KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, January 10, 2016

SIMBA, YANGA ZATUPWA NJE KOMBE LA MAPINDUZI

MABINGWA watetezi wa Kombe la Mapinduzi, Yanga na watani wao wa jadi Yanga, jana walifungasha virago mapema mwaka huu baada ya kupata vipigo kutoka kwa Mtibwa Sugar na URA.

Katika mechi hizo za nusu fainali zilizochezwa kwenye Uwanja wa Amaan, mjini Unguja, Simba ilichapwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar wakati Yanga ilifungwa kwa penalti 4-3 na URA ya Uganda.

Kwa matokeo hayo, Mtibwa na URA sasa zitamenyana katika mechi ya fainali itakayochezwa kesho kwenye uwanja huo wakati Simba na Yanga zimeshafungasha virago kurejea Dar es Salaam.

Mtibwa Sugar ilijipatia bao lake la pekee na la ushindi dakika ya 45 kupitia kwa Ibrahim Rajabu 'Jeba'.

Bao hilo lilitokana na uzembe wa kipa Manyika Peter wa Simba, kuutema mpira uliopigwa kwenye lango la timu yake na kumkuta mfungaji, aliyeukwamisha wavuni.

Katika kipindi cha kwanza, Mtibwa walionekana kucheza soka safi na ya kuonana, ambapo walifanikiwa kupeleka mashambaulizi mengi katika goli la Simba.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, ambapo Kocha wa Simba, Dylan Kerr alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Awadh Juma,Danny Lyanga,Mwinyi Kazimoto na Emily Nimuboma na nafasi zao kuchukuliwa na Ibrahimu Ajibu,Said Ndemla,  Brian Mwajegwa na Rafael Kiongera.

Kuingia kwa wachezaji hao kuliongeza kasi ya Simba kulishambulia lango la Mtibwa,lakini uimara wa golikipa wa Mtibwa Sugar, Said Mohamed, ulikuwa kizingiti kwa Simba kusawazisha.

Kwa matokeo hayo, Mtibwa Sugar imeweka rekodi ya kucheza fainali ya michuano mara tano tangu tangu ilipoanza kushiriki katika michuano hiyo.

Nazo Yanga na URA zililazimika kupigiana penalti tano tano ili kumpata ushindi baada ya kumaliza dakika 90 zikiwa sare ya bao 1-1.

Penalti za Yanga zilifungwa na Kevin Yondan, Deo Munishi ‘Dida’ na Simon Msuva huku Malimi Busungu na Geoffrey Mwashiuya
wakikosa.

Kwa upande wa URA, penalti zake zilifungwa na Deo Othieno, Said
Kyeyune, Jimmy Kulaba na Brian Bwete, wakati Sam Sekito alikosa.

Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe dakika ya 13 kwa kichwa akimalizia mpira uliorudi baada ya kutemwa na kipa wa URA, Brian Bwete kufuatia mchomo wa winga Simon Msuva.

URA ilisawazisha dakika ya 76 kwa bao lililofungwa na Peter Lwasa kutokana na uzembe wa mabeki wa Yanga.


No comments:

Post a Comment