'
Friday, January 1, 2016
IBRAHIM AJIB AING'ARISHA SIMBA LIGI KUU
Na Princess Asia, MTWARA
MSHAMBULIAJI Ibrahim Hajib Migomba, akiwa ametokea benchi na kuifungia Simba SC bao pekee ikishinda 1-0 dhidi ya wenyeji Ndanda FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
Hajib ‘Ibra Kadabra’ aliingia mwanzoni mwa kipindi cha pili kuchukua nafasi ya mshambuliaji Mkenya, Paul Raphael Kiongera na dakika ya 80 akawainua vitini mashabiki wa Simba SC.
Hajib aliukwamisha nyavuni mpira uliorudi baada ya kugonga mwamba kufuatia mshambuliaji Mganda, Hamisi Kizza ‘Diego’ kuunganisha krosi ya Danny Lyanga kutoka upande wa kulia.
Katika mchezo huo, mwamuzi msaidizi namba moja, Mohammed Mkono wa Tanga alikataa bao moja la kila timu, akisema wafungaji waliotea.
Atupele Green aliunganisha krosi ya William Lucian ‘Gallas’ dakika ya nane na kutinga nyavuni, lakini akaambiwa alikuwa ameotea kabla.
Daniel Lyanga naye aliunganishia mpira nyavuni dakika ya 62 baada ya pasi ya Hajib, lakini refa Rajab Mrope wa Songea akaafiki maamuzi ya Mkono kwamba mfungaji alikuwa ameotea kabla.
Awali ya hapo, Kiongera alikaribia kuifungia Simba SC dakika ya 43 akiwa ndani ya boksi kama si mpira kumbabatiza kipa Jackson Chove na kutoka nje.
Ushindi huo, unawafanya Simba SC wafikishe pointi 27 baada ya kucheza mechi 13 na kupanda hadi nafasi ya tatu, nyuma ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 33 na Azam FC pointi 35.
Ligi Kuu inakwenda mapumzikoni kwa mara nyingine hadi katikati ya mwezi, kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoanza keshokutwa visiwani Zanzibar.
Kikosi cha Ndanda FC kilikuwa; Abraham Chove, Bryson Raphael, Ahmed Msumi, Salvatory Ntebe, Jackson Mkwera, Aziz Sibo/Mohammed Ally dk72, Omary Mponda, Hemed Kotta, Kiggi Makassy, William Lucian ‘Gallas’ na Atupele Green,
Simba SC; Vincent Angban, Emery Nimubona, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Brian Majwega/Said Ndemla dk65, Mwinyi Kazimoto/Awadh Juma dk89, Paul Kiongera/Ibrahim Hajib dk46, Danny Lyanga na Hamisi Kizza.
IMETOLEWA BLOGU YA BINZUBEIRY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment