'
Friday, January 8, 2016
YANGA YATINGA NUSU FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI KWA KISHINDO
YANGA SC imemaliza kileleni mwa Kundi B michuano ya Kombe la Mapinduzi, kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar jioni ya leo Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ushindi huo unaifanya Yanga SC ifikishe pointi saba baada ya kushinda mechi mbili na kutoa sare moja, hivyo kuongoza Kundi B ikifuatiwa na Mtibwa inayomaliza na pointi nne, Mafunzo pointi tatu, wakati Azam FC waliovuna pointi mbili wameshika mkia na kuaga.
Yanga SC sasa itacheza na mshindi wa pili wa Kundi A katika Nusu Fainali, wakati Mtibwa Sugar itacheza na mshindi wa pili wa kundi hilo.
Mtibwa Sugar walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa kiungo wake, Shizza Kichuya aliyemalizia pasi ya mshambuliaji anayecheza kwa mkopo timu hiyo ya Manungu kutoka Yanga SC, Hussein Javu
Yanga SC walisota hadi dakika ya 42 walipofanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia kwa kiungo wake mpya kutoka Niger, Boubacar Issoufou.
Issoufou alifunga bao hilo kwa shuti zuri la mpira wa adhabu kutoka pembeni kulia nje kidogo ya boksi, baada ya mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma kuangushwa na beki wa Mtibwa, Salum Mbonde.
Kwa ujumla, kipindi cha kwanza timu zote zilicheza vizuri, Mtibwa Sugar wakitawala sehemu ya kiungo na Yanga SC wakipitisha mashambulizi yao pembezoni mwa Uwanja.
Kipindi cha pili, timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamu, lakini mwishowe bahati ilikuwa ni ya Yanga waliofanikiwa kushinda mechi.
Mshambuliaji Malimi Busungu aliyetokea benchi, aliwafungia mabingwa hao wa Bara bao la pili dakika ya 81 akimalizia krosi ya winga Simon Msuva.
Kiungo wa Mtibwa Sugar, Henry Joseph aliyetokea benchi kipindi cha pili, alitolewa kwa kadi nyekundu dakika za mwishoni baada ya kumchezea rafu Salum Telela.
Mechi za makundi zinatarajiwa kuhitimishwa kesho kwa michezo ya Kundi A, kati ya URA na Jamhuri jioni na Simba SC na JKU usiku.
Hadi sasa, Simba SC inaongoza Kundi A kwa pointi zake nne, ikifuatiwa na URA na JKU zenye pointi tatu kila moja.
CHANZO CHA HABARI: BINZUBEIRY BLOG
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment