KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, January 4, 2016

YANGA YAANZA VYEMA KOMBE LA MAPINDUZI, YAITANDIKA MAFUNZO 3-0



Na Princess Asia, ZANZIBAR
YANGA SC imeanza vyema michuano ya Kombe la Mapinduzi, baada ya kuichapa Mafunzo FC mabao 3-0 katika mchezo wa Kundi B jioni ya leo Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Mshambuliaji Mzimbabwe Donald Dombo Ngoma alifunga mabao mawili kipindi cha kwanza na mshambuliaji mpya, Paul Nonga akaingia mwishoni mwa kipindi cha pili na kufunga bao katika mpira wa kwanza kugusa.
Mafunzo waliuanza vizuri mchezo wa leo na dakika ya kwanza tu mshambuliaji wake Sadikc Habib alikaribia kufunga kama si shuti lake kuokolewa na kipa Deo Munishi ‘Dida’.
Ngoma akaifungia Yanga SC bao la kwanza dakika ya 31 akimalizia krosi ya Mzimbabwe mwenzake, Thabani Scara Kamusoko aliyemtoka vizuri beki wa Mafunzo kulia.
Dakika mbili baadaye, Ngoma tena akafunga bao akimalizia pasi ya Kamusoko tena, aliyemtoka beki upande wa kulia wa boksi na hadi mapumziko, Yanga SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili, Yanga SC walianza kucheza kwa kuwadharau wapinzani, hivyo kuwasogeza kwenye eneo lao na dakika ya 81 Mafunzo wakapoteza nafasi nzuri ya kupata bao, baada ya Dida kupangua mkwaju wa penalti wa Kheri Salum. Penalti hiyo ilitolewa na Refa Mfaume Ali baada ya Shaaban Ali kukwatuliwa na beki wa Yanga SC, Kelvin Yondani ndani ya boksi.
Paul Nonga aliyeingia dakika ya 88, aliifungia Yanga SC bao la tatu dakika ya 89 akimalizia mpira uliotemwa na kipa Khalid Mahadhi, kufuatia shuti la Godfrey Mwashiuya aliyeingia pia dakika za lala salama.
Mchezo wa pili wa Kundi B utafuatia Saa 2:15 usiku hapo hapo Uwanja wa Amaan, Azam FC wakimenyana na Mtibwa Sugar, wakati kesho kutakuwa na mechi za Kundi A, kati ya JKU na URA Saa 10:15 jioni na Simba SC, mabingwa watetezi dhidi ya Jamhuri Saa 2:15 usiku.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Mbuyu Twite, Juma Abdul, Oscar Joshua, Pato Ngonyani, Kelvin Yondani, Simon Msuva/Malimi Busungu dk88, Thabani Kamusoko/Jerome Sina dk70, Amissi Tambwe/Paul Nonga dk88, Donald Ngoma na Deus Kaseke/Geofrey Mwashiuya dk70.
Mafunzo FC: Khalid Mahadhi, Juma Mmanga, Samih Nuhu/Haji Ramadhani dk58, Kheri Salum, Hassan Juma/Haji Abdi dk66, Abdul Hassan, Ali Juma/Jermaine Seif dk72, Sadick Habib/Shaaban Ali dk58, Mohammed Abdul na Ali Mmanga.

IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

No comments:

Post a Comment