KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, January 30, 2016

SIMBA YAFUFUA MATUMAINI YA UBINGWA, YAITANDIKA AFRICAN SPORTS 4-0, YANGA HOI KWA COASTAL UNION




TIMU kongwe ya soka ya Simba jana ilifufua matumaini ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuitandika African Sports mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wakati Simba ikiibuka na ushindi huo mnono, watani wao wa jadi Yanga walipigwa mweleka wa mabao 2-0 na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Ushindi wa Simba umeiwezesha kufikisha pointi 36 baada ya kucheza mechi 16, wakati Yanga inaendelea kubaki na pointi 39 sawa na Azam.

Simba ilipata bao lake la kwanza dakika ya 14 kupitia kwa mshambuliaji Mganda, Hamisi Kiiza aliyefumua shuti kali kwa mguu wa kushoto baada ya pasi ya beki Hassan Kessy.


Kessy mwenyewe akafunga dakika ya 30 kuipatia Simba SC bao la pili kwa shuti la mguu wa kulia akimalizia pasi ya mshambuliaji Ibrahim Hajib na kumchambua vizuri kipa Zakaria Mwaluko.


Kiiza akamlamba chenga kipa Mwaluko baada ya kupata pasi ya kiungo Mwinyi Kazimoto kuifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 42.


Hajji Ugando akaifungia Simba SC bao la nne dakika ya 75 baada ya kupokea nzuri ya kiungo aliyekuwa katika kiwango kizuri jana.

 
Wakati huo huo, Yanga SC imefungwa mabao 2-0 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na matokeo hayo yanawafanya wabaki na pointi zao 39 baada ya kucheza mechi 16, sawa na Azam FC iliyocheza mechi 15.

Coastal Union walipata bao lao la kwanza dakika ya 27 kupitia kwa beki wa zamani wa Simba SC, Miraj Adam aliyefunga kwa shuti la mpira wa adhabu lililomparaza mikononi kipa Deo Munishi ‘Dida’ kabla ya kutinga nyavuni.


Refa Andrew Shamba wa Pwani aliwapa nafasi ya kupiga faulo Coastal Union, baada Miraj Adam mwenyewe kuangushwa na beki wa Yanga, Kelvin Yondan nje kidogo ya boksi.


Mshambuliaji chipukizi, Juma Mahadhi aliifungia bao la pili Coastal Union dakika ya 62 baada ya pasi nzuri ya Hamad Juma.


Bao hilo liliwavunja nguvu kabisa wachezaji wa Yanga SC na kujikuta wanacheza bila malengo. 


Refa Andrew Shamba alimtoa kwa kadi nyekundu beki wa Yanga, Kevin Yondan dakika ya 100.

Awali, dakika ya 97 Shamba alijichanganya kwa kumuonyesha kadi nyekundu Said Jeilan badala ya njano.

DIAMOND ASHINDA TUZO MBILI ZA HIPIPO


Mmiliki wa hit song ya ‘Utanipenda‘ Diamond Platnumz amezidi kuziandika headline katika ulimwengu wa sanaa baada ya usiku wa leo kuzinyakua tuzo mbili za Hipipo Awards zilizofanyika Uganda.

Ushindi alioupata ni Nyimbo bora Afrika Mashariki na Video bora Afrika Mashariki ambazo zote ni kupitia wimbo wa Nana.

Baada ya ushindi kupitia account yake ya Instagram Diamond aliandika maneno haya:

Wow! Realy wanna Thank GOD for keep blessing the innocent kid… also wana thank all Media and My Loyal fans for the Big love.. Two Awards tonight on @HipipoAwardsUGANDA…EAST AFRICA SUPER HIT#NANA and EAST AFRICA BEST VIDEO#NANA many thanks to my brother@2niteflavour
@i_am_godfather and all Behind this Hit!!!… thanks alot @HIPIPOAwards for keep supporting the real African talent!
(Wadau kijana wenu nimefanikiwa kushinda tunzo mbili Usiku wa leo kama NYIMBO BORA AFRICA MASHARIKI#NANA na VIDEO BORA AFRICA MASHARIKI #NANA nawashkuru sana kwa kura na support zote mnazoendelea kunipa….. tafadhali nisaidieni kuhesabu ni tunzo ngapi tumechkua tangu Mwaka 2016 uanze? ) shukran sana“

MAJALIWA AMWAGIZA NAPE AKUTANE NA VIONGOZI WA VYAMA VYOTE VYA MICHEZO

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongoza mbio za Wabunge za Hapa Kazi Tu Dodoma Half Marathon zilizoanzia Bungeni hadi uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Januari 30, 2016. Kushoyo kwake ni Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na kushoto ni Naibu Spika wa Bunge, Dkt Tulia Ackson. Mwansasu (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi ufunguo wa pikipiki mshindi wa kwanza wa mbio za Hapa Kazi Tu Dodoma Half Marathon upande wa wanaume, Emmanuel Giriki kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Januari 30, 2016. 

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi zawadi ya Pikipiki mshindi wa kwanza upande wa wanawake wa Mbio za Hapa Kazi Tu Dodoma Half Marathon, Angela Davile (kulia) kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Januari 30, 2016.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuandaa kikao cha haraka na viongozi wa vyama vya michezo nchini ili wamueleze kila mmoja amejipanga vipi kuinua viwango vya michezo katika chama chake.

Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumamosi, Januari 30, 2016) wakati akizungumza na mamia ya viongozi na wakazi mbalimbali wa mkoa wa Dodoma ambao walishiriki mashindano ya mbio za nusu marathon (km. 21 na km. 5) zilizofanyika leo mjini Dodoma.

Mashindano hayo yalijulikana kama “HAPA KAZI TU HALF MARATHON” yamefanyika ikiwa ni sehemu ya kuhimiza uchapakazi miongoni mwa Watanzania lakini pia ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea kuadhimisha siku 100 za utendaji kazi tangu Rais John Pombe Magufuli alipoapishwa na kuanza kazi.

“Kuna maboresho yanaendelea ndani ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo lakini haya yote hayawezi kufanikiwa kama viongozi wa michezo hawajajipanga vizuri. Ninatakata niandaliwe kikao cha siku moja na viongozi wa vyama vya michezo nchini ili waje wanieleze kila mmoja amejipanga vipi kuinua hali ya mchezo wake,” alisema huku akishangiliwa.

Alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania kwa kuandaa mbio hizo muhimu za kuhimiza Watanzania kuchapa kazi, lakini pia ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kushiriki katika mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika baadaye mwaka huu huko Rio de Janeiro, Brazil.

“Tunataka tuondokane na kauli ya Tanzania kuwa ni kichwa cha mwendawazimu na nipende kusisitiza kuwa maandalizi haya yasiwe ya mwisho bali yawe ya muda mrefu kwa sababu tunaenda kushiriki mashindano ya dunia. Nasema tena, tuache utamaduni wa maandalizi ya kukurupuka,” alisisitiza.

Aliwataka wadau mbalimbali wajitokeze kusaidia taasisi za michezo.

Waziri Mkuu Majaliwa ambaye alishiriki mbio za km. 2.5 kuanzia saa 1 asubuhi, alikimbia kutoka eneo la Bunge hadi uwanja wa Jamhuri na kuzindua mashindano ya km. 21 saa 1:47 asubuhi na yale ya km. tano aliyazindua saa 1:51 asubuhi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alikabidhi pikipiki aina ya GSM kwa washindi wa kwanza wa nusu marathon, mabati 100 kwa washindi wa pili na mabati 40 kwa washindi wa tatu. Mshindi wa tatu hadi wa 10 kwa wanawake na wanaume walikabidhiwa fedha taslimu.

Washindi wa kwanza hadi wa tatu waliokabidhiwa zawadi na Waziri Mkuu upande wa wanawake ni  Anjelina Daniel (Pikipiki); Fadhila Salum (mabati 100) na Catherine Lange (mabati 40). Wote wanatoka mkoa wa Arusha.

Kwa wanaume walioshinda nafasi kama hizo ni Emmanuel Giniki (Katesh, Babati) aliyeshinda pikipiki; Gabriel Gerald wa Arusha (mabati 100) na Fabian Joseph wa Arusha (mabati 40).

Wakati huo huo, Benki ya CRDB Dodoma ilitoa zawadi za sh. 250,000/- kila mmoja kwa washiriki watatu ambao ni walemavu walioamua kushiriki mbio hizo mwanzo hadi mwisho. Waliokabidhiwa zawadi hizo na Waziri Mkuu ni Bw. Hassan Hussein Sharif, Bw, Christian Ally Amour na Bw. Shukuru Khalfani.

Benki hiyo ilikabidhi pia vifaa vya michezo kwa ajili ya timu ya wabunge kwa ajili ya pambano la soka linalotarajiwa kufanyika leo saa 10 jioni kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma baina ya timu ya Bunge na timu ya CRDB. 

TFF YAMPONGEZA SAMATTA KUINGIA MKATABA NA GENK




Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi amempongeza mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” Mbwana Samatta kwa kufanikiwa kujiunga na klabu ya Racing Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini Ubeligiji.

Malinzi amempongeza Samatta kwa kupata nafasi ya kucheza ligi kuu ya Ubeligiji baada ya kusaini mkataba wa miaka mitatu na nusu kuichezea RC Genk inayoshika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini humo.

Kufuatia kupata nafasi hiyo, Malinzi amemtaka Samatta kujituma kwa nguvu zake zote na uwezo wake wote ili kuendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika nyanja za kimataifa na kwa sasa barani Ulaya.

Aidha Malinzi amewataka wachezaji wengine kujituma na kutumia nafasi wanazozipata katika vilabu vyao kwa kufanya vizuri na kupata nafasi ya kuvuka kwenda kucheza soka la kimataifa nchi za nje.

YASSODA AFUNGA KOZI YA MAKOCHA WA SOKA YA WANAWAKE


 Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mama Juliana Yassoda leo amefunga kozi ya ukocha wa wanawake ngazi ya juu (High Level Course) iliyoandaliwa na TFF kwa kushirikiana na FIFA.

Akiongea wakati wa kufunga kozi hiyo, Mama Yassoda amesema anaishukuru TFF/FIFA kwa kuona wanawake wanapata nafasi ya kushiriki kozi mbalimbali, ikiwemo kozi hiyo ya ukocha kwa ngazi ya juu kwa wanawake.

Mama Yassoda amewataka washiriki wa kozi hiyo kuyafanyia kazi mafunzo waliyopatiwa katika kuhamasisha wanawake wengi kuupenda mpira wa miguu na kuzalisha vipaji vya wachezaji wengi wa kike kuanzia ngazi za chini, na sio kuhitimu na kuweka vyeti ndani tu.

Naye Mariam Mchaina akiongea kwa niaba ya washiriki wenzake, ameishukuru TFF kwa kuwakumbuka wanawake na kuwapatia kozi hiyo ya ukocha, na kuahidi watakaporudi sehemu wanazoishi watatumia ujuzi walioupata kufundisha wanawake mpira miguu kwa ngazi zote.

Kozi hiyo ya ukocha kwa wanawake, ilianza Jumatatu na kumalizika leo ambapo jumla ya washiriki 25 wameshiriki kozi hiyo ya awali kutoka katika mikoa ya Dar es salaam, Iringa, Ruvuma, Pwani na Tanga na kupewa vyeti ya ushiriki na mpira kama kifaa cha kuanzia kazi ya ukocha.



Friday, January 29, 2016

HATIMAYE SAMATTA AMWAGA WINO KLABU YA GENK YA UBELGIJI, ATAMBULISHWA KWA WANAHABARI

Picha mbalimbali zikimwonyesha nahodha wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Mbwana Samatta akitambulishwa kwa waandishi wa habari baada ya kutia saini mkataba wa kuichezea klabu ya Genk ya Ubelgiji kwa miaka minne

LEO NI LEO LIGI KUU, YANGA KUKIPIGA NA COASTAL UNION, SIMBA KUIVAA AFRICAN SPORTS



Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwa michezo saba kuchezwa katika viwanja tofauti, ikiwa katika mzunguko wa 16 kwa kila timu kusaka pointi 3 muhimu katika raundi hiyo ya lala salama.

Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam siku ya Jumamosi, Simba SC watawakaribisha African Sports, JKT Ruvu watawakaribisha Majimaji FC uwanja wa Karume, huku Mtibwa Sugar wakiwakaribisha Stand United kwenye uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.

Jijini Tanga, Wagosi wa Kaya Coastal Union watakua wenyeji wa Young Africans uwanja wa Mkwakwani, Mwadui FC watakua wenyeji wa Toto Africans uwanja wa Mwadui Complex, huku wakata miwa wa Kagera Sugar wakicheza dhidi ya Mbeya City katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Ligi hiyo itaendelea siku ya Jumapili kwa mchezo mmoja ambapo Maafande wa Mgambo Shooting watawakaribsiha Ndanda FC kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

TFF YAKIRI KUFANYA MADUDU



SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limekiri kufanya madudu kwa kuiruhusu timu ya Azam kwenda Zambia huku Kuu Tanzania Bara ikiwa bado inaendelea.

TFF imeipa ruhusa ya Azam kwenda Zambia kushiriki michuano maalum kama sehemu ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika huku Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa bado inaendelea.


Hatua hiyo imezua tafrani kwa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara, na baadhi ya wadau wa soka wakipinga uamuzi huo huku baadhi ya klabu zikitishia kugomea mechi za Ligi.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Jamal Malinzi amekiri kuwepo kwa udhaifu huo na kusema kuwa kuondoka kwa Azam kumeathiri timu nyingine katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Naomba radhi kwa klabu zote 15 za Ligi Kuu Tanzania Bara, tunakiri huu ni udhaifu wa kuiruhusu Azam huku ligi ikiwa inaendelea, tunakubali tumefanya makosa na naomba klabu ziwe na utulivu,”alisema Malinzi.

Malinzi alisema kutokana na tukio hilo wanazihakikishia klabu hakutakuwa na mabadiliko yoyote katika ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kwamba Azam ndio itakayokuwa na wakati mgumu katika kulipa mechi zake za viporo.

Malinzi alisema Azam italazimika kucheza mechi mbili ndani ya wiki moja tofauti na timu nyingine ambazo zitakuwa zikicheza mechi moja kwa wiki. 


Alisema pia TFF itahakikisha kunakuwa na usawa wa michezo ili kupisha lawama za kupanga matokeo hivyo amezitaka timu kuondoa hofu juu ya jambo hilo.

“Azam ndio itakayoathirika zaidi katika jambo hili na tunaomba isije ikalalamika kwa kuwa hili wamelitaka wenyewe,”alisema.


 Malinzi Rais Malinzi amesema kamwe TFF haitarudia kosa hilo kwa kuipa ruhusa timu nyingine isafi ri huku Ligi ikiwa bado inaendelea. 

Malinzi amezitaka klabu kuzingatia kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufuata sheria zilizowekwa ili kuepusha usumbufu wa kuvuruga ratiba.

LIGI YA STARTIMES, SDL KUENDELEA LEO


Vita ya kuwania kupanda daraja msimu ujao itaendelea wikiendi hii kwa michezo 12 ya Ligi daraja la kwanza nchini (Startimes League) kuchezwa katika viwanja mbalimbali kwa makundi A, B, C, kwa kila timu kusaka pointi tatu muhimu.

Jumamosi uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, wenyeji Polisi Dodoma watakua wenyeji wa Africa Lyon, Kiluvya United wakiwakaribisha Mji Mkuu (CDA) katika uwanja wa Mabatini Mlandizi, Polisi Morogoro dhidi ya Kimondo FC uwanja wa Jamhuri, huku Kurugenzi ikiwakaribisha Burkinafaso kwenye uwanja wa Wambi mjini Mafinga.

JKT Mlale watawakaribisha Njombe Mji uwanja wa Majimaji mjini Songea, Panone dhidi ya Mbao FC uwanja wa Ushirikia Moshi, Polisi Mara watakua wenyeji wa Rhino Rangers uwanja wa Karume mjini Musoma, huku JKT Oljoro wakiwaribisha JKT Kanembwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Ligi hiyo ya StarTimes itaendelea siku ya Jumapili kwa michezo minne kuchezwa, Friends Rangers watakua wenyeji wa Ashanti United uwanja wa Karume, Polisi Dar dhidi ya KMC uwanja wa Mabatini Mlandizi, Lipuli wakicheza dhidi ya Ruvu Shooting uwanja wa Wambi Mafinga huku Polisi Tabora wakicheza dhidi ya Geita Gold uwanja wa Ali Hassani Mwinyi mjini Tabora.
 

Wakati  huo huo, ligi Daraja la Pili nchini (SDL) mzunguko wa pili unatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwa michezo 12 kuchezwa katika viwanja mbalimbali nchini, kwa timu nne za juu kutoka makundi A, B, C na D kusaka kupanda daraja msimu ujao.

Kundi A, michezo mitatu itachezwa ambapo Green Warriors watacheza dhidi ya Mvuvuma, Abajalo watawakaribisha Mirambo FC uwanja wa Ali Hassani Miwnyi Tabora, huku Transit Camp wakicheza dhidi ya Singida United uwanja wa Kambarage siku ya Jumapili.

Kundi B, Madini FC watakua wenyeji wa Alliance FC uwanja wa Mbulu, AFC Arusha watacheza dhidi ya Pamba uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha siku ya Jumapili, huku Bulyanhulu FC wakiwakaribisha JKT Rwamkoma siku ya Jumatatu uwanja wa Kambarage Shinyanga.

Kundi C, Leo Ijumaa Cosmopolitan watacheza dhidi ya Kariakoo uwanja wa Karume, Changanyikeni dhidi ya Mshikamano uwanja wa Karume siku ya Jumatatu, huku Abajalo wakicheza dhidi ya Villa Squad siku ya Jumanne.

Kundi D, Jumamosi Mbeya Warriors watacheza dhidi ya Sabasaba uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Mighty Elephant watacheza dhidi ya Mkamba Rangers siku ya Jumapili uwanja wa Majimaji mjini Songea, huku African Wanderes wakiwakaribisha Wenda FC uwanja wa Wambi Mafinga siku ya Jumatatu.

MWESIGWA AFUNGUA KOZI YA MAKOCHA WA SOKA YA WANAWAKE



Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Mwesigwa Selestine leo amefungua kozi ya ngazi ya juu ya ukocha kwa wanawake (High Level Coaching Course) iliyoandaliwa na TFF kwa kushirikiana na FIFA.

Akiongea na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa kozi hiyo, Mwesigwa amewataka washiriki wa kozi hiyo kuzingatia mafunzo hayo na kuitumia vyema fursa hiyo adimu waliyoipata.

Mwesigwa amewataka washiriki kuhakikisha kozi hiyo ya siku tano, inawasaidia na kwenda kuwa walimu wa mpira wa miguu kwa wanawake, na kuongeza mwamko kwa wanawake wengi kuupenda na kuucheza mpira wa miguu.

Aidha Mwesigwa, amewataka washiriki wa kozi hiyo kuzingatia maelekezo ya mkufunzi, nidhamu ya ndani na nje ya uwanja kwani imekua ni bahati nzuri kwao kupata nafasi ya kushiriki kozi hiyo ya ngazi ya juu.

Naye mkufunzi wa kozi hiyo anayetambulika na FIFA/CAF, Sunday Kayuni amesema atatumia uwezo wake wote kuhakikisha washiriki wa kozi hiyo wanajifunza na kuelewa vizuri mafunzo yake, ili waweze kuwa walimu wazuri watakapokwenda kuanza kufundisha.

Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Wanawake ya TFF, Amina Karuma ameishukuru TFF kwa kuendesha kozi hiyo  na kusema kupatikana waalimu wengi wa kike kutaongeza mwamko wa wanawake kuucheza mpira wa miguu.

