KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, June 14, 2013

KIFO CHA MANGWEA KIWE DIRA KUPAMBANA NA MANYANG'AU



NA STEPHEN BALIGEYA
NIMEFARIJIKA sana, nimefurahishwa sana na nimepata nguvu sana. Watanzania wamenifanya nijisikie hivyo, wamenipa ujasiri wa kugeuza mlima kuwa tambarare. Kweli nawashukuru sana.

Hali hiyo inatokana na kile nilichokiandika wiki iliyopita juu ya kifo cha Albert Mangweha. Kifo ambacho niliuliza kwa nini watu wanamlilia na kumsifu kwa maneno matamu baada ya kufa na wakati walishindwa kufanya hivyo akiwa hai?

Nikauliza tena, kwa nini baadhi ya redio zilishiriki kumuua Mangweha kisanii wakati wa uhai wake kwa kukataa kupiga nyimbo zake lakini baada ya kuaga dunia zikajifanya zilimpenda sana na kusifu uwezo wake kiusanii?

Niliuliza, kama redio hizo zingepiga nyimbo za Mangweha kama zilivyopiga wakati wa msiba wake, msanii huyo angekuwa tajiri kiasi gani kwa kupata matamasha na kuuza kazi zake ambazo zimetangazwa sana baada ya kufa?

Katikati ya dimbwi la kufikiria juu ya kifo hicho, nimepata simu nyingi na ujumbe wa maandishi kiasi cha kutisha. Kumbe Watanzania wana dukuduku lakini watasemea wapi?

Taaluma ya habari ni kazi ya jamii. Unafanya kazi kwa maslahi ya jamii pana na si kulitumikia kundi dogo, ambalo linanenepa kwa damu za walio wengi. Kazi ya taaluma hii ni kuwa msemaji na mtetezi wa jamii.

Leo napenda kutoa somo kwa wasanii, ambao kwa kuchukua kifo cha Mangweha kama darasa, wanatakiwa sasa kuamka.

Kuamka huko kuwe na mtazamo mpana miongoni mwao, kwa kutambua kwamba leo mwenzao amefariki kama ngao ya ukombozi wao. Kifo cha Mangweha kiwe kama sadaka ya ukombozi kwao.

Lazima wafikirie namna wenye mabavu watakavyowatumia baada ya kuaga dunia na namna watu hao watakavyonufaika baada ya kuwekwa kaburini.

Kifo cha Mangweha kimeonyesha usanii na unyang’au wa wenye redio, ambao walimtumia Mangweha kama njia ya kuongeza umaarufu wa vituo vyao, lakini pia kujitafutia maslahi zaidi.

Wale walioshiriki kumuua Mangweha kiusanii kiasi cha kumfanya aishi maisha magumu na ya shida, wakafikia hatua ya kusafiri hadi Afrika Kusini ili kuwapasha namna Mangweha alivyofariki.

Wakadiriki kwa mbinu za kimafia kukanusha hata taarifa ya daktari juu ya mwili wa msanii huyo kukutwa na chembe za dawa za kulevya. Kwa nini walikanusha habari za namna hiyo?

Jibu ni rahisi. Kwa sababu msanii huyo alipata msongo wa mawazo kutokana na kazi zake kutupiliwa mbali na hao, ambao wamejifanya ndugu zake.

Msongo huo wa mawazo ulimfanya msanii huyo kujifariji kwa kutumia dawa za kulevya. Lazima Watanzania watambue kwamba kama mtu anakosa mshauri wa haraka wakati anapata msongo wa mawazo, anaweza kutumia njia yoyote iwe halali au haramu kujifariji.

Mangweha alikuwa mhanga wa tatizo hilo. Akajifariji kwa kile kinachoelezwa dawa za kulevya. Marafiki wake wa karibu wanalieleza hili kwa ufasaha. Ripoti ya uchunguzi inaeleza haya kwa ufasaha.

Wale walioshiriki kumuua kwa msongo wa mawazo wakajitosa kupotosha ukweli huu kwa vile walijua fika kwamba kitendo hicho kitawatia fedheha.

