zamani wa Simba, walioachwa kwa madai ya viwango vyao kushuka, Mbaraka Yussuf na Christopher Edward, ndio waliopeleka kilio Msimbazi baada ya kuifungia Kagera Sugar mabao hayo mawili.

Mbaraka, mchezaji kinda kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa  Stars, aliifungia Kagera Sugar bao la kwanza dakika ya 27 kwa shuti kali lililomshinda kipa Daniel Agyei wa Simba. Bao  hilo lilidumu hadi mapumziko.

Christopher, aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 50 baada ya gonga safi kati yake na washambuliaji wenzake wa Kagera.

Bao la kujifariji la Simba lilifungwa na Muzamil Yassin dakika ya 65 baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la Kagera.

Simba ilijitahidi kucheza kufa na kupona ili kusawazisha, lakini kikwazo kikubwa kilikuwa kipa wa zamani wa timu hiyo, Juma Kaseja, aliyekaa imara kwenye lango la Kagera.

Sunday, April 2, 2017

YANGA YAIENGUA SIMBA KILELENI MWA LIGI KUU


BAO lililofungwa na mashambuliaji Obrey Chirwa katika kipindi cha pili, jana liliiwezesha Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo uliiwezesha Yanga kuiengua Simba kileleni mwa ligi hiyo, baada ya kufikisha pointi 56. Simba inashika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 55.

Hata hivyo, Simba inaweza kurejea kileleni mwa ligi hiyo leo, iwapo itaishinda Kagera Sugar, katika mechi nyingine ya ligi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

SERENGETI BOYS YAITUNGUA TENA BURUNDI



TIMU ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys imeendeleza wimbi la ushindi katika mechi zake za kirafiki baada ya  kuifunga Burundi mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa Serengeti Boys baada ya juzi kuichapa Burundi mabao 3-0 katika mchezo mwingine wa kirafiki.
Katika mechi hiyo, Kocha Bakari Shime, anayefanya kazi chini ya Mshauri wa Ufundi, Kim Poulsen, alifanya mabadiliko makubwa kikosini mwake, akiwapa nafasi zaidi wachezaji ambao hawakucheza mechi ya kwanza.
Wafungaji wa mabao ya Serengeti Boys walikuwa Issa Abdi Makamba dakika ya 36 na Ibrahim Abdallah Ali dakika ya 89.
Serengeti Boys ilitawala sehemu kubwa ya mchezo huo huku wapinzani wao wakicheza rafu nyingi. 
Serengeti Boys imerejea Dar es Salaam, ambako kesho watakuwa na mchezo wa mwisho wa kirafiki dhidi ya Ghana, kabla ya kwenda Morocco kwenye kambi ya mwezi mmoja, kujiandaa na fainali za U-17 Afrika, Mei mwaka huu nchini Gabon.