Jumla ya washiriki 25 wanashiriki kozi hiyo kutoka mikoa mbalimbali nchini ambao ni Fatuma Omary, Esther Chabruma, AMina Mwinchum, Sweetie Charles, Pendo John, Berlina Mwaipungu, Mariam Mchaina, Elizabeth Sokoni, Sophia Mkumba, Marry Masatu, Aziza Mbwele, Fadhila Yusuph.

 Wengine ni Veneranda Mbano, Mariam Aziz, Hilda Masanche, Chichi Mwidege, Sophia Edward, Asha Rashid, Fatuma Khatibu, Neema Sanga, Hindu Muharami, Tatu Malogo, Komba Alfred, Veroinca Ngonyani, Judith nyatto na Ingfridy Kimaro.

Thursday, January 28, 2016

MWENYEKITI WA FA SIMIYU AFARIKI




Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Simiyu, Epaphra Swai amefariki dunia leo asubuhi katika hospitali ya Muhimbili jijini Dar es salaam.

TFF itawajulisha mipango ya msiba na mazishi ya marehemu Epaphra Swai baada ya kukaa na familia ya marehemu na kupanga utaraibu huo.

Bwana ametoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.

SIMBA YATISHIA KUGOMEA MECHI YAO NA YANGA


KLABU ya Simba imetishia kugombea mchezo wake wa mzunguko wa 20 wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga.

Simba imetoa tishio hilo endapo timu ya Azam na zinginezo, zinazoshiriki michuano hiyo, zitabakiwa na mechi za viporo mkononi.

Mchezo wa Simba na Yanga utachezwa katika mzunguko wa pili wa ligi hiyo, Machi mwaka huu. Katika mechi ya mzunguko wa kwanza, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilipigwa mweleka wa mabao 2-0.

Tishio hilo la Simba limekuja siku chache baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuiruhusu Azam kwenda Zambia, kushiriki katika michuano maalumu, huku ikiacha mechi za viporo dhidi ya Prisons na Ndanda.

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, TFF na Bodi ya Ligi Kuu zimevunja kanuni ya ligi kuiruhusu Azam kwenda Zanzibar.

Manara alisema Azam imekwenda Zambia kushiriki bonanza na kuacha kuendelea na ligi, hatua ambayo itaathiri timu zingine katika harakati za kutwaa ubingwa msimu huu.

Alisema TFF imevunja kanuni ya 9 ya kuahirisha mechi, ambapo kifungu (a), kinaeleza mchezo unaweza kuahirishwa endapo timu itakuwa na wachezaji kuanzia watano katika kikosi cha timu ya taifa.

Alisema kifungu (b) kinaeleza kuwa ili timu iweze kuahirisha mchezo wake ni lazima iwe na mechi ya kimataifa na taarifa zitolewe ndani ya siku sita kabla ya kushuka dimbani.

Manara alisema TFF haikupaswa kuiruhusu Azam kwenda Zambia kwa kuwa michuano inayokwenda kushiriki haitambuliwi na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Aidha, alisema sababu zilizotolewa na TFF kwamba Azam inakwenda huko kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Shirikisho nazo hazina mantiki.

Manara alisema wataiandikia barua TFF kutaka ratibaya ligi isibadilishwena ikifika mzunguko wa 20 kila timu ishuke dimbani kucheza.

"Isionekane mwingine anacheza mechi ya mzunguko wa 20 huku timu nyingine zikiwa na mechi za viporo, hatutacheza na tutaigomea ligi,"alisema.

Sunday, January 24, 2016

YANGA YAIFUATA SIMBA 16 BORA KOMBE LA SHIRIKISHO


MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga wametinga hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho, baada ya kuibanjua Friends Rangers mabao 3-0.

Katika mechi hiyo iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Yanga sasa imeungana na Simba kucheza hatua hiyo, baada ya juzi kuicharaza Burkina Faso mabao 3-0 mjini Morogoro.

Mshambuliaji Simon Msuva alikuwa wa kwanza kuzifumania nyavu dakika ya tano, akimalizia kona iliyochongwa na Issoufou Boubacar.

Dogo huyo aliiongezea Yanga bao la pili dakika ya 23 baada ya kupokea pasi safi ya Paul Nonga, ambaye naye alipewa pande maridhawa na Salum Telela.

Bao la tatu la Yanga lilifungwa kwa kichwa na Matheo Anthony, akimalizia  krosi ya Telela.

MANJI AMLIPUA TIBOROHA




TAARIFA KWA WANAYANGA KUPITIA VYOMBO YA HABARI
1. Baada ya kuupitia uamuzi wa Kamati ya Nidhamu kuamua sababu kuvunja mkataba kati ya klabu Yanga na mchezaji Haruna Niyonzima, nilihisi kulikuwa kuna kasoro hasa kwa mchezaji anayelipwa mshahara wa Sh milioni 6 anaweza vipi kupuuzia maisha yake na kuanzisha mgogoro usiokuwa na tija kwa maisha ya kipato. (angalia kiambatanisho 1)
Niliamua uchunguzi wa ndani ufanyike katika suala hilo zima na mwisho, Jonas Tiboroha alibainika kuwa hakuwasilisha ushahidi ya mawasiliano sahihi kwa Kamati ya Nidhamu kuhusiana na Haruna Niyonzima, hali iliyosababisha kamati kuchukua uamuzi ambao haukuwa sahihi kwa sababu;
Kulifanyika mambo ambayo hayakuwa sahihi, mfano barua za Niyonzima kutoka kwa Shirikisho la Soka la Rwanda (Ferwafa) ambazo zilitumwa kwa TFF na kupokelewa kama ambavyo Azam FC walipokea ya mchezaji wao kupitia kwa Afisa Mtendaji Mkuu wao. Lakini barua ya Niyonzima kuja Yanga, ilionekana haikupokelewa kama ilivyokuwa kwa barua yake ya utetezi na ile ya kuomba radhi alizoandika, nazo zilipokelewa lakini hazikuwasilishwa kwenye kamati ya nidhanmu na hili, mhusika ni Tiboroha. Ukiachana na kamati kufanya uamuzi usio sahihi, hili pia limemjengea mchezaji chuki kubwa kwa wanachama na mashabiki. (angalia kiambatanisho 2 & kiambatanisho 3)
Kamati ya Utendaji (EXCOM), bada ya kupitia kwa kina iliona uamuzi ilichukua haukuwa haukuwa ya haki kutokana na kupotoshwa na Tiboroha tena aliendelea kuipotosha kamati kwa makusudi kutokana na kuficha nyaraka hizo ili Niyonzima afukuzwe. Tulifikia maamuzi Tiboroha alikuwa na ajenda yake binafsi.
Hii kama ilikuwa haijagunduliwa mapema, ilikuwa na hatari ya kusababisha upotevu kifedha za Yanga kulingana na kanuni za TFF/FIFA na ukilichimba suala hili kwa undani, kwa kufuata weledi. Kamwe hauwezi kusema yalikuwa ni makosa ya kibinadamu badala yake ni chuki ya kibinadamu ambayo haistahili kufanywa na kiongozi wa Klabu kubwa yenye heshima kama Yanga.
Zaidi, Katika hali nyingine, uamuzi wa Kamati ya Nidhamu uliandikwa na Gazeti la Uhuru na mwisho wa uchunguzi ulidhibitisha mtoa habari hizo alikuwa ni Tiboroha, akilenga kutaka kuuchafua uongozi wa Klabu, mchezaji mwenyewe dhidi ya jamii na kuusukuma uongozi kufanya uamuzi usio sahihi kwa faida zake yeye binafsi na si klabu.
2. Aidha, EXCOM ilifanya uchunguzi wa ziada na kugundua vitendo, Tiboroha hakuweza kufikia malengo aliyekuwa ameyawekewa na EXCOM kwa kuwa zaidi alionekana kutaka kujiendeleza binafsi, kusikika peke yake na kujulikana mwenyewe kama “Mungu Mtu”, jambo ambalo lilichochea kelele ndani ya klabu kama vile yeye ni malaika:

