'
Friday, June 14, 2013
MTIBWA YAITEGA YANGA
UONGOZI wa klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro umesema hauna mpango kupokea mchezaji yoyote kutoka Yanga kwa ajili ya kumsajili kwa mkopo.
Mratibu wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, hawako tayari kufanya makubaliano ya aina hiyo na Yanga kwa sababu viongozi wake vigeugeu.
Bayser alisema wamefikia uamuzi huo kutokana na viongozi wa Yanga kuwageuka msimu uliopita kwa kumuuza kipa Shaaban Kado kwa klabu nyingine bila ridhaa yao.
"Hivi sasa tuko makini sana na Yanga. Msimu uliopita walikuja kwetu na kumtaka Said Bahanuzi, tukawapa kwa masharti kwamba watupatie Shaaban Kado kwa mkopo, lakini wakaja kumuuza bila ya kutupatia taarifa,"alisema.
Kutokana na kufanyiwa kitendo hicho, Bayser alisema hawako tayari kuingia makubaliano yoyote na viongozi wa Yanga kuhusu usajili wa wachezaji wao.
"Kuanzia msimu ujao, hatutamsajili mchezaji yoyote kutoka Yanga kwa mkopo kwa vile viongozi wake vigeugeu na tumekuwa tukishindwa kuwaelewa,"alisisitiza.
Akizungumzia usajili wa kikosi chake, Bayser alisema kazi hiyo inaendelea vizuri na imekuwa ikifanyika kwa umakini mkubwa ili kuepuka kufanya makosa.
Bayser alisema usajili wao utalenga zaidi kuziba mapengo ya wachezaji waliohama na wale, ambao kiwango chao kimeshuka.
Hadi sasa, Mtibwa Sugar imewapoteza mabeki wake wa kati, Issa Rashid, alisajiliwa na Simba na Rajab Zahir, aliyesajiliwa na Yanga.
Hata hivyo, Bayser amesema hawana taarifa yoyote kuhusu klabu za Simba na Yanga kuwasajili wachezaji hao wawili kwa vile hazijafuata taratibu za kuwahamisha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment