KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, April 9, 2017

HATIMAYE ROMA MKATOLIKI APATIKANA AKIWA MZIMA WA AFYA


HATIMAYE kitendawili cha kutekwa kwa msanii nyota wa muziki za bongo fleva, Ibrahim Mussa, maarufu kwa jina la Roma Mkatoliki kimeteguliwa baada ya jana kuonekana katika kituo cha polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam.

Roma na wenzake wawili, waliodaiwa kutekwa hivi katibuni, walionekana kituoni hapo wakihojiwa na polisi kuhusu kutoonekana kwao kwa zaidi ya siku tano.

Madai ya kutekwa kwa wasanii hao, ambayo yalitapakaa kila kona ya nchi na kuzua taharuki miongoni mwa mashabiki, yalisababisha baadhi ya wasanii kupatwa na wasiwasi kuhusu hatma ya maisha yao na kulitaka Jeshi la Polisi kuwatafuta kwa udi na uvumba.

Chanzo cha kuaminika kutoka kwenye kituo hicho cha polisi kilieleza kuwa, Roma na wenzake hao walifikishwa kituoni hapo asubuhi. Hata hivyo, hakikueleza walifikishwa kituoni hapo kwa tuhuma zipi.

" Ni kweli kuwa Roma na wenzake wapo hapa na wapo katika hali nzuri. Kinachofanyika sasa ni kuwahoji ili kujua walikuwa wapi na kama ni kweli walitekwa na hao waliowateka ni kina nani,"kilisema chanzo hicho.

Hadi ilipofika saa 11 jioni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Suzan Kaganda hakuweza kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo.

Roma na wenzake wanadaiwa kutekwa nyara wakati walipokuwa kwenye studio za Tongwa Records, Dar es Salaa, Ilidaiwa kuwa, watu waliowateka pia waliondoka na kompyuta na seti ya televisheni ya studio hiyo.


No comments:

Post a Comment