Angalia kiambatanisho (3), eti Mwenyekiti wa Matawi (nafasi ambayo haitambuliki kwenye katiba ya Yanga), amekuwa akiniagiza kubadili nafasi za  waajiriwa, mfano ile ya (Tiboroha) ni lazima abaki kwa sababu mchango wake ni mkubwa na bila yeye hatuwezi kushinda au kufanya vizuri. Ukisoma barua yake utafikiri Tiboroha alikuwa akifanya kazi zake bure wakati anajua alikuwa ni mwajiriwa wa Klabu, tena kazi zake nyingi alikuwa akizifanya kwa kufuata “maagizo”  anayopewa kama mwajiriwa. Tayari kupinga kuondolewa kwake kumeanza kuripotiwa kwenye vyombo vya habari kama shinikizo la chinichini kupitia Msumi, huenda anafikiri kufanya hivyo inanitisha ili nibadili mambo kwa matakwa ya wasioelewa mamlaka ya Katiba. Naendelea kukumbusha Tiboroha alikuwa mwajiriwa anayelipwa mshahara (angalia kiambatanisho 4) huku mimi kama Mwenyekiti au Wajumbe wa EXCOM tumekuwa tukijitolea na kutolipwa hata posho. 
Ajabu Kichekesho zaidi, kila kizuri kilichokuwa kikifanyika, vyombo vya habari viliripoti kuwa ni kazi nzuri ya Tiboroha, lakini wakasahau kila zuri, yeye alikuwa ni mtekelezaji tu baada ya kuagizwa kutoka kwangu mimi mwenyekiti au baada ya ushauri wa kamati ya utendaji na baada ya hapo, yeye alipewa kibali cha kutekeleza jambo husika. Kila zuri lilikuwa lake, mabaya yakiwemo yale ya kuisaidia TFF kuiangamiza shingo ya Yanga, aliyeficha kapuni.
Kuna taarifa kwenye vyombo vya habari ambazo zilithibitisha wazi kuwa Tiboroha alipania kujijenga binafsi kama Katibu Mkuu Bora zaidi kuwahi kutokea Yanga; hoja potofu kwa sababu wakati akiwa Katibu, hata mwalimu wa Klabu alifanikiwa kupatikana kwa ubingwa moja tu. Lakini akasahau kabla yake, Yanga ilishachukua ubingwa mara 24. Tena, propaganda ya kuwa yeye ndiye aliyeisaidia  Klabu kusajili wachezaji wa kiwango cha juu zaidi huku akijua wazi kwamba wachezaji hao walikuwa ni pendekezo la Kocha Mkuu, huu ni uputofu wa hali ya juu kabisa. 
Ndani ya miezi yake 12 ya uongozi amechangia kushuka kwa kasi kubwa kwa mapato ya klabu huku matumizi ya klabu yakipanda mara nne zaidi kutoka Sh milioni 500 kwa mwaka hadi sasa takriban Sh bilioni 2. Kabla hajaja klabuni, tulikuwa tumekaribia kujikomboa na kuanza kujitegemea. Hii pia ni kwa yeye kukubaliana na ujinga wa kuitetea TFF ambayo mikataba yake, kwa kiasi kikubwa imeporomosha mapato yetu na kutuweka katika wakati mgumu kabisa, ajabu Tiboroha alikuwa upande huo.  
3.   Masuala ya kupotosha ya Tiboroha si mapya:
a. Wakati FIFA ilipoialika Yanga kwenye semina ya mafunzo iliyofanyika nchini Ghana, Tiboroha alijichagua mwenyewe asafiri kwa niaba ya Klabu bila kuitaarifa EXCOM, halafu akachukua “Cheti cha ugonjwa” na kukiwasilisha kwa mwajiri wake Yanga ili apate nafasi ya kusafiri kwenda nchini Ghana. Kujichagua yeye mwenyewe, ilikuwa ni kutofuata weledi.
b. Daktari (jina linahifadhiwa) aliajiriwa kwa ajili ya mechi dhidi ya MGAMBO likiwa ni pendekezo la Tiboroha, lakini baadaye Kamati ya Mashindano (baada ya kuwa imesababisha tatizo ndani ya Klabu), iligundua daktari huyo alikuwa ni mwanachama tena mwenye kadi wa Simba, akaondolewa’ pia.

c. Ngoma alipewa taarifa na Tiboroha kwamba anatakiwa kwenda kufanya majaribio na klabu moja nchini Uturuki. Tiboroha alifanya hivyo akijua Ngoma alikuwa anakwenda kushiriki michuano ya MAPINDUZI Cup, mbaya zaidi hakuwa amewasiliana na EXCOM kuhusiana na hilo kabla kumfahamisha mchezaji na kumpa taarifa hiyo. Baadaye kocha Kocha Mkuu, alilalamika kwamba kufanya vile ilikuwa ni kuondoa morali ya mchezaji katika michuano hiyo ya MAPINDUZI CUP na baada ya hapo, angekuwa akiwaza kuhusiana na Uturuki tu. Mwisho, kocha alisema, Ngoma alicheza chini ya kiwango katika michuano hiyo, akiamini Yanga inamzuia kusonga mbele kimaisha.

d. BDF ya Botswana ilianzima US$ 5,000/- ambazo hadi sasa hazijarejeshwa: EXCOM iligundua taarifa kuhusiana na deni hili, imekuwa ikifichwa na hakuna maelezo mrejesho kuhusiana hilo kutoka kwa Tiboroha ambaye amekuwa na ukaribu na wahusika kutoka Botswana.

e. Kuna mtu aliajiriwa kama Katibu Muktasi (PS) pamoja na mtu mwingine pia, lakini haikuidhinisha wala mwanasheria wa Yanga, hakutaarifiwa kuhusiana na hilo lilifanyika bila ridhaa ya EXCOM, badala yake alilifanya kwa kuwa anaona yeye ni mtu maarufu sana!

f. Hakufuata ushauri aliopewa na wataalamu wa TRA, hali iliyosababisha akaunti za Yanga kufungwa, hivyo mimi kulazimika kuanza kutoa fedha zangu za mfukoni katika uendeshaji wa Klabu kwa kipindi chote na wakati huo wachezaji walikuwa wakidai mishahara na tuko katikati ya msimu. 

g. Alikuwa akitetea maslahi ya TFF na sio Yanga na kukubali kila TFF ilichokipendekeza. Mtu mwenye akili anaweza kufanya hivyo utadhani alikuwa mwajiriwa wa TFF na si Yanga? Hii inaonyesha hakuwa akifanya kazi kwa maslahi ya Yanga kama ilivyotakiwa, angalia katika masuala dhidi ya TFF, ukijumuisha.

h. Lile la kushindwa kumpigania msemaji Msemaji wa Klabu, Jerry Murro asifungiwe na TFF, huku akimchimba huku akijua alikuwa akipitia taarifa zote kabla ya Jerry kuzitoa. Alikuwa na roho mbaya kwa kuwa Jerry alipata umaarufu zaidi kwa wanachama kutokana na kuipigania klabu.

i. Ukiangalia hayo juu, ni kati ya machache ambayo nimeona ninaweza kuyaanika kwenye vyombo vya habari, lakini yako mengi ambayo ni nyeti na haitakuwa sahihi kuyaanika kwenye vyombo vya habari kwa maslahi ya klabu. Yanga ilianza kung’amua mambo yanayomhusu Tiboroha muda sasa, alipoona mengi yamegundulika. Januari 14, 2016 aliandika barua kuomba radhi kwangu, akikiri kufanya makosa na kusema alikuwa akiyajutia. (angalia kiambatanisho 6)


4. Sisi, hatukukubaliana na kutoa msamaha kutokana na hofu ya unafiki wake, na nilitoa ushauri; kwamba vizuri akachukua hatua ya kujiuzulu mara moja na huenda ingekuwa vizuri aeleze ana matatizo ya kifamilia pia kiafya, lengo lilikuwa ni kumpa nafasi ya kuachana na Yanga kwa amani pia kuilinda familia maisha yake huko mbeleni. Lakini nilimtaka ahakikishe zile fedha tunazowadai BDF kutoka Botswana, mara moja zinawasilishwa Klabuni na baada ya hapo, rasmi atakuwa amejiondoa.

5. Tiboroha alikubaliana na hilo na kuandika barua ya kujiuzulu alioiwasilisha Januari 22, 2016 (angalia kiambatanisho 7)

6. Pamoja na kumshauri ili ajiuzulu kwa heshima, lakini alionekana kuanza kutengeneza “Presha ya wanachama” kama vile mtu aliyeonewa. Kuna mkutano wa ujanjaujanja uliitishwa makao makuu ya Klabu, Tiboroha akiwa mshiriki mkuu nyuma ya pazia, hii ilikuwa ni Januari 23, 2016. Lengo ni kutengeneza hali ya hofu kwa Wanachama, jambo ambalo si sahihi. (angalia kiambatanisho 8)

7. Kwa yote hayo hapo juu:
a. Kamati ya Utendaji (EXCOM) inapenda kutoa taarifa kuwa imevunja mkataba wa Tiboroha kama Katibu Mkuu wa Yanga.
a. Klabu inatangaza, mara moja kuwa: 
i. Baraka Deudeit atashikilia nafasi hiyo ya Katibu Mkuu wa klabu.
ii. Omar Kaya atachukua majukumu yanayohusiana na wanachama wa klabu. Pia atahakikisha anasimamia mikutano yote ya matawi, kusaidia maandalizi ya uchaguzi ujao pamoja na masuala ya wanachama wapya.
iii. Jerry Muro ataendelea kubaki katika nafasi ya msemaji wa klabu,
iv. Faidhal Mike ni Mkuu wa Kitengo cha Fedha cha Klabu, akisaidiwa na Justina ambaye amepandishwa cheo na kuwa mhasibu mkuu msaidizi,
v. Klabu ipo katika kipindi cha kuboresha kitengo cha masoko cha klabu na hivi karibuni itatangazwa lakini kabla ya hivyo, Omar atashikilia kwa muda kitengo hicho.
vi. Mwanasheria Frank Chacha kama mkuu wa kitengo cha Sheria Klabuni, yeye tunamuacha aendelee na mambo yake na masuala yote ya kisheria, klabu itayafanya kutumia wanasheria, nje ya klabu.

8. Kuhusiana na uchaguzi na maneno ya kinafiki ya nungunungu ya chinichini kuwa eti ninaogopa uchaguzi; huku wakiwa hawajui kuwa katika maisha yangu sijawahi kushindwa uchaguzi: Ukweli mimi ndiyo nimekuwa nikusukuma kuitishwa kwa uchaguzi uitishwe ili nistaafu kupitia nafasi yangu ya uenyekiti. Nilimwaandika Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, kuitisha uchaguzi mara moja, akishindwa basi itabidi niivunje Kamati ya Uchaguzi na kuunda nyingine. (angalia kiambatanisho 9)

9. Kutokana na kuuguliwa na baba yake mzazi, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi alishindwa kutekeleza hilo na akaamua kujiuzulu. (angalia kiambatanisho 10)

