KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, January 24, 2016

SIMBA YATINGA 16 BORA KOMBE LA SHIRIKISHO



SIMBA SC imefuzu Raundi ya Nne ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports HD TFF Cup, baada ya kuwachapa wenyeji Burkina Faso mabao 3-0 jioni ya leo Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Shujaa wa Simba SC inayokwenda hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo ambayo itatoa mwakilishi wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mwakani, alikuwa ni mshambuliaji Mganda, Hamisi Friday Kiiza aliyefunga mabao mawili, wakati lingine limefungwa na kiungo Said Ndemla.
Kiiza alifunga mabao yake dakika ya 77 kwa shuti kali akimalizia krosi ya Abdi Banda na la tatu dakika ya 90 kwa penalti, baada ya kiungo Said Ndemla kuangushwa kwenye boksi.
Ndemla alifunga bao la pili la Simba SC hii leo dakika ya 89 kwa shuti la umbali wa mita 38, bao lililowasisimua zaidi mashabiki uwanjani.
Mapema kipindi cha kwanza, Simba SC ilipoteza nafasi mbili nzuri za mabao, kwanza dakika ya 11 wakati winga Joseph Kimwaga alipowalamba chenga vizuri mabeki wa Burkina Faso, lakini akapiga nje na dakika ya 39 beki Mrundi, Emery Nimubona alipopiga nje akiwa karibu na lango. Burkina Faso nayo iliyoongozwa na mkongwe, Ulimboka Alfred Mwakingwe aliyewahi kuwika Simba SC ilipoteza nafasi pia.
Dakika ya 39 Ulimboka alimdakisha kipa Muivory Coast wa Simba SC, Vincent Angban shuti dhaifu akiwa kwenye nafasi nzuri na dakika nne baadaye akachelewa kupiga akiwa kwenye boksi, hadi mabeki wakaokoa.
Katika mechi nyingine za michuano hiyo leo, Toto Africans imeifunga 4-1 Pamba Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, wakati Ndanda FC imeifunga 5-0 Mshikamano Uwanja wa Nagwanda SIjaona mjini Mtwara.

No comments:

Post a Comment