KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, June 5, 2013

INAUMA SANA


MAMIA ya wananchi jana walijitokeza kwa wingi kuuaga mwili wa msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Albert Mangwea kwenye viwanja vya Leaders vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam.

Miongoni mwa waliojitokeza kuuaga mwili wa msanii huyo ni pamoja na wasanii kadhaa maarufu wa muziki wa kizazi kipya na wasanii wa filamu nchini.

Baadhi ya wasanii hao ni pamoja na Naseeb Abdul 'Diamond', Khaleed Mohammed 'TID', Ommy Dimpoz, Ally Ahmed 'Madee', Khadija Shaaban 'Keysher', Akili The Brain, P Funky, Saidi Fela, Daf Assey, Bico Hoza, Dagmar Iddi, Mchizi Mox, Mez B, Mully B na Edward Muhoza.

Kwa upande wa wasanii wa filamu, walikuwepo Jacob Steven 'JB', Natasha, Yvonne Cherry 'Monalisa', Steve Nyerere, Mzee Magari, Raymond Kigosi 'Ray' na Mainda.

Ndugu wa marehemu walioshiriki katika shughuli ya kuuaga mwili wa Mangwea ni pamoja na dada yake, Consolata Mangwea, baba yake mdogo, David Mangwea na mama yake mdogo, Ellah Mangwea.

Shughuli za kuuaga mwili wa msanii huyo, aliyefariki dunia wiki iliyopita nchini Afrika Kusini, zilianza saa tatu asubuhi baada ya kuwasili kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam na kumalizika saa saba mchana chini ya usimamizi mkali wa jeshi la polisi.

Akisoma risala kwa niaba ya wasanii wenzake, msanii Mez B alisema kifo chake kimeacha pengo kubwa katika kundi lake la Chamber Squad.

Alisema walishirikina vyema na marehemu Mangwea kwa hali na mali huku wakitumia muda mwingi kujipanga kwa ajili ya kazi zao na maisha yao.

"Sijui niseme nini, lakini najua kila mtu anajua jinsi msiba huu ulivyotuchanganya kwani umetokea katika kipindi ambacho hatujatarajia licha ya kuwa kifo hutokea bila kujua saa wala dakika," alisema Mez B.

Gari lililobeba mwili wa marehemu na magari mengine yasiyopungua 30 likiwemo gari la doria na gari la kubeba wagonjwa, yaliondoka katika viwanja hivyo saa saba mchana na kuanza safari ya kwenda Morogoro.

IDD AZAN
Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan alisema aliposikia kifo cha msanii huyo na mazingira yake, alisikitika na kuamua kuacha shughuli za Bunge na kurudi Dar es Salaam kujumuika na waombolezaji wengine.

Azzan alisema kifo cha msanii huyo ni pigo kwa wasanii wa muziki nchini na hata wale waliokuwa wakifanya naye kazi katika kundi la Chamber Squad.

Alisema kifo cha masanii huyo kinatoa funzo kubwa kwa wasanii la kuwataka kuimarisha upendo na ushirikiano kwao bila kujali wanatoka katika makundi gani.

Alisema uhusiano baina ya wasanii utazidi kuwajenga na kuwafanya wawe kitu kimoja na kusaidiana katika shida na raha kama walivyofanya kwa Mangwea.

WASANII WA FILAMU
Jacob Steven 'JB' alisema kifo cha msanii huyo kinazidi kuwaumiza wasanii nchini kwani kimetokea wakati bado wasanii wakiwa na kumbukumbu ya kifo cha Steven Kanumba.

Hata hivyo, JB alisema yote hiyo ni mipango ya Mungu na kuongeza kuwa, hakuna kiumbe kitakachobaki hai.

Raymond Kigosi 'Ray' alisema ameshukuru kuona ushirikiano mkubwa ulioonyeshwa baina ya wasanii wa filamu na muziki katika kufanikisha shughuli za maandalizi ya msiba huo.

Alisema wasanii wamejitoa na kuhakikisha mwenzao anakwenda kupumzika katika nyumba yake ya milele kwa kupata heshima zote alizostahili katika jamii.

WASANII WA MUZIKI
Khaleed Mohamed 'TID' alisema haamini kama kweli Mangwea na rafiki yake wa karibu amefariki, lakini tukio la kuaga limemfanya kuamini na kukubali matokeo.

"Nakubali kilichotokea na ninajua ni mapenzi ya Mungu na hakuna mtu yeyote katika dunia hii atakayeepuka kifo," alisema TID.

TID alisema anasikia uchungu kuona jinsi mama wa marehemu atakavyopata tabu na uchungu kwa kumpoteza mtoto wake, lakini anaomba awe mvumilivu na kumshukuru Mungu.

Alisema akiwa rafiki wa karibu wa marehemu, atahakikisha anakuwa bega kwa bega na mama wa marehemu katika kipindi hiki kigumu na kutoa msaada wa hali na mali.

MAZIKO
Marehemu Mangwea anatarajia kuzikwa leo mjini Morogoro nyumbani kwa mama yake mzazi.

Mangwea alifariki Mei 28 nchini Afrika Kusini na kusafirishwa hadi Dar es Salaam na kuwasili Juni 4 mwaka huu kabla ya kuagwa jana na kusafirishwa kwenda Morogoro.

Wakati huo huo, Shirikisho la Wanamuziki Tanzania limesema limepokea kwa majonzi makubwa taarifa za kifo cha msanii Albert Mangwea kilichotokea nchini Afrika Kusini.

Rais wa shirikisho hilo, Addo Mwasongwe alisema jana kuwa, kifo hicho ni pigo kubwa kwa tasnia ya muziki wa kizazi kipya nchini kutokana na umahiri aliokuwa nao katika fani hiyo.

"Marehemu tutamkumbuka kwa mengi, hasa msimamo aliouonyesha katika mambo aliyoyaamini. Alikuwa ni mtu mwenye jitihada kwani hadi mauti yalipomfika, alikuwa katika jitihada za kujitafutia riziki,"alisema.

Addo alisema shirikisho lake limeshirikiana vyema na kamati ya mazishi katika kuhakikisha shughuli ya kuuaga mwili wa msanii huyo inafanyika kwa mafanikio.

Aliwashukuru Watanzania kwa heshima waliyompa Mangwea katika safari yake ya mwisho na kuongeza kuwa, kitendo hicho kimewafariji.

Addo pia aliishukuru serikali, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Zitto Kabwe (mbunge) na Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia, January Makamba kwa jitihada walizozifanya kuhakikisha mwili wa Mangwea unarejeshwa nchini.

Rais huyo wa shirikisho la muziki alivilaumu vyombo vya habari nchini kwa kuripoti taarifa kuhusu kifo cha msanii huyo kabla ya mwili wake kufanyiwa uchunguzi.

"Maadam kuna ripoti ya daktari kuhusu uchunguzi wa kifo hicho, ingekuwa busara kuisubiri familia yake iitoe hadharani iwapo itapenda kufanya hivyo,"alisema Addo.

No comments:

Post a Comment