KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, January 11, 2016

JK AMPONGEZA SAMATTA KWA KUTWAA TUZO YA AFRIKA

Mchezaji Mbwana Samatta aliyeshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani,  akimkabidhi jezi  yake anayoivaa akiwa katika timu yake ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rais Mstaafu na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, Jakaya Kikwete. Kulia anayeshuhudia ni  Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye  wakati walipokutana leo katika ofisi ndogo ya CCM Makao makuu Lumumba jijini Dar es salaam.
ALIYEKUWA Rais wa Awamu ya Nne  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amempongeza  mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania,  Mbwana Samatta kwa kutwaa tuzo ya  mchezaji bora wa Afrika 2015  kwa wachezaji wa ligi za ndani  na kumtakia kila la kheri kwenye safari yake ya soka.

Rais mstaafu, Dk. Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), alitoa pongezi hizo jana,  kwenye Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya Chama,  zilizoko mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam.

Dk. Kikwete alisema Watanzania wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu ili kuziona timu zao na wachezaji wao bila ya mafanikio kufanya vizuri  na kung'ara vema kwenye michuano ya kimataifa.

Alisema kitendo cha Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kumtangaza Samatta, ambaye anaichezea klabu ya kulipwa ya T.P Mazembe ya DR Congo,  kuwa mwanasoka bora wa Afrika, imekuwa chachu na dira kwake ya kusakwa na klabu nyingi za Ulaya.

"Kwanza nachukuaa fursa hii kumpongeza Samatta kwani kwa tuzo yake ya uchezaji bora wa Afrika 2015, aliyoipata, imetupa furaha na nina imani itatoa mwelekeo mzuri kwa wachezaji wengine wengi wa Tanzania, ambao wana kiu kubwa ya kupata mafanikio kwenye medani hiyo ya soka," alisema Dk. Kikwete.

Aidha, Kikwete amemtaka Samatta kutobweteka na mafanikio ambayo tayari ameanza kuyapata kwenye soka, kwani kufanya hivyo kutamwezesha kufikia ndoto zake za muda mrefu za kucheza soka barani Ulaya.

Alisema Watanzania wengi siku  za Jumamosi na Jumapili wanajazana pembezoni mwa luninga zao kuungalia ligi kubwa za soka za bara la Ulaya, ikiwemo ligi maarufu ya England.

"Mafanikio aliyoanza kuyapata Samatta yanamfanya sasa aanze kufuatiliwa na mawakala wengi wa nje ili akazitumikie klabu zao. Lakini nadhani mafanikio ya mchezaji huyo, hatimaye yatachangia mawakala wengi kuja kusaka wachezaji hapa nchini," alisema.

Naye, Samatta akizungumza  na vyombo vya habari kwenye hafla hiyo kabla ya kukabidhi jezi ya klabu yake ya T.P Mazembe yenye namba tisa mgongoni  kwa Dk. Kikwete, amewashukuru wadau, serikali na Watanzania wote ambao wamemuunga mkono kwa hali na mali.


"Kama ambavyo  nimekuwa nasema mara nyingi kwamba siku za nyuma nilikutana na Rais Kikwete kule Lubumbashi (DRC) na kuzungumza naye kwa kina kuhusu soka. Lakini kikubwa aliniaasa niongeze bidii ili nisiishie tu kucheza  T.P Mazembe na kweli ushauri wake nimeufanyia kazi na matunda yake yameanza kuonekana," alisema Samatta ambaye kwa sasa ametangazwa kuwa nahodha wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars.

Samatta amewataka Watanzania  hususan wadau wa soka, kuendelea kumuunga mkono kwenye harakati zake za kusaka kucheza soka ya kulipwa barani Ulaya.

Alisema anaamini kufanikiwa kwake katika hilo, kutakuwa na tija kwenye medani ya soka ya kimataifa, ambayo siku hizi imekuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa kuwashirikisha vijana wengi na wa kila jinsia.

Katika hatua nyingine, Samatta alimkabidhi Dk. Kikwete jezi ya T.P Mazembe ya DR Congo,  yenye namba tisa mgongoni kama sehemu ya kutambua mchango wa kiongozi huyo mstaafu  kwenye tasnia yake ya soka ya kulipwa.

No comments:

Post a Comment