10. Ikiwa ni sehemu ya majukumu yangu, kwa ushauri wa EXCOM niliomba kwao majina mapya ya Kamati ya Uchaguzi ili mchakato ufanyike (angalia kiambatanisho 11)
Hitimisho, nimegundua potofu ya kufikiri Tiboroha ni Katibu Mkuu wa kuchaguliwa, badala yake ni mwajiriwa wa kawaida ambaye aliingia mkataba kwa maslahi ya mapato yake. Tena kosa kumchukulia kama mtu ambaye amekuwa akitoa fedha zake za mfukoni kwa ajili ya kuendesha Klabu, mtu ambaye mimi nilipendekeza aajiriwe kama nililivyopendekeza kwa Mwalusako, Njovu, Mwesigwa, Maximo na wengine na nina mamlaka ya kuamua hatma ya mwajiriwa kulinda heshima na maslahi ya Klabu.
Kwa sababu mimi nimewekea dhamira ya uchaguzi ufanyike kwa haraka, huu unaweza ukawa wakati mwafaka wa wanachama kumpa Tiboroha imani ya kura zao ili awanie nafasi Mwenyekiti wa Klabu na wanipe uhuru wangu wa kuendelea na mambo yangu mengine, ambayo yapo karibu na moyo wangu kama vile kusaidi mandeleo ya Mbagala Kuu.
Katika maisha yangu, sijawahi kutanguliza au kupigania cheo, ndani ya Yanga maendeleo yanaonekana lakini wapo watu ndani ya Yanga wanaona mandeleo ipo kwake. Basi tuache demokrasia itawale; lakini na mimi nitatangaza kugombea tena nafasi hiyo, ingawa sidhani kama nitamaliza kipindi chote cha uongozi iwapo nitashinda kwa kuwa kutoka awali nilieleza Yanga kuwa yenye mafanikio ni katika Ligi ya Mabingwa Afrika lakini hilo halitawezekana bila ya Klabu kumiliki uwanja wake binafsi pale Jangwani.
Daima Mbele, Nyuma Mwiko
_____________
YUSUF MANJI
(MWENYEKITI YOUNG AFRICANS SPORTS CLUB)

TIBOROHA ABWAGA MANYANGA YANGA


KATIBU Mkuu wa Yanga SC, Dk. Jonas Tiboroha amejiuzulu na tayari amewasilisha barua kwa Mwenyekiti, Yussuf Mehboob Manji.
Tiboroha amesema kwamba amechukua uamuzi huo ili apate muda zaidi wa kufanya shughuli zake za Uhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Mimi ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitivo cha Elimu ya Viungo (PE), na kwa kuondoka Yanga SC maana yake napata wasaa mzuri wa kumtumikia mwajiri wangu, UDSM,”amesema.
Pamoja na Tiboroha kutozama ndani sana juu ya kujiuzulu kwake, lakini inaelezwa alikuwa hana maelewano na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya klabu, Isaac Chanji ambaye kwa sasa ndiye mtu anayesikilizwa na kuaminiwa zaidi na Manji.
Tiboroha alipoulizwa kuhusu mahusiano yake na Chanji alisema: “Nilichoandika katika barua yangu ya kujiuzulu ndiyo sababu za msingi, kikubwa ninawapisha watu ambao wanaweza kuiongoza vizuri Yanga SC kuliko mimi,”amesema.
Tiboroha aliingia Yanga SC Desemba mwaka 2014 akichukua nafasi ya Benno Njovu aliyeondolewa kwa tuhuma mbalimbali. Aliingia Yanga SC akitokea Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama Ofisa Maendelezo ya Ufundi

SIMBA YATINGA 16 BORA KOMBE LA SHIRIKISHO



SIMBA SC imefuzu Raundi ya Nne ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports HD TFF Cup, baada ya kuwachapa wenyeji Burkina Faso mabao 3-0 jioni ya leo Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Shujaa wa Simba SC inayokwenda hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo ambayo itatoa mwakilishi wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mwakani, alikuwa ni mshambuliaji Mganda, Hamisi Friday Kiiza aliyefunga mabao mawili, wakati lingine limefungwa na kiungo Said Ndemla.
Kiiza alifunga mabao yake dakika ya 77 kwa shuti kali akimalizia krosi ya Abdi Banda na la tatu dakika ya 90 kwa penalti, baada ya kiungo Said Ndemla kuangushwa kwenye boksi.
Ndemla alifunga bao la pili la Simba SC hii leo dakika ya 89 kwa shuti la umbali wa mita 38, bao lililowasisimua zaidi mashabiki uwanjani.
Mapema kipindi cha kwanza, Simba SC ilipoteza nafasi mbili nzuri za mabao, kwanza dakika ya 11 wakati winga Joseph Kimwaga alipowalamba chenga vizuri mabeki wa Burkina Faso, lakini akapiga nje na dakika ya 39 beki Mrundi, Emery Nimubona alipopiga nje akiwa karibu na lango. Burkina Faso nayo iliyoongozwa na mkongwe, Ulimboka Alfred Mwakingwe aliyewahi kuwika Simba SC ilipoteza nafasi pia.
Dakika ya 39 Ulimboka alimdakisha kipa Muivory Coast wa Simba SC, Vincent Angban shuti dhaifu akiwa kwenye nafasi nzuri na dakika nne baadaye akachelewa kupiga akiwa kwenye boksi, hadi mabeki wakaokoa.
Katika mechi nyingine za michuano hiyo leo, Toto Africans imeifunga 4-1 Pamba Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, wakati Ndanda FC imeifunga 5-0 Mshikamano Uwanja wa Nagwanda SIjaona mjini Mtwara.

WAIMBAJI WA INJILI WATAKIWA KUJISAJILI BASATA



BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata) limezidi kutoa wito kwa waimbaji wa muziki wa Injili kujisajili katika baraza hilo ili stahiki zao zitambulike inavyotakiwa.

Mkurugenzi wa ukuzaji Sanaa na Matukio wa Basata, Maregesi Kwirujira Ng’oko alisema waimbaji wengi wa muziki wa Injili wa Tanzania kuzingatia hilo.

Ng’oko alisema kujisajili Basata kuna faida na fursa nyingi ambazo ni msaada ambao utasaidia kupata haki zao kupitia kazi zao.

Ng’oko alisema kwa kuwa wao ndio wasimamizi wa kazi za sanaa ni jukumu lao kuwakumbusha mara kwa mara wasanii kujisajili.

Aidha Ng’oko alisema wanatoa salamu hizo kwa wasanii pindi inapotokea mikinzano katika ufanikishaji wa kazi zao.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Abihudi Mang’era alisema wanafikiria kuongeza msukumo kwa waimbaji wa muziki wa Injili kuhusu kujisajili Basata katika baadhi ya matukio.

Mang’era alisema wanafikiria kutoa elimu ya kujisajili Basata katika matamasha yao ama kusaka namna ya kufanikisha utambuzi wa waimbaji katika baraza hilo.

KAMATI YA MISS TANZANIA YAJITOA


Mwenyekiti wa Kamati ya kuratibu Miss Tanzania Juma Pinto akiongea na waandishi wa habari(hawapo pichani) leo  jijini Dar-es-Salaam juu ya kujitoa kwao kama kamati ya kuratibu Miss Tanzania ambayo ilichagulia na kampuni ya Lino International Agency, kushoto ni Msemaji wa kamati hiyo Joketi Mwegelo na kulia ni Mjumbe wa kamati Gladys Shao .

Lilian Lundo- Maelezo
Kamati ya kuratibu Miss Tanzania imejitoa rasmi kusimamia mashindano ya Miss Tanzania kuanzia leo tarehe 21/01/2016.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo  Juma Pinto alisema hayo leo, alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jijini Dar-es-Salaam.
“Tumekuja kutoa taarifa kwamba, kama tulivyo teuliwa na kampuni ya Lino International Agency, kuandaa, kuendesha na kusimamia mashindano ya Miss Tanzania, kamati yangu imeamua kujitoa kutokana na majukumu ya kamati kuingiliwa na kampuni ya Lino,” alisema Pinto.
Pinto aliongeza kwa kusema kuwa kamati yake ilipewa jukumu la kuendesha mashindano na kuwajibika kufanya kila kitu na Lino itakuwa kama washauri, lakini badala yake Lino imetaka kuhodhi majukumu yote na kamati ikawa ni ya kutafuta wadhamini.
Kamati hiyo imefanya vikao vingi vya kuhakikisha mashindano yanaboreshwa na kubadilisha mfumo ili kuifanya Miss Tanzania kuwa na mwonekano tofauti kama ambavyo Lino ilivyoamua kuweka kamati mpya ili kuboresha mashindano hayo.
Kutokana na kutopata muafaka katika vikao hivyo vya kuboresha mashindano ya Miss Tanzania, Kamati ya kuratibu mashindano hayo kwa nia njema na wala si kwa ubaya imeamua kujitoa katika Mashindano hayo.
Aidha, Pinto amewaomba radhi wadhamini ambao wameshaongea nao kama kamati na walioonesha nia ya kuwasaidia, amewataka kuendelea kufanya mawasiliano na kampuni ya Lino kwani madhumuni ni kudhamini mashindano na sio kamati.

Friday, January 22, 2016

KOMBE LA SHIRIKISHO KUENDELEA WIKIENDI HII



Mzunguko wa tatu wa michuano wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) unatarajiwa kuendelea wikiendi hii mpaka katikati ya juma lijalo kwa michezo 13 kuchezwa katika viwanja mbalimbali nchini.

Kesho Jumamosi michezo mitatu itachezwa, mjini Morogoro Burkinfaso FC watawakaribisha Simba SC katika uwanja wa Jamhuri mjini humo,  Pamba FC watawakaribisha Toto Africans uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, huku Ndanda FC wakichea dhidi ya Mshikamno FC katika uwanja wa Nagwanda Sijaona Mtwara.

Jumapili michuano hiyo itaendelea kwa michezo mitatu, jijini Dar es salaam Young Africans watawakaribisha Friends Rangers uwanja wa Taifa, Njombe Mji watakua wenyeji wa Tanzania Prisons uwanja wa Amani Njombe, huku Stand United wakicheza dhidi ya Mwadui FC katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Michuano hiyo itaendelea Jumatatu, Kagera Sugar wakiwa wenyeji wa Rhino Rangers katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, Panone FC dhidi ya Madini FC uwanja wa Ushirika mjini Moshi na Africa Lyon wakiwa wenyeji wa Azam FC uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

Jumanne Mtibwa Sugar watawakaribisha Abajalo FC uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Lipuli dhidi ya JKT Ruvu uwanja wa Wambi Mafinga, Africa Sports dhidi ya Coastal Union Mkwakwani jijini Tanga, na Geita Gold watakua wenyeji wa Mgambo Shooting katika uwanja wa Nyankumbu mjini Geita.