Lakini kwa vile hawana soni katika nyuso zao na mioyo yao, wakajifanya wasemaji wa familia ya Mangweha. Wakawateka baadhi ya ndugu wawe wasemaji kupitia redio zao. Huku kote ni kuzidi kuonyesha uibilisi wao uliokamaa.

Tabia hii ya kishetani haikuishia hapo. Bado wakajifanya watalaamu wa kualika wasanii katika redio zao ili wawe wanaeleza uzuri wa Mangweha, lakini nadiriki kusema kwamba wamefanikiwa kidogo maana Watanzania walio wengi wamenasua usanii huo.

Kifo cha Mangweha kiwe funzo kwa wasanii, ambao wamekuwa wakitumikishwa na watu hao, ambao wanasubiri wafe ili waweze kuwasimulia na kuwaeleza kwa uzuri, ambao hawawezi kuelezwa wakiwa hai.

Wananyimwa matamasha, wananyimwa nyimbo zao kupigwa kwenye redio za manyang’au hao, lakini wanasubiri wasanii, ambao wanatumia nafasi hiyo kama ajira badala ya kuiba wafe ili waeleze uzuri wa marehemu.

Marehemu alikuwa mtu mzuri sana, marehemu alikuwa msanii wa kisasa, marehemu alikuwa na malengo makubwa, marehemu alikuwa mtu wa watu, marehemu alikuwa na singo aliyotaka kuachia na ujinga mwingine mwingi tu juu ya sifa za marehemu.

Leo wasanii wanapeleka nyimbo zao zinakaliwa kama hawatakubali masharti ya kinyonyaji. Msanii anatumiwa kwenye matamasha kwa sh. 100,000 na akidai malipo mazuri, anafungiwa duniani na kuzimu.

Matokeo yake wasanii wamekuwa vijibwa vya watu hao. Wasanii wamekuwa watumwa, wanatumikishwa kwa stahili zote, hata zile ambazo hawazitaki.

Wanavumilia upuuzi wote ambao unaua utu wao, lakini fadhila zao watazipata wakifa, pale watakaposifiwa na kunakishiwa kwa rangi zote. Huu ni ujinga ambao Watanzania wanatakiwa kuupinga.

Wasanii sasa waungane, waache kujiona kwamba kwa vile baadhi yao mambo yanawaendea vizuri, basi hawana haja ya kuungana na wenzao wanaouawa kisanii na magabachori hao.

Umoja wao utakuwa nguzo yao kuu kujikomboa, utengano wao utashuhudia sifa zao baada ya kufa, sifa ambazo zitakuwa mithili za malaika aliyeishia duniani.

Lazima wapiganie sifa hizo wapewe wangali hai, hali itakayowasaidia kuinua vipato vyao, kwa maslahi yao, familia na taifa kwa jumla.

Lazima wajiulize ni wasanii wangapi wamekufa kisanii kwa sababu ya uhuni wa watu hao, ambao bado wanaendeleza mapambano kwa wasanii wenye fikra hai?

Kama mgogoro unaofukuta leo na baadhi ya wasanii ungekuwa unahusu wasanii wadogo, kifo cha wasanii hao kingekuwa karibu lakini kazi bado imekuwa ngumu kwao.

Naandika haya si kwa maslahi ya wasanii na umma wa Watanzania kwa jumla, kwani watoto wenye vipaji wanatoka katika jamii zetu, hawana ajira na wanategemea vipaji vyao kujiajiri.

Taifa haliwezi kuendelea kwa watu wote kufanyakazi ofisini. Kazi ya sanaa itaajiri watu wengi kama kutakuwa na fursa sawa kwa vijana hao kufanya kazi zao na kunufaika na kazi zao.

Kwa msingi huo, wasanii na jamii nzima lazima kuungana kupambana na watu hawa ambao wanadhani wako juu ya sayari nyingine katika kuua vipaji vya vijana na kisha wawatumie katika vifo vyao.

Kwa maoni na ushauri, 0752646838,0713976894.

No comments:

Post a Comment