KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, January 30, 2016

SIMBA YAFUFUA MATUMAINI YA UBINGWA, YAITANDIKA AFRICAN SPORTS 4-0, YANGA HOI KWA COASTAL UNION




TIMU kongwe ya soka ya Simba jana ilifufua matumaini ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuitandika African Sports mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wakati Simba ikiibuka na ushindi huo mnono, watani wao wa jadi Yanga walipigwa mweleka wa mabao 2-0 na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Ushindi wa Simba umeiwezesha kufikisha pointi 36 baada ya kucheza mechi 16, wakati Yanga inaendelea kubaki na pointi 39 sawa na Azam.

Simba ilipata bao lake la kwanza dakika ya 14 kupitia kwa mshambuliaji Mganda, Hamisi Kiiza aliyefumua shuti kali kwa mguu wa kushoto baada ya pasi ya beki Hassan Kessy.


Kessy mwenyewe akafunga dakika ya 30 kuipatia Simba SC bao la pili kwa shuti la mguu wa kulia akimalizia pasi ya mshambuliaji Ibrahim Hajib na kumchambua vizuri kipa Zakaria Mwaluko.


Kiiza akamlamba chenga kipa Mwaluko baada ya kupata pasi ya kiungo Mwinyi Kazimoto kuifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 42.


Hajji Ugando akaifungia Simba SC bao la nne dakika ya 75 baada ya kupokea nzuri ya kiungo aliyekuwa katika kiwango kizuri jana.

 
Wakati huo huo, Yanga SC imefungwa mabao 2-0 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na matokeo hayo yanawafanya wabaki na pointi zao 39 baada ya kucheza mechi 16, sawa na Azam FC iliyocheza mechi 15.

Coastal Union walipata bao lao la kwanza dakika ya 27 kupitia kwa beki wa zamani wa Simba SC, Miraj Adam aliyefunga kwa shuti la mpira wa adhabu lililomparaza mikononi kipa Deo Munishi ‘Dida’ kabla ya kutinga nyavuni.


Refa Andrew Shamba wa Pwani aliwapa nafasi ya kupiga faulo Coastal Union, baada Miraj Adam mwenyewe kuangushwa na beki wa Yanga, Kelvin Yondan nje kidogo ya boksi.


Mshambuliaji chipukizi, Juma Mahadhi aliifungia bao la pili Coastal Union dakika ya 62 baada ya pasi nzuri ya Hamad Juma.


Bao hilo liliwavunja nguvu kabisa wachezaji wa Yanga SC na kujikuta wanacheza bila malengo. 


Refa Andrew Shamba alimtoa kwa kadi nyekundu beki wa Yanga, Kevin Yondan dakika ya 100.

Awali, dakika ya 97 Shamba alijichanganya kwa kumuonyesha kadi nyekundu Said Jeilan badala ya njano.

No comments:

Post a Comment