Singida United watacheza dhidi ya Mvuvuma siku ya Jumatano katika uwanja wa Namfua mjini Singida, na mchezo wa mwisho utachezwa Februari Mosi katika ya Wenda FC dhidi ya Mbeya City uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Mpaka sasa timu ya JKT Mlale pekee ndio imeshafuzu kwa mzunguko wa nne baada ya kuiondosha Majimaji kwa mabao 2-1, katia mchezo uliochezwa wiki iliyopita kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea.

TFF YATUMA RAMBIRAMBI PRISONS




Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametuma salamu za rambi rambi kwa klabu ya Tanzania Prisons inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom kufuatia kifo cha Mwenyekiti wake Hassan Mlilo kilichotokea jana katika hospital ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam.

Katika salamu zake, Malinzi amewapa pole familia ya marehemu Hassan Mlilo, ndugu, jamaa, marafiki na klabu ya Tanzania Prisons, na kusema kwa niaba ya familia ya mpira wa miguu nchini amesema TFF ipo pamoja nao katika kipindi hichi kigumu cha maombolezo.

Mwili wa marehemu Hassan Mlilo unatarajiwa kusafirishwa leo mchana kuelekea mkoani Mbeya, ambapo mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho katika mji wa Rujewa mkoani humo.

TAARIFA KUHUSU KUSIMAMISHWA KWA VIONGOZI WA TEFA



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linapenda kutoa taarifa kuhusu uamuzi Kamati ya Maadili ya Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) wa kuwasimamisha kwa muda wa miaka miwili viongozi watatu wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Wilaya ya Temeke iliyotolewa hivi karibuni katika vyombo vya habari hususan gazeti la HabariLeo la tarehe 17 Januari 2016, ukurasa wa 30 yenye kichwa cha habari: “DRFA yatangaza kufungia viongozi wa Tefa”.

TFF ina maelezo yafuatayo kuhusu uamuzi huo wa DRFA



YANGA YATAKATA LIGI KUU, YAIBUGIZA MAJIMAJI 5-0


Refa John Fanuel wa Shinyanga akimkabidhi mpira Amissi Tambwe baada ya mechi kwa kufunga hat trick

Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
YANGA SC imerudi tena kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Majimaji ya Songea jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 39, sawa na Azam FC wanaorudi nafasi ya pili – na vijana wa kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm wanakaa juu kwa wastani mzuri wa mabao.
Mshambuliaji Mrundi Amissi Joselyn Tambwe amefunga mabao matatu leo, wakati Wazimbabwe, kiungo Donald Ngoma na mshambuliaji Thabani Kamusoko wamefunga bao moja kila mmoja.
Katika mchezo huo uliokuwa wa upande mmoja, dalili za Yanga kuwafanya ‘vibaya’ Majimaji zilianza mapema tu dakika ya nne, baada ya Kamusoko kufunga bao la kwanza akimalizia krosi ya kiungo Deus Kaseke.
Baada ya bao hilo, pamoja na Yanga SC kuendelea kuwashambulia Majimaji, lakini hawakufanikiwa kuongeza mabao hadi kipindi cha pili.
Ngoma alifunga bao la pili dakika 47 kabla ya Tambwe kufunga mara tatu mfululizo dakika za 57, 82 na 84 kuunenepesha ushindi wa mabingwa hao watetezi.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Mwadui FC imeshinda 2-1 dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga na African Sports imelazimishwa sare ya 0-0 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

CHANZO CHA HABARI: BLOGU YA BINZUBEIRY

Thursday, January 21, 2016

SIMBA YAWAPA RAHA MASHABIKI WAKE



NYOTA ya Kocha Jackson Mayanja kutoka Uganda imeendelea kung'ara baada ya kuiwezesha Simba kushinda mechi ya pili mfululizo katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mayanja aliiongoza Simba kwa mara ya kwanza na kuichapa Mtibwa Sugar bao 1-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kama vile haikutosha, Mayanja jana aliiongoza tena Simba kuichapa JKT Ruvu mabao 2-0 kwenye uwanja huo na hivyo kufufua matumaini ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.

Ushindi huo umeiwezesha Simba kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo,ikiwa na pointi 33 baada ya kucheza mechi 15.

Simba ilipata bao la kuongoza dakika ya 51 lililofungwa kwa njia ya penalti na mshambuliaji Hamisi Kiiza baada ya Daniel Lyanga kuchezewa madhambi ndani ya eneo la hatari.


Lyanga aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 61 kwa kiki kali iliyomshinda kipa Hamisi Seif wa JKT Ruvu.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Prisons iliichapa Coastal Union mabao 2-1 mjini Mbeya, Azam iliicharaza Mgambo JKT mabao 2-1 mjini Tanga.

Wednesday, January 20, 2016

KIGOGO WA FIFA ATEMBELEA WIZARA YA HABARI



Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Bw. Salman Bin Ebrahim Al Khalifa katikati akiongea na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel kulia kuhusiana na maendeleo ya michezo nchini, wa kwanza kushoto ni Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania Bw. Jamali Malinzi.

(Picha na Benjamin Sawe-WHUSM)

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Asia (AFC), na Makamu wa Rais wa FIFA, Sheikh Salman Bin Ebrahim Al Khalifa leo ametembelea wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, ambapo alifanya mazungmzo mafupi na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Elisante Ole Gabriel.

Katika mazugmzo hayo, Sheikh Salman ameielezea Serikali ya Tanzania nia ya FIFA kuendelea  kushirikiana na Serikali na TFF katika kuendeleza programu mbalibali za maendeleo ya mpira hasa wa vijana na wanawake.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara, Profesa Elisante  ameihakikishia FIFA kuwa nia ya Serikali ni kuona mpira unakua nchini na Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa TFF na FIFA ili kufikia azama hiyo.

Aidha pia ametoa wito kwa AFC kusaidiana na TFF katika masuala ya exchange programmes ili vijana wetu wapate uzoefu wa nje.

Sheikh Salman na ujumbe wake walitembelea ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) wakiwa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi, ambapo walikutana na Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanya na shirikisho, ikiwemo uwanja wa Karume, na Hostel zilizopo Karume.

Kiongozi huyo wa AFC, aliwasali nchini jana mchana kwa matembezi ya siku mbili chini ya mwenyeji wake Rais wa TFF, Jamal Malinzi na anatarajiwa kuondoka nchini kesho.

KALALE PEMA SULEIMAN SAID 'YELSTIN'


KWA kawaida mauti huua mwili wa binadamu ukabaki vumbi tupu kaburini, lakini yale yote mema aliyoyafanya katika kipindi chote alichokuwepo hapa duniani, yatabaki kwenye kumbukumbu milele. Kamwe hayatafutika.

Hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa marehemu Suleiman Said Suleiman, maarufu kwa jina la 'Yelstin', ambaye alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).

Yelstin, ambaye aliwahi kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Simba kati ya mwaka 1997 hadi 1999, alifariki dunia Jumatatu asubuhi, alipokuwa akiogelea katika Bahari ya Hindi na kuzikwa siku hiyo hiyo jioni kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

Mwanamichezo huyo alipatwa na mauti wakati akipelekwa Hospitali ya Agha Khan, baada ya misuli kukaza ghafla alipokuwa akiogelea katika bahari hiyo, ukiwa ni utaratibu wake wa kawaida wa kila siku asubuhi.

Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu na Ofisa Uhusiano wa TAA, Ramadhani Maleta, marehemu alikuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi ya kuogelea kila siku wakati wa asubuhi kutoka Feri hadi Kigamboni.

Maleta alisema siku ya tukio, marehemu alikwenda Feri kwa ajili ya kuogelea saa 12 asubuhi, ambapo aliogelea hadi Kigamboni na alipokuwa anarudi, akapatwa na tatizo la kukaza kwa misuli na kuishiwa nguvu.

Ofisa huyo wa TAA amekielezea kifo cha Suleiman kwamba kimeacha pigo kubwa kwa mamlaka hiyo kwa kumpoteza kiongozi mahiri, ambaye hakuwa na majigambo wala kuweka matabaka baina yake na wafanyakazi wenzake.

Marehemu Suleiman atakumbukwa kwa mchango mkubwa alioutoa katika kusimamia ujenzi wa viwanja vya ndege vya Songwe na Mpanda. Pia ndiye aliyekuwa akisimamia ujenzi wa awamu ya tatu wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA).

Kifo cha Suleiman pia kimeacha pigo kubwa katika tasnia ya michezo, hasa mchezo wa soka. Alikuwa shabiki na mwanachama damu wa Simba, ikiwa ni pamoja na kuiongoza miaka ya 1990.

Aliingia Simba akiwa mmoja wa viongozi wa kamati ya muda, iliyokuwa chini ya mwenyekiti, marehemu Saleh Ghulum. Kamati hiyo iliundwa baada ya wanachama kuuondoa madarakani uongozi wa mwenyekiti, marehemu Ismail Kaminambeo na katibu mkuu, marehemu Priva Mtema.

Wakati wote alipokuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Simba, marehemu Suleiman alikuwa kiongozi makini na mwenye msimamo. Hakuwa tayari kuyumbishwa na wanachama wakorofi ama wafadhili wa zamani wa klabu hiyo waliokuwa na uwezo mkubwa kifedha.

Hata hivyo, marehemu Suleiman alikuwa tayari kushirikiana na watu wa aina hiyo iwapo misaada yao haikuwa na masharti au dhamira ya kuudhalilisha uongozi wa Simba.

Kuna wakati Simba ilipokuwa ikijiandaa kwenda Kenya kucheza mechi ya kimataifa huku uongozi ukiwa hauna pesa, mmoja wa wakurugenzi wa zamani wa klabu ya Sigara, Kassim Dewji, alijitolea kuigharamia timu hiyo na Suleiman aliukubali msaada huo.

