'
Wednesday, January 13, 2016
SIMBA YAMTIMUA KERR
HATIMAYE kocha wa timu ya Simba, Dylan Kerr, ametupiwa virago, muda mfupi, baada ya klabu hiyo kupokwa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi. Kerr, aliwasili Dar es Salaam jana kutoka Zanzibar, baada ya Simba kutolewa katika nusu fainali kwa kuchapwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar.
Kerr, alilazimika kurejea Dar es Salaam mara moja kusomewa ‘mashitaka’ yanayomkabili na Kamati ya Utendaji kutokana na kutoridhishwa na utendaji wake wa kazi. Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema kuwa anatarajia kutoa taarifa rasmi leo kwa vyombo vya habari.
“Kwa sasa siwezi kuzungumzia lolote kuhusu suala hilo, taarifa zaidi nitazitoa baadaye au kesho ambapo nitazungumza na waandishi wa habari,” alisema Manara.
Lakini taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zilisema nafasi ya Kerr imechukuliwa na Mganda Jackson Mayanja, ambaye awali alitangazwa kocha msaidizi.
Mayanja, mmoja wa viungo mahiri wa pembeni waliong’ara Afrika Mashariki na kikosi cha Uganda, alikuwa kocha wa Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’.
Chanzo hicho kilisema kuwa Kamati ya Utendaji ilifanya kikao cha dharura juzi na kufi kia makubaliano ya kuachana na kocha huyo ambaye alitia saini mkataba wa mwaka mmoja. Pia katika mkataba huo kulikuwa na kipengele cha kuongezwa mwaka mmoja endapo angefanya vizuri. Kerr, anadaiwa kutokuwa na uhusiano mzuri na baadhi ya viongozi, wachezaji sanjari na kutokuwa mbunifu katika kazi.
“Kerr ameondolewa baada ya kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi na kujituma, pia hana mahusiano mazuri na baadhi ya viongozi na wachezaji,” kilisema chanzo hicho.
Kocha huyo amedaiwa kutimuliwa jana ambapo ameiacha Simba ikiwa nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 27, nyuma ya Yanga yenye pointi 33 na Azam inaongoza kwa pointi 35. Kerr, anaiacha Simba ikiwa imeshinda mechi nane, imetoka sare mara tatu na kupoteza mechi mbili.
Katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, Simba imepoteza mechi moja, ilitoka sare moja na kufungwa mchezo mmoja na ilishinda michezo miwili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment