KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 5, 2013

TUNAMLILIA MANGWEA BAADA YA KUFA!


NA STEPHEN BALIGEYA

KAMA kuna kitu ambacho kimenipa kichefuchefu, kunitia kinyaa na kunijengea dhambi ya chuki juu ya baadhi ya watu wanaojinasibisha wema mbele za uso wa dunia na Watanzania, basi ni kifo cha msanii Albert Mangwea.

Niliwasikiliza kwa umakini na wamenifanya nitakafakari na kunipa fursa ya kuchambua kwa umakini kiasi cha kuandika pia kwa umakini juu ya namna Watanzania walivyomlilia msanii huyo.

Ngwea, ‘Mzee wa mikasi’ kama nilivyopenda kumwita, ametutoka, amechoka kuishi kwa fitina, majungu, unafiki na uzandiki wa hapa duniani. Kwangu mimi naona amefanya uamuzi sahihi na makini wa kuamua kwenda kupumzika katika nyumba ya milele.

Nasema kachoka kuishi kwa unafiki, fitina, majungu na uzandiki kwa sababu, kinachozungumzwa na kufanywa juu yake leo, kama kingekuwa kinafanywa wakati yuko hai, inawezekana Mangwea asingechukua uamuzi wa haraka namna hii.

Si kwamba nasema Mangwea kajiua, hapana. Nasema Mangwea angeondoka kwa furaha zaidi kuliko huzuni aliyoondoka nayo. Ameondoka na huzuni huku manyang’au, wanafiki, wafitini na wazandiki wakibaki wakifaidi furaha yake.

Kwa nini baada ya Mangwea kuaga dunia ndipo kila kituo cha redio kinapiga nyimbo zake kwa wingi na kumsifia kuwa alikuwa akiimba nyimbo bora kabisa? Kwa nini wakati akiwa hai, nyimbo hizo zilikuwa hazisikiki katika baadhi ya vituo vya redio nchini?

Nimetafakari kwa kina jambo hili, ambalo limenitia kichefuchefu na kinyaa kisichomithilika. Kwa sababu wasanii wanategemea nyimbo zao kupigwa mara kwa mara katika vituo vya redio na televisheni ili waweze kujitangaza.

Nyimbo zao zinapigwa bure na vituo hivyo, lakini hawalipwi chochote. Hata katika kupigwa huko, bado nyimbo za baadhi ya wasanii akiwemo Mangwea zilikuwa nadra kupigwa.

Kimsingi, nyimbo za wasanii zinapokuwa zinapigwa kwenye redio na televisheni, husaidia vyombo hivyo vya habari kupata wasikilizaji na watazamaji wengi, ambao ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha na kuendeleza biashara zao.

Bila wasikilizaji na watazamaji, hakuna redio wala televisheni inayoweza kuwa na ubavu wa kushawishi watangazaji kufanya nayo kazi. Watatangaza vipi na redio na televisheni isiyokuwa na wasikilizaji wala watazamaji wa matangazo yao?.

Ndiyo maana leo kuna vipindi vya muziki, kila redio na televisheni inaweka mbinu za kuwa na wasanii ili iweze kusikilizwa na kuangaliwa na watu wengi ili wafanyabiashara nao wafurahie kuwapa matangazo.

Lakini wakati redio na televisheni zinapata mabilioni ya fedha kupitia wasanii, wahusika hawaingizi kitu. Kibaya zaidi wanaombwa hata fedha ili nyimbo zao ziweze kupigwa katika redio na televisheni.

Kinachokera zaidi ni kwamba bado kuna makupe wanaotumia fursa walizonazo kwenye redio kuwakandamiza wasanii. Wapo wanaokataa kupiga nyimbo za wasanii wanaokataa kunyonywa.

Msanii akikataa kuingia mikataba ya kunyonywa na makupe hao, adhabu yake ni nyimbo zake kutopigwa redioni wala kwenye televisheni wanazoziongoza. Msanii akigoma kwenda kwenye tamasha la makupe hao kwa kudai maslahi mazuri, tishio lake ni kutopigwa nyimbo zake au kutoalikwa kwenye matamasha mengine.

Mangwea alikuwa mmoja wa waathirika. Waliomfanya aishi maisha ya shida na tabu wakati akiwa msanii mkubwa, ndio hao walioubeba msiba wake na kujifanya walimpenda sana.

Wanamsifu kwa nyimbo na mapambio, wanamtukuza mtu aliyekufa, lakini walishindwa kumtukuza na kumsifu akiwa hai. Makupe hawa, ambao wamekuwa na tabia ya kunyonya wasanii, wamejifanya mama na baba wa Mangwea wakati wa mauti.

Walikataa kupiga nyimbo zake kama njia ya kumtangaza na kumfanya apate fursa nyingi za kimuziki. Walikataa kumwalika kwenye matamasha, ambayo wamekuwa wakiyaandaa kama njia ya kumpatia kipato, leo wanajigamba kuwa kijana huyu alikuwa mpole na hakuwa na ugomvi na watu.

Wanamsifu kwa upole wake, kwani wanajua kuwa upole huo ndio walioutumia kumfanya aishi kinyonge mpaka mauti yanamkuta. Walimfanya mbuzi wa kafara, ambaye nina imani kifo chake kitakuwa chachu katika kuleta mabadiliko katika fikra katika vichwa vya wasanii wengine.

Haiwezekani mtu afe ndipo nyimbo zake zinapigwa siku nzima, lakini wakati akiwa hai, nyimbo hizo hizo, ambazo zinasifiwa, zilikuwa hazisikiki wala kuzungumzwa kama zenye ubora. Ubora huo unakuja baada ya kufa kwake.

Unafiki, ujinga na upuuzi huu, ambao unazidi kuwa kasumba ya makupe kuwasifu waliokufa, unazidi kuwafanya watu waliokufa kwa sababu ya mateso yaliyojengwa na wazandiki hawa kumea.

Hebu fikiria, kama nyimbo hizo za Mangwea zingepigwa kama zinavyopigwa leo, angekuwa tajiri kiasi gani? Sifa anazopewa leo, angepewa miaka ya nyuma, angeshiriki matamasha mangapi, ambayo yangempatia fedha?

Leo kila mtoto anamfahamu Mangwea. Wanamfahamu kwa sababu kafariki dunia, lakini kabla ya hapo, waliomfahamu walikuwa wale waliofuatilia kazi zake tangu zamani. Ghafla Mangwea kawa maarufu kama enzi zake, kwa sababu tu amefariki dunia.

Nimesikiliza baadhi ya watangazaji walioko katika redio zilizoshiriki kuua majina ya wasanii wakimsifu Mangwea kwa namna, ambayo mpaka inakera. Wanajulikana namna walivyomfanya Mangwea awe mtumwa na ajutie kuwa msanii.

Nafsi zao zinajua namna walivyoshiriki kumuua Mangwea kiusanii na pengine hata kiroho, lakini leo wanajifanya ndio wasemaji wa Mangwea, ndugu wa Mangwea na familia ya Mangwea. Wanajaribu kuwaaminisha Watanzania kwamba ni watu wema na makini katika kazi zao.

Kwa jumla watu hawa wanatia kichefuchfeu kwani kama wasanii wetu wangekuwa wanatukuzwa namna hii wanapokuwa hai, wangekuwa matajiri kuliko kuwaua na kisha kujifanya tunawalilia siku ya msiba.

Maoni na ushauri 0752646938.

No comments:

Post a Comment