Mbali na Dewji, aliyekuwa Katibu wa Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Ismail Aden Rage, naye alijitolea kuisaidia Simba katika safari hiyo na marehemu Suleiman alikuwa tayari kuupokea msaada huo.

Pengine kitu pekee, ambacho Suleiman hakuwa akikifurahia wakati wote alipokuwa kiongozi wa Simba bila kuonyesha waziwazi hisia zake hizo, ni kujazana kwa wanachama maarufu kwa jina la 'makomandoo' ofisini kwake, kuanzia asubuhi hadi jioni.

Tabia hiyo pia haikuwa ikiwafurahisha wafanyakazi wenzake na kila walipowaona wanachama hao, waliwaeleza kwamba Suleiman hakuwepo ofisini na pengine hakutarajiwa kufika kwa siku hiyo.

Lakini cha ajabu ni kwamba kila marehemu Suleiman alipotoka nje ya ofisi yake na kuwakuta wanachama hao nje, aliwaita na kuwasalimia na pengine kuwaachia 'kitu kidogo' kwa wale waliokuwa na matatizo.

Sifa nyingine ya Suleiman ni kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari. Aliwapenda waandishi wa habari na alikuwa tayari wakati wowote kuwapa taarifa walizozihitaji kuhusu Simba.

Hata kama hakuwa na taarifa yoyote ya kuwapa, marehemu Suleiman alipenda kuwakaribisha ofisini kwake au klabuni na kubadilishana nao mawazo kuhusu Simba huku akiwasisitizia kutoandika chochote kuhusu walichozungumza.

Hivyo ndivyo alivyokuwa marehemu Suleiman, aliyeacha mke na watoto watatu. Mungu aipumzishe roho ya marehemu mahali pema.

Monday, January 18, 2016

YANGA YAITUNGUA NDANDA UNITED 1-0 NA KUREJEA KILELENI LIGI KUU

MABINGWA watetezi Yanga mwishoni mwa wiki walirejea kileleni mwa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Ndanda United bao 1-0.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilijipatia bao hilo la pekee kipindi cha kwanza kupitia kwa beki wake Kevin Yondan.

Ushindi huo uliiwezesha Yanga kuwa na pointi 36 sawa na Azam, lakini inaongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena kesho wakati mabingwa wa zamani Simba watakapomenyana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa wakati Azam itavaana na Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Katika mechi zingine, Stand United watakuwa wenyeji wa Toto Africans, Mbeya City watakuwa wageni wa Ndanda FC wakati Prisons itavaana na Coastal Union mjini Mbeya.

Yanga wanatarajiwa kushuka tena dimbani keshokutwa wakati Yanga watakapoikaribisha Majimaji kwenye Uwanja wa Taifa,
Mwadui itavaana na Kagera Sugar mjini Shinyanga wakati African Sports itavaana na Kagera Sugar mjini Tanga.

Sunday, January 17, 2016

URA MABINGWA WAPYA KOMBE LA MAPINDUZI


URA ya Uganda imetwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2016 kufuatia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ushindi huo ambao unakwenda sambamba na kitita cha Sh. Milioni 10, unaifanya URA iwe timu ya pili ya Uganda kutwaa taji hilo, baada ya KCCA mwaka juzi.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Mfaume Ali Nassor, hadi mapumziko, URA walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa na Julius Ntambi kwa kichwa, akimalizia krosi ya Villa Oromchani kutoka upande wa kushoto.
URA walikaribia kupata bao la pili dakika ya 37 baada ya Elkannah Nkugwa kupiga nje na kupoteza pasi ya Moor Semakula.
Kwa ujumla, URA ilitawala mchezo na kuishika Mtibwa Sugar, ambayo safu yake ya ushambuliaji ikiongozwa na Hussein Javu anayecheza kwa mkopo kutoka Yanga SC, iliishindwa kupasua ukuta wa timu ya Mamlaka ya Mapato Uganda.
Kipindi cha pili, Mtibwa Sugar inayofundishwa na Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mecky Mexime ilijaribu kuongeza kasi ya mashambulizi kusaka bao la kusawazisha, lakini wakasahau kuongeza umakini wa kujilinda, hivyo kuwapa fursa URA kupata mabao mawili zaidi.
Peter Lwasa aliyeingia dakika ya 53 kuchukua nafasi ya Villa Oromchani, aliifungia URA mabao mawili ndani ya dakika tatu – kwanza dakika ya 85 baada ya kuunasa mpira uliopigwa fyongo na beki Dickson Daud na lingine dakika ya 88 akimalizia pasi ya Julius Ntambi.
Jaffar Salum aliyeingia kuchukua nafasi ya Hussein Javu mwishoni mwa kipindi cha pili, aliifungia bao la kufutia machozi Mtibwa Sugar dakika ya 90, baada ya kumlamba chenga Jimmy Kulaba.
Pamoja na kutwaa ubingwa, URA pia imetoa mfungaji bora, ambaye ni Peter Lwasa aliyemaliza na mabao matatu, akifuatiwa na Villa Oramchani wa URA pia, mabao mawili sawa na Awadh Juma wa Simba SC, Donald Ngoma wa Yanga SC, Mohammed Abdallah wa JKU na Kipre Tchetche wa Azam FC.
Mtibwa Sugar wamepatiwa Sh. Milioni 5 kwa kushika nafasi ya pili.
Kikosi cha URA FC kilikuwa; Brian Bwete, Simon Massa, Alan Munaaba, Jimmy Kulaba, Sam Senkoom, Oscar Agaba, Julius Ntambi, Said Kyeyune, Moor Semakula/Shafiq Kagimu dk48, Villa Oramuchani/Peter Lwasa dk53 na Elkannah Nkugwa/Sam Sekito dk74.
Mtibwa Sugar; Said Mohammed, Ally Shomary, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Dickson Daudi, Salim Mbonde, Shaaban Nditi, Mohammed Ibrahim, Muzammil Yassin, Hussein Javu/Jaffar Salum dk81, Ibrahim Rajab ‘Jeba’ na Shiza Kichuya/Said Bahanuzi dk69.

ORODHA YA MABINGWA KOMBE LA MAPINDUZI
Mwaka     Bingwa             Mshindi wa Pili
2007         Yanga SC          Mtibwa Sugar
2008         Simba SC          Mtibwa Sugar
2009         Miembeni          KMKM
2010         Mtibwa Sugar   Ocean View
2011         Simba SC         Yanga SC
2012         Azam FC           Simba SC
2013         Azam FC           Tusker FC
2014         KCCA                Simba SC
2015         Simba SC          Mtibwa Sugar
2006         URA                   Mtibwa Sugar

SIMBA YAITUNGUA MTIBWA SUGAR BAO 1-0



BAO lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Kiiza, jana liliiwezesha Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Katika mechi hiyo ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Kiiza alifunga bao hilo dakika ya tano ya mchezo.

Mganda huyo alifunga bao hilo kwa kichwa, akimalizia krosi maridhawa iliyopigwa na Ibrahim Ajib kutoka pembeni ya uwanja.

Kwa ushindi huo, Simba sasa imefikisha pointi 30 baada ya kucheza mechi 14 huku ikiwa nafasi ya tatu, nyuma ya mabingwa watetezi Yanga, wenye pointi 32 na Azam yenye pointi 35.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa juzi, Azam ilitoka sare ya bao 1-1 na African Sports, JKT Ruvu ilipata kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa Mgambo Shooting, Mbeya City iliichapa Mwadui bao 1-0, Coastal Union ilitoka sare ya bao 1-1 na Majimaji wakati Prisons iliichapa Toto African bao 1-0.

Wednesday, January 13, 2016

SERIKALI YAMZAWADIA SAMATTA KIWANJA NA MAPESA LUKUKI



SERIKALI imemzawadia nahodha mpya wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Mbwana Samatta, kiwanja kwa ajili ya kujenga nyumba, kilichoko Kigamboni, Dar es Salaam.

Mbali na zawadi hiyo ya kiwanja, serikali pia imempa mchezaji huyo fedha taslim, lakini kiwango chake hakikuwekwa wazi.

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, katika hafla iliyofanyika kwenye Hoteli ya Hyyat Regency, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi kadhaa wa serikali.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni Waziri wa Habari, Utamaduni,  Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Elisante Ole Gabriel.

Uamuzi wa serikali kumpatia Samatta zawadi hiyo, umekuja siku chache baada ya mchezaji huyo kushinda tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani.

Samatta, aliyekuwa akicheza mpira wa kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, anatarajiwa kujiunga na klabu ya  KRC Genki ya Belgium.

Wakati huo huo, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana  Samatta jana alipatiwa viza ya kwenda Ubelgiji kujiunga na klabu ya KRC Genk.

Taarifa ya Ubalozi wa Ubelgiji nchini imesema mwanasoka huyo bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani, alifika kwenye ofisi hizo na kupatiwa viza hiyo.

SIMBA YAMTIMUA KERR


HATIMAYE kocha wa timu ya Simba, Dylan Kerr, ametupiwa virago, muda mfupi, baada ya klabu hiyo kupokwa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi. Kerr, aliwasili Dar es Salaam jana kutoka Zanzibar, baada ya Simba kutolewa katika nusu fainali kwa kuchapwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar.

Kerr, alilazimika kurejea Dar es Salaam mara moja kusomewa ‘mashitaka’ yanayomkabili na Kamati ya Utendaji kutokana na kutoridhishwa na utendaji wake wa kazi. Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema kuwa anatarajia kutoa taarifa rasmi leo kwa vyombo vya habari.

“Kwa sasa siwezi kuzungumzia lolote kuhusu suala hilo, taarifa zaidi nitazitoa baadaye au kesho ambapo nitazungumza na waandishi wa habari,” alisema Manara.

Lakini taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zilisema nafasi ya Kerr imechukuliwa na Mganda Jackson Mayanja, ambaye awali alitangazwa kocha msaidizi.

