'
Sunday, June 16, 2013
TAIFA STARS YACHAPWA 4-2 NA IVORY COAST
MATUMAINI ya timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014 leo yameyeyuka baada ya kuchapwa mabao 4-2 na Ivory Coast katika mechi ya kundi C iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kipigo hicho kimeifanya Taifa Stars iporomoke nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi tano, ikiwa nyuma ya Ivory Coast inayoongoza kwa kuwa na pointi 13, ikifuatiwa na Morocco yenye pointi nane. Gambia inashika mkia kwa kuambulia pointi moja.
Licha ya kufungwa, Taifa Stars ilionyesha kiwango cha juu cha soka na magoli yake yalikuwa ya kifundi zaidi ikilinganishwa na wapinzani wao, ambao mabao yao yalitokana na makosa ya kizembe ya mabeki wa Tanzania.
Mshambuliaji Yaya Toure anayechezea klabu ya Manchester City ya England ndiye aliyeibeba Ivory Coast baada ya kuifungia mabao mawili kati ya manne.
Taifa Stars ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya kwanza mfungaji akiwa Amri Kiemba baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mbwana Samatta kufuatia mpira wa kurushwa na Erasto Edward Nyoni kusababisha kizazaa langoni mwa Tembo wa Abidjan.
Ivory Coast ilisawazisha bao hilo dakika ya 15 kupitia kwa Lacina Traore baada ya mabeki wa Stars kuzembea kuokoa na Yaya Toure akafunga la pili kwa mpira wa adhabu dakika ya 23, nje kidogo ya eneo la hatari.
Stars ilirudi mchezoni na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 35 mfungaji Ulimwengu aliyeunganisha krosi maridadi ya Shomary Kapombe. Hata hivyo, Ivory Coast wakapata penalti rahisi baada ya Gervinho kujiangusha wakati anakabiliana na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ . Bao hilo lilifungwa na Yaya Toure dakika ya 43.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mdenmark, Kim Poulsen dakika ya 87 kumtoa kiungo Mwinyi Kazimoto na kumuingiza mshambuliaji Vincent Barnabas yaliigharimu Tanzania kwa kufungwa bao la nne na kupotea kabisa mchezoni.
Baada ya kutoka Kazimoto, aliyetekeleza majukumu yake vizuri leo, Ivory Coast wakatawala sehemu ya kiungo na kutengeneza bao la nne lililofungwa na Bonny Wilfred dakika ya 88.
Taifa Stars: Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomary Kapombe/Khamis Mcha dk 85, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Mwinyi Kazimoto/Vincent Barnabas dk 87, Salum Abubakar, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta na Amri Kiemba.
Ivory Coast: Boubakar Barry, Arthur Boca, Didier Zakora, Solomon Kalou/Sio Giovanni, Gervais Yao, Jean Jarques Gosso Gosso, Alain Aurier, Lacina Traore/Bonny Wilfred, Yaya Toure, Geoffrey Serey na Suleiman Bamba/Nori Koffi Christian.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment