KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, April 15, 2017

SIMBA, TOTO HATUMWI MTOTO DUKANI LEO


VINARA wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba leo wanateremka dimbani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, kumenyana na Toto Africans.

Simba inashuka dimbani kucheza mechi hiyo, ikiwa ni siku chache baada ya kuichapa Mbao FC mabao 3-2 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja huo Jumatano iliyopita.

Kabla ya kucheza na Mbao, Simba ilikuwepo mjini Bukoba, ambako ilimenyana na Kagera Sugar na kuchapwa mabao 2-1, lakini ikaambulia ushindi wa mezani baada ya kubainika kuwa, wapinzani wao walimchezesha mchezaji aliyekuwa na kadi tatu za njano.

Katika mechi ya leo, Simba imepania kuifunga Toto African ili kujiimarisha zaidi kileleni mwa ligi hiyo na hivyo kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa, ambao imekuwa ikiukosa kwa miaka mitatu sasa.

Hata hivyo, mechi hiyo haitarajiwi kuwa nyepesi kwa Simba kwa vile Toto African nayo itacheza kufa na kupona ili kujinasua katika janga la kushuka daraja.

Katika mechi ya awali iliyochezwa Oktoba, mwaka jana, mjini Dar es Salaam, Simba iliinyuka Toto mabao 3-0.

Simba inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 61, baada ya kucheza mechi 26, ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 56 baada ya kucheza mechi 25.

No comments:

Post a Comment