Mayanja, mmoja wa viungo mahiri wa pembeni waliong’ara Afrika Mashariki na kikosi cha Uganda, alikuwa kocha wa Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’.

Chanzo hicho kilisema kuwa Kamati ya Utendaji ilifanya kikao cha dharura juzi na kufi kia makubaliano ya kuachana na kocha huyo ambaye alitia saini mkataba wa mwaka mmoja. Pia katika mkataba huo kulikuwa na kipengele cha kuongezwa mwaka mmoja endapo angefanya vizuri. Kerr, anadaiwa kutokuwa na uhusiano mzuri na baadhi ya viongozi, wachezaji sanjari na kutokuwa mbunifu katika kazi.

“Kerr ameondolewa baada ya kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi na kujituma, pia hana mahusiano mazuri na baadhi ya viongozi na wachezaji,” kilisema chanzo hicho.

Kocha huyo amedaiwa kutimuliwa jana ambapo ameiacha Simba ikiwa nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 27, nyuma ya Yanga yenye pointi 33 na Azam inaongoza kwa pointi 35. Kerr, anaiacha Simba ikiwa imeshinda mechi nane, imetoka sare mara tatu na kupoteza mechi mbili.

Katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, Simba imepoteza mechi moja, ilitoka sare moja na kufungwa mchezo mmoja na ilishinda michezo miwili.

Monday, January 11, 2016

JK AMPONGEZA SAMATTA KWA KUTWAA TUZO YA AFRIKA

Mchezaji Mbwana Samatta aliyeshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani,  akimkabidhi jezi  yake anayoivaa akiwa katika timu yake ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rais Mstaafu na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, Jakaya Kikwete. Kulia anayeshuhudia ni  Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye  wakati walipokutana leo katika ofisi ndogo ya CCM Makao makuu Lumumba jijini Dar es salaam.
ALIYEKUWA Rais wa Awamu ya Nne  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amempongeza  mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania,  Mbwana Samatta kwa kutwaa tuzo ya  mchezaji bora wa Afrika 2015  kwa wachezaji wa ligi za ndani  na kumtakia kila la kheri kwenye safari yake ya soka.

Rais mstaafu, Dk. Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), alitoa pongezi hizo jana,  kwenye Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya Chama,  zilizoko mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam.

Dk. Kikwete alisema Watanzania wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu ili kuziona timu zao na wachezaji wao bila ya mafanikio kufanya vizuri  na kung'ara vema kwenye michuano ya kimataifa.

Alisema kitendo cha Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kumtangaza Samatta, ambaye anaichezea klabu ya kulipwa ya T.P Mazembe ya DR Congo,  kuwa mwanasoka bora wa Afrika, imekuwa chachu na dira kwake ya kusakwa na klabu nyingi za Ulaya.

"Kwanza nachukuaa fursa hii kumpongeza Samatta kwani kwa tuzo yake ya uchezaji bora wa Afrika 2015, aliyoipata, imetupa furaha na nina imani itatoa mwelekeo mzuri kwa wachezaji wengine wengi wa Tanzania, ambao wana kiu kubwa ya kupata mafanikio kwenye medani hiyo ya soka," alisema Dk. Kikwete.

Aidha, Kikwete amemtaka Samatta kutobweteka na mafanikio ambayo tayari ameanza kuyapata kwenye soka, kwani kufanya hivyo kutamwezesha kufikia ndoto zake za muda mrefu za kucheza soka barani Ulaya.

Alisema Watanzania wengi siku  za Jumamosi na Jumapili wanajazana pembezoni mwa luninga zao kuungalia ligi kubwa za soka za bara la Ulaya, ikiwemo ligi maarufu ya England.

"Mafanikio aliyoanza kuyapata Samatta yanamfanya sasa aanze kufuatiliwa na mawakala wengi wa nje ili akazitumikie klabu zao. Lakini nadhani mafanikio ya mchezaji huyo, hatimaye yatachangia mawakala wengi kuja kusaka wachezaji hapa nchini," alisema.

Naye, Samatta akizungumza  na vyombo vya habari kwenye hafla hiyo kabla ya kukabidhi jezi ya klabu yake ya T.P Mazembe yenye namba tisa mgongoni  kwa Dk. Kikwete, amewashukuru wadau, serikali na Watanzania wote ambao wamemuunga mkono kwa hali na mali.


"Kama ambavyo  nimekuwa nasema mara nyingi kwamba siku za nyuma nilikutana na Rais Kikwete kule Lubumbashi (DRC) na kuzungumza naye kwa kina kuhusu soka. Lakini kikubwa aliniaasa niongeze bidii ili nisiishie tu kucheza  T.P Mazembe na kweli ushauri wake nimeufanyia kazi na matunda yake yameanza kuonekana," alisema Samatta ambaye kwa sasa ametangazwa kuwa nahodha wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars.

Samatta amewataka Watanzania  hususan wadau wa soka, kuendelea kumuunga mkono kwenye harakati zake za kusaka kucheza soka ya kulipwa barani Ulaya.

Alisema anaamini kufanikiwa kwake katika hilo, kutakuwa na tija kwenye medani ya soka ya kimataifa, ambayo siku hizi imekuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa kuwashirikisha vijana wengi na wa kila jinsia.

Katika hatua nyingine, Samatta alimkabidhi Dk. Kikwete jezi ya T.P Mazembe ya DR Congo,  yenye namba tisa mgongoni kama sehemu ya kutambua mchango wa kiongozi huyo mstaafu  kwenye tasnia yake ya soka ya kulipwa.

Sunday, January 10, 2016

SAMATTA NAHODHA MPYA TAIFA STARS

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa, amemteua mshambuliaji Mbwana Samattam kuwa nahodha mpya wa timu hiyo.

Samatta amechukua nafasi ya nahodha wa zamani wa timu hiyo Nadir Haroub 'Cannavaro'.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mkwasa alisema uteuzi huo umetokana na kazi nzuri iliyofanywa na Samatta, kuitangaza Tanzania kimataifa.

"Samatta anastahili kuwa nahodha wa Taifa Stars kwa sasa, ingewa tumekuwa na nahodha, ambaye anastahili kuendelea,"alisema Mkwasa.

Aliongeza: "Tumeona kitu pekee cha kumlipa mchezaji huyo kutokana na heshima aliyoiletea nchi yetu ni kumpa beji ya unahodha wa Taifa Stars." 

Hata hivyo, Mkwasa amesema Cannavaro ataendelea kuwa nahodha wa timu ya Tanzania, inayoshiriki michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ndani, akisaidiwa na John Bocco.

Uteuzi wa Samatta kuwa nahodha wa Taifa Stars, umekuja siku chache baada ya kuibuka mshindi wa tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani.

Alishinda tuzo hiyo baada ya kupata pointi 127, na kuwabwaga mchezaji mwenzake wa TP Mazembe, Robert Muteba Kidiaba aliyepata pointi 88, Baghdad Bounedjah wa Etoile du Sahel ya Tunisia, aliyepata pointi 63.

SIMBA, YANGA ZATUPWA NJE KOMBE LA MAPINDUZI

MABINGWA watetezi wa Kombe la Mapinduzi, Yanga na watani wao wa jadi Yanga, jana walifungasha virago mapema mwaka huu baada ya kupata vipigo kutoka kwa Mtibwa Sugar na URA.

Katika mechi hizo za nusu fainali zilizochezwa kwenye Uwanja wa Amaan, mjini Unguja, Simba ilichapwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar wakati Yanga ilifungwa kwa penalti 4-3 na URA ya Uganda.

Kwa matokeo hayo, Mtibwa na URA sasa zitamenyana katika mechi ya fainali itakayochezwa kesho kwenye uwanja huo wakati Simba na Yanga zimeshafungasha virago kurejea Dar es Salaam.

Mtibwa Sugar ilijipatia bao lake la pekee na la ushindi dakika ya 45 kupitia kwa Ibrahim Rajabu 'Jeba'.

Bao hilo lilitokana na uzembe wa kipa Manyika Peter wa Simba, kuutema mpira uliopigwa kwenye lango la timu yake na kumkuta mfungaji, aliyeukwamisha wavuni.

Katika kipindi cha kwanza, Mtibwa walionekana kucheza soka safi na ya kuonana, ambapo walifanikiwa kupeleka mashambaulizi mengi katika goli la Simba.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, ambapo Kocha wa Simba, Dylan Kerr alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Awadh Juma,Danny Lyanga,Mwinyi Kazimoto na Emily Nimuboma na nafasi zao kuchukuliwa na Ibrahimu Ajibu,Said Ndemla,  Brian Mwajegwa na Rafael Kiongera.

Kuingia kwa wachezaji hao kuliongeza kasi ya Simba kulishambulia lango la Mtibwa,lakini uimara wa golikipa wa Mtibwa Sugar, Said Mohamed, ulikuwa kizingiti kwa Simba kusawazisha.

Kwa matokeo hayo, Mtibwa Sugar imeweka rekodi ya kucheza fainali ya michuano mara tano tangu tangu ilipoanza kushiriki katika michuano hiyo.

Nazo Yanga na URA zililazimika kupigiana penalti tano tano ili kumpata ushindi baada ya kumaliza dakika 90 zikiwa sare ya bao 1-1.

Penalti za Yanga zilifungwa na Kevin Yondan, Deo Munishi ‘Dida’ na Simon Msuva huku Malimi Busungu na Geoffrey Mwashiuya
wakikosa.

Kwa upande wa URA, penalti zake zilifungwa na Deo Othieno, Said
Kyeyune, Jimmy Kulaba na Brian Bwete, wakati Sam Sekito alikosa.

Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe dakika ya 13 kwa kichwa akimalizia mpira uliorudi baada ya kutemwa na kipa wa URA, Brian Bwete kufuatia mchomo wa winga Simon Msuva.

URA ilisawazisha dakika ya 76 kwa bao lililofungwa na Peter Lwasa kutokana na uzembe wa mabeki wa Yanga.